Rio de Janeiro—Maridadi na Lenye Kuvutia
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI
RIO DE JANEIRO lina kila kitu—fuo, vilima, maziwa, na msitu wa kitropiki. “Linavutia hivi kwamba unashindwa utatazama wapi kwanza!” akasema mgeni mmoja. Rio de Janeiro, au Rio tu, huonwa na wengi kuwa mojawapo ya majiji maridadi zaidi ulimwenguni. Japo neno “rio” lamaanisha “mto,” jiji hilo liko hasa kwenye ghuba.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 18.
Kwa kuwa Rio lina wakazi milioni 11 katika eneo lake, bila shaka lina matatizo pia—ujeuri, ukosefu wa kazi, na uhaba wa nyumba, kuongezea uchafuzi na msongamano wa magari. Japo mambo hayo, wakazi wa Rio hulirejezea kuwa Cidade Maravilhosa (Jiji Maridadi Ajabu). Yafuatayo ni maneno ya Cariocaa mmoja: “Rio ni jiji lenye furaha. Siku yenye jua, fuo na vilima tunavyoona tunapokwenda kazini na tunaporudi hutufanya tufurahi.” Je, kweli ndivyo ilivyo? Ebu tuone.
Ghuba, Fuo, na Jua Tele
Twaanzia Ghuba ya Guanabara—chimbuko la Rio. Eneo lake lenye kilometa 380 za mraba lina visiwa vyenye misitu vilivyotapakaa huku na huku, nalo limezingirwa na vilima na milima, ule mashuhuri zaidi ukiwa Corcovado (linalomaanisha “-enye Kibyongo”) na Mlima Sugarloaf (Kireno, Pão de Açúcar). Kwenye kilele cha Corcovado, chenye kimo cha meta 704 juu ya ghuba, kuna sanamu ya Kristo iliyonyosha mikono, nayo ina kimo cha meta 30 na uzito wa tani 1,145. Mlima Sugarloaf, wenye kimo cha meta 395, umepata jina lake kutokana na umbo fulani la mviringo ambalo lilikuwa likitumiwa na wakoloni waliokuwa wakitengeneza sukari. Wageni waweza kupanda Corcovado kwa gari-moshi dogo au kwa motokaa, na kigari cha kamba huwasafirisha wageni hadi kilele cha Sugarloaf. Rio linavutia sana likiwa kati ya bahari ya buluu yenye kina upande mmoja na msitu uliokolea rangi ya kijani na Ziwa Rodrigo de Freitas yenye kupinda-pinda kwa upande mwingine.
Fuo zenye mchanga mzuri mweupe pamoja na jua—tena tele—hufanya Rio livutie sana watalii. Kama unavyoweza kutarajia, fuo 70 zenye urefu wa kilometa 90 kwenye pwani ya Rio hujaa watu kwa sababu wakati wa kiangazi joto hufikia digrii 40 Selsiasi. Ni ufuo gani ulio bora? Jibu lategemea mtu mwenye kwenda ufuoni. Kwa Carioca ufuo ni mahali panapopendwa, mahali pa kusomea, uwanja wa kandanda, uwanja wa voliboli, mahali pa kununulia vinywaji, mikahawa, uwanja wa michezo, mahali pa kuchezea dansi, mahali pa kunyosha viungo vya mwili, na ofisi na vilevile mahali pa kuogelea. Kila asubuhi sehemu za matembezi za Rio hujaa wakimbiaji na waendesha-baiskeli. Na katika siku yenye jua, fuo hujaa wakati wote. Lakini, japo inaonekana kama Carioca wana maisha yenye starehe, ni lazima wafanye kazi kwa bidii ili wafurahie.
Kufikia mwisho wa karne ya 19, jiji la Rio lilikuwa limejengwa kandokando za fuo za Ghuba ya Guanabara. Kisha, mahandaki yaliyojengwa ya kuunganisha ghuba na fuo za bahari yalifanya jiji lianze kupanuka likielekea kusini. Kwa kuzinduliwa kwa Copacabana Palace Hotel mwaka wa 1923, ambayo ni mojawapo ya hoteli za kwanza za hali ya juu katika Amerika Kusini, Copacabana, “Kibibi wa Bahari,” ukawa ufuo wa kwanza kuwa mashuhuri. Baadaye, katika miaka ya 1960, ufuo wa Ipanema ukawa mahali ambapo wasomi na vikundi vya watu hukutania. Ikiwa kitu hakikuonwa kuwa cha kisasa katika Ipanema, basi hakikuwa cha kisasa. Ufuo wa karibuni zaidi na ulio mkubwa zaidi miongoni mwa fuo za Rio ni Barra da Tijuca (wenye urefu wa kilometa 18). Ufuo huo una maduka makubwa zaidi katika jiji hilo na majengo mengi mapya ya makazi.
Msitu Uliozingirwa na Jiji
Rangi ya kijani-kibichi hujitokeza sana katika mandhari ya Rio, na bustani yake tulivu ya mimea yenye ukubwa wa ekari 350 na ambayo ipo katikati ya jiji, iko umbali wa dakika chache tu kutoka kwenye kelele za fuo. Bustani hiyo ilitayarishwa katika karne ya 19 na ina zaidi ya aina 6,200 za mimea na miti ya kitropiki.
Mahali pengine patulivu katika jiji hilo ni Msitu wa Tijuca. Msitu huo upo kilometa 20 hivi kutoka katikati ya jiji la Rio nao umeenea zaidi ya kilometa za mraba 100, na labda huo ndio msitu mkubwa zaidi unaopatikana mjini ulimwenguni pote. Pia msitu huo una sehemu ya Msitu wa Atlantiki, ambao zamani ulienea kotekote katika pwani ya Brazili. Wageni waweza kuona mti aina ya pink jequitiba wenye fahari pamoja na canelas-santas wenye maua ya manjano maridadi. Vilevile kuna vipepeo maridadi wenye rangi ya buluu wa jamii ya Morpho. Kwa habari ya ndege, tanagers wenye vichwa vya kijani au wenye shingo nyekundu hupatikana kwa wingi.
Kuzuru Katikati ya Jiji
Mna shughuli nyingi sana katikati ya Rio—watu wakitembea haraka-haraka kila mahali na kelele nyingi na joto jingi. Watu hung’ang’ania nafasi na wachuuzi ambao huuza karibu kila kitu, tokea vitu vya elektroni vilivyoingizwa nchini hadi mavazi, vikolezo, na dawa za sugu za miguu. Unaweza kufurahia kupanda tramu juu ya matao 42 yaliyotengenezwa kwa itale ambayo huitwa Arcos da Lapa. Matao hayo yalijengwa na Wahindi na watumwa baina ya mwaka wa 1712 na 1750, na awali matao hayo yalikuwa mfereji uliopeleka maji katikati ya Rio. Lakini, mnamo mwaka wa 1896 tramu zilianza kukimbia juu ya mfereji huo, ukiugeuza kuwa daraja.
Vilevile katikati ya jiji mna eneo la Kizungu. Jumba la Taifa la Makumbusho la Michoro, lililojengwa baina ya mwaka wa 1906 na 1908, lina sehemu ya mbele inayofanana na Jumba la Ukumbusho la Louvre mjini Paris, na paneli zake zenye rangirangi na michoro yake hukumbusha mtu ule Mvuvumko wa Italia. Jengo jingine muhimu ni Jumba la Manispaa la Michezo ya Tamthilia, lililozinduliwa mwaka wa 1909 na ambalo linatoshea watazamaji 2,357 na kujengwa kufuatia mtindo wa Jumba la Opera la Paris.
Kandanda na Samba
Carioca hufurahia mechi safi ya kandanda, na mechi muhimu za ligi zinapochezwa, mambo yote huelekea Stediamu ya Maracanã. Uwanja huo wajulikana kuwa stediamu kubwa zaidi ya kuchezea kandanda ulimwenguni, nao umekuwa na mechi zilizohudhuriwa na mashabiki wapatao 200,000. Kwa wakati huu, ni watu 100,000 tu wanaoruhusiwa ndani kwa sababu ya usalama na vilevile kuzuia kusongamana kwa mashabiki.
Dansi inayopendwa na Carioca ni samba ambayo ilitokea Afrika. Kotekote jijini shule zinazofundisha jinsi ya kusakata samba huvutia maelfu ya wacheza-dansi—wanaume, wanawake, na watoto—mara nyingi wakitoka mtaa mmoja. Wakati wa sherehe za carnival, kabla tu ya Kwaresima, shule hizo—kila moja ikiwa na wacheza-dansi 5,000—hupitia Sambódromo, ambalo ni baraza kubwa lililojengwa kipekee, kati ya jukwaa mbili zinazokabiliana na ambazo zina paa na ambazo zinaweza kutoshea watu 100,000. Kwa kusikitisha, carnival imekuwa maarufu kwa matendo yenye kupita kiasi, kama vile watu kuendesha gari wakiwa wamelewa hadi kutumia dawa za kulevya na kufanya ngono kiholela.
Rio Lina Matatizo Yake
Kwa miongo mingi, hadi kufikia wakati lilipopitwa na São Paulo katika miaka ya 1950, Rio de Janeiro lilikuwa kituo cha viwanda cha Brazili. Tamaa ya kuishi maisha bora ilifanya wengi watoke mashambani na kuhamia Rio, jambo lililofanya wakazi wengine wasongamane kwenye majengo yenye vyumba vingi na walio maskini kuishi milimani na kujenga mitaa ya mabanda inayoitwa favelas. Awali mabanda hayo yalijengwa kwa vipande vya masanduku yaliyoharibiwa, na mikebe kisha yakafunikwa kwa mabati. Hawakuwa na umeme, mfumo wa kuondolea takataka, wala maji ya mfereji, lakini angalau jambo la kwamba mahali hapo palikuwa karibu na mahali pa kazi lilifanya maisha yawe rahisi kwa wakazi wake. Leo, mitaa mikubwa ya mabanda imejaa kandokando za milima karibu sana na majengo mazuri ya kuishi ambayo yamejaa kandokando ya Copacabana na Ipanema. Ni sehemu chache ulimwenguni ambazo zinatokeza tofauti kubwa hivyo kati ya matajiri na maskini.
Mitaa mipya ya mabanda sasa inajengwa kwa matofali. Wapangaji wa miji wamejaribu kufanya hali iwe bora kwa kutengeneza barabara za mitaa na kuweka vifaa vinavyohitajika; lakini hiyo si kazi rahisi. Kulingana na uchunguzi mmoja wa karibuni, zaidi ya watu 900,000 huishi katika zaidi ya mitaa 450 ya mabanda. Mtaa mkubwa zaidi wa mabanda, Rocinha, una wakazi 150,000. “Ni kama jiji ndani ya jiji,” aeleza Antônio, anayeishi hapo na ambaye anafanya kazi katika benki moja kule Ipanema. Wakazi wa huko wana televisheni za kebo, redio ya jumuiya, stesheni ya redio ya FM na vilevile timu ya kandanda ya kulipwa pamoja na shule ya kufundisha dansi ya samba. Lakini maisha katika mtaa wa mabanda yana magumu pia. Mvua za majira ya kiangazi husababisha maporomoko ya ardhi kwenye vilima, ambayo hujeruhi watu na hata kusababisha vifo. Programu iliyoanzishwa karibuni ya kupanda upya misitu imeondoa nyumba ambazo zilikuwa zimejengwa kwenye maeneo hatari, na hivyo basi ikiboresha hali.
Tatizo jingine kubwa ni uhalifu uliopangwa. Wanaoathiriwa sana ni vijana ambao hufanya kazi ya ulanguzi wa dawa za kulevya. Uhusiano baina ya walanguzi wa dawa za kulevya na wakazi huongozwa na kanuni fulani zilizowekwa. “Ni kama hakuna unyang’anyi, ujambazi, au kubakwa katika mitaa hii ya mabanda. Hakuna mtu awezaye kuthubutu kufanya makosa hayo. Watu wanajua kwamba watauawa wakifanya mambo hayo,” aeleza João, ambaye ameishi katika mtaa huo wa mabanda kwa miaka 40. Walanguzi wa dawa za kulevya huadhibu watu wanaofanya uhalifu usiohusu dawa za kulevya ili wapendwe na wakazi. “Japo mambo yamebadilika kidogo,” João aongezea, “bado ni kawaida kwa wakazi kuwaomba walanguzi wa dawa za kulevya kuwalipia gharama za mazishi, kuwanunulia dawa au chakula, kuwalipia kodi iliyochelewa ya nyumba, au kugharimia vitumbuizo.”
Magumu Mengine
Likiwa kati ya bahari na milima, Rio limekua katika uwanda wa bwawa—mahali ambapo hapafai sana ukuzi wa jiji kubwa. Katika miaka ambayo imepita, imekuwa lazima “kupigana na vitu hivi vitatu: mabwawa, bahari, na milima,” chaeleza kitabu Rio de Janeiro—Cidade e Região (Rio de Janeiro—Jiji na Eneo). Ili kushinda magumu hayo, mahandaki mengi yamejengwa na mchanga kujazwa ili kuunganisha mitaa mbalimbali. Reli vilevile zimechangia sana watu kuishi viungani mwa jiji hilo, ingawa siku hizi safari za reli zina visa vingi. “Kuna watu wengi sana wanaojaribu kupanda gari-moshi hivi kwamba hata mtu hahitaji kufanya jitihada yoyote ya kupanda. Umati wakusukuma tu,” aeleza Sérgio, ambaye analazimika kupanda gari-moshi saa kumi na moja alfajiri kwenye viunga vya jiji ili aweze kufika kazini saa moja. Magari-moshi hujaa pomoni hivi kwamba mara nyingi yanaondoka stesheni milango ikiwa haiwezi kujifunga na abiria wakining’inia kandokando za mabehewa. Carioca wenye kujasiria zaidi hata hupanda juu ya magari-moshi, tendo hilo linaitwa kupaa juu ya gari-moshi. Hakika wanaweza kufa endapo wafanye kosa dogo tu wanapojaribu kuepa waya za umeme.
Ugumu mwingine ni kuhifadhi Ghuba ya Guanabara, ambayo ni ishara ya umaridadi wa jiji hilo. Kulingana na ripoti ya Benki ya Ulimwengu, katika sehemu fulani maji yake “karibu yafanane na maji machafu kwa sababu ya kutiliwa takataka nyingi zinazotoka kwenye viwanda na ambazo hazitiwi dawa (au huwekwa dawa kidogo).” Kuna madhara makubwa nayo yatia ndani kupungua kwa aina fulani za samaki, na kuathiri wavuvi 70,000 wanaotegemea ghuba hiyo kwa riziki. Fuo zilizochafuliwa vilevile huogofya watalii. Serikali imejaribu kupanua mfumo wa kuondoa takataka na kudhibiti viwanda. Kampeni ya Rio inayopinga uchafuzi ina ishara ya dolfini wawili. Watayarishaji wa kampeni hiyo watabiri kwamba kufikia mwaka wa 2025 dolfini watakuwa wakiogelea kwenye Ghuba ya Guanabara!
Rio Lingali Maridadi!
Baada ya kuchunguza Rio kwa ufupi, waonaje? Kwa watalii wengi na Carioca wengi, Rio lingali maridadi! Na vipi juu ya magumu yake? Ingekuwa vizuri kama yangesuluhishwa. Lakini hadi yasuluhishwe, Carioca waweza tu kung’ang’ana kwa kadiri wawezavyo na matatizo ya jiji hilo na kufurahia eneo lake maridadi. Wamejifunza kufanya hivyo, kwa ubunifu na kwa ucheshi.
[Footenote]
a Siku hizi Carioca hurejezea mwenyeji au mkazi awaye yote wa Rio de Janeiro.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]
Matukio Muhimu Katika Historia ya Rio
1502: Januari 1, André Gonçalves, baharia Mreno, akosea mwingilio wa Ghuba ya Guanabara kuwa ni lango la mto, akayaita maji hayo Rio de Janeiro (Mto wa Januari).
1565: Estácio de Sá, mkuu wa majeshi ya Ureno, aanzisha kijiji kidogo kati ya vilima vya Mlima Sugarloaf na Cara de Cão ili awakabili Wafaransa, ambao pia walikuwa wamedai eneo hilo. Kijiji hicho kikawa jiji la Rio.
1763: Wareno waipandisha cheo Rio iwe jiji kuu katika jitihada za kudhibiti dhahabu nyingi na almasi nyingi zilizokuwa zikitoka Jimbo jirani la Minas Gerais na kupitia bandari hiyo kuelekea Ureno. Biashara ya utumwa wa Waafrika yanawiri.
1808: Familia ya kifalme ya Ureno yafika, wakitoroka mashambulizi yaliyokuwa yamekaribia ambayo yangefanywa na Napoléon wa Kwanza dhidi ya Ureno, na Rio lapata kuwa kiti cha utawala cha Ureno kwa muda. Rio laendelea kuwa jiji kuu mpaka wakati Brasília lilipojengwa mwaka wa 1960.
[Hisani]
PICHA: MOURA
[Picha katika ukurasa wa16, 17]
Ufuo wa Barra da Tijuca
[Picha katika ukurasa wa 17]
Maracanã, stediamu kubwa zaidi ya kuchezea kandanda ulimwenguni
[Picha katika ukurasa wa 18]
Arcos da Lapa, mfereji wa maji uliogeuka kuwa daraja