Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 3/8 kur. 22-24
  • Mawe ya Mviringo na ya Ajabu ya Kosta Rika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mawe ya Mviringo na ya Ajabu ya Kosta Rika
  • Amkeni!—1999
  • Habari Zinazolingana
  • Kosta Rika—Nchi Ndogo, Unamna Mwingi
    Amkeni!—1995
  • Matendo ya Mashahidi wa Yehova Katika Nyakati za Kisasa
    1988 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Ni Nani Aliyetunga Sheria Zinazoongoza Ulimwengu Wetu?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2011
  • Je! Sayansi Imefanya Biblia Ikawa Bure?
    Amkeni!—1991
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 3/8 kur. 22-24

Mawe ya Mviringo na ya Ajabu ya Kosta Rika

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KOSTA RIKA

KWA MUDA upatao karne 16 zilizopita, wenyeji wa kusini-magharibi mwa Kosta Rika walikuwa wakitengeneza namna mbalimbali za mawe ya mviringo, mengine yakiwa na udogo wa kipenyo cha sentimeta 10 na mengine yakiwa na kipenyo cha meta 2.4. Yameundwa kwa njia nzuri sana hivi kwamba mtu husukumwa kuuliza, ‘Yalitengenezwaje? Yalitimiza kusudi gani?’

Majabali ya mviringo yamepatikana katika nchi nyinginezo, kutia ndani Chile, Mexico, na Marekani. Lakini matale ya mviringo ya Kosta Rika ni ya kipekee. Ubora wake ni wenye kutokeza sana, mengine yakiwa mviringo kabisa na laini. Mara nyingi yamepatikana katika vikundi vya mawe 20 au zaidi. Jambo linalopendeza hata zaidi ni kwamba mengi yake yanapatikana yakiwa katika maumbo ya jiometria, kama vile pembetatu, mistatili, na mistari iliyonyooka. Mara nyingi mistari hii huelekeza kwenye upande wa kaskazini wa dira.

Mawe kadhaa yamepatikana katika Delta ya Mto Di­quis. Mengine yamepatikana karibu na majiji ya kusini ya Palmar Sur, Buenos Aires, na Golfito na vilevile katika mkoa wa Guanacaste kuelekea kaskazini na kwenye bonde la kati. Vitu vya kale kadhaa vilivyopatikana pamoja na mawe hayo vimetoa madokezo mazuri kuhusu umri wake. Waakiolojia wanakadiria kwamba baadhi ya majabali haya ya kifumbo ni ya mwaka wa 400 W.K. Idadi kubwa zaidi ya mawe hayo yalijitokeza kati ya mwaka wa 800 na 1200 W.K. Mengine yamepatikana karibu na sehemu ambayo yaelekea ilikuwa makao au karibu na makaburi. Kwa miaka iliyopita, mawe fulani yameharibiwa na watu waliodhania watapata hazina zikiwa zimefichwa ndani yake. Hata hivyo, Jumba la Makumbusho ya Taifa la Kosta Rika lina orodha ya mawe ya mviringo yapatayo 130. Lakini kuna mengi zaidi ambayo hayajaorodheshwa. Imekuwa vigumu kuhesabu mawe haya ya kale kwa sababu mengi yameondolewa kutoka mahali pao pa awali na kuwekwa kuwa madoido katika sehemu za kibinafsi, kama vile kwenye bustani na makanisani. Bila shaka, bado kuna mengi ambayo hayajavumbuliwa—mengine yakiwa chini ya ardhi, mengine yakiwa ndani ya misitu minene.

Yalitengenezwaje? Hili ni fumbo. Yaelekea kwamba mashine fulani zilitumiwa ili kuyatengeneza yawe bila kasoro. Kwa kufikiria sanamu nyingi za kipindi hicho, tunajua kwamba watengenezaji wa mawe ya mviringo walikuwa wachongaji stadi. Kwa kuongezea, vitu vya kale vya dhahabu vya mwaka wa 800 W.K. huthibitisha kwamba walikuwa na uzoefu wa kufanya kazi kwa kutumia moto mwingi. Nadharia moja inaonyesha kwamba kuchongwa kwa mawe ya mviringo kungeweza kuhusisha kutumia moto mwingi na kisha kuyapoesha, ili kuondoa tabaka za juu. Kazi hiyo ingemalizwa kwa kung’arisha mawe hayo ya mviringo kwa kutumia mchanga au ngozi.

Mwanasayansi mmoja alieleza kwamba mawe ya mviringo makubwa “yalitengenezwa na wasanii stadi kabisa, na [mawe ya mviringo] karibu yalikuwa bila kasoro hivi kwamba kwa kupima kipenyo kwa kutumia utepe na pima-maji hakuna kasoro yoyote iliyoonekana.” Usahihi huu waonyesha kwamba wenyeji hao walikuwa na uwezo mkubwa wa hisabati, ujuzi wa hali ya juu wa kuchonga mawe, na walijua kutumia vifaa. Hata hivyo, kwa kuwa yaonekana watu hawa hawakuwa na lugha iliyoandikwa, hakuna rekodi zozote zinazoonyesha kwa usahihi jinsi walivyotengeneza mawe ya mviringo.

Mengi ya mawe haya ya mviringo yamefanyizwa kwa majabali yanayofanana na matale. Machimbo ya matale yanayojulikana yaliyo karibu yako juu ya milima kilometa zipatazo 40 hadi 50 kutoka kwenye Delta ya Mto Diquis. Wachongaji hao walisukumaje mawe hayo mazito? Ikiwa mawe hayo ya mviringo yalichongwa kwenye machimbo, wachimbaji wangehitaji kuzuia kwa uangalifu namna ambavyo yangeteremka. Je, waweza kuwazia ugumu wa kusukuma kitu kizito namna hiyo kufikia umbali huo bila kuwa na vifaa vya kisasa? Mawe ya mviringo yana uzito gani hasa? Mengine yana uzito unaozidi tani 16!

Ikiwa matale yalichimbwa na kusukumwa kabla ya kuchongwa, mchemraba wa meta 2.7 ambao ungehitajiwa kwa duara lenye kipenyo cha meta 2.4 ungekuwa na uzito wa tani 24! Yaelekea kwamba ili kutengeneza barabara pana iliyo laini ili kuyasafirisha, wenyeji wangehitaji kufyeka njia kwenye msitu mnene. Utimizo mkubwa kama nini! Mawe mengine ya mviringo yalitengenezwa kwa chokaa ya aina fulani, yanayoweza kupatikana kwenye fuo karibu na mdomo wa Mto Diquis. Hili laweza kuonyesha kwamba jiwe hilo lilisafirishwa kwenye mto kwa karibu kilometa 50 kuelekea juu. Mawe fulani ya mviringo yamepatikana kwenye Kisiwa cha Caño, karibu kilometa 20 kando ya pwani ya Pasifiki.

Hakuna mtu awezaye kueleza kwa uhakika kusudi la awali la mawe haya ya mviringo. Huenda yalikuwa ishara ya cheo au ya mamlaka ya chifu wa kabila au wa kijiji. Pia yawezekana kuwa yalikuwa ishara za kidini au za kisherehe. Huenda siku fulani uchunguzi wa baadaye wa kiakiolojia ukafunua fumbo la mawe ya mviringo ya Kosta Rika.

[Ramani katika ukurasa wa 22, 23]

Kosta Rika

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Garimoshi nyuma ya jiwe la mviringo laonyesha ukubwa wa jiwe hilo

[Hisani]

Courtesy of National Museum of Costa Rica

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mawe ya mviringo kwenye Jumba la Makumbusho ya Taifa la Kosta Rika

Jiwe la mviringo kubwa zaidi ambalo limepatikana kufikia sasa, lenye kipenyo cha meta 2.4

[Hisani]

Courtesy of National Museum of Costa Rica

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki