Vijana Huuliza . .
Kwa Nini Ninahangaikia Sana Uzito Wangu?
“Kuna pambano kali akilini mwangu. Ninapotaka kula, wazo jingine hunijia la kutokula kwa sababu ninahofu kwamba nitaongeza uzito mwingi zaidi.”—Jaimee.
NI NINI unachohofu zaidi ya kitu kingine cho chote? Bila kusita, wasichana wengi watajibu: kuongeza uzito. Kwa hakika, uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba wanawake vijana leo huhofu zaidi kuongeza uzito kuliko vita ya nyuklia, kansa, au hata kuwapoteza wazazi wao!
Kwa kushangaza, nyakati nyingine kuhangaikia uzito huanza katika umri mchanga zaidi. Hata kabla ya utineja, wasichana wengi hukutana ili kuwa na “mazungumzo juu ya uzito”—mazungumzo yanayofunua jinsi ambavyo wanachukia miili yao, asema Dakt. Catherine Steiner-Adair. Kwa msingi wa uthibitisho uliopo, ni zaidi ya mazungumzo ya kivivi hivi tu. Katika uchunguzi wa wasichana 2,379, asilimia 40 walikuwa kwa hakika wakijaribu kupunguza uzito. Wale waliohojiwa walikuwa wenye umri wa miaka tisa na kumi tu!
Baada ya muda, huenda wengi wa vijana hawa wakaanza kula milo ya kimtindo. Na lililo baya zaidi ni kwamba huenda baadhi yao watakuwa kama Jenna mwenye umri wa miaka 20. Akiwa na kimo cha futi tano na inchi nne, mwanamke huyu kijana ana uzito wa kilo 40 tu! “Mimi sitaki kula tu,” asema Jenna. “Hangaiko langu kubwa ni kwamba nilitumia muda wa miaka mitatu kupoteza uzito, na kwa kula nitaurudisha katika kipindi cha mwezi mmoja.”
Labda unaweza kuelewa hisia za Jenna. Huenda ikawa kwamba hata wewe umekuwa ukitaka kuwa mwembamba ili uonekane bora zaidi. Kwa hakika, si kosa kuhangaikia sura yako. Hata hivyo, tamaa ya Jenna ya kuwa mwembamba karibu imuue. Jinsi gani?
Kufa Njaa
Jenna anakabiliana na ugonjwa wa ulaji hatari sana wa kukosa hamu ya chakula. Na ndivyo na Jaimee, aliyetajwa mwanzoni. Kwa wakati fulani, wasichana hawa walikuwa wakifa njaa, na ndivyo na wengine. Inakadiriwa kwamba msichana 1 kati ya 100 ana ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula. Hilo lamaanisha kwamba mamilioni ya wanawake vijana wameathiriwa—labda hata mtu fulani umjuaye!a
Ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula waweza kuibuka kwa njia rahisi sana. Msichana mdogo aweza kuamua kula mlo usioonekana kuwa na madhara, ili labda apoteze kilo chache tu. Hata hivyo, anakosa kuridhika afikiapo mradi wake. “Mimi bado ni mnene sana!” yeye asema anapojitazama bila furaha kwenye kioo. Hivyo anaamua kupunguza kilo chache zaidi. Kisha kilo nyingine chache. Na nyingine zaidi. Linakuwa zoea, na ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula unaanza kusitawi.
Bila shaka, si wote wenye kujinyima chakula walio na ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula. Wengine wana hangaiko halali la uzito wao, na kwa watu hawa, kupunguza kilo chache kwaweza kuwa na manufaa. Lakini wasichana wengi wana maoni yaliyopotoka juu ya mwili wao. Gazeti la FDA Consumer hulinganisha kuwa na umbo baya la mwili na kujitazama katika kioo kinachopotosha kuonekana kwa umbo la mwili. “Unajiona ukiwa mnene kuliko ulivyo,” gazeti hilo lasema.
Kwa sababu hiyo, mtu aliye na ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula huwa na hofu isiyofaa ya kuongeza uzito—hata ajapokuwa mwembamba kama kijiti. Huenda akafanya mazoezi kwa bidii ili abaki akiwa mwembamba na kujipima uzito mara kadhaa kwa siku ili kuhakikisha kwamba harudishi uzito aliopunguza. Anaweza kula chakula kidogo sana. Au huenda asile kabisa. “Kila siku ningeenda shuleni na chakula cha mchana alichonitayarishia mama, na karibu kila siku ningetupa chakula hicho,” asema Heather. “Punde si punde nikazoea kutokula hivi kwamba hata nilipotaka kula, nilishindwa. Sikuhisi njaa.”
Mwanzoni, watu wenye ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula kama Heather hufurahi sana wanapopunguza uzito. Lakini hatimaye ukosefu wa lishe inayofaa huanza kuwaathiri. Mtu mwenye kukosa hamu ya chakula huwa mchovu na mwenye kusinzia. Kazi yake ya shule huanza kuathiriwa. Huenda akakosa hedhi.b Baada ya muda, huenda mpigo wa moyo na msongo wa damu ukashuka sana. Na bado, mtu mwenye kukosa hamu ya chakula huwa hatambui hatari yoyote. Kwa hakika, hatari moja tu anayoona ni kurudisha uzito aliopunguza—hata kilo moja tu ya uzito huo.
Hata hivyo, ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula si tatizo pekee la ulaji, na wala si tatizo pekee lililoenea sana. Kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida ni ugonjwa unaoathiri idadi ya wasichana inayopita kwa mara tatu ile ya ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula. Kisha kuna kula kusikodhibitiwa, kunakohusiana kwa ukaribu na ugonjwa wa kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida. Acheni tuchunguze kwa ukaribu magonjwa haya.
Tatizo la Siri
“Hivi karibuni rafiki yangu aliungama kwamba yeye huleta chakula na kukila kwa siri. Kisha hujilazimisha kutapika. Yeye adai kwamba amekuwa akifanya hivyo kwa miaka miwili.” Kwa maneno haya, kijana mmoja, akiandikia safu moja ya ushauri kwenye gazeti, aeleza dalili zinazofanana na zile za tatizo la kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida.
Mwenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida hula chakula kingi sana kwa kipindi kifupi cha wakati. Kisha mara nyingi huondoa chakula hicho mwilini kwa kujilazimisha kutapika.c Kwa kweli, wazo la kuondoa chakula tumboni kwa njia hii laweza kuonekana kuwa lenye kuchukiza. Hata hivyo, mfanya-kazi wa huduma za jamii Nancy J. Kolodny aandika hivi: “Kadiri unavyokula kwa wingi na kusafisha tumbo, ndivyo iwavyo rahisi kwako. Hisi zako za mapema za kuchukizwa au hata hofu hubadilishwa mara moja na kichocheo cha kurudia mazoea haya ya kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida.”
Tatizo la kukosa hamu ya chakula na la kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida limeonwa kuwa “dalili tofauti za kisababishi kimoja.” Huku yakiwa na dalili zinazotofautiana, matatizo yote mawili huchochewa na tamaa kubwa ya chakula.d Hata hivyo, tofauti na tatizo la kukosa hamu ya chakula, kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida huweza kufichwa kwa urahisi. Kwa vyovyote, kula chakula kingi humzuia aliye na tatizo hilo kupunguza uzito, na kusafisha tumbo humzuia kuongeza uzito. Kwa sababu hiyo, yaelekea kwamba mwenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida hatakuwa mnene sana wala mwembamba, na huenda mazoea yake ya kula yakaonekana kuwa ya kawaida hadharani. “Kwa miaka tisa,” asema mwanamke aitwaye Lindsey, “nilikula kupita kiasi na kutapika mara nne au tano kila siku. . . . Hakuna yeyote aliyejua tatizo langu la kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida, kwa sababu kwa unafiki nilionyesha sura ya uhodari, furaha, na uzito wa mwili wa wastani.”
Hata hivyo, kwa njia fulani tatizo hilo ni tofauti na kula kusikodhibitiwa. Sawa na mwenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida, mtu huyu huweza kula chakula kingi sana kwa wakati mmoja. Kitabu The New Teenage Body Book chasema: “Kwa kuwa tabia ya kula kupita kiasi hutukia bila kusafisha tumbo, huenda uzito wa mlaji asiyejidhibiti ukaongezeka kidogokidogo hadi anapoonekana akiwa mwenye uzito wa kupita kiasi au mnene.”
Hatari za Kiafya
Matatizo yote matatu ya ulaji yanaweza kuhatarisha sana afya ya mtu. Kukosa hamu ya chakula kwaweza kusababisha utapiamlo mbaya sana, na katika visa vingi—wengine hukadiria kwamba asilimia 15 ya visa—huweza kusababisha kifo. Kula kupita kiasi, kuwe kunafuatwa na usafishaji wa tumbo au la, ni hatari kwa afya. Baada ya muda, kunenepa sana kwaweza kutokeza maradhi ya mishipa ya moyo yaliyo hatari kwa uhai, kisukari, na hata aina fulani za kansa. Kujilazimisha kutapika kwaweza kuharibu umio, na matumizi ya kupita kiasi ya dawa za kuharisha na kukojoza yaweza katika visa vibaya zaidi kusababisha shtuko la moyo.
Hata hivyo, kuna jambo jingine kuhusu matatizo ya ulaji linalohitaji kufikiriwa. Kwa kawaida wale walio na tatizo la kukosa hamu ya chakula, kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida, na kula kusikodhibitiwa hukosa furaha. Wao huelekea kukosa kujistahi, kuwa na mahangaiko na kuwa na mshuko-moyo. Kwa wazi, wanahitaji msaada. Lakini wale walio na tatizo la ulaji wanaweza kusaidiwaje kuepuka kuhangaikia sana uzito? Swali hili litazungumziwa katika makala ya wakati ujao katika mfululizo huu.
[Maelezo ya Chini]
a Wanaume pia hupatwa na ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula. Hata hivyo, kwa kuwa wengi wenye ugonjwa huo ni wasichana, tutawarejezea kwa jinsia ya kike wale walio nao.
b Kitiba, mwanamke huonwa kuwa na ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula wakati uzito wake unapungua hadi kufikia angalau asilimia 15 chini ya uzito wa kawaida naye amekosa hedhi kwa miezi mitatu au zaidi.
c Njia nyingine za kusafisha tumbo hutia ndani matumizi ya dawa za kuharisha au kukojoza.
d Hali ya baadhi ya watu wenye tatizo hilo hubadilika kati ya kukosa hamu ya chakula na kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida.
[Sanduku katika ukurasa wa 14]
Maoni Yaliyopotoka Kuhusu Umbo la Mwili
Wasichana wengi wanaohangaikia uzito wao hawana sababu ya kuhangaika. Katika uchunguzi mmoja, asilimia 58 ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 5 na 17 walijiona kuwa wazito kupita kiasi, wakati ambapo, kwa hakika ni asilimia 17 tu waliokuwa wazito kupita kiasi. Katika uchunguzi mwingine, asilimia 45 ya wanawake waliokuwa na uzito wa chini sana walijifikiria kuwa wazito sana! Uchunguzi mmoja wa Kanada ulionyesha kwamba asilimia 70 ya wanawake katika nchi hiyo wanahangaikia sana uzito wao, na asilimia 40 hula bila utaratibu wowote—likiwa ni zoea la kupunguza na kuongeza uzito tena.
Ni wazi kwamba maoni yaliyopotoka kuhusu umbo la mwili yanaweza kuwafanya wasichana fulani wahangaikie kupita kiasi jambo ambalo kwa kweli si tatizo. “Nina rafiki anayemeza vibonge vya kupunguza uzito nami nawajua wasichana kadhaa walio na tatizo la kukosa hamu ya chakula,” asema Kristin mwenye umri wa miaka 16. Yeye aongeza hivi: “Kwa hakika hakuna yeyote kati yao aliye mnene.”
Ni kwa sababu nzuri kwamba gazeti FDA Consumer lapendekeza hivi: “Badala ya kujinyima chakula kwa sababu ‘kila mtu’ anafanya hivyo au kwa sababu wewe si mwembamba kama utakavyo kuwa, kwanza wasiliana na daktari au mtaalamu wa mambo ya lishe ujue ikiwa u mzito kupita kiasi au una mafuta mengi ya mwili kulingana na umri na kimo chako.”
[Picha katika ukurasa wa 15]
Wengi wanaohangaikia uzito wao hawana sababu ya kufanya hivyoy