Kujinyima Chakula na Kuwa na Hamu ya Chakula Isiyo ya Kawaida—Mambo Hakika, Hatari
“Chakula hubeba mzigo wa kihisia-moyo ulio mzito zaidi ya kitu chochote kiwezacho kupimwa kwa kalori au kwa gramu.”—Janet Greeson, mwandishi.
MATATIZO mawili ya kula yaliyo ya kawaida zaidi ni kujinyima chakula na kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida. Kila moja lina mambo yake ya kipekee. Lakini kama tutakavyoona, yote mawili yaweza kuwa hatari—hata yenye kufisha.
Kujinyima Chakula—Njaa ya Kujiletea
Watu wanaoteseka kwa kujinyima chakula, ama hukataa kula au hula kiasi kidogo sana hivi kwamba wanakosa lishe ya kutosha. Mfikirie Antoinette mwenye umri wa miaka 17, anayesema kwamba wakati fulani huenda uzito wake ulipungua kufikia kilogramu 37—uzito kidogo sana kwa kijana mwenye urefu wa futi tano na inchi saba. “Sikula zaidi ya kalori 250 kwa siku na niliandika kwenye kitabu chakula nilichokula,” yeye asema.
Watu wanaojinyima chakula wana hofu ya chakula, na watafanya yote wawezayo ili kujizuia kuongeza uzito. “Nilianza kutema chakula changu kwenye karatasi ya kupangusia mdomo nikijifanya kwamba nilikuwa nikipangusa mdomo wangu,” asema Heather. Susan alifanya mazoezi kwa bidii ili kupunguza uzito wake. “Karibu kila siku,” asema, “nilikimbia kilometa 12, au kuogelea kwa muda wa saa moja, au sivyo nilihisi wasiwasi na hatia iwapo sikufanya mazoezi. Na kila asubuhi nilifurahia sana, kwa kawaida furaha yangu pekee, kupanda juu ya mizani ili kuthibitisha kwamba uzito wangu ulipungua kilogramu 45.”
Jambo la kinyume, watu fulani wanaojinyima chakula huwa wapishi bora na wataandaa chakula kitamu sana ambacho wao wenyewe hukataa kukionja. “Hali yangu ilipokuwa mbaya sana,” asema Antoinette, “nilitayarisha chakula chote cha mchana nyumbani na kuwatayarishia ndugu na dada yangu mdogo chakula cha kubeba. Singewaruhusu wakaribie friji. Nilihisi kana kwamba jiko lilikuwa langu peke yangu.”
Kulingana na kitabu A Parent’s Guide to Anorexia and Bulimia, watu fulani wanaojinyima chakula “huwa safi kupita kiasi na waweza kuwadai wengine katika familia nzima wafikie viwango vyao visivyo halisi na visivyofikika. Hakuna gazeti au viatu au kikombe cha kahawa kiwezacho kuachwa mahali pasipopafaa hata kwa dakika chache. Huenda wakahangaikia sana afya ya kibinafsi na sura, wakitumia muda mwingi kuvalia, mlango ukiwa umefungwa na kuwakataza wengine wasiingie ili kujitayarisha kwenda shuleni au kazini.”
Tatizo hili la kujinyima chakula husitawi namna gani? Hasa, tineja au mtu mzima mchanga—mara nyingi mwanamke—huanza harakati za kupunguza ratili kadhaa. Hata hivyo, anapofikia mradi wake, hukosa kuridhika. Anapojitazama kwenye kioo, bado hujiona kuwa mnene, na kwa hiyo anaamua kwamba litakuwa jambo bora kupunguza ratili nyingine chache. Jambo hili huendelea mpaka mwenye kupunguza uzito anapofikia asilimia 15 au zaidi chini ya kiwango cha kawaida kwa urefu wake.
Kufikia kiwango hiki marafiki na washiriki wa familia huanza kuonyesha wasiwasi kwamba mwenye kupunguza uzito anaonekana mwembamba sana, hata kuwa amedhoofika. Lakini mtu anayejinyima chakula huona mambo kwa njia tofauti. “Sikudhani nilionekana nimekonda,” asema Alan, mwanamume mwenye urefu wa futi tano na inchi tisa anayejinyima chakula ambaye wakati mmoja uzito wake ulipungua na kufikia kilogramu 33. “Kadiri upunguzavyo uzito,” asema, “ndivyo akili yako hupotoka na kukosa kujiona waziwazi.”a
Baada ya muda, kujinyima chakula kwaweza kuongoza kwenye matatizo makubwa ya afya, kutia ndani kupoteza ugumu wa mifupa na kuharibika kwa figo. Hata kwaweza kuua. “Daktari wangu aliniambia kwamba nilikuwa nimeunyima mwili wangu virutubishi vingi sana hivi kwamba ningaliendelea na mazoea yangu ya kula kwa miezi miwili, ningalikufa kutokana na utapiamlo,” asema Heather. Jarida The Harvard Mental Health Letter laripoti kwamba kwa pindi inayozidi miaka kumi, karibu asilimia 5 ya wanawake wanaobainishwa kuwa wanajinyima chakula hufa.
Hamu ya Chakula Isiyo ya Kawaida —Kula kwa Wingi na Kusafisha Tumbo
Tatizo la kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida hutambuliwa na kula kwa wingi (kula upesi kiasi kikubwa cha chakula, labda kalori 5,000 au zaidi) na kisha kusafisha tumbo (kuacha tumbo likiwa tupu, mara nyingi kwa kutapika au kwa kutumia dawa za kuharisha).b
Kwa kutofautishwa na kujinyima chakula, kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida hakutambuliwi kwa urahisi. Huenda mwenye tatizo hili asiwe mwembamba isivyo kawaida, na mazoea yake ya kula yaweza kuonekana kuwa ya kawaida—angalau kwa watu wengine. Lakini kwa mtu aliye na hamu ya chakula isiyo ya kawaida, kwa hakika maisha si ya kawaida. Kwa kweli, yeye huhangaikia chakula kupita kiasi hivi kwamba kila kitu kingine huwa hakina maana. “Kadiri nilivyokula kwa wingi na kutapika, ndivyo nilivyokosa kujali juu ya mambo mengine au watu wengine,” asema Melinda mwenye umri wa miaka 16. “Kwa kweli nilisahau kufurahia ushirika wa marafiki zangu.”
Geneen Roth, mwandishi na mwalimu katika uwanja wa kitaaluma wa matatizo ya kula, afafanua kula kwa wingi kuwa “kichaa cha dakika thelathini, kuingia kwenye eneo lisilokuwa na vizuizi.” Asema kwamba wakati wa kula kwa wingi, “hakuna kitu kinachokuwa cha maana—si marafiki, si familia . . . Hakuna kitu kinachokuwa cha maana ila chakula.” Lydia mwenye umri wa miaka 17 aliye na tatizo hili afafanua hali yake kwa kutumia mfano ulio wazi. “Ninahisi kuwa kama kifaa cha kuponda takataka,” asema. “Kula chakula kingi, kitafune, kitapike. Kwa kurudia jambo hilo hilo.”
Mtu mwenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida hujaribu sana kuzuia kuongeza uzito ambao kwa kawaida ungeletwa na kula kusikodhibitiwa. Kwa hiyo, mara tu baada ya kula kwa wingi, ama hujaribu kutapika ama kunywa dawa za kuharisha ili kuondoa chakula kabla hakijageuzwa kuwa mafuta ya mwili.c Ingawa wazo hilo laweza kuonekana kuwa lenye kuchukiza, mtu mwenye kula kwa wingi halioni hivyo. “Kadiri unavyokula kwa wingi na kusafisha tumbo, ndivyo iwavyo rahisi kwako,” aeleza mfanyakazi wa huduma za jamii Nancy Kolodny. “Hisi zako za mapema za kuchukizwa au hata hofu hubadilishwa mara moja na kichocheo cha kurudia mambo haya ya kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida.”
Kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida ni jambo lililo hatari sana. Kwa kielelezo, kurudia-rudia kusafisha tumbo kwa kutapika hufanya mdomo upatwe na asidi kali za tumbo, ambazo zinaweza kumomonyoa tabaka ya nje ya meno ya mtu mwenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida. Zoea hilo pia laweza kuharibu umio, ini, mapafu, na moyo wa mwenye tatizo hili. Katika visa vinavyopita kiasi, kutapika kwaweza kusababisha tumbo lipasuke na hata kifo. Dawa za kuharisha zinapotumiwa kupita kiasi zaweza kuwa hatari pia. Zaweza kuharibu matumbo na pia kusababisha kuharisha mfululizo na kuvuja damu kwa utumbo mpana. Kama vile kutapika mara kwa mara, matumizi mabaya ya dawa za kuharisha, katika visa vinavyopita kiasi, husababisha kifo.
Kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Akili, athari za matatizo ya kula zinaongezeka daima. Ni nini kinachomchochea mwanamke mmoja kijana achezee kifo kwa kujinyima chakula? Kwa nini mwingine anatamani sana chakula hivi kwamba anakula kwa wingi na kisha ahangaishwa sana na uzito wake hivi kwamba ashurutika kutapika alichokula? Maswali haya yatachunguzwa katika makala inayofuata.
[Maelezo ya Chini]
a Wataalamu fulani wanadai kwamba upungufu wa asilimia 20 hadi 25 wa uzito wa mtu kwa ujumla waweza kuchochea mabadiliko ya kemikali katika akili yanayoweza kubadili mtazamo wake, yakimfanya aone mafuta mahali hayapo.
b Kula kupita kiasi kusikodhibitiwa bila kusafisha tumbo pia huonwa na wengine kuwa tatizo la kula.
c Ili wasiongeze uzito, watu wengi wenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida hufanya mazoezi kwa bidii kila siku. Baadhi yao hufaulu sana katika kupunguza uzito hivi kwamba baada ya muda hujinyima chakula, na baada ya hapo hali yao yaweza kuwa ikibadilika kati ya kujinyima chakula na kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida.