Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 1/22 kur. 6-9
  • Ni Nini Husababisha Matatizo ya Kula?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ni Nini Husababisha Matatizo ya Kula?
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Utamaduni Unaotukuza Wembamba
  • Kula na Hisia-Moyo
  • Matatizo ya Kula—Ni Nini Kinachoweza Kusaidia?
    Amkeni!—1999
  • Chakula Kinapokuwa Adui Yako
    Amkeni!—1999
  • Kwa Nini Ninahangaikia Sana Uzito Wangu?
    Amkeni!—1999
  • Kujinyima Chakula na Kuwa na Hamu ya Chakula Isiyo ya Kawaida—Mambo Hakika, Hatari
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 1/22 kur. 6-9

Ni Nini Husababisha Matatizo ya Kula?

“Tatizo la kula haliibuki ghafula tu bila sababu. Ni dalili, ishara ya kwamba kuna tatizo fulani katika maisha ya mtu.”—Nancy Kolodny, mfanyakazi wa huduma za jamii.

MATATIZO ya kula si mapya. Kujinyima chakula ni tatizo lililogunduliwa rasmi katika mwaka wa 1873, na dalili zake zimejulikana kwa miaka 300 iliyopita. Hata hivyo, tangu Vita ya Ulimwengu ya Pili, idadi ya watu wenye tatizo la kujinyima chakula imeongezeka kwa njia yenye kutazamisha. Hali hiyo inafanana na ile ya kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida. Tatizo hili limejulikana kwa karne kadhaa, lakini katika miongo ya karibuni, kama kitabu kimoja kuhusu habari hii kisemavyo, “limeongezeka kwa njia yenye kutazamisha.”

Ni nini kisababishi cha matatizo ya kula? Je, yanarithiwa, au ni itikio lisilo la kawaida kwa utamaduni unaotukuza wembamba? Familia inatimiza fungu gani? Si rahisi kuyajibu maswali haya. Kama asemavyo mfanyakazi wa huduma za jamii Nancy Kolodny, kufasiri tatizo la kula “si jambo lililo la moja kwa moja kama vile kutambulisha hali fulani ya kitiba kama surua, au tetewanga, ambapo daktari hujua kisababishi hasa, namna unavyoweza kupatwa na ugonjwa huo, muda ambao ugonjwa huo utadumu, na matibabu yaliyo bora ni yapi.”

Hata hivyo, watafiti wanataja mambo kadhaa yanayoweza kuchangia ukuzi wa matatizo ya kula. Acheni tuchunguze machache kati yake.

Utamaduni Unaotukuza Wembamba

Katika nchi zenye utajiri, viwanda vya mitindo ya nguo huonyesha vigezo vya wanawake wembamba kwa watazamaji wachanga wenye kuvutiwa, wakichochea wazo la kwamba msichana huwa mrembo tu kwa kadiri alivyo mwembamba. Ujumbe huu uliopotoka huwashurutisha wanawake wengi wajitahidi kufikia uzito wa mwili usio na afya na usio halisi. Dakt. Christine Davies asema: “Mwanamke wa kawaida ana urefu wa futi tano na inchi tano na uzito wa kilogramu 66. Kigezo cha kawaida ni mwanamke mwenye urefu wa futi tano na inchi 11 na uzito wa kilogramu 50. Asilimia 99 kati yetu hatujafikia kiwango hicho na hatutakifikia kamwe.”

Licha ya uhakika huu, wanawake fulani wanapita kiasi ili kuwa na mwili wanaouona kuwa bora. Kwa kielelezo, katika uchunguzi wa mwaka wa 1997 uliofanyiwa wanawake 3,452, asilimia 24 ya wanawake walisema kwamba wangekuwa tayari kudhabihu miaka mitatu ya maisha yao ili kufikia mradi wao wa uzito. Kwa wale wanaotambuliwa kuwa tofauti, uchunguzi huo ulisema, “maisha yana thamani tu ikiwa wewe ni mwembamba.” Kwa kuwa asilimia 22 ya wale waliofanyiwa uchunguzi walisema kwamba vigezo wa kike walio katika magazeti ya mitindo waliathiri umbo la miili yao walipokuwa wachanga, ripoti hiyo ilimalizia kwa kusema kwamba: “Haiwezekani tena kukanusha uhakika wa kwamba sura za vigezo katika vyombo vya habari zinaathiri sana jinsi wanawake wanavyojiona.”

Bila shaka, wale wanaoelekea kunaswa zaidi na mawazo bandia ya vyombo vya habari ni wale ambao kwanza hawajistahi wenyewe. Kama asemavyo mfanyakazi wa huduma za jamii kuhusu utibabu, Ilene Fishman, “jambo la msingi ni kujistahi.” Imeonwa kwamba watu wanaokubali namna wanavyoonekana huwa nadra sana wahangaikie chakula kupita kiasi.

Kula na Hisia-Moyo

Wataalamu wengi wanasema kwamba kuna mengi yanayohusika katika tatizo la kula kuliko chakula. “Tatizo la kula ni onyo,” asema mfanyakazi wa huduma za jamii, Nancy Kolodny, “likuambialo kwamba unahitaji kukazia uangalifu hali fulani maishani mwako ambayo unapuuza au kuepuka. Tatizo la kula ni kikumbusha kwamba unakosa kuzungumza kuhusu mikazo na kukatishwa tamaa ambako huenda unakabili.”

Ni aina zipi za mikazo na kukatishwa tamaa? Kwa wengine yaweza kuhusisha taabu nyumbani. Kwa kielelezo, Geneen Roth akumbuka kwamba wakati wa utoto wake, chakula,—hasa peremende—zilikuwa “ulinzi dhidi ya ugomvi wa wazazi.” Asema hivi: “Nilipohisi kwamba wazazi wangu walikaribia kupigana, ningegeuza fikira zangu kwa urahisi kama vile ugeuzavyo idhaa ya televisheni, ziondoke kwenye udhibiti wa mama na baba hadi kwenye hali isiyokuwa na lolote ila mimi na utamu uliopo mdomoni mwangu.”

Nyakati nyingine tatizo la kula linasababishwa na kitu kikuu zaidi. Kwa kielelezo, The New Teenage Body Book chasema: “Uchunguzi unaonyesha kwamba wale walio na vurugu ya ngono (kutendwa vibaya au kusumbuliwa kingono) bila kufahamu wanaweza kujilinda wenyewe kwa kufanya miili yao isivutie kingono na kwa kuelekeza uangalifu wao kwa kitu kilicho salama kama vile chakula.” Bila shaka, watu hawapaswi kufikia mkataa wa kwamba mtu anayeteseka kutokana na tatizo la kula ametendwa vibaya kingono.

Tatizo la kula laweza kukua katika hali inayoonekana kuwa tulivu. Kwa kweli, mtu anayeweza hasa kujinyima chakula aweza kuwa msichana anayeishi katika mazingira ambayo hana uhuru wa kujifanyia maamuzi yoyote au kuonyesha hisia zake zisizofaa. Kwa nje, akubali; lakini kindani, ana msukosuko na ahisi kwamba hadhibiti maisha yake. Kwa kutothubutu kulalamika waziwazi, anaelekeza fikira kwenye sehemu moja ya maisha yake anayoweza kudhibiti—mwili wake.

Hata hivyo, inapasa kutambuliwa kuwa sikuzote matatizo ya kula hayawi tokeo la msukosuko wa familia au vurugu ya ngono. Kwa wengine, matatizo ya kula husitawi kwa sababu familia hukazia zaidi suala la uzito. Labda mzazi ni mnene kupita kiasi au anafuata miiko ya milo na kusababisha athari inayopita kiasi—au hata mtazamo—wenye hofu kuelekea chakula. Kwa wengine, mwanzo wa kubalehe wenyewe ni jambo linalochangia. Mabadiliko ya mwili ambayo ni sehemu ya maana katika kuwa mtu mzima yanaweza kumfanya msichana ahisi kuwa mnene—hasa ikiwa anakomaa upesi kuliko marika zake. Anaweza kuchukua hatua kali za kuondoa makunyanzi ya wanawake ikiwa aona badiliko hili kuwa lenye kuogofya.

Kwa kuongezea kutaja mambo ya kihisia-moyo, watafiti fulani wanasema kwamba huenda kukawa na jambo fulani la kimwili linalohusika. Kwa kielelezo, wanataja kwamba kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida ni tatizo linaloweza kuwa na chanzo kwenye utendaji wa akili ya mwenye tatizo hilo. Wanadai kwamba sehemu ya akili inayodhibiti hali ya moyo na hamu ya chakula inahusika na kwamba hili laweza kuonyesha sababu gani nyakati nyingine dawa za kupunguza hamu ya chakula huwa na matokeo katika kupunguza dalili za mtu mwenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida.

Kwa vyovyote vile, ni vigumu kwa watafiti kutaja kitu fulani hususa kinachosababisha kujinyima chakula au kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida. Lakini ni nini kinachoweza kufanywa kusaidia wale wanaong’ang’ana na matatizo haya ya kula?

[Picha katika ukurasa wa 7]

Mara nyingi watu wanaojinyima chakula wana maoni yaliyopotoka kuhusu sura yao

[Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Vyombo vya habari huendeleza wazo la kwamba kuwa mwembamba ni urembo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki