Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 5/22 kur. 10-13
  • ‘Watoto Ni Dhaifu’

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • ‘Watoto Ni Dhaifu’
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kanuni Bora Kabisa
  • Mambo Halisi ya Kisasa
  • Utatuzi Halisi
  • Kuwalea Watoto Wako Wampende Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1983
  • Zoeza Mtoto Wako Tangu Utoto Mchanga Sana
    Siri ya Furaha ya Familia
  • Kujenga Familia Yenye Nguvu Kiroho
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
  • Kulea Watoto Wenye Furaha Katika Ulimwengu Wenye Mchafuko Mwingi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1982
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 5/22 kur. 10-13

‘Watoto Ni Dhaifu’

‘Watoto ni dhaifu; nitakwenda polepole, kwa kipimo cha mwendo wa watoto.’ —Yakobo, baba mwenye watoto wengi, karne ya 18 K.W.K.

KUTENDWA vibaya kwa watoto si jambo jipya. Ustaarabu wa kale—kama Waazteki, Wakanaani, Wainka, na Wafoinike—una sifa mbaya ya kuwa na zoea la kudhabihu watoto. Uchimbuaji wa jiji la Carthage huko Foinike (sasa ni kitongoji cha Tunis, Afrika Kaskazini) ulifunua kwamba watoto wapatao 20,000 walitolewa dhabihu kwa mungu Baali na mungu-mke Tanit, kati ya karne ya tano na tatu K.W.K.! Idadi hii ni yenye kushtua zaidi ufikiriapo kwamba wakati wa kusitawi kwa Carthage idadi ya watu ilikadiriwa kuwa takriban 250,000 peke yake.

Hata hivyo, kulikuwako jamii moja ya kale iliyokuwa tofauti. Licha ya kwamba waliishi katikati ya majirani waliokuwa wakatili kwa watoto, taifa la Israeli lilionekana waziwazi kuwa tofauti katika kuwashughulikia watoto. Baba wa taifa hilo, mzee wa ukoo Yakobo, aliweka kielelezo. Kulingana na kitabu cha Biblia cha Mwanzo, alipokuwa akirejea kwa nchi ya nyumbani, Yakobo alipunguza mwendo wa msafara wote ili safari isiwe ngumu kwa watoto. ‘Watoto ni zaifu [dhaifu],’ yeye akasema. Wakati huo watoto wake walikuwa na umri wa kati ya miaka 5 na 14. (Mwanzo 33:13, 14, Zaire Swahili Bible) Uzao wake, Waisraeli, walionyesha staha iyo hiyo kwa mahitaji na adhama ya watoto.

Bila shaka, watoto katika nyakati za Biblia walikuwa na mengi ya kufanya. Vijana walipoendelea kukua, walizoezwa na baba zao kilimo au kazi fulani, kama vile useremala. (Mwanzo 37:2; 1 Samweli 16:11) Wasichana wakiwa nyumbani, walifundishwa na mama zao kazi za nyumbani ambazo zingewafaidi sana wanapokuwa watu wazima. Raheli, mke wa Yakobo, alikuwa mchungaji alipokuwa msichana mdogo. (Mwanzo 29:6-9) Wanawake vijana walifanya kazi kwenye mashamba wakati wa kuvuna nafaka na katika mashamba ya mizabibu. (Ruthu 2:5-9; Wimbo Ulio Bora 1:6)a Kazi hizo zilifanywa chini ya usimamizi wenye upendo wa wazazi na zilikuwa zenye kuelimisha.

Na wakati huohuo, watoto wachanga katika Israeli walipata shangwe ya pumziko na burudani. Nabii Zekaria alisema juu ya ‘njia za mji zikiwa zimejaa wavulana na wasichana, wakicheza.’ (Zekaria 8:5) Na Yesu Kristo alitaja watoto wachanga ambao wameketi katika mahali pa masoko wakipiga filimbi na kucheza dansi. (Mathayo 11:16, 17) Ni nini kilichochangia hali hii ya kuwatendea watoto kwa adhama?

Kanuni Bora Kabisa

Maadamu Waisraeli walitii sheria za Mungu, hawakuwatendea vibaya au kuwatumikisha kamwe watoto wao. (Linganisha Kumbukumbu la Torati 18:10 na Yeremia 7:31.) Waliwaona wana wao na binti zao kuwa “urithi wa BWANA,” “thawabu.” (Zaburi 127:3-5) Mzazi aliwaona watoto wake kama ‘miche ya mizeituni ikiizunguka meza yake’—na mizeituni ilikuwa yenye thamani sana katika jamii hiyo ya kilimo! (Zaburi 128:3-6) Mwanahistoria Alfred Edersheim asema kwamba mbali na maneno yaliyotumiwa kwa ajili ya mwana na binti, Kiebrania cha kale kilikuwa na maneno tisa kwa ajili ya watoto, kila neno likiwa linasimamia vipindi mbalimbali vya ukuzi. Yeye akata kauli hivi: “Kwa hakika, wale wote waliochunguza kwa makini ukuzi wa kitoto hata wakaipa kila hatua ya ukuzi huo jina fulani linalofafanua hatua hiyo, ni lazima wawe waliwapenda sana watoto wao.”

Katika enzi ya Ukristo, wazazi walionywa kwa upole wawatendee watoto wao kwa adhama na staha. Yesu aliweka kielelezo bora kabisa cha kushughulika na watoto wa watu wengine. Katika pindi moja kuelekea mwisho wa huduma yake ya kidunia, watu walianza kumletea watoto wao wachanga. Wanafunzi walijaribu kuwazuia watu wasimsumbue, kwa wazi wakiamini kwamba Yesu alikuwa mwenye shughuli sana. Lakini Yesu aliwakemea wanafunzi wake: “Waacheni watoto wachanga waje kwangu; msijaribu kuwakomesha.” Yesu hata ‘aliwachukua watoto akawakumbatia.’ Hapana shaka yoyote kwamba aliwaona watoto kuwa wenye thamani na wanaostahili kutendewa kwa fadhili.—Marko 10:14, 16; Luka 18:15-17.

Baadaye, mtume Paulo aliwaambia akina baba: “Msiwe mkiwachochea watoto wenu wakasirike, ili wasishuke moyo.” (Wakolosai 3:21) Kwa kupatana na amri hii, wazazi Wakristo wa nyakati za kale na wa leo, hawangeweza kamwe kuwaruhusu watoto wao waathiriwe na hali mbaya za kazi. Wao wanatambua kwamba ili watoto wasitawi kimwili, kihisia-moyo, na kiroho, ni lazima wawe katika mazingira yenye upendo, utunzaji, na yaliyo salama. Ni lazima wazazi wadhihirishe upendo halisi. Hili lingetia ndani kuwalinda watoto wao kutokana na hali za kazi zenye kudhuru.

Mambo Halisi ya Kisasa

Bila shaka, tunaishi katika “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.” (2 Timotheo 3:1-5) Kwa sababu ya hali mbaya za kiuchumi katika nchi nyingi, huenda hata familia za Kikristo zikalazimika kuwaruhusu watoto wao wafanye kazi. Kama ilivyoonyeshwa tayari, hakuna ubaya wowote kwa watoto kufanya kazi nzuri na yenye kuelimisha. Kazi ya aina hiyo inaweza kuboresha ukuzi wa mtoto kimwili, kiakili, kiroho, kiadili, au kijamii bila kuhitilafiana na elimu inayohitajika, tafrija yenye usawaziko, na pumziko linalohitajiwa.

Bila shaka, wazazi Wakristo wanataka watoto wao wafanye kazi chini ya usimamizi wao wenye kujali, wala si kuwa watumwa wa waajiri wakatili, wasiojali, na wenye ufidhuli. Wazazi hawa watahakikisha kwamba kazi wanayofanya watoto wao haina hatari ya kutendwa vibaya kimwili, kingono, au kihisia-moyo. Watataka pia, watoto wao wawe karibu. Katika njia hii wanaweza kutimiza wajibu wao wa Kibiblia wa kuwa waelimishaji wa kiroho: “Nawe uwafundishe [maneno ya Mungu] watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.”— Kumbukumbu la Torati 6:6, 7.

Isitoshe, Mkristo anahimizwa kuonyesha hisia-mwenzi, kuwa na shauku, na kuwa mwenye huruma kwa njia ya wororo. (1 Petro 3:8) Anatiwa moyo ‘kufanya lililo jema kuelekea wote.’ (Wagalatia 6:10) Ikiwa unapaswa kuonyesha watu kwa ujumla sifa hizi za kimungu, si zaidi sana watoto wako! Kwa kutii ile Kanuni Bora—“mambo yote mtakayo watu wawafanyie nyinyi, lazima mwafanyie wao pia hivyohivyo”—Wakristo hawangeweza kamwe kujiruhusu wawatendee vibaya watoto wa wengine, wawe ni wa Wakristo wenzao au la. (Mathayo 7:12) Kwa kuongezea, kwa kuwa Wakristo ni raia wanaotii sheria, watakuwa waangalifu kutovunja sheria za serikali zinazohusu kiwango cha umri wa watu wanaowafanyia kazi.—Waroma 13:1.

Utatuzi Halisi

Namna gani wakati ujao? Kuna wakati ujao bora kwa watoto na watu wazima pia. Wakristo wa kweli wana uhakika kwamba utatuzi wa kudumu kwa tatizo la kuwaajiri watoto ni serikali inayokuja ya ulimwengu inayoitwa na Biblia “ufalme wa mbingu.” (Mathayo 3:2) Watu wenye kumhofu Mungu wamesali juu yake kwa karne nyingi wanaposema: “Baba yetu uliye katika mbingu, jina lako na litakaswe. Acha ufalme wako uje. Mapenzi yako na yatendeke, kama ilivyo katika mbingu, pia juu ya dunia.”—Mathayo 6:9, 10.

Miongoni mwa mambo mengine, Ufalme huu utaondoa hali zinazosababisha kuajiriwa kwa watoto. Utaondoa kabisa umaskini. ‘Nchi itatoa mazao yake; MUNGU, Mungu wetu, atatubariki.’ (Zaburi 67:6) Ufalme wa Mungu utahakikisha kwamba kila mtu atapokea elimu inayofaa inayotegemea sifa za kimungu. ‘Hukumu za [Mungu] zikiwapo duniani, watu wakaao duniani watajifunza haki.’—Isaya 26:9.

Serikali ya Mungu itaondoa kabisa mifumo ya kiuchumi inayoendeleza tofauti za kitabaka. Ubaguzi wa kimbari, kijamii, umri, au wa kijinsia hautakuwapo tena, kwa kuwa sheria kuu ya serikali hiyo itakuwa sheria ya upendo, inayotia ndani amri hii: “Lazima umpende jirani yako kama wewe mwenyewe.” (Mathayo 22:39) Chini ya serikali hiyo ya ulimwengu yenye haki, tatizo la kuajiriwa kwa watoto litakomeshwa kabisa!

[Maelezo ya Chini]

a Jambo hili halikuwashusha wanawake kuwa washiriki wa familia wa tabaka la pili waliostahili kufanya kazi nyumbani au mashambani tu. Ufafanuzi wa “mke mwema” katika Mithali hufunua kwamba mwanamke aliyeolewa licha ya kusimamia nyumba yake angeweza pia kuendesha biashara zilizohusu mali isiyohamishika, angetafuta shamba lenye kuzalisha, na kuendesha biashara ndogo.— Mithali 31:10, 16, 18, 24.

[Sanduku katika ukurasa wa 12]

Msimamizi wa Danguro Awaruhusu Wasichana Wake Waende

KWA miaka 15, Ceciliab alimiliki na kufanya kazi kwenye madanguro katika mojawapo ya visiwa vya Karibea. Alinunua wasichana 12 hadi 15 kwa wakati mmoja, wengi wao wakiwa na umri wa chini ya miaka 18. Wasichana hawa walitumikishwa dhidi ya mapenzi yao kwa ajili ya madeni ya familia zao. Cecilia alilipa madeni hayo na kisha akawachukua wasichana hao ili wamtumikie. Kutoka kwa fedha walizochuma, aliwanunulia chakula na kulipia gharama nyinginezo huku akiweka akiba ya kiasi fulani kwa ajili ya fedha alizokuwa amelipia kuwapata. Waliwekwa huru baada ya miaka mingi sana. Wasichana hawa hawakuruhusiwa kamwe kutoka nyumbani isipokuwa wawe wanaandamana na mlinzi.

Cecilia akumbuka vema kisa kimoja mahususi. Mama ya msichana mmoja kahaba alikuja kila juma kupokea vifurushi vya chakula —chakula alichopewa kwa sababu ya “kazi” ya bintiye. Binti huyo alikuwa anamlea mwana. Hangeweza kulipa madeni aliyokuwa nayo na kwa hiyo hakuwa na tumaini la kuwekwa huru. Siku moja alijiua, akaacha barua iliyosema kwamba msimamizi wa danguro amtunze mwana wake. Cecilia alimlea mwana huyu pamoja na watoto wake wanne.

Mmoja wa binti za Cecilia akaanza kujifunza Biblia pamoja na wamishonari walio Mashahidi wa Yehova. Cecilia alitiwa moyo ashiriki katika funzo, lakini mwanzoni alikataa kwa sababu hakuwahi kujifunza kusoma au kuandika. Ingawa hivyo, hatua kwa hatua, kwa kusikiliza mazungumzo ya Biblia, akapata kufahamu upendo wa Mungu na subira yake na kuthamini sana msamaha wake. (Isaya 43:25) Akiwa na hamu ya kujifunza Biblia mwenyewe, baada ya muda akaanza kujifunza kusoma na kuandika. Ujuzi wake wa Biblia ulipoongezeka, aliona umuhimu wa kujipatanisha na viwango vya Mungu vya adili vilivyo juu sana.

Siku moja, wasichana hao walishangaa sana, alipowaambia kwamba walikuwa huru kwenda! Alieleza kuwa waliyokuwa wakifanya yalimchukiza sana Yehova. Hakuna hata mmoja wao aliyelipa fedha alizowadai kamwe. Hata hivyo, wawili kati yao wakaja kuishi naye. Hatimaye mwingine akawa Shahidi aliyebatizwa. Cecilia amekuwa mwalimu wa Biblia wa wakati wote kwa miaka 11 sasa, huku akiwasaidia watu wengine kuacha mazoea yenye kumvunjia Mungu heshima.

[Maelezo ya Chini]

b Si jina lake halisi.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki