Kuutazama Ulimwengu
Kuvuta Sigareti Hugharimu Mabilioni
Ingawa idadi ya wavutaji wa sigareti katika nchi nyingi inapungua, katika Uswisi imebaki hivyo hivyo, lasema gazeti la habari la Berner Oberländer. Takriban thuluthi moja ya watu wa huko huvuta sigareti. Vifo zaidi ya 8,000 kila mwaka vinahusiana na uvutaji wa sigareti—ni vifo vingi zaidi ya vile vinavyosababishwa na UKIMWI, heroini, kokeini, vileo, mioto, aksidenti za magari, uuaji, na kujiua vinapojumlishwa pamoja. Uchunguzi uliotolewa na Idara ya Serikali ya Afya ya Umma katika Uswisi ulikata kauli kwamba gharama ya matumizi ya tumbaku kwa jamii mwaka wa 1995 ilikuwa faranga bilioni kumi za Uswisi, zaidi ya dola bilioni sita za Marekani. Uchunguzi huo ulijaribu kupima gharama za kitiba na za kutunzwa hospitalini, kupungua kwa uzalishaji kazini, kupungua kwa ubora wa maisha ya wavutaji wa sigareti wagonjwa na watu wanaowategemea, na kuteseka kwa washiriki wa familia waliofiwa.
Linda Moyo Wako
“Sikuzote tumejua kwamba halihewa yenye joto huongeza hatari za kupatwa na mshiko wa moyo—lakini sasa tunajua kwamba halihewa yenye baridi huongeza hatari hizo pia,” asema Dakt. Anthony Graham, mtaalamu wa maradhi ya moyo na msemaji wa shirika la Heart and Stroke Foundation of Ontario, Kanada. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti la habari The Globe and Mail, uchunguzi wa miaka kumi uliofanyiwa wanaume 250,000 katika Ufaransa waonyesha kwamba kuongezeka kwa joto au baridi kwa nyuzi kumi za Selsiasi katika wastani wa halijoto “huongeza hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo kwa kiwango cha asilimia 13.” Halijoto inapopungua, moyo hufanya kazi kwa nguvu zaidi na kwa uharaka zaidi kwa sababu damu inaelekezwa mbali kutoka kwa ngozi hadi kwenye maeneo ya ndani ya mwili ili kuhifadhi joto. Hatari hiyo huongezeka watu wanapojikaza sana au wanapokosa kuvalia ifaavyo. Dakt. Graham atoa tahadhari hii: “Huwezi kuwa ukijikalia tu ukitazama televisheni kwa miezi mitano kisha kwa ghafula uanze kuondoa theluji kunapokuwa na baridi. Unapaswa kufanya badiliko hilo hatua kwa hatua.”
Muziki Wenye Sauti Kubwa Ukiwa Njia ya Kukwepa Kusumbuliwa
Licha ya maonyo ya madaktari kwamba muziki wenye sauti kubwa kupita kiasi “unadhuru mwili wote,” idadi inayoongezeka ya vijana wanashindwa kuacha stirio zao, laripoti gazeti la kila juma la Poland Przyjaciółka. Kwa nini? Wengine hutumia stirio zao ili “kujiondoa kutoka kwenye mambo yanayowazunguka. Akiwa na vipokea-sauti vinavyobanwa kichwani, kijana hahitaji tena kusikiliza wazazi wake wanapomsumbua au kuitikia, mathalani, wanapomwomba afanye jambo fulani,” lasema gazeti hilo. Likisema kwamba muziki wenye sauti kubwa kupita kiasi waweza pia kusababisha “uchovu, kuumwa kichwa, kutoweza kumakinika, au kukosa usingizi,” gazeti la Przyjaciółka haliwashauri wazazi wawakataze watoto wao kutumia stirio bali linapendekeza kwamba wazazi wawafundishe watoto wao kuwa na kiasi. “Azima Walkman kutoka kwa watoto wako pindi kwa pindi,” ladokeza gazeti hilo. “Watapata pumziko kutokana na vyombo vya kusikilizia, na utapata kujua aina yao ya maisha.”
Kutoweka Kabisa kwa Lugha
“Nyakati nyingine ningejikasirikia kwa kutowafunza watoto wangu lugha hiyo,” asema Mkuu Marie Smith Jones, aliyekuwa mtu wa mwisho wa utamaduni wao kuzungumza lugha ya Eyak, ya Alaska. Mielekeo inaonyesha kwamba kati ya lugha zinazokadiriwa kuwa 6,000 zinazozungumzwa ulimwenguni pote, huenda kati ya asilimia 40 na 50 zikatoweka kabisa katika karne ijayo. Australia ambayo wakati mmoja ilikuwa na lugha 250, tayari zimepungua kufikia 20 hivi. Kwa nini jambo hili linatukia? Gazeti la Newsweek ladokeza kwamba lugha zinazidi “kusahauliwa kabisa kwa sababu ya kuenea kwa Kiingereza na lugha nyinginezo ‘kubwakubwa.’” Profesa Stephen Wurm, mhariri wa Atlas of the World’s Languages in Danger of Disappearing, kinachochapishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni, aongezea hivi: “Mara nyingi kuna lile wazo kwamba unapaswa kusahau lugha ‘ndogondogo,’ lugha za makabila madogo-madogo, kwa sababu hazina thamani.”
Mzungumzie Mtoto Wako
Kuzungumzia watoto angalau kwa dakika 30 kila siku kwaweza kuongeza kwa kiwango kikubwa akili yao na stadi zao za lugha, laripoti Daily Telegraph la London. Watafiti waliwachunguza watoto 140 wenye umri wa miezi tisa. Wazazi wa nusu ya kikundi hicho walishauriwa juu ya njia bora ya kuzungumzia watoto wao, huku nusu ile nyingine hawakupewa madokezo ya kufanya hivyo. Baada ya miaka saba “wastani wa akili ya kikundi cha watoto [waliozungumziwa] ulikuwa mwaka mmoja na miezi mitatu mbele ya kikundi kile kingine,” na stadi zao za lugha zilionekana “kuwa za juu zaidi,” yasema ripoti hiyo. Mtafiti Dakt. Sally Ward aamini kwamba leo wazazi hawazungumzi sana na watoto wao kama zamani kwa sababu ya mabadiliko makubwa katika jamii. Mathalani, mama wengi zaidi huenda kazini, na kanda za vidio zimechukua mahali pa mazungumzo katika nyumba nyingi.
Kuepuka Hasira za Barabarani
“Madereva ambao ni wachokozi kupita kiasi hawapasi kuchukuliwa kivivihivi,” ashauri mshindani wa mbio za magari mwenye uzoefu aliyenukuliwa katika gazeti Fleet Maintenance & Safety Report. Kubaki ukiwa mtulivu na kuepuka hali zisizofaa kwaweza kusaidia kupunguza hatari za hasira za barabarani. Watetezi wa usalama wanatoa mapendekezo yafuatayo:
◼ Endesha gari kwa heshima nyakati zote.
◼ Mwondokee mwendesha-gari mchokozi ikiwa unaweza kufanya hivyo kwa njia salama.
◼ Usishindane kamwe na dereva mwingine kwa kumfuata kwa ukaribu sana au kwa kuendesha kwa kasi sana.
◼ Usitoe vitisho unapotishwa, na epuka kuonyesha ishara zinazoweza kueleweka vibaya.
◼ Usimtazame dereva mwenye hasira kwenye macho.
◼ Usisimamishe gari lako kando ili kukabiliana na dereva mwingine.
Majeraha ya Utoaji-Mimba na Kifo
Kunakuwa na visa vya utoaji-mimba karibu 500,000 katika Mexico kila mwaka, asema Francisco Javier Serna Alvarado, msimamizi wa Tume ya Afya na Huduma za Jamii katika Mexico City. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti la habari la El Universal, asilimia kubwa ya visa hivi hutokeza vifo kwa akina mama, na visa vingine vingi hutokeza matatizo mabaya sana yanayohitaji tiba na hata kulazwa hospitalini. Utoaji-mimba unaofanywa kwa siri ndicho kisababishi kikuu cha tatu cha vifo vya akina mama katika Mexico. Katika visa fulani, mbinu zisizofaa za utoaji-mimba hufanywa bila ujuzi—kutumia vitu vyenye ncha kali, kutumia dawa za kutoa mimba au miti-shamba, hata kujirusha kwenye ngazi. Mara nyingi matokeo hutia ndani “kuvuja damu kubaya sana, kutoboka kwa mji wa mimba, utasa, maambukizo, na kupoteza tumbo la uzazi,” yasema ripoti hiyo.
Sema Waziwazi
Hata ujumbe wako uwe wa maana kadiri gani, watu walio wengi hawatataka kukusikiliza ikiwa hawapendezwi na jinsi unavyozungumza, asema mtaalamu wa sauti Dakt. Lillian Glass. Kama ilivyoripotiwa na gazeti la habari la The Citizen la Afrika Kusini, kusema kwa sauti ya chini, sarufi isiyofaa, sauti ya namna moja yenye kuchosha, kuzungumza haraka sana, matusi, na kutawala mazungumzo yote huwavunja moyo wasikilizaji. Kwa upande mwingine, kwa kawaida watu watasikiliza ukitabasamu ili kuwastarehesha, ukizungumza waziwazi na polepole, ukiwatazama kwenye macho, na kusikiliza kwa makini maoni yao bila kumkatisha. “Fikiri kabla ya kusema,” yaongezea makala hiyo, “na utajieleza ukiwa na uhakika zaidi.”
Kula Kupita Kiasi Huongeza Hatari ya Kula Chakula Kibaya
Hatari za kuwa mgonjwa kutokana na kula chakula kibaya huongezeka mtu anapokula kupita kiasi, kulingana na Dakt. Adolfo Chávez, wa Taasisi ya Kitaifa ya Lishe ya Salvador Zubirán nchini Mexico. Anasema kwamba bakteria chache kwenye chakula tunachokula kwa kawaida huharibiwa na asidi katika matumbo yetu. Lakini baada ya kula kupindukia, chakula cha ziada huzidi uwezo wa asidi za tumbo, kukipunguza uwezo wa tumbo kuua bakteria. Dakt. Chávez aliliambia Amkeni! hivi: “Mtu akila chapati ngumu 15 na moja iwe imeharibika, huenda mtu huyo akawa mgonjwa kwa sababu ya kiasi alichokula. Mtu huyo akila chapati ngumu moja tu iliyoharibika, huenda kusiwe na tatizo lolote.”
Ukosefu wa Kicheko
Kulingana na uthibitisho uliotolewa hivi karibuni kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Kujadili Kicheko, uliofanywa nchini Uswisi, wakati wa miaka ya 1950 iliyokuwa na magumu ya kiuchumi, mtu wa kawaida alicheka kwa dakika 18 kwa siku moja, ikilinganishwa na dakika 6 kwa siku katika miaka ya 1990 yenye utajiri. Kwa nini kuna upungufu huo? “Wataalamu wanalaumu jitihada ya daima ya kutafuta mafanikio ya vitu vya kimwili na mafanikio ya kibinafsi kuwa yametokeza mwelekeo huo, wakiunga mkono ukweli wa msemo wa kale kwamba pesa haiwezi kununua furaha,” laeleza gazeti la habari la London Sunday Times. Hivyo, mwandishi Michael Argyle amalizia hivi: “Wale wanaothamini pesa zaidi ndio wasioridhika zaidi na ndio walio na matatizo ya akili zaidi. Huenda sababu ikawa kwamba pesa huandaa aina ya uradhi wa kijuujuu tu.”
Haki ya Kupokea Matibabu Yahifadhiwa
Hivi majuzi Mahakama Kuu Zaidi ya El Salvador iliharamisha sheria ya Hospitali ya Umma iliyowataka wagonjwa watoe damu ili wapate kutibiwa. Hapo awali, sera ya hospitali iliwataka wagonjwa wote watoe painti mbili za damu kabla ya kufanyiwa upasuaji. Sasa, wale wanaotaka kutibiwa katika Hospitali ya Umma wana haki ya kisheria ya kuchagua kutotoa damu.