Kahawa, Chai, Au Guarana?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI
“UNGEPENDA kunywa nini?” auliza mkaribishaji mwenye haiba. “Kahawa, chai, au guarana?” Mara nyingi swali hilo huzushwa kwenye vikusanyiko vya kijamii huko Brazili. Lakini wageni kutoka ugenini wanatatanishwa na swali hilo. Hivyo kwa kuitikia, mkaribishaji awaonyesha wageni wake chupa yenye kibandiko kinachoonyesha matunda matatu mekundu yanayofanana na buni. Wageni hao wanatulia wanapong’amua kwamba guarana si namna fulani ya mnyama wa nchi kavu wa kigeni, badala yake, ni refrigerante, au kinywaji baridi.
Huenda ikawa wewe pia hujasikia kuhusu guarana. Ingawa kahawa na chai hupendwa sana ulimwenguni pote, guarana hupendwa hasa katika Brazili. Hata hivyo, vinywaji vyote vitatu vinafanana katika jambo moja: Vina kafeini. Kwa kweli, kikombe cha guarana chaweza kuwa na kafeini mara tatu zaidi kuliko kikombe cha kahawa! Kwa kuchochewa na udadisi, wageni wanaamua kunywa guarana. Wanapokunywa kinywaji hicho chenye kuburudisha na kufurahia ladha yake kali ya matunda, wanapendezwa kusikia hadithi ya guarana.
Wanapata habari kwamba guarana ni mmea wenye nyuzinyuzi, unaotambaa, ambao kwa asili hupatikana katika bonde la Amazon. Hukua kwa njia ya asili karibu na miji ya Maués na Parintins na katika sehemu nyingine za mkoa wa Amazonas. Hata hivyo, guarana hukuzwa pia katika mikoa mingine ya Brazili, kama vile Pará, Goiás, na Mato Grosso.
Mmea huu waweza kutambaa hadi kufikia urefu wa meta kumi. Matawi yake ya rangi iliyokoza yana majani yenye umbo la yai yakiwa na ncha zilizochongoka na vichala vya maua yenye vitawi vifupi. Mmea huo huzaa matunda katika mwaka wake wa tatu, mwezi wa Januari au Februari. Mmea wa miaka mitano unaweza kuzaa takriban kilogramu tatu za matunda.
Tunda la guarana, lenye ukubwa unaokaribia wa zabibu, lina mbegu moja au mbili zilizo laini, zenye umbo la yai. Tunda hilo ni la rangi nyekundu nyangavu kwenye sehemu ya juu na sehemu ya chini ni ya rangi ya manjano. Nyama ya tunda la guarana inapotayarishwa, matunda hayo hulowekwa. Hivyo kutenganisha sehemu inayofunika mbegu yenye nyama na mbegu zenyewe. Kisha mbegu hizo huoshwa, hukaushwa, hubanikwa, na kusagwa kuwa unga. Baadaye, unga huo, ambao una kafeini, huchanganywa na maji na labda na kakao na mhogo.
Muda mrefu kabla wakoloni waliotawala Brazili hawajatambua guarana, tayari Wahindi walikuwa wamejua ubora wa tunda hili. Ili kutokeza kinywaji bora, Wahindi walikuwa waangalifu kuteua matunda yaliyokomaa peke yake, pasipo kuchanganya matunda mabivu na mabichi au yaliyochacha. Kisha mbegu hizo zilipondwa na kuchanganywa na maji ili kufanyiza kinyunya. Kinyunya kiliundwa katika umbo la vijiti vyenye urefu wa sentimeta 15 hivi na kipenyo cha sentimeta 2.5. Vijiti hivyo vilikaushwa vikawa vigumu kama mawe—njia ya kale ya kuhifadhi chakula katika maeneo yenye tabia ya nchi iliyo na joto na unyevunyevu. Baadaye vijiti vya guarana vilivyokaushwa vilikunwa kwenye mfupa wa kaakaa ya samaki mkubwa aliyeitwa pirarucu. Kisha unga huo uliongezwa maji au maji ya matunda.
Wahindi wa Brazili walithamini sana kinywaji hicho kwa ajili ya uwezo wake wa kutibu magonjwa. Kwa kawaida waganga waliagiza wagonjwa watumie kinywaji cha guarana katika njia mbalimbali. Kwa kazi iliyochukua muda mrefu na iliyo ngumu, Wahindi walitumia guarana kama ponyo la uchovu.
Karibu mwaka wa 1816, tunda la guarana lilipelekwa Ufaransa. Baadaye, katika mwaka wa 1826, mwanabotania Mjerumani Karl von Martius alimhimiza nduguye, Theodore, afanyie tunda hilo uchunguzi wa kemikali wa kwanza. Hata hivyo, tunda la guarana halikutumiwa sana Ulaya kwa sababu wanatiba wa huko walihisi kwamba bidhaa za bei ya chini zingeweza kutumiwa badala yake.
Hata hivyo, huko Brazili, idadi kubwa ya watu waliona guarana kuwa tiba ya kila kitu. Mnamo mwaka wa 1905, Luís Pereira Barreto, daktari Mbrazili, alimpongeza mtu wa kwanza kuonja guarana na kutambua manufaa yake kuwa mmojawapo wa wafadhili wakuu zaidi wa binadamu.
Watetezi wa kinywaji cha guarana, bado hukiona kuwa kinywaji cha thamani sana. Wengine hudai kwamba si kinywaji cha kutia nguvu tu, bali pia ni kitulizo cha moyo na dawa yenye matokeo ya kupambana na mrundamano wa vitu vyenye mafuta-mafuta katika ateri. Pia imedaiwa kwamba guarana husaidia kutibu kuhara, ugonjwa wa kuhara damu, na kipandauso vilevile uvimbe wa neva, au maumivu ya neva. Kama madai haya ni yenye kusadikisha baada ya utafiti wa kitiba kufanywa, ni jambo litakalojulikana baadaye. Kwa vyovyote, tangu mwaka wa 1929, guarana kimekuwa kinywaji baridi kinachopendwa sana katika Brazili.
Wageni wamejifunza mambo mengi kupitia mazungumzo haya. “Je, mngependa kunywa guarana zaidi?” auliza mkaribishaji. Kwa pamoja, watoa ishara ya kichwa na kusema ndiyo. Vipi wewe? Je, ungependa guarana pia?
[Picha katika ukurasa wa 23]
“Guarana”—kabla haijafanywa kuwa kinywaji