Hangaiko juu ya Damu Iliyoambukizwa
DEMETRIO Pessoa, mwanabiokemia wa Bolivia alipoambukizwa ugonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji, alipelekwa haraka kwenye kliniki. Huko alitiwa damu mishipani na hali yake ikawa nafuu. Hata hivyo, punde si punde, kwa ghafula mwanabiokemia huyo akashikwa na homa. Baada ya kumchunguza, madaktari wakampa habari yenye kusikitisha: Bw. Pessoa alitiwa damu iliyoambukizwa kimelea cha Trypanosoma cruzi. Kama tokeo, alipata maradhi ya Chagas.
Kisa kama hicho cha Bw. Pessoa ni cha kawaida katika Bolivia, lasema shirika la habari la Panos lililoko London. Uchunguzi wa muda mrefu uliofanywa katika nchi 12 za Amerika ya Latini unaonyesha kwamba katika nchi hizo, maradhi yanayosababishwa na damu iliyoambukizwa ni mambo ya kawaida. Katika nchi moja ya Amerika ya Latini, kwa kila wagonjwa 10,000 waliotiwa damu mishipani, 220 walishikwa na maradhi ya kuambukizwa. Hilo lamaanisha kwamba mtu 1 kati ya kila 45 waliotiwa damu mishipani aliambukizwa maradhi!
Ingawa hivyo, maradhi ya Chagas si tisho peke yake. Uchunguzi huohuo unaonyesha kwamba nchi kadhaa za Amerika ya Latini hazikupima damu kwa ajili ya mchochota wa ini aina ya C na kwamba katika nchi fulani upimaji damu kwa ajili ya kaswende haukufanywa kwa kawaida. Kwa kuongezea, nchi kadhaa hazikuwa na mashine za kutosha kupima damu kwa ajili ya virusi vya HIV. Alipokuwa akizungumza juu ya damu iliyoambukizwa, Tonchi Marinkovic, waziri wa afya wa Bolivia, alisema hivi: “Mungu tuokoe kutoka kwa hali ya hatari, kwa kuwa huenda tukawa na tatizo la kitiba la kaswende, mchochota wa ini, maradhi ya Chagas au UKIMWI.”
Pasipo kujua, ofisa huyu wa serikali alikuwa akionyesha njia inayofaa ya kukomesha tatizo hilo la kitiba lenye kutisha. Miaka kadhaa iliyopita jarida Notícias Bolivianas lilisema hivi katika makala juu ya hatari za kutiwa damu mishipani: “Kujiepusha na damu kunapendekezwa kupatana na amri ya Biblia.” Amri hiyo ya Biblia ambayo jarida hilo linarejezea iko katika Matendo 15:29. Inasema: ‘Endeleeni kujiepusha na vitu vilivyotolewa dhabihu kwa sanamu na damu na kutokana na vitu vilivyonyongwa na uasherati. Mkijitunza wenyewe kwa uangalifu kutokana na mambo haya, mtafanikiwa.’—Ona pia Mwanzo 9:4; Mambo ya Walawi 3:17.