“Si Kila Mtu Anayenufaika na Ufanisi”
RIPOTI ya kila mwaka iitwayo Human Development Report 1998, inayotungwa na shirika la UM la Maendeleo, au UNDP, ilikazia utumiaji usio na kifani wa mambo ya kiuchumi. Ripoti hiyo ilionyesha kwamba tufeni pote, sasa twatumia vitu vya kiuchumi mara sita zaidi ya tulivyotumia mwaka wa 1950 na mara mbili zaidi ya tulivyotumia mwaka wa 1975. Ujapokuwa utumiaji huu wa kiuchumi, mkurugenzi mkuu wa UNDP, James Gustave Speth, asema hivi: “Si kila mtu anayenufaika na ufanisi.”
Kwa mfano: Asilimia 20 ya watu ulimwenguni walio matajiri zaidi hula samaki mara saba kuliko asilimia 20 ya watu ulimwenguni ambao ndio maskini zaidi. Hiyo asilimia 20 ya walio matajiri zaidi pia hula nyama mara 11 zaidi, hutumia umeme mara 17 zaidi, wana simu mara 49 zaidi, hutumia karatasi mara 77 zaidi, na huwa na magari mara 149 kuliko asilimia 20 walio maskini zaidi ulimwenguni.
Ikieleza juu ya uchunguzi huu, Redio ya UM ilitaarifu kwamba ili kupunguza mwendo wa kumalizwa kwa mali za dunia, mfumo wa uchumi wa viwanda wapaswa kubadili matumizi yake. Wakati uleule, nchi zenye utajiri mwingi zahitaji kushiriki baadhi ya mali zake na maskini wa ulimwengu ili wao pia waweze kunufaika na mali za dunia. Ni kiasi gani cha mali kitakachohitajiwa?
Bw. Speth afikiria kwamba kama nchi zenye viwanda zingeongeza maradufu kiwango chao cha sasa cha msaada wa maendeleo—kuanzia dola bilioni 50 hadi dola bilioni 100 kwa mwaka—maskini wote ulimwenguni wangeweza kufurahia chakula, afya, elimu, na makao. Dola bilioni 50 huenda zikaonekana kuwa fedha nyingi mno. Lakini, Bw. Speth akumbusha hivi: “Ndicho kiwango ambacho Ulaya hutumia kila mwaka kwenye sigareti, na ni nusu ya kile ambacho Marekani hutumia leo kwenye vinywaji vya vileo.”
Basi, ni wazi kwamba jitihada ya pamoja ili kushiriki mali za tufe hili kwa njia sawa kabisa zingesaidia sana kukomesha umaskini wenye kuumiza. Ni nini kinachohitajiwa ili kuwezesha jambo hilo? Mfanyakazi mmoja wa UM alisema: “Jambo linalohitajiwa hatimaye ni mgeuzo wa mioyo, akili na nia.” Watu walio wengi hukubali lakini pia wanatambua kwamba mbali na kuondoa sifa kama vile pupa, mashirika ya siku hizi ya kutunga sera hayawezi kufanya migeuzo hiyo, hata yawe na nia njema kadiri gani.
Hata hivyo, kuna tumaini kwa watu wenye kuhangaishwa na wakati ujao wa jamii ya kibinadamu na tufe letu. Inatia moyo kujua kwamba Muumba wa dunia ameahidi kutatua matatizo ya mwanadamu kwa njia yenye matokeo. Mtunga-zaburi alitabiri hivi: ‘Nchi imetoa mazao yake; MUNGU, Mungu wetu ametubariki. Na uwepo wingi wa nafaka katika ardhi juu ya milima.’ (Zaburi 67:6;72:16) Naam, ndipo kila mkazi wa dunia ‘atakaponufaika na ufanisi’!