Kutumia Ngazi—Je, Wewe Hufanya Ukaguzi Huu wa Usalama?
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Ireland
PAUL alihitaji kubadili balbu katika taa ya nje ya nyumba yake. Alihitaji pia kusafisha upande wa nje wa madirisha ya orofa—alikuwa amekumbushwa mara kadhaa na mke wake. Lakini Paul aliahirisha-ahirisha kazi hizi. Kwa nini? Kwa sababu ilimlazimu kutumia ngazi.
Alikuwa na sababu nzuri ya kuhofu. Alijua kwamba aksidenti zinazohusisha ngazi zaweza kusababisha majeraha mabaya na hata kifo. Mara nyingi hili hutukia kwa sababu mfanyakazi hajafikiria kwa uzito namna ya kutumia ngazi kwa njia inayofaa.
Paul alihitaji kuzingatia nini juu ya ngazi kabla ya kushughulikia kazi hizo? Hapa pana madokezo kumi ambayo yalimsaidia kufanya mambo kwa usalama.
Je, Ngazi Hiyo Ni Salama?
1 Tumia ngazi inayofaa. Huenda ukahitaji kujinyoosha sana ikiwa ngazi ni fupi sana. Huenda ukahitaji kuiweka katika pembe hatari ikiwa ni ndefu sana. Epuka kutumia ngazi ndogo unapopanda kwenye dari. Weka ngazi inayofaa kuelekea darini, au utumie ngazi ya kuegemezwa.
2 Kagua ngazi yako kwa uangalifu. Je, ilikuwa imewekwa nje? Ngazi za mbao hupanuka zinapolowa na kukunjamana zinapokauka. Baada ya muda, vidato vyake vyaweza kulegea, na kuifanya ngazi iwe legelege. Je, kuna kidato cho chote kilichovunjika, au je, vina dalili za kuoza? Kwa kawaida, chini ya kila kidato cha mbao huwa na ufito wa chuma wa kukitegemeza. Je, fito hizi zipo zinapopasa zikiwa zimekazwa imara? Je, skurubu au ribiti zilizotumiwa kukazia vidato vya chuma kwa juu zimevunjika au kupata kutu? Ngazi ndefu zinazoweza kuunganishwa huenda zikawa na makapi na kamba. Je, makapi yanafanya kazi sawasawa? Je, kamba ina dalili za kuchakaa, na je, ingali ndefu vya kutosha? Fanya marekebisho au mabadiliko yoyote bila kukawia.
Kwa kawaida vidato huwa vimetiwa vifuo ili kuzuia kuteleza. Hakikisha kwamba umeondoa uchafu wowote ambao huenda ukawa umerundikana kwenye vifuo. Ngazi zote zinapasa kuwa na pedi kwenye miguu za kuzuia kuteleza. Hakikisha kwamba ziko na kwamba hazijachakaa mno.
3 Safirisha ngazi kwa usalama. Unaposafirisha ngazi kwa gari, ifunge kwa nguvu katika angalau sehemu mbili kwenye shubaka la ngazi, au kwenye trela. Huenda ngazi ndefu ikaning’inia nyuma ya gari, kwa hiyo fungilia kitambaa chekundu kinachoonekana kwenye ncha ya ngazi ili kuonya mtu aliye nyuma yako.
Ni salama zaidi iwapo watu wawili watabeba ngazi ndefu. Inapokubidi kubeba ngazi peke yako na kuamua kuibeba kimlalo, iweke begani mwako, na uisawazishe kwa mkono mwingine. Ili kuepuka kumgonga mtu awaye yote, inua sehemu ya mbele juu ya kichwa chako. Hata hivyo, kumbuka kuibebea katikati! Wachekeshaji hulifanya lionekane jambo la kuchekesha watu wanapogongwa na ngazi. Hata hivyo, katika maisha halisi hili haliwi jambo la mzaha kamwe—hasa unapokuwa umejeruhiwa.
Unapobeba ngazi wima, iegemeze kwenye sehemu ya juu ya mwili wako, kisha uibebe kwa mkono mmoja huku ukiisawazisha sehemu ya juu kwa mkono mwingine. Uwe mwangalifu kuona nyaya zilizo juu, vifaa vya umeme, na vibao vilivyo barabarani!
4 Isimamishe ngazi kwa njia inayofaa. Kwa ajili ya usalama, ngazi haipasi kulala upande na lazima iwekwe kwenye pembe ya nyuzi 75 kutoka kwenye sakafu.
5 Itegemeze juu na chini. Uwe mwangalifu kuhusu unapoegemeza sehemu ya juu ya ngazi. Hakikisha kwamba mahali unapoegemeza ngazi pako imara na hapatelezi. Usiegemeze kamwe ngazi kwenye kioo au plastiki. Iwezekanapo, ifunge kwenye kifaa fulani, huku sehemu ya juu ya ngazi ikiinuka hadi meta moja juu ya sehemu ambapo inaegemezwa.
Uwe mwangalifu sana kwamba unapoipanda ngazi mwanzoni hakikisha unaifunga kwenye sehemu ya juu. Inakuwa hatari unapoipanda mwanzoni na unaposhuka, baada ya kufungua ilipofungiliwa. Ili kuwa salama unapopanda mwanzoni na unaposhuka mwishowe, tafuta msaidizi atakayeshikilia ngazi kwenye sehemu ya chini unapopanda. Hata hivyo, hili linawezekana tu iwapo ngazi si ndefu zaidi ya meta tano hivi.
Ikiwa ardhi iliyo karibu na jengo ina mteremko, weka kifaa kizito chini ya ngazi au ufungilie kifaa fulani kwenye kidato cha chini. Ikiwa ardhi ni ngumu yenye mabonde-mabonde, tia chembeo ili upate usawa. Iwapo udongo ni mwepesi au ni tifutifu, weka ubao au kifaa kinginecho imara chini yake.
Unapotumia ngazi ndogo, hakikisha kwamba miguu yote minne inasimama imara kwenye ardhi, huku sehemu zake mbili zikiwa mbalimbali na vifaa vya usalama vikiwa vimekazwa.
Je, Hali Yako Ni Salama?
6 Kagua viatu vyako. Kabla ya kupanda ngazi, hakikisha kwamba soli za viatu vyako ni kavu. Ondoa kitu chochote kama vile matope, kinachoweza kukufanya uteleze.
7 Beba vitu kwa uangalifu. Inapowezekana bebea vifaa katika kishikio kilichofungiliwa kwenye mshipi wako, ili mikono iwe huru unapopanda. Jaribu kutumia njia za badala unapopandisha vitu visivyobebeka kwa urahisi, lakini inapokubidi kutumia ngazi, shikilia ngazi kwa mkono mmoja kila mara na kuusogeza ngazini unapopanda. Panda kwa uthabiti na taratibu, usipande haraka-haraka.
Iwapo unatumia vifaa vinavyotumia nguvu za umeme, usitumie kamwe mikono yote miwili. Kwa mfano, huenda keekee ikakwama ghafula au ikateleza, ikikufanya upoteze usawaziko na kuanguka. Usiache vifaa hivyo vizunguke daima; huenda vikaanguka vikiwa vinazunguka.
8 Uwafikirie wengine. Ikiwa unafanya kazi katika eneo la umma, weka ishara ili ngazi ionekane kwa urahisi na ikiwezekana, zingira mahali ilipo. Unapolazimika kuipitisha ngazi kwa kona, fahamu kwamba wengine hawatarajii kukutana nawe. Toa onyo la kirafiki, na tazama uone kama njia iko wazi.
Unapokuwa na vifaa kwenye ngazi, kumbuka kwamba hata bisibisi ndogo sana yaweza kusababisha jeraha inapoangushwa kutoka juu. Unapolazimika kwenda kwa sababu fulani na hujafunga imara ngazi, mwambie mtu ailinde, au uilaze chini kwa uangalifu ngazi hiyo hadi utakaporudi. Usiiache tu bila ulinzi.
9 Chunguza afya yako. Kwa kuwa kupanda kunahusisha sana usawaziko na wizani, usipande unapojihisi ukiwa mgonjwa au unapopatwa na kichefuchefu au ikiwa unashikwa na kisunzi.
10 Panda kwa usalama. Kazia uangalifu usalama nyakati zote. Usiruhusu kamwe watu wawili au zaidi wapande ngazi moja wakati uleule. Usipande kamwe ngazi kunapokuwa na upepo mkali wenye nguvu. Usisimame kamwe kwenye kidato cha juu cha ngazi ndogo au kupita kidato cha nne kutoka juu cha ngazi ndefu. Usiunganishe kamwe ngazi nyingi kupita kiasi; sikuzote hakikisha kwamba angalau vidato vitatu vya ngazi hizo vinapitana. Usijinyooshe kamwe kupita kiasi. Ukijinyoosha sana unapokuwa kwenye ngazi, unaweza kupoteza usawaziko na kuanguka kwa urahisi. Badala ya kuwa katika hatari ya kujeruhiwa, isogeze ngazi, hata ikiwa inamaanisha kutumia muda mrefu zaidi kumaliza kazi. Unapopanda, tazama mbele.
Japo utazingatia tahadhari zozote zile, sikuzote kutakuwa na hatari unapotumia ngazi. Labda unaweza kuzipunguza kwa msaada wa madokezo haya. Yalimsaidia Paul. Kwa kuyafuata, alitia kwa usalama balbu mpya katika taa ya nje. Namna gani kusafisha madirisha? Bila shaka, atafanya hivyo wakati mwingine . . . labda!
[Picha katika ukurasa wa 22, 23]
1 Tumia ngazi inayofaa
2 Kagua ngazi yako kwa uangalifu
3 Safirisha ngazi kwa usalama
4 Isimamishe ngazi kwa njia inayofaa
5 Itegemeze juu na chini
6 Kagua viatu vyako
7 Beba vitu kwa uangalifu
8 Uwafikirie wengine
9 Chunguza afya yako
10 Panda kwa usalama