Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kunawa Mikono Nina umri wa miaka 11 na ninataka kuwashukuru kwa makala “Nawa Mikono na Uipanguse!” (Novemba 22, 1998) Ilinitia moyo kunawa mikono yangu kabla ya kula na baada ya kwenda msalani. Mjini kwetu, maambukizo ni ya kawaida, kwa hiyo makala hiyo ilikuwa yenye msaada sana.
M. F., Italia
Vichangamshi Sahili Asanteni kwa sehemu iliyo katika “Kuutazama Ulimwengu,” “Watoto Hupendelea Vichangamshi Sahili.” (Novemba 22, 1998) Naishi mbali na watoto wangu, nami nimeruhusiwa kuwaona mara moja tu baada ya kila miezi mitatu. Sijui la kufanya tunapokuwa pamoja, kwa hiyo mimi hupangia mambo mengi, nikiogopa wasichoshwe. Kabla tu ya siku ya kuonana nao, nilisoma sehemu hii. Ilikuja tu kwa wakati unaofaa!
M. Y., Japani
Nyoka Asanteni sana kwa makala yenu “Uwongo wa Kawaida Kuhusu Nyoka.” (Oktoba 22, 1998) Kwa hakika mambo saba mliyotaja yalielimisha umma kuhusu wanyama hawa wenye kuvutia ambao wameeleweka vibaya.
R. K., Marekani
Kuzuia Kuchomeka Nilihangaishwa niliposoma sehemu “Tahadhari Wakati wa Kupika,” katika “Kuutazama Ulimwengu.” (Desemba 8, 1998) Ilirejezea gazeti ambalo lilidokeza kupikia kwenye meko yaliyo katika sehemu ya mbele ya jiko. Hata hivyo, hilo lapingana na shauri ambalo nimesikia wazazi wakipewa—kwamba sikuzote wanapaswa kutumia meko yaliyo katika sehemu ya nyuma, ambayo watoto hawawezi kufikia.
M. B., Uingereza
Twathamini kikumbusha hiki cha usalama. Shauri tulilotoa liliwahusu hasa wazee-wazee, ambao baadhi yao wamechoma mikono ya mavazi yao na moto walipokuwa wakitaka kufikia sufuria zilizo kwenye meko ya sehemu ya nyuma. Ingawa hivyo, akina mama wenye watoto wachanga, kwa kawaida huweka sufuria za kupikia mbali ili wasiweze kuzifikia.—Mhariri.
Jinsi Yesu Alivyofanana Shukrani nyingi kwa mfululizo wa makala “Yesu—Kwa Kweli Alifananaje? Yeye Ni Nani Sasa?” (Desemba 8, 1998) Mara nyingi Yesu huchorwa isivyo sahihi makanisani, kwenye picha na kwenye sinema. Nilifurahia hasa kusoma juu ya fungu ambalo Yesu anatimiza sasa na atakalotimiza wakati ujao. Yeye si mtoto mchanga tu katika hori.
M. W., Austria
Nilipendezwa sana na makala hiyo! Ninasadiki kwamba mfululizo huu utasaidia watu wengi wawatumaini Mashahidi wa Yehova na magazeti yetu.
B. D., Yugoslavia
Ilipendeza kusoma kwamba Yesu hakuwa mtu dhaifu na kwamba hakuwa na sura ileile yenye huzuni, kama inavyoonyeshwa kwenye picha nyingi. Badala yake, yeye alikuwa mwanamume kabambe aliyemwiga Baba yake, “Mungu mwenye furaha.”—1 Timotheo 1:11.
R. O. R., Brazili
Kwenye ukurasa wa 8, mliandika kwamba “Mungu aliuhamisha uhai wa Yesu hadi kwenye tumbo la uzazi la bikira Myahudi.” Kwa kuwa Yesu alikuwa mkamilifu, je, hiyo yamaanisha kwamba hakuna hata chembe za Adamu zilizokuwa ndani yake?
J. G., Marekani
Kabla ya Maria kutungwa mimba ya Yesu, malaika Gabrieli alimwambia hivi: “Roho takatifu itakuja juu yako, na nguvu ya Aliye Juu Zaidi Sana itakufunika kivuli. Kwa sababu hiyo pia kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.” (Luka 1:35) Ni dhahiri kwamba, roho takatifu ya Mungu ilitunga mimba yai lililo katika tumbo la uzazi la Maria, ikihamisha uhai wa Mwana mzaliwa wa kwanza wa Mungu kutoka makao ya roho hadi duniani. Bila shaka roho takatifu ilihakikisha kwamba kani ya uhai mkamilifu ya Mwana huyo ilifuta kutokamilika kokote kwa Adamu katika yai la Maria, huku ikiacha tabia fulani za urithi. Yaelekea kwamba Yesu alifanana na Maria.—Mhariri.