Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 9/22 kur. 24-25
  • Walisimama Imara Wakati wa Utawala wa Nazi Nchini Uholanzi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Walisimama Imara Wakati wa Utawala wa Nazi Nchini Uholanzi
  • Amkeni!—1999
  • Habari Zinazolingana
  • Jumba la Hifadhi ya Uangamizo na Mashahidi wa Yehova
    Amkeni!—1993
  • Washika Uaminifu-Maadili Walio Wajasiri Washinda Mnyanyaso wa Nazi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
  • Uthibitisho Uonekanao wa Yale Maangamizo
    Amkeni!—1993
  • Mamilioni Waliuawa—Je, Itatokea Tena?
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 9/22 kur. 24-25

Walisimama Imara Wakati wa Utawala wa Nazi Nchini Uholanzi

JUMBA la Makumbusho ya Maangamizi Makubwa la Marekani (USHMM) lina mmojawapo wa mkusanyo mkubwa zaidi ulimwenguni wa vitu na sinema zinazoonyesha uhalifu uliofanywa na Wanazi wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili. Tangu Jumba hilo lifunguliwe kwa umma mwaka wa 1993, wageni wapatao milioni 12 wamezuru mahali hapo panapopendwa, kule Washington, D.C.

Jumba hilo la makumbusho pia lina mambo yanayoonyesha jinsi Mashahidi wa Yehova walivyonyanyaswa kikatili wakati wa utawala wa Nazi. Kwa kuongezea maonyesho machache ya kudumu, USHMM limetoa programu za kipekee zinazohusu Mashahidi wa Yehova. Programu hizo zimezingatia mifano hususa inayoonyesha uvumilivu na uaminifu-maadili wa Mashahidi wa Yehova. Mnamo Aprili 8, 1999, jumba hilo lilifadhili wonyesho wa kipekee wenye kichwa “Mashahidi wa Yehova Nchini Uholanzi Wakati wa Utawala wa Nazi.” Wonyesho huo ulifanyika katika kumbi mbili kubwa za jumba hilo la makumbusho.

Programu hiyo ilifunguliwa na Bi. Sara Jane Bloomfield, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa USHMM. Bi. Bloomfield alipendezwa sana na masimulizi ya Mashahidi wa Yehova. Alipohojiwa na Amkeni! alisema kwamba wanafanya jitihada kubwa za kufahamisha umma juu ya uaminifu-maadili wa Mashahidi wa Yehova wakati wa mnyanyaso. “Matukio kama haya,” alisema, “hutangazwa kama programu nyingine kubwa zinazofanywa kwenye jumba hilo la makumbusho.”

Wanahistoria kadhaa walikuwapo na kushiriki kwenye programu jioni hiyo. Mmoja wao alikuwa Dakt. Lawrence Baron, profesa wa historia ya kisasa ya Ujerumani na historia ya Kiyahudi kwenye chuo cha San Diego State University. Katika hotuba yake, Dakt. Baron alisema kwamba “Mashahidi wa Yehova walikataa katakata kuridhiana na Utawala wa Nazi.” Alisema kwamba Mashahidi “walitia imani yao kwa Mungu kuliko madai ya serikali ya Nazi. Wao waliona uongozi wa kufuata Hitler kuwa aina ya ibada ya kilimwengu nao walikataa madai yake ya kutaka kuabudiwa kwa kutoa salamu za Wanazi au kusema, ‘Mwokozi Ni Hitler.’ . . . Kwa kuwa Mungu aliwaamuru wawapende majirani na wasiue wengine, wao walikataa utumishi wa kijeshi . . . Walipoamriwa na Utawala wa Nazi wakomeshe ibada yao, Mashahidi walijibu tu kama kawaida yao, ‘Lazima sisi tumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.’” Kwa sababu hiyo, Mashahidi wengi katika nchi kadhaa za Ulaya walifungwa kwenye kambi za mateso, wakateswa, na hata kuuawa.

Jumba hilo la USHMM lilialika watafiti wa Uholanzi na kikundi cha watu waliookoka yale Maangamizi Makubwa ili waonyeshe jinsi Mashahidi wa Yehova walivyonyanyaswa na Wanazi nchini Uholanzi. Mnamo Mei 29, 1940, punde tu baada ya Wanazi kutwaa Uholanzi, Mashahidi wa Yehova wapatao 500 walipigwa marufuku katika nchi hiyo. Katika miezi iliyofuata, mamia ya Mashahidi walikamatwa. Watawala waliwatesa Mashahidi waliokamatwa wakijaribu kupata majina ya Mashahidi wengine. Kufikia mwisho wa vita, zaidi ya Mashahidi 450 walikuwa wamekamatwa. Kati yao, zaidi ya 120 walikufa kwa mnyanyaso.

Mtafiti mmoja wa Uholanzi alieleza kwamba ofisi ya tawi ya Uholanzi ya Watch Tower Society ina hifadhi ambayo ina “zaidi ya mahoji 170 ya vidio na masimulizi 200 ya Mashahidi wa Yehova nchini Uholanzi ambao waliokoka yale Maangamizi Makubwa. Yote hayo yanaonyesha kwamba kile kilichowachochea Mashahidi kilikuwa upendo wao kwa Mungu na kwa wenzao.”

Wasemaji kadhaa walikazia kwamba tofauti na vikundi vingine vilivyoandamwa na Wanazi, wengi wa Mashahidi wa Yehova wangeweza kupata uhuru kwa kutia tu sahihi tangazo linalokanusha itikadi zao. Lakini, wasemaji na vilevile wale waliohojiwa walieleza kwamba wengi wa Mashahidi walifanya uamuzi timamu waliofahamu wa kukubali kunyanyaswa badala ya kuridhiana. Watu wachache walitia sahihi tangazo hilo ili waache kushirikiana na Mashahidi wa Yehova.

Kuna wengine waliotia sahihi tangazo hilo kwa sababu ya kuvurugika. Watu hawa hawakutaka kamwe kuacha ibada yao. Wachache walihisi walitenda ifaavyo kimaadili kwa kuwapotosha watesi wao ili wapate uhuru na kuendelea kuhubiri. Pindi fulani baada ya kuachiliwa, wao walitambua kwamba hata kama walikuwa na nia nzuri, walikosea kutia sahihi tangazo hilo.

Kufanya uamuzi usiofaa hakukufanya watengwe. Waliporudi makwao na kwenye makutaniko yao, wao walipokea msaada wa kiroho. Barua moja kutoka kwenye ofisi ya tawi ya Uholanzi ya Watch Tower Society, ya Juni 1942, iliwatia moyo Mashahidi katika nchi hiyo waelewe hali zilizowafanya wengine watie sahihi tangazo hilo na wawatendee kwa rehema. Ijapokuwa Wanazi wangali walikuwa wakitawala, punde si punde Mashahidi hao waliokuwa wamefungwa awali walikuwa tena wakishiriki katika kazi ya kuhubiri, wakijihatarisha mno. Wengine walishikwa kwa mara ya pili. Mmoja wao hata aliuawa kwa sababu alikataa kushiriki utumishi wa kijeshi.

Japo mateseko mengi na miaka mingi ya kazi ya bidii ya kichinichini, Mashahidi wa Yehova nchini Uholanzi waliongezeka tokea 500 hivi katika mwaka wa 1940 hadi zaidi ya 2,000 wakati utawala wa Nazi ulipokoma mwaka wa 1945. Ujasiri wao na azimio lao la kumtii Mungu ni ushahidi mkubwa hadi leo hii.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Watafiti walihutubia kikundi kilichokusanyika

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mahoji ya waokokaji wa Uholanzi wa yale Maangamizi Makubwa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki