Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 9/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Useja wa Kidini—Wa Nini?
  • Kukokota Nyavu Kunaua
  • Vichezeo Vyenye Kemikali
  • Parokia Zisizokuwa na Makasisi
  • Kufilisika Kwaongezeka
  • Je, Ni Mavazi Yasiyo na Uvundo?
  • Wasiwasi Kuhusu Maji Waongezeka
  • Wafungwa Waongezeka Marekani
  • Kucheza Kamari Kuhusu Har–Magedoni
  • Kemikali—Je, Ni Rafiki na Adui?
    Amkeni!—1998
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1998
  • Vitu vya Kuchezea vya Zamani na vya Sasa
    Amkeni!—2005
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 9/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Useja wa Kidini—Wa Nini?

“Pambano juu ya useja wa kidini katika Kanisa Katoliki ni mojawapo ya matatizo makubwa zaidi kwa makasisi,” laripoti gazeti Veja. “Mnamo 1970, iliripotiwa kwamba makasisi 10,000 walikuwa wameacha wadhifa wao ili waoe. Leo, ni makasisi 120,000—mara 12 zaidi ya idadi hiyo. Katika Brazili, idadi ya makasisi wanaofanya uamuzi huu imepanda mara 20 katika kipindi kilekile.” Ingawa bishano lao haliungwi mkono na Maandiko, viongozi wa kidini wa Katoliki ya Roma hutetea zoea la useja wa kidini kwa kusema kuwa linamruhusu kasisi aweze “kumtumikia Mungu zaidi” na kukazia uangalifu kazi yake. “Lakini sababu halisi inayoendeleza useja wa kidini haitoshi hata kidogo,” lasema Veja. “Zoea hilo liliibuka katika Enzi za Kati ili kuhifadhi urithi wa kanisa, na kuwazuia wazao kumiliki ardhi na mali nyinginezo.”

Kukokota Nyavu Kunaua

“Kila mwaka, nyavu hukokotwa kwenye eneo la bahari ulimwenguni lenye ukubwa unaopita nchi ya Kanada,” yasema ripoti moja katika The Globe and Mail. “Wakati wa kukokota na kuvua, nyavu kubwa huvutwa chini ya bahari, zikiangamiza kihobelahobela samaki na wanyama wengine wa baharini walio muhimu katika mlishano wa chakula baharini. Aina nyingi za samaki wasiohitajiwa na wavuvi hunaswa pia nyavuni na kisha kuuawa.” Watafiti wanakadiria kwamba “kwa kila uduvi anayevuliwa kwa nyavu zinazokokotwa, samaki 10 au zaidi aina ya turiboti au chewa wachanga hunaswa kwenye nyavu kisha hufa.” Kwenye eneo la bahari lililokokotwa kwa nyavu, sifongo, kome, na krateshia zakaribia kuangamizwa, yasema ripoti hiyo. Mtafiti wa bahari katika Chuo Kikuu cha Maine profesa Les Watling aeleza hivi: “Huhitaji kuwa mwanabiolojia wa elimu ya baharini ili kutambua kwamba njia hizi za uvuvi zinadhuru viumbe vya baharini. Ndio uharibifu mbaya zaidi wa bahari uliowahi kusababishwa na mwanadamu.” Wanabiolojia wanatoa mwito wa kutenga kando maeneo fulani kuwa hifadhi za baharini, wanapolinganisha uharibifu huu na uangamizaji wa misitu kwenye nchi.

Vichezeo Vyenye Kemikali

“Aina fulani za kemikali zinazotumiwa kwa kawaida kulainisha vichezeo vya watoto ni hatari mara 20 zaidi ya ilivyofikiriwa hapo awali,” laripoti gazeti The Independent, la London. Utafiti uliofanyiwa Uholanzi unaonyesha kwamba phthalates—vilainishaji vya plastiki ngumu, kama vile polyvinyl chloride—hupatikana kwenye vitu vya watoto kunyonya na katika vichezeo vingine vinavyotafunwa na watoto na kwamba kemikali hizi huchanganyika na mate. Uchunguzi ulionyesha kwamba kiasi kikubwa cha phthalates mbili za kawaida “zaweza kusababisha kansa ya ini na figo, na kunywea kwa mapumbu.” Watoto wachanga wako hasa hatarini kwa sababu “uzito wao mdogo, ukuzi wao na matumizi ya muda mrefu huwafanya waathiriwe zaidi na kemikali,” yataarifu makala hiyo. Profesa James Bridges, mwanasayansi Mwingereza wa Tume ya Ulaya, alihangaishwa hasa na “watoto walio kwenye vituo, kwa mfano katika kituo cha kutunza watoto wadogo mchana au hospitali, kwa kuwa wao huelekea kutafunatafuna vichezeo kwa sababu hawana jambo jingine la kufanya.” Tayari nchi sita zimepiga marufuku kemikali za vichezeo, na nyingine nne zaidi zinajitayarisha kufanya hivyo.

Parokia Zisizokuwa na Makasisi

Uchunguzi uliofanywa na Kituo cha Maelekezo ya Ukasisi cha Kanisa Katoliki ulifunua kwamba parokia nyingi za Katoliki huko Italia—hususan 3,800—hazina kasisi mkazi wa parokia. Parokia hizi haziko mashambani au katika maeneo ya mbali tu. Kwa mujibu wa gazeti la La Repubblica, “kwa kawaida ‘kasisi mkazi wa parokia’ hukosekana hata kwenye vituo vyenye ukubwa wa wastani katika miji (yenye watu wapatao elfu moja hadi elfu tatu).” Ili kuficha upungufu huo, kwa kawaida vikundi vya parokia huwekwa chini ya uangalizi wa mtu mmoja aliyeteuliwa au chini ya kikundi cha makasisi. “Lakini, kwa njia hii,” laeleza gazeti hilo, “uhusiano wa moja kwa moja na wa kawaida kati ya kasisi na waparokia hukosekana, na . . . makasisi hulazimika kukimbia huku na huku.” Upungufu huo unashughulikiwa katika njia mbalimbali. Majiji makubwa kama Roma yameandikisha makasisi wa kutoka ugenini. Angalau parokia mbili za Italia sasa zinaongozwa na watu wasiozoezwa, ambao hawawezi kuongoza Misa wanaoweza tu kutoa Komunyo au kubatiza katika hali za dharura.

Kufilisika Kwaongezeka

“Marekani imekumbwa na tatizo la kufilisika,” asema mbunge wa Marekani Charles Grassley. Tangu kutungwa kwa sheria za kufilisika za Marekani karne moja iliyopita, takriban Wamarekani milioni 20 waliomba korti iwatangaze kuwa wamefilisika, na zaidi ya nusu kati yao wametangazwa tangu mwaka wa 1985. Kufikia katikati ya 1998, idadi ya waliotangazwa kuwa wamefilisika ilikuwa imevunja rekodi kwa kufikia watu milioni 1.42 katika miezi 12 iliyotangulia. Mbona kuna ongezeko kubwa hivyo? Kulingana na Alan Greenspan, mwenyekiti wa shirika la Marekani la Federal Reserve, kuongezeka ghafula kwa waliofilisika kwaweza kuwa ni kwa sababu ya kubadilika “kwa maoni juu ya aibu inayohusishwa na kufilisika.” Sababu nyingine yasemekana ni “kuongezeka kwa matumizi ya kadi za mikopo ambazo zinawafanya wanunuzi wawe na madeni ya kibinafsi chungu nzima,” lasema jarida la The Wall Street Journal.

Je, Ni Mavazi Yasiyo na Uvundo?

“Kwa miaka miwili sasa, wataalamu wa mavazi wamegundua umuhimu wa vitambaa vyenye kemikali, vyenye vibandiko mbalimbali kama vile vya kufisha bakteria . . . au visivyovunda,” lataarifu gazeti la Ufaransa Le Monde. Watu wengi wananunua mavazi yenye kufisha bakteria. Ijapokuwa kitambaa hiki hutumiwa hasa kwa matandiko, hivi sasa kinatumiwa pia kushonea soksi na chupi. Hata hivyo, si kila mtu anayependa kutumia vitambaa vyenye misombo ya kemikali na metali zenye uzani mkubwa mahususi ambazo zinabadili utendaji wa bakteria, kwa kuwa bakteria nyingi hunufaisha wanadamu. “Ili ngozi yetu iweze kutenda sawasawa inahitaji bakteria zote zenye kunufaisha za kiasili,” lasema Le Monde. “Watengenezaji wa mavazi yenye kufisha bakteria watalazimika kutatua tatizo kubwa”—la kukomesha ukuzi wa bakteria zenye kudhuru bila kufisha bakteria zinazozuia maambukizo.

Wasiwasi Kuhusu Maji Waongezeka

“Licha ya kwamba maji yetu ya kunywa yana viuadudu vingi, yaonekana pia kwamba yamejaa dawa,” lasema New Scientist. Dawa hizo zatokana na vyanzo kadhaa. Nyakati nyingine dawa zisizotakikana hutupwa chooni na husombwa na maji. Kwa kuongezea, dawa hupitishwa kwa mkojo. “Kati ya asilimia 30 na 90 ya dawa nyingi zinazotumiwa na wanadamu na wanyama hutoka pamoja na mkojo,” asema Bent Halling-Sorensen, wa Royal Danish School of Pharmacy. Kwa muda mrefu wakulima wametumia mkojo wa wanyama na mbolea kwenye mashamba yao. Dawa hizo zifikapo kwenye mazingira, zaweza kuwa katika hali yake ya asili, au zibadilishwapo katika mwili wa mwanadamu, zaweza kuwa katika hali yenye kuathiri au hatari kuliko hali ya awali ambayo mara nyingi ni mumunyifu. “Dawa ni mojawapo ya vikundi vichache vya kemikali zilizo katika maji ambazo hatuchunguzi,” asema Steve Killeen, wa Shirika la Mazingira la Uingereza.

Wafungwa Waongezeka Marekani

“Idadi ya wafungwa Marekani sasa haiwezi kulinganishwa na ya nchi nyingineyo yote, na ni kubwa zaidi hata kuliko ya serikali nyingi za kiimla,” lasema The Economist. “Mwaka uliopita mkazi mmoja kati ya wakazi [Wamarekani] 150 (kutia ndani watoto) alitiwa mbaroni.” Idadi ya wafungwa ni mara 20 zaidi ya ile ya Japani, mara 6 zaidi ya Kanada, na mara 5 hadi 10 zaidi ya nchi za Ulaya Magharibi. Idadi ya wafungwa Marekani imeongezeka mara nne zaidi tangu 1980. Zaidi ya wafungwa 400,000 wametiwa mbaroni sasa kwa sababu ya matumizi mabaya ya dawa, lakini idadi ya watu wanaotumia vibaya dawa haijabadilika tangu 1988. Gazeti The Economist lauliza: “Jela iwe inasaidia kukabiliana na uhalifu au la, Marekani itaendelea mpaka lini kushughulikia idadi ya wafungwa inayoongezeka?”

Kucheza Kamari Kuhusu Har–Magedoni

Kila juma watu chungu nzima huko Uingereza “hucheza kamari kuhusu Har–Magedoni,” laripoti The Guardian. Uchunguzi uliofanyiwa watu 1,001 ulifunua kwamba asilimia 33 wanafikiri kwamba mwisho wa ulimwengu utaletwa na vita ya ulimwengu, ilhali asilimia 26 wanafikiri kwamba mwisho utaletwa na kuongezeka kwa joto la dunia. Wengine wanakisia kwamba mwisho utasababishwa na mgongano na sayari ndogo. Kwa kweli, asilimia 59 ya watu waliofanyiwa uchunguzi “wanafikiri kwamba itakuwa rahisi kwao kuona mwisho wa ulimwengu kuliko kushinda Shindano la Kitaifa la Bahati Nasibu,” lasema The Guardian. Sababu gani watu wanakisia-kisia juu ya Har–Magedoni? “Huenda watu wamesisimuliwa na mwaka wa 2000 unaokuja pamoja na makisio ya siku ya mwisho kuhusiana na mwaka huo,” laeleza gazeti hilo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki