Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 12/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matayarisho kwa Ajili ya Misiba Yanahitajiwa
  • Mwanzi Unapochanua Hutokeza Hatari
  • Nyanya na Maradhi ya Kansa
  • Matatizo ya Kiakili ya Watoto
  • Kinachoenda juu Hurudi Chini
  • Kutovumiliana kwa Kidini Kwaongezeka
  • Je, Wapata Usingizi wa Kutosha?
  • Kuongezeka kwa Watoto Wahalifu
  • Eneo Jipya Nchini Kanada
  • Kukabiliana na Matatizo ya Tezi-kibofu
    Amkeni!—2000
  • Pambano la Mwanadamu Dhidi ya Misiba
    Amkeni!—1995
  • Sababu ya Mwili Wako Kuhitaji Usingizi
    Amkeni!—1995
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1991
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 12/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Matayarisho kwa Ajili ya Misiba Yanahitajiwa

Taarifa ya Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na Shirika la Mwezi Mwekundu yasema, “kwa mujibu wa World Disasters Report 1999, misiba ya asili ya mwaka uliopita ilikuwa mibaya zaidi ya misiba iliyowahi kutukia na ilisababisha uharibifu mkubwa usiopata kuonekana kamwe.” Ukame, kupungua kwa rutuba udongoni, mafuriko, na kuharibiwa kwa misitu kuliwafanya watu milioni 25 waache mashamba yao na kukimbilia mijini wakiwa maskwota, kulitokeza “idadi kubwa ya ‘wakimbizi’ kuliko ile inayotokezwa na vita na mapambano.” Nchi zilizoathiriwa zaidi ni zile zinazositawi, asilimia 96 ya vifo vyote vilivyosababishwa na misiba ya asili vilitukia katika nchi hizo. Misaada ya kifedha kutoka kwa mashirika ya kutoa misaada imepungua kwa asilimia 40 katika miaka mitano iliyopita. Mkurugenzi wa shirika hilo wa mpango wa kupambana na misiba, Peter Walker, alisema hivi alipokazia uhitaji wa kubadili maoni kuhusu kuwa tayari wakati wa misiba: “Kuitikia ghafula wakati wa misiba hakujafua dafu . . . Huwa hatungoji nyumba ishike moto, ndipo tuanze kuichangia fedha idara ya wazima-moto.”

Mwanzi Unapochanua Hutokeza Hatari

Maeneo makubwa ya kaskazini-mashariki ya India yamefunikwa kwa misitu ya mianzi. Hofu ilizuka katika majimbo ya Manipur na Mizoram mianzi ya huko ilipoanza kuchanua maua. Kwa nini? Kwa sababu mianzi ya pekee inayopatikana katika maeneo haya, inayoitwa mautang, huchanua maua mara moja tu baada ya miaka 50, nayo huvutia panya. Panya hao huzaana kwa haraka wanapokula maua hayo, na huanza kushambulia mazao ya chakula, na hatimaye husababisha njaa kuu. Kulingana na gazeti la The Times of India, njaa kuu ilitukia katika mwaka wa 1957 baada ya mianzi kuchanua maua mnamo 1954 na 1955. Serikali ya Jimbo la Mizoram ilidhamini kampeni ya kuua panya katika jitihada ya kuzuia njaa nyingine kuu. Waliahidi kutoa kiasi cha rupee moja kwa kila mkia wa panya. Kufikia Aprili, takriban mikia 90,000 ilikuwa imekusanywa, na maombi ya fedha zaidi yalikuwa yanatolewa ili kuendeleza kampeni hiyo ya kuangamiza panya.

Nyanya na Maradhi ya Kansa

Uchunguzi uliofanywa majuzi na Shirika la Marekani la Utafiti wa Kansa unadokeza kwamba nyanya yaweza kuwa na dutu inayozuia kuenea kwa kansa ya tezi-kibofu. Dutu hiyo ya lycopene inayofanya nyanya ziwe na rangi nyekundu, yaweza kupunguza ukubwa wa uvimbe wa tezi-kibofu unaosababisha kansa na kuzuia kuenea kwa kansa kwenye tishu nyingine mwilini. Uchunguzi uliochapishwa na Taasisi ya Kitaifa ya Kansa huko Marekani “ulionyesha kuwa nyanya pamoja na sehemu zake zote mbali na kuzuia kansa ya tezi-kibofu zilizuia pia kansa ya kongosho, mapafu, na ya utumbo mpana.”

Matatizo ya Kiakili ya Watoto

Ripoti moja ya Taasisi ya Afya ya Kiakili ilisema kwamba sehemu moja kwa tano ya vijana wa Uingereza wenye umri wa chini ya miaka 20 wana matatizo ya kiakili. Ingawa “Serikali, wataalamu na vyombo vya habari vinakazia sana afya ya kimwili ya watoto na mafanikio shuleni,” akasema mkurugenzi wa taasisi hiyo, June McKerrow, watoto “hawasitawi kihisia-moyo.” Ripoti hiyo inasema kwamba tatizo hilo huenda linasababishwa na mambo kadhaa. Watoto “hulazimika kujilinganisha na wenzao shuleni kuanzia umri mdogo sana kupitia kwa mitihani na mazoezi,” na wengi huacha shule wakijiona kuwa wajinga. Kompyuta na televisheni zimechukua mahali pa michezo ya uwanjani, inayowasaidia vijana “wafikiri wanapofanya maamuzi na kuwa na uhakika zaidi, na uthabiti zaidi.” Matangazo ya biashara “huchochea tamaa ya kupata vitu wasivyokuwa navyo au kuwa na utu mwingine.” Kwa kuongezea, kukiwa na asilimia 50 ya talaka na wazazi wengi wakiwa wameajiriwa, watoto hupata mikazo “zaidi kwa sababu hawawezi kutegemea hali ya kihisia-moyo ya familia zao,” lasema gazeti la The Daily Telegraph.

Kinachoenda juu Hurudi Chini

Katika maeneo fulani Marekani na katika nchi kadhaa za Amerika ya Latini, ni jambo la kawaida kwa watu kusherehekea mwanzo wa mwaka mpya kwa kurusha risasi hewani. Lakini polisi wanawasihi sana wasifanye hivyo. “Unaporusha risasi hewani,” akasema msimamizi wa idara ya polisi ya Los Angeles, Willie Williams, “risasi hiyo hurudi chini mahali fulani.” Na huenda mahali hapo pakawa kichwani mwa mtu mwingine. Zaidi ya watu 12 wameuawa kwa njia hii katika muda wa miaka michache huko Marekani. Kwa kuongezea, mamia ya visa vya waliojeruhiwa na mali kuharibiwa nyakati nyingine na risasi zilizorushwa kutoka mbali sana vimeripotiwa. Kwa kawaida, watu wanaorusha risasi hewani hufikiri kimakosa kwamba risasi husambaratika hewani au kwamba haziwezi kumdhuru yeyote zirudipo chini. Lakini risasi inayorushwa juu yaweza kurudi ikiwa na nguvu nyingi “kiasi cha kuweza kupenya ngozini, kupofusha jicho au kupenya sehemu laini ya fuvu la mtoto mchanga,” kulingana na Fred King, msemaji wa Idara ya Polisi ya Houston.

Kutovumiliana kwa Kidini Kwaongezeka

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Helsinki, tengenezo la kutetea haki za binadamu, “mnyanyaso mbalimbali” wa zile zinazoitwa eti dini mpya umezuka katika Ulaya, laripoti gazeti Catholic International. Ili kukomesha dini zisizo mashuhuri, serikali kadhaa zinajaribu kuanzisha sheria mpya zinazokiuka wajibu wake wa kudumisha uhuru wa dhamiri na wa kidini. Ripoti zenye kubishaniwa za bunge na orodha za yale yanayofikiriwa kuwa “mafarakano hatari” katika Ubelgiji, Ufaransa, na Ujerumani zimezidisha kutovumiliana na ubaguzi. Hata hivyo, Willy Fautré, msimamizi wa Shirika la Human Rights Without Frontiers, asema kwamba ni dini “chache sana” kati ya hizo zinazohatarisha jamii na kwamba hofu hiyo imetiwa chumvi. Dini mashuhuri, akasema, zimezidisha tatizo hilo kwa kutenda zikiwa “wanachama na waamuzi” katika ubishi na kwa kutetea “mashindano badala ya majadiliano.”

Je, Wapata Usingizi wa Kutosha?

Watu ambao “kwa kawaida hutaka kulala kidogo wakati wa mchana, wanaosinzia mikutanoni, au wanaoshindwa kukaza fikira” hawapati usingizi wa kutosha usiku, lasema gazeti la Toronto Star. Kwa kawaida watu wengi wanahitaji kulala kwa muda wa kati ya saa saba hadi tisa kila usiku ili wawe na nguvu siku ifuatayo. Haya ni baadhi ya madokezo yanayotolewa na wataalamu kuhusu kupata usingizi wa kutosha: Thamini usingizi. Nyoosha mwili wako kabla ya kulala. Matembezi ya starehe yaweza kusaidia, lakini usifanye mazoezi magumu saa tatu kabla ya kulala. Lala na uamke wakati uleule kila siku. Uamkapo usiku, usibabaike wala kujaribu kutatua matatizo—badala yake, tafakari juu ya mambo yenye kupendeza. Iwapo ungali macho baada ya nusu saa, toka kitandani na ufanye jambo linalostarehesha, kama usomaji unaopendeza. Uwe mwangalifu usile wala kunywa kupita kiasi wakati wa kulala, lakini usilale njaa pia.

Kuongezeka kwa Watoto Wahalifu

Idadi ya uhalifu uliofanywa na vijana huko Ujerumani mwaka uliopita iliongezeka, laripoti gazeti la Hessische-Niedersächsische Allgemeine. “Idadi ya watoto waliotuhumiwa kuwa waliwadhuru wengine kimwili” iliongezeka kwa asilimia 14.1. Jambo lenye kutokeza hata zaidi ni ongezeko la idadi ya watoto watuhumiwa wenye umri wa chini ya miaka 14—152,774—ongezeko la asilimia 5.9. Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Otto Schily, alikazia uhitaji wa kuchukua hatua madhubuti ili kuzuia tatizo hilo huku akilitaja kuwa “lenye kushtua sana.” Ingawa serikali inaweza kusaidia, hasa katika nyanja za elimu na kazi, alisema kwamba ni familia hasa iliyo na fungu muhimu la kuzuia uhalifu.

Eneo Jipya Nchini Kanada

Katika Aprili 1, 1999, eneo jipya la kaskazini mwa Kanada, Nunavut, lilifanyizwa. Hii ni mara ya kwanza kwa ramani ya Kanada kubadilishwa tangu Newfoundland ilipojiunga na mwungano huo mnamo 1949. Nunavut liko kwenye eneo lenye ukubwa wa takriban sehemu moja kwa tano ya ardhi ya Kanada, kulingana na ripoti moja katika gazeti la Toronto Star, jambo hilo linaufanya uwe mkoa mkubwa zaidi ya Quebec ambao ndio mkoa mkubwa zaidi nchini. Ni mkoa wa pekee pia nchini Kanada kwa sababu una idadi ndogo zaidi ya watu na wengi wao wakiwa vijana. Watu wapatao 27,000 huishi kwenye eneo hilo, asilimia 56 kati yao wakiwa na umri wa chini ya miaka 25. Nunavut, jina limaanishalo “Bara Letu” katika lugha ya Inuktitut, ni tokeo la mwafaka baina ya Wainuiti na serikali ya muungano kuhusiana na makazi na haki za Wenyeji.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki