Kuutazama Ulimwengu
Watu 13,000 kutoka nchi 26 waliohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza walisema kwamba “ufisadi ndilo tatizo linalozungumziwa zaidi ulimwenguni.” Hata hivyo, umaskini ulisemekana kuwa ndilo tatizo kubwa zaidi ulimwenguni.—SHIRIKA LA HABARI LA UINGEREZA.
“Makanisa kote nchini Marekani yanatia vifaa vya Mfumo wa Kupokea Habari Kutoka kwa Setilaiti (GPS) kwenye sanamu za Yesu akiwa mtoto ili kusaidia kuzipata zinapoibwa. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na wizi mkubwa wa sanamu hizo kote nchini.”—THE WEEK, MAREKANI.
“Halmashauri inayotoa ushauri kwa Shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa la Marekani inapendekeza kwamba watu wenye tatizo la kuchoka daima (chronic fatigue syndrome) wazuiwe kutoa damu, kutokana na hofu ya kwamba damu hiyo ina virusi vyenye ugonjwa huo.”—THE WALL STREET JOURNAL, MAREKANI.
Mwangaza Unaua Viini Sugu
Chuo Kikuu cha Strathclyde, Glasgow, nchini Scotland kimegundua teknolojia mpya ya kutumia mwangaza ulio na nguvu sana ili kuua bakteria sugu hospitalini. Mbinu hiyo mpya ya kuua viini ni bora kwa kupunguza virusi kuliko kuosha tu kwa kutumia kemikali za kuua viini. Mbinu hiyo “hufanya kazi kwa kuelekeza mwangaza mwembamba ambao huchochea molekuli fulani zitende ndani ya bakteria hizo na kuziua,” anaeleza mtaalamu wa biolojia Profesa John Anderson.
Ukataji wa Miti Unaongeza Malaria
Ukataji wa miti katika misitu ya kitropiki umechangia ongezeko la malaria kwa asilimia 50 hivi. Hivyo ndivyo watafiti fulani ambao wamekuwa wakichunguza habari kutoka wilaya 54 za afya nchini Brazili, pamoja na picha za satelaiti zinazoonyesha shughuli za ukataji miti wanavyosema. Malaria inasambazwa sana katika eneo hilo na aina ya mbu anayejulikana kama Anopheles darlingi. Sarah Olson, aliyeandika ripoti hiyo anasema, “Eneo lililokatwa miti, na kuachwa wazi na lenye vidimbwi vya maji vinavyopata kiasi kidogo cha mwangaza wa jua, huandaa mahali pazuri pa mbu hao kuzaana.” Maeneo ambayo yaliyoripotiwa kuwa na visa vingi vya malaria ni yale yaliyokatwa miti.
Ngisi Wanaoruka
Picha fulani zimepigwa kuthibitisha kwamba spishi fulani za ngisi wanaruka kwa kujirusha juu kwa nguvu. Wataalamu wanaochunguza viumbe wa baharini waliona kwamba “ngisi wadogo wenye urefu wa sentimita 20 hivi walijirusha umbali wa mita mbili hivi juu ya maji na kusonga kwa kupigapiga mapezi na minyiri yao kufikia umbali wa mita 10,” linasema gazeti Scientific American. Ngisi hao hunywa maji na kuyatema kwa nguvu na hilo huwawezesha kujirusha hadi nje ya maji. Picha zinaonyesha kwamba wanaporuka, wao hutumia mapezi yao kama mabawa.