Sura 2
Dini Ilianzaje?
1, 2. Ni nini kimeonwa kwa habari ya ukale na unamna-namna mkubwa wa dini?
HISTORIA ya dini ni ya tangu kuwapo kwa binadamu mwenyewe. Ndivyo watuambiavyo waakiolojia na waanthropolojia. Hata kati ya walio “wa kikale” zaidi, yaani, staarabu zisizostawika, kunapatikana uthibitisho wa ibada ya namna fulani. Kwa kweli The Encyclopædia Britannica chasema kwamba “kadiri ambayo wasomi wamevumbua, hakujapata kuwako watu, popote, wakati wowote ule, ambao hawakuwa wa kidini katika maana fulani.”
2 Zaidi ya ukale wake, dini pia hupatikana ikiwa yenye unamna-namna mkubwa. Wawinda vichwa katika mapori ya Borneo, Waeskimo katika Aktiki yenye barafu, wahamaji katika Jangwa Sahara, wakaaji wa mjini katika majiji makubwa ya ulimwengu—kila kikundi cha watu na kila taifa duniani lina kijimungu au vijimungu vyao na njia yao ya kuabudu. Utofautiano katika dini kwa kweli ni mkubwa ajabu.
3. Ni maswali gani kuhusu dini za ulimwengu yanayopasa kufikiriwa?
3 Kwa kufikiri kuzuri maswali yanakuja akilini. Dini hizi zote zilitoka wapi? Kwa kuwa kuna tofauti kubwa na ufanani kati yazo, je! zilianza kila moja ki-vyake, au zaweza kuwa zilisitawi kutoka chanzo kimoja? Kwa kweli huenda tukauliza: Hasa kwa nini dini ikaanza? Na jinsi gani? Majibu ya maswali hayo ni yenye umaana mkubwa kwa wote wanaopendezwa na kujua ukweli juu ya dini na imani za kidini.
Suala Juu ya Asili
4. Twajua nini juu ya waanzilishi wa dini nyingi?
4 Inapohusu suala la asili, watu wa dini tofauti-tofauti hufikiria majina kama Muhammad, Buddha, Confucius, na Yesu. Karibu katika kila dini, kuna mhusika mkuu ambaye hupewa sifa ya kuanzisha ‘imani ya kweli.’ Baadhi ya hao walikuwa ni wapinduzi wa kidini wachukiao sanamu. Wengine walikuwa ni wanafalsafa wa kiadili. Na bado wengine walikuwa ni mashujaa wa taifa wasio na ubinafsi. Wengi wao wameacha maandishi au semi ambazo zilifanyiza msingi wa dini mpya. Baada ya muda kupita mambo waliyosema na kufanya yalifafanuliwa, yakatiwa madoido, na kufanywa kuwa ya kifumbo. Baadhi ya viongozi wao hata walifanywa kuwa viabudiwa.
5, 6. Dini nyingi zilianzaje?
5 Hata ingawa watu hao mmoja mmoja walionwa kuwa waanzilishi wa dini zile kubwa-kubwa ambazo tumezizoelea, yapasa kuangaliwa kwamba wao hawakuanzisha dini hasa. Katika visa vilivyo vingi, mafundisho yao yalitokana na mawazo ya kidini yaliyokuwapo tayari, hata ingawa wengi wa waanzilishi hawa walidai upulizio wa kimungu kuwa chanzo chayo. Au walibadili na wakarekebisha upya mifumo ya kidini iliyokuwapo ambayo ilikuwa imekuwa isiyoridhisha katika njia hii au hii.
6 Kielelezo, kwa usahihi ambao historia inaweza kutuambia, Buddha alikuwa mwana-mfalme aliyeudhiwa sana na mateso na hali zenye kusikitisha alizokuta zinamzunguka katika jamii iliyotawalwa na Uhindu. Dini ya Buddha ilisababishwa na jitihada yake ya kutafuta suluhisho la matatizo ya maisha yenye kuumiza. Hali moja na hiyo, Muhammadi alihangaishwa sana na ibada ya sanamu na ukosefu wa adili alioona katika mazoea ya kidini yaliyomzunguka. Baadaye yeye alidai alipokea wahyi (mafunuo maalumu) mbalimbali kutoka kwa Mungu, ambayo yakawa ndiyo Kurani na kuwa msingi wa chama kipya cha kidini, Uislamu. Uprotestanti ulikuwa chipukizi la Ukatoliki ukiwa tokeo la Mapinduzi Makubwa ya Kidini yaliyoanza mapema katika karne ya 16, wakati Martin Lutheri alipopinga kanisa Katoliki kuuza hati za rehema.
7. Ni swali gani kuhusu dini ambalo lingali lahitaji kujibiwa?
7 Basi, kwa habari ya dini zilizopo sasa, hakuna ukosefu wa habari kuhusu asili yazo na usitawi wazo, waanzilishi, maandishi yazo matakatifu, na kadhalika. Lakini namna gani juu ya dini zilizokuwapo kabla yazo? Na zile za hata kabla ya hizo? Tukirudi nyuma vya kutosha katika historia, muda si muda tutakabiliwa na swali hili: Dini ilianzaje? Kwa wazi, ili kupata jibu la swali hilo, ni lazima tuangalie mbali zaidi ya mipaka ya dini moja moja.
Nadharia Nyingi
8. Kwa karne nyingi, ni nini mtazamo wa watu kuelekea dini?
8 Funzo la asili na usitawi wa dini ni uwanja mpya kwa kulinganisha. Kwa karne nyingi, kwa ujumla watu walikubali pokeo la dini ambamo katika hilo walizaliwa na ambamo katika hilo walilelewa. Wengi wao waliridhika na maelezo waliyopokezwa na mababu zao, wakihisi kwamba dini yao ilikuwa ndio ukweli. Ni mara chache kulipokuwako sababu ya kuwa na tashwishi ya lolote, au uhitaji wa kuchunguza jinsi, lini, au kwa nini mambo yakaanza. Kwa kweli, kwa karne nyingi, kukiwapo uchache wa njia za usafiri na uwasiliano, hata ni watu wachache waliojua kuna mifumo mingine ya kidini.
9. Tangu karne ya 19, ni majaribio gani yamefanywa kuvumbua jinsi na kwa nini dini ilianza?
9 Hata hivyo, wakati wa karne ya 19, picha hiyo ilianza kubadilika. Nadharia ya mageuzi ilikuwa ikisambaa kati ya wenye elimu kubwa. Jambo hilo, pamoja na kuwadia kwa utafiti wa kisayansi, vilisababisha wengi wawe na tashwishi ya mifumo iliyoimarishwa, kutia na dini. Wakitambua vizuizi vya kutafuta vidokezi ndani ya dini iliyokuwapo, wasomi fulani waligeukia masalio ya staarabu za mapema au kwenye ncha za mbali za ulimwengu ambako watu walikuwa wangali wakiishi katika jumuiya za kikale. Walijaribu hayo kwa kutumia mbinu za saikolojia, sosholojia, anthropolojia, na kadhalika, wakitumaini kuvumbua dokezi juu ya jinsi dini ilivyoanza na kwa nini.
10. Kukawa nini kwa sababu ya machunguzo ya asili ya dini?
10 Kukawa nini? Ghafula, kukatokea nadharia nyingi—nyingi kama hesabu ya wachunguzi wenyewe—kila mchunguzi akipinganisha za mwenzake, na kila mmoja akijitahidi kumshinda yule mwingine katika kuthubutu na uvumbuzi. Baadhi ya watafiti hao walifikia mikataa ya maana; kazi ya wengine imefanya kusahauliwa tu. Sisi tunapotupia macho matokeo ya utafiti huo tunaelimika na kunurishwa. Itatusaidia tupate uelewevu bora zaidi wa mitazamo ya kidini kati ya watu tunaokuta.
11. Fafanua nadharia ya animism.
11 Nadharia ambayo kwa kawaida inaitwa animism (ibada ya maumbile), ilipendekezwa na mwanthropolojia Mwingereza Edward Tylor (1832-1917). Yeye alidokeza kwamba mambo kama vile ndoto, njozi, chechele, na maiti kutokuwa na uhai yalisababisha watu wa kikale wakate maneno kwamba mwili ni makao ya nafsi (Kilatini, anima). Kulingana na nadharia hiyo, kwa kuwa mara nyingi waliota juu ya wapendwa wao waliokufa, walidhani kwamba nafsi iliendelea kuishi baada ya kifo, kwamba iliuacha mwili na kukaa katika miti, miamba, mito, na kadhalika. Hatimaye, wafu na vitu ambavyo ilisemekana nafsi inakaa ndani yavyo vikaja kuabudiwa kuwa vijimungu. Na hivyo, asema Tylor, dini ikazaliwa.
12. Fafanua nadharia ya animatism.
12 Mwanthropolojia mwingine, R. R. Marett (1866-1943), alipendekeza animism inolewe zaidi, akaiita animatism. Baada ya kuchunguza imani za Wamelanesia wa visiwa vya Pasifiki na wenyeji wa Afrika na Amerika, Marett alikata maneno kwamba badala ya kuwa na wazo la nafsi ya kibinafsi, watu wa kikale waliamini kuna kani isiyo na utu au nguvu fulani zinazozidi zile za kibinadamu zilizohuisha kila kitu; imani hiyo ilitokeza hisia-moyo zenye kutisha na kutia hofu binadamu, hayo yakawa msingi wa dini hii ya kikale. Kwa Marett, dini kwa sehemu kubwa ilikuwa itikio la hisia-moyoni la binadamu kwa yale yasiyojulikana. Taarifa yake aliyopenda zaidi ilikuwa kwamba dini “haikuwa imefikiriwa sana kwa kiasi ambacho ilifuatwa.”
13. Ni nadharia gani ya dini aliyopendekeza James Frazer?
13 Mwaka 1890 mtaalamu wa Scotland wa masimulizi ya wenyeji, James Frazer (1854-1941), alichapisha kitabu chenye uvutano The Golden Bough, ambamo alitoa hoja kwamba dini ilitokana na mizungu. Kulingana na Frazer, binadamu kwanza alijaribu kuongoza uhai wake mwenyewe na mazingira yake kwa kuiga aliyoona yanatukia katika maumbile ya asili. Kwa kielelezo, aliwaza kwamba angeweza kuita mvua inye kwa kunyunyiza maji kwenye ardhi kwa kuambatana na midundo ya ngoma yenye kusikika kama radi au kwamba angeweza kumdhuru adui yake kwa kudunga pini kisanamu fulani. Jambo hilo liliongoza kwenye matumizi ya sherehe, ulozi, na vidude vya uchawi katika sehemu nyingi za maisha. Viliposhindwa kufanya yaliyotazamiwa, ndipo alipogeukia kutambika na kusihi msaada wa nguvu zinazozidi zile za kibinadamu, badala ya kujaribu kuziongoza. Sherehe na maneno ya kunuizia uchawi yakawa dhabihu na sala, na kwa njia hiyo dini ikaanza. Kwa maneno ya Frazer, dini ni “upatanisho au usuluhisho wa nguvu zinazozidi binadamu.”
14. Sigmund Freud alifafanuaje asili ya dini?
14 Hata yule Mwaustria mchanganua akili maarufu Sigmund Freud (1856-1939), katika kitabu chake Totem and Taboo, alijaribu kueleza asili ya dini. Kwa kupatana na kazi yake, Freud alieleza kwamba dini ya mapema kabisa ilikuwa chipukizi la kile alichoita hamaniko lisababishwalo kwa kuhofu umbo-baba. Yeye alitoa nadharia kwamba, kama ilivyo na farasi-mwitu na ng’ombe, katika jumuiya ya kikale baba alitawala jamii. Wana, ambao walimchukia baba na pia kumstaajabia, waliasi na wakamwua huyo baba. Ili wajipatie uwezo wa baba, akadai Freud, ‘washenzi hao wala-watu walimla waliyemwua.’ Baadaye, kwa sababu ya kusikitika, wakabuni desturi za kufunika kitendo chao. Kulingana na nadharia yake Freud, umbo hilo la baba likawa Mungu, sherehe hizo zikawa dini ya mapema kabisa, na kuliwa kwa baba aliyechinjwa kukawa lile pokeo la kula kishirika linalozoewa katika dini nyingi.
15. Nadharia nyingi zilizopendekezwa kuhusu asili ya dini zimepatwa na nini?
15 Nadharia nyingine nyingi ambazo ni majaribio ya kufafanua asili ya dini zingeweza kutajwa. Hata hivyo, nyingi za hizo zimekwisha sahauliwa, na hakuna yoyote ya hizo ambayo imetokeza kuwa yenye kuthibitika zaidi au kukubaliwa zaidi ya zile nyingine. Kwa nini? Kwa sababu tu hakujapata kuwapo ushuhuda au uthibitisho wowote wa kihistoria kwamba nadharia hizo zilikuwa za kweli. Zilikuwa mazao tu ya kuwaza au dhana ya mchunguzi fulani, ambazo upesi mahali pazo pakachukuliwa na ile nyingine iliyofuata.
Msingi Wenye Kosa
16. Ni kwa nini miaka mingi ya uchunguzi imeshindwa kutokeza ufafanuzi juu ya jinsi dini ilivyoanza?
16 Baada ya miaka mingi ya kung’ang’ana na suala hilo, wengi sasa wamefikia mkataa kwamba haielekei sana kwamba kutakuwako fanikio lolote la kupata jibu la swali la jinsi dini ilivyoanza. Kwanza, hii ni kwa sababu mifupa na masalio ya watu wa kale havituambii jinsi watu hao walivyofikiri, walichohofu, au ni kwa nini wao waliabudu. Mikataa yoyote inayofikiwa kutokana na vitu hivyo vya kale ni makisio yenye msingi wa kielimu. Pili, mazoea ya kidini ya wanaoitwa leo washenzi, kama vile Waaborijini wa Kiaustralia, kwa lazima si kipimio chenye kutegemeka cha kupima mambo ambayo watu wa nyakati za kale walifanya au kuwaza. Hakuna anayejua kwa uhakika kama au jinsi utamaduni wao ulivyobadilika wakati wa karne nyingi zilizopita.
17. (a) Wanahistoria wa dini wa ki-siku-hizi wanajua nini? (b) Ni nini linaloonekana kuwa hangaikio kuu wakati wa kuchanganua dini?
17 Kwa sababu ya yote hayo yasiyo ya hakika, kitabu World Religions—From Ancient History to the Present kinakata maneno kwamba “mwanahistoria wa ki-siku-hizi wa dini anajua kwamba haiwezekani kuzifikia asili za dini.” Hata hivyo, kwa habari ya jitihada za wanahistoria, kitabu hicho chaonelea hivi: “Wakati uliopita wananadharia wengi walihangaikia si kusimulia au kufafanua tu dini bali kutoa ufafanuzi wa kuibatilisha, wakihisi kwamba kama namna za zamani zingeonyeshwa zilitegemea udhanifu basi dini za baadaye na za hali ya juu zaidi huenda zikazoroteshwa.”
18. (a) Ni kwa nini wachunguzi wengi wamekosa kufaulu kufafanua asili ya dini? (b) Yaonekana kuwa ni nini yaliyokuwa madhumuni ya wachunguza dini wa “kisayansi”?
18 Katika maelezo hayo ya mwisho mna kidokezi cha ni kwa nini wachunguzi mbalimbali wa “kisayansi” wa asili ya dini hawajatokeza ufafanuzi wowote wenye kuthibitika. Kufikiri vizuri hutuambia kwamba mkataa sahihi waweza kufikiwa kutokana tu na dhana sahihi. Mtu akianza na dhana yenye kosa, haielekei yeye atafikia mkataa timamu. Kushindwa tena na tena kwa wachunguzi wa “kisayansi” kutokeza ufafanuzi wa kiakili kwatokeza tashwishi kubwa zilizo juu ya dhana ambayo walitegemeza maoni yao. Kwa kufuata wazo lao lililofikiriwa kimbele, katika jitihada zao za ‘ufafanuzi wa kuibatilisha dini’ wamejaribia kutoa ufafanuzi wa kupuuza kuwapo kwa Mungu.
19. Ni nini iliyo kanuni ya msingi yenye kuongoza machunguzo ya kisayansi yenye kufanikiwa? Tafadhali toa kielezi.
19 Hali hiyo yaweza kulinganishwa na zile njia nyingi ambazo wataalamu wa nyota na anga kabla ya karne ya 16 walijaribu kufafnua mwendo wa sayari. Kulikuwako nadharia nyingi, lakini hakuna yoyote ya hizo iliyokuwa yenye kuridhisha kweli kweli. Kwa nini? Kwa sababu zilitegemea udhanifu wa kwamba dunia ilikuwa ndicho kitovu cha ulimwengu wote mzima ambacho nyota na sayari zilizunguka. Maendeleo halisi hayakufanywa mpaka wanasayansi—na Kanisa Katoliki—walipokuwa na nia ya kukubali uhakika wa kwamba dunia haikuwa kitovu cha ulimwengu wote mzima bali ilizunguka jua, kitovu cha mfumo wa jua. Kushindwa kwa nadharia hizo nyingi kufafanua mambo ya hakika kulisukuma watu mmoja mmoja wenye akili zilizo wazi, wasijaribu kutokeza nadharia mpya, bali kuchunguza tena msingi wa machunguzo yao. Na hilo likaongoza kwenye kufanikiwa.
20. (a) Ni nini uliokuwa msingi wa dhana yenye makosa ya uchunguzi wa “kisayansi” juu ya asili ya dini? (b) Voltaire alirejeza kwenye uhitaji gani wa msingi?
20 Kanuni iyo hiyo yaweza kutumiwa kuhusu uchunguzi wa asili ya dini. Kwa sababu ya ongezeko la uatheisti (kutodai kuwa na dini yoyote) na kuenea kwa ukubali wa nadharia ya mageuzi, watu wengi wamesadiki ki-vivi hivi tu kwamba Mungu hayupo. Kwa kutegemea udhanifu huo, wanahisi kwamba ufafanuzi wa kuwapo kwa dini wapaswa upatikane tu kwa binadamu mwenyewe—katika hatua zake za kufikiri, mahitaji yake, hofu zake, “mahamaniko” yake. Voltaire alitoa taarifa hii, “Kama Mungu hayupo, ingekuwa lazima kumbuni yeye”; kwa hiyo wao hutoa hoja kwamba binadamu amebuni Mungu.—Ona kisanduku, ukurasa 28.
21. Twaweza kufikia mkataa gani wa kufikiri kuzuri kutokana na kushindwa kwa nadharia hizo nyingi juu ya asili ya dini?
21 Kwa kuwa nadharia hizo nyingi zimeshindwa kutoa jibu lenye kuridhisha kikweli, je! sasa huu sio wakati wa kuchunguza tena dhana ambayo juu yayo machunguzo haya yametegemezwa? Badala ya kumenyeka bila ya matokeo katika kawaida ile ile, je! lisingekuwa jambo la akili kutafuta jibu kwingine? Ikiwa tuna nia ya kuwa na akili iliyo wazi, tutakubali kwamba kufanya hivyo ni jambo la akili na la kisayansi. Na hasa tuna kielelezo kimoja cha kutuonyesha tuone fikira nzuri ya kuchukua mwendo huo.
Ulizio la Kale
22. Nadharia nyingi za Waathene juu ya vijimungu vyao ziliathirije njia yao ya kuabudu?
22 Katika karne ya kwanza ya Wakati wa Kawaida wetu, Athene, Ugiriki, lilikuwa kitovu maarufu cha usomi. Hata hivyo, kati ya Waathene kulikuwako vikundi vingi vyenye mawazo tofauti, kama vile Waepikureo na Wastoiki, kila kimoja kikiwa na wazo lacho chenyewe juu ya vijimungu. Kwa kutegemea mawazo hayo mbalimbali, viabudiwa vingi viliheshimiwa sana, na njia tofauti za ibada zikasitawi. Matokeo ni kwamba, jiji hilo lilijaa sanamu na mahekalu yaliyofanyizwa na watu.—Matendo 17:16.
23. Mtume Paulo aliwatolea Waathene maoni gani yaliyo tofauti kabisa juu ya Mungu?
23 Wapata mwaka 50 W.K., mtume Mkristo Paulo alizuru Athene na kuwatolea Waathene maoni tofauti kabisa. Yeye aliwaambia: “Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote.”—Matendo 17:24, 25.
24. Hasa Paulo alikuwa akiwaambia nini Waathene juu ya ibada ya kweli?
24 Kwa maneno mengine, Paulo alikuwa akiwaambia Waathene kwamba Mungu wa kweli, “aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo,” si ubuni wa kuwaza kwa mtu, wala yeye hatumikiwi kwa njia ambazo mtu huenda akatunga. Dini ya kweli si jitihada ya upande mmoja ya mtu kujaribu kujazia uhitaji fulani wa kisaikolojia au kutuliza hofu fulani. Tofauti na hilo, kwa kuwa Mungu wa kweli ndiye Muumba, ambaye alimpa mtu uwezo wa kufikiri na nguvu za kusababu, ni jambo la akili kwamba Yeye angempa mtu njia ya kuja katika uhusiano wenye kuridhisha pamoja Naye. Hilo, kulingana na Paulo, ndilo Mungu alifanya hasa. “Alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika [mtu] mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, . . . ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.”—Matendo 17:26, 27.
25. Fafanua jambo kuu la hoja ya Paulo juu ya asili ya ainabinadamu?
25 Angalia hoja kuu ya Paulo: Mungu “alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika [mtu] mmoja.” Hata ingawa leo kuna mataifa mengi ya watu, wanaoishi duniani pote, wanasayansi wanajua kwamba, kwa hakika, ainabinadamu yote ni ya asili ile ile. Fikira hiyo ni yenye umaana mkubwa kwa sababu tunaposema juu ya ainabinadamu yote kuwa ya asili ile ile, inamaanisha mengi zaidi ya wao kuwa na uhusiano wa kiuzaliwa na kiurithi tu. Wana uhusiano katika maeneo mengine pia.
26. Ni nini kinachojulikana juu ya lugha kinachounga mkono hoja kuu ya Paulo?
26 Kwa mfano, angalia yanayosemwa na kitabu Story of the World’s Worship juu ya lugha ya binadamu. “Wale ambao wamefanya uchunguzi wa lugha za ulimwengu na kuzilinganisha wana jambo la kusema, nalo ndilo hili: Lugha zote zaweza kuwekwa katika vikundi vya familia za usemi, na familia hizi zote zaonwa kuwa zilianza kutokana na chanzo kile kile.” Kwa maneno mengine, lugha za ulimwengu hazikuanza zikiwa tofauti-tofauti na kwa kujitegemea, kama ambavyo wanamageuzi wangetuaminisha. Wao hutoa nadharia ya kwamba watu wenye kuishi ndani ya mapango katika Afrika, Ulaya, na Asia walianza kwa mikoromo na miguno na hatimaye wakasitawisha lugha zao wenyewe. Sivyo ilivyokuwa. Uthibitisho ni kwamba “zilianza kutokana na chanzo kimoja.”
27. Kwa nini ni kufikiri kuzuri kwamba mawazo ya mtu juu ya Mungu na dini yalianza kutokana na chanzo kimoja?
27 Ikiwa ndivyo ilivyo kwa kitu cha kibinafsi na cha kutokeza sana kama ilivyo lugha ya kibinadamu, basi je! lisingekuwa jambo la akili kufikiri kwamba mawazo ya mtu juu ya Mungu na dini yapasa pia kuwa yalianza kutokana na chanzo kimoja? Na ilivyo, dini inahusiana na kufikiri, na kufikiri kunahusiana na uwezo wa mtu kutumia lugha. Si kwamba dini zote kwa kweli zilikua kutokana na dini moja, bali mawazo na mafikira yapasa kufuatiwa mpaka kwenye asili ile ile au dimbwi moja la mawazo ya kidini. Je! kuna uthibitisho wa kuunga mkono hilo? Na ikiwa, kwa kweli, dini za watu zilitokana na chanzo kimoja, ni nini hicho? Twaweza kujuaje?
Tofauti Lakini Zafanana
28. Twaweza kujuaje kama kuna asili moja ya dini za ulimwengu?
28 Twaweza kupata jibu katika njia ile ile ambayo wataalamu wa lugha walipata majibu yao juu ya asili ya lugha. Kwa kuzilinganisha lugha na kuona ufanani wazo, mtaalamu wa etimolojia (elimu ya kuchunguza asili ya maneno) aweza kufuatisha lugha mbalimbali kurudi mpaka kwenye chanzo chazo. Hali moja na hiyo, kwa kulinganisha dini, twaweza kuchunguza mafundisho yazo, hekaya, sherehe za ibada, sherehe za heshima, desturi, na kadhalika, na kuona kama kuna uzi wowote wa msingi wenye utambulishi mmoja na, ikiwa ndivyo, uzi huo unatuongoza kwenye nini.
29. Ni nini inayoweza kuwa sababu ya tofauti nyingi kati ya dini?
29 Kijuu-juu, dini nyingi zilizopo leo zaonekana kuwa zenye kutofautiana sana. Hata hivyo, tukizivua mambo ambayo ni madoido tu na ambayo ni nyongeza ya baadaye, au tukiondoa zile tofauti ambazo ni tokeo la hali za hewa, lugha, hali za kipekee-pekee za nchi yao ya kuzaliwa, na mambo mengine, inastaajabisha jinsi nyingi za dini hizo zinavyoonekana zinafanana.
30. Wewe waona ufanani gani kati ya Ukatoliki wa Roma na Dini ya Buddha?
30 Kwa kielelezo, watu walio wengi wangefikiri kwamba hakungeweza kuwako dini nyingine mbili zozote zinazotofautiana zaidi ya Kanisa Katoliki la Roma la nchi za Magharibi na Dini ya Buddha ya nchi za Mashariki. Hata hivyo, tunaona nini tunapoondoa tofauti ambazo zaweza kusemwa ni kwa sababu ya lugha na utamaduni? Tukiangalia mambo yalivyo kikweli, twalazimika kukubali kwamba kuna mengi yanayofanana katika dini hizo mbili. Ukatoliki na Dini ya Buddha zinashika sana kawaida za ibada na sherehe za kufanya mambo. Hizo ni kutia na matumizi ya mishumaa, ubani, maji matakatifu, tasbihi, taswira za watakatifu, nyimbo na vitabu vya sala, hata ishara ya msalaba. Dini hizo mbili huendesha makao ya watawa wa kiume na kike na zajulikana kwa ajili ya kutofunga ndoa kwa makasisi, kanzu za pekee, siku takatifu, vyakula maalumu. Orodha hii si kamili, lakini inatumika kuonyesha hoja hiyo. Swali ni hili, Kwa nini dini hizo mbili zinazoonekana kuwa tofauti zina mambo mengi yenye kufanana?
31. Unaona ufanani gani kati ya dini nyinginezo?
31 Jinsi ulinganishi wa dini hizo mbili unavyonurisha, ndivyo inavyoweza kufanywa kwa dini zile nyingine. Tufanyapo hivyo, twakuta kwamba mafundisho na imani nyingi karibu zapatikana miongoni mwazo. Wengi wetu tumezoelea mafundisho kama kutoweza kufa kwa nafsi ya kibinadamu, thawabu ya kimbingu kwa ajili ya watu wote wema, mateso ya milele kwa ajili ya waovu katika ulimwengu wa chini, purgatori (toharani), kijimungu cha utatu au kijimungu chenye vijimungu vingi, na mama ya kijimungu au kijimungu-kike malkia wa mbingu. Hata hivyo, zaidi ya hayo, kuna hekaya nyingi na ngano ambazo pia ni zenye kuenea pote hali moja. Kwa kielelezo, kuna hekaya juu ya binadamu kupoteza neema ya kimungu kwa sababu ya jaribio lake haramu la kujipatia hali ya kutoweza kufa, uhitaji wa kutoa dhabihu ili kufunika dhambi, jitihada ya kutafuta mti wa uzima au bubujiko la ujana, vijimungu na vijimungu-nusu vilivyoishi kati ya wanadamu vikazaa watoto wenye nguvu zipitazo za kibinadamu, na furiko lililoleta msiba ulioangamiza karibu wanadamu wote.a
32, 33. (a) Twaweza kufikia mkataa gani kutokana na ufanani mwingi wenye kutokeza kati ya dini za ulimwengu? (b) Ni swali gani linalohitaji jibu?
32 Twaweza kufikia mkataa gani kutokana na hayo yote? Tunaona kwamba wale walioamini ngano na hekaya hizi waliishi kijiografia mbali na wengine. Utamaduni na mapokeo yao yalikuwa tofauti na mbali sana na yale ya wengine. Desturi zao za kijamii hazikuhusiana. Na bado, inapohusu dini, wao waliamini mawazo yale yale. Ingawa si kila kimoja cha vikundi hivi vya watu kilichoamini mambo yote yaliyotajwa, vyote viliamini baadhi yayo. Swali lililo wazi ni hili, Kwa nini? Ilikuwa kama kwamba kulikuwa na dimbwi moja ambalo kutoka hilo kila dini ilichota imani zayo za msingi, nyingine zikichota nyingi, nyingine kidogo. Wakati ulivyopita, mawazo hayo ya msingi yakatiwa madoido na kurekebishwa, na mafundisho mengine yakasitawishwa kutokana na hayo. Lakini umbo la msingi ni dhahiri.
33 Ni kufikiri kuzuri kwamba ufanani katika mawazo ya msingi ya dini nyingi za ulimwengu ni uthibitisho madhubuti kwamba kila moja haikuanza peke yake na kwa kujitegemea. Badala yake, tukirudi nyuma vya kutosha, mawazo yazo lazima yawe yalitoka kwenye asili moja. Asili hiyo ilikuwa nini?
Muhula Murua wa Mapema
34. Ni hekaya gani kuhusu mwanzo wa mtu inayopatikana katika dini nyingi?
34 Yenye kuvuta fikira kati ya hekaya iliyo kawaida ya dini nyingi ni ile inayosema mwanzo wa ainabinadamu ni muhula murua ambao katika huo mtu alikuwa bila hatia, aliishi kwa furaha na kwa amani katika shirika la ukaribu na Mungu, naye alikuwa huru na magonjwa na kifo. Ingawa huenda habari hiyo ikatofautiana kindani, wazo lilo hilo la paradiso kamilifu ambayo ilikuwapo wakati moja lapatikana katika maandishi na hekaya za dini nyingi.
35. Simulia imani ya Dini ya Zoroaster ya kale juu ya muhula murua wa mapema.
35 Avesta, kitabu kitakatifu cha dini ya Kizoroaster ya Uajemi ya kale, chaeleza juu ya “Yima mwenye kufuata haki, mchungaji mwema,” aliyekuwa mtu wa kwanza ambaye Ahura Mazda (muumba) aliongea naye. Aliagizwa na Ahura Mazda “kulisha, kutawala, na kutunza ulimwengu wangu.” Ili afanye hivyo, alipaswa kujenga “Vara,” makao ya chini ya ardhi, kwa ajili ya viumbe wote walio hai. Humo, “hamkuwamo ama kupiga ubwana wala roho ya unyimivu, wala upumbavu wala jeuri, wala umaskini wala udanganyifu, wala uduni wala hitilafu ya mwili, wala meno makubwa mno wala miili inayopita ukubwa wa kawaida. Wakaaji hawakuchafuliwa kwa vyovyote na roho mbovu. Walikaa kati ya miti yenye kutoa harufu tamu na nguzo za dhahabu; walikuwa ndio wakubwa kabisa, bora kabisa na wazuri kabisa duniani; wao wenyewe walikuwa jamii ya watu warefu na wazuri.”
36. Mtunga mashairi Mgiriki Hesiod alisimuliaje “Muhula Murua”?
36 Kati ya Wagiriki wa kale, shairi lake Hesiod Works and Days lasema juu ya Mihula Mitano ya Binadamu, wa kwanza ambao ulikuwa “Muhula Murua” wakati ambao watu walionea shangwe furaha kamili. Yeye aliandika hivi:
“Miungu isiyoweza kufa, inayotembea kwenye nyua za mbingu,
Kwanza ilifanya jamii ya watu murua.
Kama miungu waliishi, wakiwa na nafsi zenye furaha, zisizo na mahangaiko,
Wakiwa bila kumenyeka na maumivu; wala haukuwapata
Uzee wenye kusumbua, bali maisha yao yote yalitumiwa
Katika kula karamu, na viungo vyao vya mwili havikubadilika.”
Muhula murua huo wa kihekaya ulipotezwa, kulingana na ngano za Kigiriki, wakati Epimetheo alipomkubali Pandora mrembo awe mke, zawadi aliyopewa na kijimungu Zeu cha Olimpia. Siku moja Pandora alifungua gubiko (funiko) la chombo chake kikubwa, na ghafula humo mkatoka matata, huzuni, na maradhi ambayo kutoka hayo ainabinadamu haingepata nafuu kamwe.
37. Eleza lile simulizi la kale la kihekaya la Uchina juu ya “paradiso” mwanzoni mwa historia.
37 Hekaya za Kichina za kale pia zasimulia juu ya muhula murua katika siku za Huang-Ti (Maliki wa Manjano), ambaye yasemekana alitawala kwa miaka mia moja katika karne ya 26 K.W.K. Yeye alisifiwa kwa kubuni kila kitu kinachohusiana na ustaarabu—mavazi na makao, magari ya uchukuzi, silaha na vita, usimamizi wa ardhi, ufanyizaji vitu, ukulima wa hariri, muziki, lugha, hisabati (hesabu), kalenda, na kadhalika. Wakati wa utawala wake, yasemekana, “hakukuwako wezi wala mapigano katika China, na watu waliishi kwa unyenyekevu na amani. Mvua na hali ya hewa ya majira yanayofaa vikatokeza mavuno tele mwaka baada ya mwaka. La kustaajabisha zaidi lilikuwa ni kwamba hata wanyama-mwitu hawakuua, na ndege wala-wengine hawakudhuru. Kwa ufupi, historia ya China ilianza na paradiso.” Hata leo hii, Wachina wangali hujidai kuwa wazao wa Maliki wa Manjano.
38. Ni mkataa gani tunaoweza kufikia kutokana na masimulizi hayo yote yenye kufanana ya kihekaya juu ya mwanzo wa binadamu?
38 Masimulizi ya kihekaya kama hayo kuhusu wakati fulani wa furaha na ukamilifu mwanzoni mwa historia ya binadamu yaweza kupatikana katika dini za vikundi vingine vingi vya watu—Wamisri, Watibet, Waperu, Wameksiko, na wengine. Je! ilitukia tu kiaksidenti kwamba vikundi hivi vyote, vilivyoishi mbali na vingine na ambavyo vilikuwa na tamaduni, lugha, na desturi tofauti-tofauti kabisa vikawa na mawazo yale yale juu ya asili yavyo? Je! ilikuwa nasibu tu au sadifu tu kwamba vyote vikachagua kufafanua mianzo yavyo katika njia ile ile? Kufikiri kuzuri na mambo tuliyojionea hutuambia kwamba haiwezi kuwa hivyo hata. Kinyume cha hilo, ndani ya mchanganyiko wa hekaya hizi zote, lazima kuwe visehemu fulani vya ukweli vinavyofanana juu ya mwanzo wa binadamu na dini yake.
39. Ni picha gani ya ujumla inayoweza kukusanywa kutokana na visehemu vinavyofanana vya hekaya nyingi juu ya mwanzo wa mtu?
39 Hakika, kuna visehemu vingi vyenye kufanana vinavyoonekana kati ya hekaya zote tofauti-tofauti zinazohusu mwanzo wa binadamu. Tunapoziunganisha, picha kamili yaanza kutokea. Husimulia jinsi Mungu alivyoumba mwanamume na mwanamke wa kwanza na kuwaweka katika paradiso. Hapo kwanza walikuwa na uradhi sana na furaha sana, lakini upesi wakawa waasi. Uasi huo uliongoza kwenye kupoteza paradiso kamilifu, mahali payo pakawa tu ni taabu na kumenyeka, maumivu na kuteseka. Hatimaye ainabinadamu ikawa mbaya sana hivi kwamba Mungu akaiadhibu kwa kupeleka gharika ya maji iliyoiharibu yote isipokuwa familia moja. Familia hii ilipoongezeka, baadhi ya wazao walisongamana pamoja wakaanza kujenga mnara mkubwa sana kwa kumkaidi Mungu. Mungu alivunja njama yao hiyo kwa kuvuruga lugha yao na kuwatawanya kwenye pembe za mbali za dunia.
40. Fafanua uhusiano wa Biblia na hekaya hizo juu ya asili ya dini za binadamu.
40 Je! picha hii yenye kujumlisha mengi imetokana tu na utumizi wa akili ya mtu? La. Kwa msingi, hii ndiyo picha inayotolewa katika Biblia, katika sura 11 za kwanza za kitabu cha Mwanzo. Ingawa hatutaingilia maongezi ya uasilia wa Biblia hapa, na iangaliwe kwamba simulizi la Biblia la historia ya mapema ya binadamu huakisiwa (huonyeshwa) katika sehemu kuu zinazopatikana katika hekaya nyingi.b Maandishi hufunua kwamba jamii ya kibinadamu ilipoanza kutawanyika kutoka Mesopotamia, walienda kotekote pamoja na kumbukumbu zao, mambo waliyojionea, na mawazo. Baada ya muda yalitiwa madoido na kubadilishwa yakawa msingi wa dini katika kila sehemu ya ulimwengu. Maana yake, tukirudia ulinganifu uliotumiwa mapema, lile simulizi katika Mwanzo ndilo dimbwi dhahiri kabisa ambalo kutoka hilo yakachipuka mawazo ya msingi juu ya mwanzo wa binadamu na ibada inayopatikana katika dini mbalimbali za ulimwengu. Wakaziongezea hizo mafundisho na mazoea yao ya kipekee, lakini kiunganishi chenyewe ni kile kile.
41. Imekupasa kuzingatia nini akilini unapotalii sura zifuatazo katika kitabu hiki?
41 Katika sura zinazofuata za kitabu hiki, tutazungumza kwa urefu zaidi jinsi dini fulani fulani zilivyoanza na kusitawi. Utakuta inanurisha si kujua tu jinsi kila dini ilivyo tofauti na nyinginezo bali pia jinsi inavyofanana nazo. Pia utaweza kujua jinsi kila dini inavyoingia katika mpangilio wa wakati wa historia ya kibinadamu na historia ya dini, jinsi kitabu au maandishi yayo matakatifu yanavyohusiana na mengine, jinsi mwanzilishi au kiongozi wayo alivyovutwa na mawazo mengine ya kidini, na jinsi imekuwa na uvutano juu ya mwenendo na historia ya ainabinadamu. Ukizingatia mambo haya akilini, kujifunza juu ya jitihada ya ainabinadamu ya kutafuta Mungu ambayo imechukua muda mrefu Mungu kutakusaidia uone kwa uwazi zaidi ukweli juu ya dini na mafundisho ya kidini.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa ulinganishi wa kina kirefu wa hekaya juu ya furiko zinazopatikana kati ya vikundi mbalimbali vya watu, tafadhali ona kitabu Insight on the Scriptures, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., 1988, Buku 1, kurasa 328, 610, na 611.
b Ili kupata maelezo kwa urefu juu ya habari hii, tafadhali rejeza kwenye kitabu Biblia—Neno la Mungu au la Binadamu?, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., 1991.
[Blabu katika ukurasa wa 23]
Kuwasili kwa utafiti wa kisayansi na nadharia ya mageuzi kulifanya wengi wawe na tashwishi juu ya dini
[Blabu katika ukurasa wa 34]
Ni kama kwamba kulikuwako dimbwi moja ambalo kutoka hilo kila dini ilichota imani zayo za msingi
[Sanduku katika ukurasa wa 28]
Kwa Nini Mwanadamu Ni wa Kidini?
▪ John B. Noss afichua katika kitabu chake Man’s Religions: “Dini zote husema kwa njia hii au hii kwamba binadamu hasimami peke yake, wala hawezi. Yeye kwa lazima anahusiana na hata anategemea nguvu katika Asili na Jamii iliyo nje yake. Kwa njia iliyo wazi au isiyo wazi, ajua kwamba yeye si kitovu cha kani chenye kujitegemea kinachoweza kusimama peke yacho mbali na ulimwengu.”
Hali moja na hiyo, kitabu World Religions—From Ancient History to the Present chasema: “Uchunguzi wa dini hufunua kwamba sehemu ya maana yayo ni tamanio la kanuni maishani, itikadi ya kwamba uhai haukujitokeza tu wala si usio na maana. Jitihada ya kutafuta maana huongoza kwenye imani katika nguvu iliyo kubwa zaidi ya binadamu, na hatimaye kwenye akili ya ulimwengu wote mzima au inayopita uwezo wa kibinadamu ambayo ina madhumuni na azimio la kudumisha kanuni za juu zaidi kwa ajili ya uhai wa kibinadamu.”
Hivyo dini hutosheleza uhitaji wa msingi wa kibinadamu, kama vile chakula kinavyotosheleza njaa yetu. Twajua kwamba kula ovyo-ovyo tunapokuwa na njaa kwaweza kukomesha kusokotwa na njaa; hata hivyo, baada ya muda mrefu, kutadhuru afya yetu. Ili kudumisha maisha yenye afya, twahitaji chakula kinachofaa na chenye kujenga mwili. Hali moja na hiyo, twahitaji chakula cha kiroho kinachofaa ili kudumisha afya yetu ya kiroho. Ndiyo sababu Biblia hutuambia: “Mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila [neno] litokalo katika kinywa cha BWANA [Yehova, NW].”—Kumbukumbu la Torati 8:3.
[Ramani katika ukurasa wa 39]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Jamii ya kibinadamu ilipotawanyika kutoka Mesopotamia, mawazo yao ya kidini na kumbukumbu ziliambatana nao
BABULONI
LIDIA
SIRIA (SHAMU)
MISRI
ASHURU
UMEDI
ELAMU
UAJEMI
[Picha katika ukurasa wa 21]
Wanadamu kama vile Buddha, Confucius, na Lutheri walibadili mifumo ya kidini iliyokuwapo; wao hawakuanzisha dini
[Picha katika ukurasa wa 25]
Mchanganuzi wa akili Mwaustria Sigmund Freud alisema kuwako kwa dini ni kwa sababu ya hofu ya umbo la baba
[Picha katika ukurasa wa 27]
Dhana ya kwamba dunia ilikuwa kitovu cha ulimwengu wote mzima iliongoza kwenye mikataa yenye makosa juu ya kusonga kwa sayari
[Picha katika ukurasa wa 33]
Dini ya Buddha na Ukatoliki wa Roma—kwa nini zaonekana zina mambo mengi yanayofanana?
Mfuasi Mchina wa Dini ya Buddha kijimungu-kike cha rehema kikiwa na mtoto mchanga
Madonna wa Katoliki akiwa na mtoto mchanga Yesu
Mfuasi Mtibet wa Dini ya Buddha akitumia gurudumu la sala na tasbihi
Mkatoliki akitumia tasbihi
[Picha katika ukurasa wa 36]
Ngano za China husema juu ya muhula murua wakati wa utawala wa Huang-Ti (Maliki wa Manjano) katika nyakati za ngano