Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • sh sura 7 kur. 161-186
  • Dini ya Tao na Dini ya Confucius—Jitihada ya Kutafuta Njia ya Mbinguni

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Dini ya Tao na Dini ya Confucius—Jitihada ya Kutafuta Njia ya Mbinguni
  • Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Tao—Ni Nini?
  • Dini ya Tao—Mwanzo wa Kifalsafa
  • Kupata Ufahamu Mdogo Juu ya “Tao Te Ching”
  • Mwenye Hekima wa Pili wa Dini ya Tao
  • Kutoka Kwenye Falsafa Kuwa Dini
  • Kukabili Tisho la Dini ya Buddha
  • Mwenye Hekima Mwingine Mashuhuri wa China
  • Confucius Mwalimu
  • “Mbingu Ndizo Zanijua Mimi!”
  • Kiini cha Mawazo ya Dini ya Confucius
  • Dini ya Confucius Ikawa Kidhehebu cha Serikali
  • Urithi wa Hekima ya Mashariki
  • Wazo Hilo Laingia Dini za Mashariki
    Ni Nini Hutupata Tunapokufa?
  • Ile Kanuni Bora—Ni Fundisho la Ulimwenguni Pote
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
  • Jitihada Ya Ainabinadamu Kutafuta-tafuta Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Jitihada ya Kutafuta Kisichojulikana Kupitia Mizungu na Uwasiliani-Roho
    Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
Pata Habari Zaidi
Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
sh sura 7 kur. 161-186

Sura 7

Dini ya Tao na Dini ya Confucius—Jitihada ya Kutafuta Njia ya Mbinguni

Dini ya Tao, Dini ya Confucius, na Dini ya Buddha ni mjumlisho wa dini tatu kubwa za China na Mashariki ya Mbali. Hata hivyo, tofauti na Dini ya Buddha, Dini ya Tao na Dini ya Confucius hazijapata kuwa dini za ulimwengu lakini kwa msingi zimebaki katika China na kokote ambako utamaduni wa Kichina umepenyeza uvutano wao. Ingawa hakuna tarakimu rasmi za hesabu ya wakati huu ya wafuasi wazo zinazopatikana katika China, Dini ya Tao na Dini ya Confucius pamoja zimetawala maisha za kidini za karibu robo moja ya idadi ya watu ulimwenguni kwa miaka 2,000 iliyopita.

1. (Tia ndani utangulizi.) (a) Dini ya Tao na Dini ya Confucius zinazoewa wapi, na zimeenea kadiri gani? (b) Sasa twageukia kipindi gani cha wakati ili tuchunguze mafundisho hayo?

‘ACHA maua mia moja yachanue; acha vikundi vyenye mawazo tofauti mia moja vishindane.’ Usemi huo, uliofanywa maarufu na Mao Tse-tung wa Jamhuri ya Watu wa China katika hotuba moja mwaka 1956, kwa kweli ulikuwa ni kunukuu usemi ambao wasomi Wachina wametumia kueleza enzi katika China kuanzia karne ya tano mpaka ya tatu K.W.K., inayoitwa kipindi cha Wilaya Zenye Kupigana. Kufikia wakati huo nasaba ya kifalme ya Chou yenye nguvu (yapata 1122-256 K.W.K.) ilikuwa imezorota ikawa mfumo wa wilaya zenye kuzozana zisizo na muungano imara ambazo zilijitia katika vita yenye kuendelea, ikawa huzuni kubwa kwa watu wa kawaida.

2. (a) Ni nini kilichotokeza “vikundi vyenye mawazo tofauti mia moja”? (b) Ni nini kimesalia katika ukuzi huo wa “vikundi vyenye mawazo tofauti mia moja”?

2 Machafuko na mateso yaliyoletwa na vita hivyo yalidhoofisha sana mamlaka ya tabaka ya watawala wa kimila. Watu wa kawaida hawakuridhika tena na ufuataji wa msisimuko na hila za makabaila na kuvumilia matokeo yake wakiwa kimya. Kwa hiyo, mawazo na tamaa zilizokuwa zimekandamizwa kwa muda mrefu zilijitokeza kama kuchanua kwa “maua mia moja.” Vikundi vyenye mawazo tofauti viliendeleza mawazo yavyo juu ya serikali, sheria, utengemano wa kijamii, mwenendo, na maadili, na pia juu ya habari za kilimo, muziki, na fasihi, kuwa njia ya kurudisha ukawaida fulani katika maisha. Vikaja kuitwa “vikundi vyenye mawazo tofauti mia moja.” Vingi vyavyo havikutokeza matokeo ya kudumu. Hata hivyo, vikundi vyenye mawazo tofauti viwili vilipata umaarufu mkubwa hivi kwamba vimevuta maisha katika China kwa miaka zaidi ya 2,000. Ni vile ambavyo hatimaye vilikuja kuitwa Dini ya Tao na Dini ya Confucius.

Tao—Ni Nini?

3. (a) Ni nini wazo la Kichina juu ya Tao? (b) Badala ya Muumba, Wachina waliamini kisababishi cha vitu vyote ni nini? (Linganisha Waebrania 3:4.)

3 Ili kuelewa ni kwa nini Dini ya Tao (hutamkwa dao) na Dini ya Confucius zilikuja kuwa na uvutano mkubwa na wenye kudumu juu ya watu wa China, na pia juu ya wale wa Japan, Korea, na nchi nyinginezo jirani, ni lazima kuelewa kadiri fulani wazo la msingi la Kichina juu ya Tao. Neno lenyewe humaanisha “njia, barabara, au kijia.” Kwa kuongezea, laweza pia kumaanisha “mbinu, kanuni, au fundisho.” Kwa Wachina, upatano na utaratibu waliouona katika ulimwengu wote mzima ulikuwa ni udhihirisho wa Tao, namna fulani ya mapenzi ya kimungu au utungaji wa sheria uliopo katika ulimwengu wote mzima na unaouongoza. Kwa maneno mengine, badala ya kuamini katika Mungu Muumba, anayeongoza ulimwengu wote mzima, waliamini neema fulani, mapenzi fulani ya mbingu, au mbingu yenyewe tu kuwa kisababishi cha kila kitu.

4. Wachina walitumiaje wazo la Tao kwa mambo ya kibinadamu? (Linganisha Mithali 3:5, 6.)

4 Kwa kutumia wazo la Tao kwa mambo ya kibinadamu, Wachina waliamini kwamba kuna njia ya asili na iliyo sahihi ya kufanya kila kitu na kwamba kila kitu na kila mtu ana mahali pa kufaa na kazi ya kufaa. Kwa kielelezo, waliamini kwamba ikiwa mtawala alitimiza wajibu wake kwa kushughulika kihaki na watu na kushughulikia ibada za sherehe za kidhabihu zilizohusu mbingu, kungekuwako amani na fanaka kwa ajili ya taifa. Vivyo hivyo, ikiwa watu wangekuwa na nia ya kutafuta njia, au Tao, na kuifuata, kila jambo lingekuwa lenye upatano, amani, na lenye mafanikio. Lakini kama wangefanya kinyume au kukinza hilo, matokeo yangekuwa ni machafuko na msiba.

5. (a) Dini ya Tao hutwaa mwendo gani? (b) Dini ya Confucius hutwaa mwendo gani? (c) Ni maswali gani yanayohitaji kujibiwa?

5 Wazo hilo la kuambatana na Tao na kutoingiliana na mwendo wayo ni jambo la msingi la ufikirio wa kifalsafa na kidini wa Wachina. Yaweza kusemwa kwamba Dini ya Tao na Dini ya Confucius ni maonyesho mawili tofauti ya wazo lile lile moja. Dini ya Tao hutwaa mwendo wa kifumbo na, katika fani yao ya awali, inatetea kutotenda, ukimya, na kukaa tu, kuepuka jamii na kurudia asili. Wazo layo la msingi ni kwamba kila kitu kitakuwa sawa kama watu wataketi kitako, wasifanye lolote, na kuacha asili ijiendeshe. Kwa upande mwingine, Dini ya Confucius hutwaa mwendo wa utendaji. Hufundisha kwamba utengemano wa kijamii utadumishwa wakati kila mtu atimizapo fungu lake alilokusudiwa na kutimiza wajibu wake. Kwa sababu hiyo, huweka amri za kuongoza mahusiano yote ya kibinadamu na kijamii— kati ya mtawala na raia, baba na mwana, mume na mke, na kadhalika—na hutoa miongozo kwa wote. Hivyo hilo latokeza maswali yafuatayo: Mifumo hiyo miwili ilikujaje kuwapo? Waanzilishi walikuwa nani? Leo hufuatwaje? Nayo imetimiza nini kwa habari ya jitihada ya ainabinadamu kutafuta Mungu?

Dini ya Tao—Mwanzo wa Kifalsafa

6. (a) Ni nini kinachojulikana juu ya mwanzilishi wa Dini ya Tao? (b) Mwanzilishi wa Dini ya Tao alikujaje kujulikana kuwa Lao-tzu?

6 Katika hatua zayo za mapema, Dini ya Tao ilikuwa hasa falsafa kuliko kuwa dini. Mwanzilishi wayo, Lao-tzu, hakuridhika na machafuko na misukosuko ya nyakati hizo naye akatafuta kitulizo kwa kujiepusha na jamii na kurudia asili. Si mengi sana yanayojulikana juu ya mtu huyo, ambaye yasemekana aliishi katika karne ya sita K.W.K., ingawa hata hilo si hakika. Sana sana aliitwa Lao-tzu, maana yake “Bwana Mzee” au “Jamaa Mzee,” kwa sababu, kulingana na hekaya, mama yake mwenye mimba alimchukua kwa muda mrefu sana hivi kwamba alipozaliwa, nywele zake zilikuwa zimekwisha kuwa nyeupe.

7. Twajifunza nini juu ya Lao-tzu kutokana na “Maandishi ya Kihistoria”?

7 Maandishi rasmi pekee juu ya Lao-tzu yamo katika Shih Chi (Maandishi ya Kihistoria), ya Ssu-ma Chʹien, mwanahistoria wa barazani mwenye kuheshimika wa karne ya pili na ya kwanza K.W.K. Kulingana na chanzo hicho, jina halisi la Lao-tzu lilikuwa ni Li Erh. Alitumika akiwa karani katika majumba ya kifalme ya kuhifadhi maandishi ya kale katika Loyang, China ya kati. Lakini la maana zaidi, yanatoa simulizi hili juu ya Lao-tzu:

“Sehemu kubwa ya maisha yake Lao Tzu alikaa katika Chou. Alipoona kuzorota kwa Chou, aliondoka akaenda mpakani. Ofisa wa nyumba ya forodha Yin Hsi akasema: ‘Bwana, kwa kuwa inakupendeza kuondoka, nakuomba kwa niaba yangu uandike kitabu.’ Basi Lao Tzu akaandika kitabu chenye sehemu mbili kilicho na maneno elfu tano na zaidi, ambamo alizungumza mawazo ya ile Njia [Tao] na ile Nguvu [Te]. Kisha akaondoka. Hakuna anayejua alikofia.”

8. (a) Ni kitabu gani ambacho Lao-tzu husemekana kuwa alitokeza? (b) Kwa nini kitabu hicho chaweza kufasiriwa kwa njia nyingi tofauti?

8 Wasomi wengi hutilia shaka uasilia wa simulizi hilo. Vyovyote vile, kitabu kilichotungwa chaitwa Tao Te Ching (kwa ujumla hutafsiriwa “Kitabu Bora Sana cha Njia na Nguvu”) na huonwa kuwa maandishi makuu ya Dini ya Tao. Kimeandikwa kikiwa na beti fupi zenye mafumbo, baadhi yazo zikiwa na urefu wa maneno matatu au manne tu. Kwa sababu hiyo na kwa sababu maana ya herufi fulani imebadilika sana tangu wakati wa Lao-tzu, kitabu hicho chaweza kufasiriwa kwa njia nyingi tofauti-tofauti.

Kupata Ufahamu Mdogo Juu ya “Tao Te Ching”

9. Lao-tzu alielezaje juu ya Tao katika Tao Te Ching?

9 Katika Tao Te Ching, Lazo-tzu alifafanua juu ya Tao, njia iliyo upeo wa asili, akaihusisha na kila eneo la utendaji wa kibinadamu. Hapa twanukuu kutoka tafsiri ya kisasa ya Gia-fu Feng na Jane English ili kupata ufahamu mdogo juu ya Tao Te Ching. Kuhusu Tao, chasema yafuatayo:

“[Kulikuwako] kitu fulani kilichofanyizwa kifumbo,

Kilizaliwa kabla ya mbingu na dunia. . . .

Labda ndicho mama ya vitu kumi elfu.

Sijui jina lacho.

Kiite Tao.”—Sura 25.

“Vitu vyote hutoka kwa Tao.

Hulishwa na Wema [Te].

Hufanyizwa kutoka mata.

Hupewa umbo na mazingira.

Kwa hiyo vitu hivyo kumi elfu vyote huheshimu Tao

na kuheshimu Wema [Te].”—Sura 51.

10. (a) Kusudi la Dini ya Tao ni nini? (b) Maoni hayo ya Dini ya Tao hutumiwaje kwa mwenendo wa kibinadamu?

10 Twaweza kufikia maoni gani kutokana na aya hizo za kifumbo? Ya kwamba kwa wafuasi wa Tao, Tao ni kani fulani kubwa mno ya kifumbo ambayo ilitokeza ulimwengu unaoonekana. Lengo la Dini ya Tao ni jitihada ya kutafuta Tao hiyo, kuuacha ulimwengu, na kuwa na umoja na asili. Wazo hilo laonyeshwa pia katika maoni ya wafuasi wa Dini ya Tao juu ya mwenendo wa kibinadamu. Huu ni usemi juu ya wazo hilo katika Tao Te Ching:

“Afadhali kuacha upungufu kidogo kuliko kujaza pomoni.

Noa mno makali, na ncha itakuwa butu upesi.

Rundika ghala la dhahabu na yaspi, na hakuna anayeweza kuilinda.

Jipatie utajiri na nyadhifa, na msiba utafuata.

Staafu kazi ikiisha fanywa.

Hiyo ndiyo njia ya mbinguni.”—Sura 9.

11. Wazo la Dini ya Tao laweza kuelezwaje?

11 Vielelezo hivyo vichache vyaonyesha kwamba angalau hapo mwanzoni, kwa msingi Dini ya Tao ilikuwa kikundi chenye mawazo tofauti ya falsafa. Kutokana na ukosefu wa haki, kuteseka, kuangamizwa, na ubatili uliotokana na utawala wa ukatili wa mfumo wenye kuzozana wa wakati huo, wafuasi wa Tao waliamini kwamba njia ya kupata amani na upatano ilikuwa ni kurudia mila za wakale kabla hakujawa wafalme na mawaziri waliopiga ubwana juu ya watu wa kawaida. Wazo lao lilikuwa ni kuishi maisha ya utulivu, ya mashambani, kwa kuungana na asili.—Mithali 28:15; 29:2.

Mwenye Hekima wa Pili wa Dini ya Tao

12. (a) Chuang Chou alikuwa nani? (b) Aliongeza nini kwenye mafundisho ya awali ya Lao-tzu?

12 Falsafa ya Lao-tzu ilisogezwa hatua moja mbele na Chuang Chou, au Chuang-tzu, maana yake “Bwana Chuang” (369-286 K.W.K.), ambaye alionwa kuwa ndiye mwandamizi mashuhuri zaidi wa Lao-tzu. Katika kitabu chake, Chuang Tzu, hakufafanua juu ya Tao tu bali pia alifafanua juu ya mawazo ya yin na yang, ambayo kwanza yalitokezwa katika I Ching. (Ona ukurasa 83.) Kwa maoni yake, hakuna kitu cha kudumu hasa wala kilicho kamili, bali kila kitu kimo katika hali ya kubadilika-badilika kati ya pande mbili zilizo kinyume. Katika sura “Furiko la Vuli,” aliandika hivi:

“Hakuna chochote katika ulimwengu kilicho cha kudumu, kwa kuwa kila kitu kinaishi muda wa kutosha tu kije kife. Tao pekee, ikiwa haina mwanzo wala mwisho, ndiyo hudumu milele. . . . Maisha yaweza kufananishwa na farasi mwenye kasi akienda mbio kabisa—hubadilika daima na wakati wote, kwa kila kisehemu cha sekunde. Ufanye nini? Usifanye nini? Kwa kweli ni mamoja tu.”

13. (a) Kwa ufafanuzi wa Chuang-tzu, ni nini maoni ya Dini ya Tao juu ya maisha? (b) Ni ndoto gani ya Chuang-tzu inayokumbukwa zaidi?

13 Kwa sababu ya falsafa hiyo ya kutotenda, maoni ya mfuasi wa Dini ya Tao ni kwamba hakuna haja mtu yeyote afanye lolote la kuingiliana na yale ambayo asili imeyatia mwendoni. Punde si punde, kila kitu kitarudia kinyume chalo. Hata hali iwe isiyovumilika kadiri gani, karibuni itakuwa afadhali. Hata hali iwe yenye kupendeza jinsi gani, karibuni itakwisha. (Kwa kutofautisha, ona Mhubiri 5:18, 19.) Maoni hayo ya kifalsafa juu ya maisha yaonyeshwa katika ndoto ya Chuang-tzu ambayo ndiyo inayofanya watu wa kawaida wamkumbuke zaidi:

“Safari moja Chuang Chou aliota akiwa kipepeo, kipepeo anayeruka na kupiga-piga mabawa, akijifurahia na kufanya apendavyo. Hakujua alikuwa ndiye Chuang Chou. Ghafula akaamka na kumbe, akajikuta akiwa Chuang Chou halisi mwenyewe. Lakini yeye hakujua kama alikuwa Chuang Chou ambaye alikuwa ameota akiwa kipepeo, au kipepeo mwenye kuota akiwa Chuang Chou.”

14. Uvutano wa Dini ya Tao waonekana wazi katika nyanja gani?

14 Uvutano wa falsafa hiyo huonekana katika mtindo wa ushairi na usawiri uliositawishwa na wasanii Wachina wa vizazi vya baadaye. (Ona ukurasa 171.) Hata hivyo, Dini ya Tao, haingeendelea kwa muda mrefu kuwa falsafa ya kutotenda tu.

Kutoka Kwenye Falsafa Kuwa Dini

15. (a) Kuvutiwa na asili kuliongoza wafuasi wa Dini ya Tao kwenye wazo gani? (b) Ni taarifa gani katika Tao Te Ching zilizochangia wazo hilo?

15 Katika jitihada yao ya kuwa na umoja pamoja na asili, wafuasi wa Tao walijishughulisha mno na uwezo wa mwili wa kutozeeka na wa kujiponya. Walikisia kwamba labda kwa kuishi kwa kupatana na Tao, au njia ya asili, mtu angeweza kwa njia fulani kujua siri za asili na apate kinga kutokana na dhara la kimwili, maradhi, na hata kifo. Ingawa Lao-tzu hakufuatia hilo kuwa suala kubwa, aya katika Tao Te Ching zilielekea kudokeza wazo hilo. Kwa kielelezo, sura ya 16 inasema: “Kuwa na umoja na Tao ni kwa milele. Na ingawa mwili hufa, Tao haitakufa kamwe.”a

16. Maandishi ya Chuang-tzu yaliongezeaje imani za Dini ya Tao za kimizungu?

16 Chuang-tzu pia alichangia makisio hayo. Kwa kielelezo, katika mazungumzo yaliyo katika Chuang Tzu, jamaa fulani wa kingano aliuliza mwingine, “Wewe una umri mkubwa, na hali una sura ya mtoto. Ikawaje hivyo?” Yule wa pili akajibu: “Nimejifunza Tao.” Kuhusu mwanafalsafa mwingine mfuasi wa Dini ya Tao, Chuang-tzu aliandika: “Basi Liehtse angeweza kuruka na upepo. Akiruka kwa furaha katika pepezi baridi, yeye angeenda hivyo kwa siku kumi na tano kabla ya kurudi. Kati ya wanadamu wanaofikia furaha, mwanadamu wa jinsi hiyo ni vigumu kupatikana.”

17. Ni mazoea gani ya Dini ya Tao yaliyotokezwa na udhanifu mwingi wa mapema, na matokeo yalikuwa nini? (Linganisha Warumi 6:23; 8:6, 13.)

17 Hadithi kama hizo zilichochea mawazo ya wafuasi wa Dini ya Tao, nao wakaanza kufanya jaribio la kutafakari, kula vyakula fulani tu, na mazoezi ya kupumua ambayo yalidhaniwa yangeweza kuahirisha kuchakaa kwa mwili na kifo. Upesi, hadithi za kimapokeo zikaanza kusambaa kuhusu watu wasioweza kufa ambao wangeweza kuruka kwenye mawingu na kutokea na kutoweka wapendavyo, ambao waliishi juu ya milima mitakatifu au visiwa vya mbali kwa miaka isiyohesabika wakila umande au matunda ya kimwujiza. Historia ya Kichina huripoti kwamba katika 219 K.W.K., maliki wa Ch’in, Shih Huang-Ti, alipeleka msafara wa meli zenye wavulana na wasichana 3,000 wakatafute kisiwa P’eng-lai cha kihekaya, kilichokuwa makao ya wasioweza kufa, ili wakalete dawa ya mti-shamba ya hali ya kutoweza kufa. Kwa wazi, hawakurudi na maponya hayo ya kurefusha maisha, lakini mapokeo yanasema kwamba wakawa wakaaji wa visiwa vilivyokuja kuitwa Japan.

18. (a) Ni nini msingi wa wazo la Dini ya Tao juu ya ‘vidonge vya kutoweza kufa’? (b) Ni mazoea gani mengine ya kimizungu yaliyositawishwa na Dini ya Tao?

18 Wakati wa nasaba ya kifalme ya Han (206 K.W.K.-220 W.K.), mazoea ya kimizungu ya Dini ya Tao yalifikia kilele kipya. Ilisemwa kwamba Maliki Wu Ti, ingawa alidhamini Dini ya Confucius kuwa fundisho rasmi la Serikali, alivutiwa sana na wazo la Dini ya Tao la kutokufa kwa mwili. Hasa alivutiwa sana na kufanyiza mchanganyo wa ‘vidonge vya kutoweza kufa’ kupitia alkemia. Kwa maoni ya Dini ya Tao, uhai hutokea wakati zile kani zenye kupingana yin na yang (kike na kiume) zinapoungana. Kwa hiyo, kwa kuunganisha risasi (nyeusi, au yin) na zebaki (nyangavu, au yang), wataalamu hao wa alkemia walikuwa wanaigiza utaratibu wa asili, na matokeo ya hilo, walidhani, yangekuwa ni kidonge chenye kupatia hali ya kutoweza kufa. Wafuasi wa Tao pia walisitawisha mazoezi kama ya Yoga, mbinu za kudhibiti kupumua, vizuizi vya kula vyakula fulani tu, na mazoea ya ngono yaliyoaminiwa kuwa hutia nguvu nishati-uhai ya mtu na kurefusha maisha ya mtu. Vifaa vyao vilitia ndani talasimu za mizungu zilizosemekana humfanya mtu asionekane na asiyeweza kudhuriwa na silaha au zenye kuwezesha mtu atembee juu ya maji au kuruka angani. Pia walikuwa na mihuri ya kimizungu, kwa kawaida ikiwa na alama ya yin-yang, iliyopandikizwa juu ya majengo na juu ya milango ili kuzuia roho waovu na hayawani-mwitu.

19. Dini ya Tao ilikujaje kuwa tengenezo?

19 Kufikia karne ya pili W.K., Dini ya Tao ikawa tengenezo. Jamaa fulani aitawaye Chang Ling, au Chang Tao-ling, alianzisha jamii ya siri ya Dini ya Tao katika magharibi ya China na akawa akifanya maponyo ya kimizungu na alkemia. Kwa sababu kila mshiriki alitozwa ada ya vipimo vitano vya mchele, chama chake kikaja kujulikana kuwa Dini ya Tao ya Vipimo-Vitano-vya-Mchele (wu-tou-mi tao). Akidai kwamba alipokea ufunuo wa kibinafsi kutoka kwa Lao-tzu, Chang akawa “bwana wa kimbingu” wa kwanza. Hatimaye, ilisemekana kwamba alifaulu kutengeneza maponya ya kurefusha uhai na kupaa mbinguni akiwa hai, amepanda simba-milia, kutoka Mlima Lung-hu (Mlima Drakoni-Simba-Milia) katika Mkoa wa Kiangsi. Chang Tao-ling alianzisha uandamizi wa karne nyingi wa “mabwana wa kimbingu” wa Dini ya Tao, kila mmoja akisemwa kuwa ni Chang aliyezaliwa katika umbo jipya.

Kukabili Tisho la Dini ya Buddha

20. Dini ya Tao ilijaribuje kushinda uvutano wa Dini ya Buddha?

20 Kufikia karne ya saba, wakati wa nasaba ya kifalme ya T’ang (618-907 W.K.), Dini ya Buddha ilikuwa ikijipenyeza katika maisha ya kidini ya Uchina. Ili kuzuia hilo, Dini ya Tao ilijidhamini kuwa dini ambayo mizizi yayo ni China. Lao-tzu alifanywa kuwa kijimungu, na maandishi ya Dini ya Tao yakakubaliwa kuwa maandishi rasmi ya kidini. Mahekalu, makao ya watawa, na makao ya watawa wa kiume na wa kike yalianzishwa, na vyeo vya watawa wa kiume na wa kike vikaanzishwa kwa kufuatia hasa mtindo wa Dini ya Buddha. Kuongezea hayo, Dini ya Tao iliingiza katika jamii yayo ya vijimungu, vijimungu-vike, mazimwi, na wasioweza kufa wa hadithi za Kichina, kama vile wale Wanane Wasiokufa (Pa Hsien), kijimungu cha meko (Tsao Shen), jiji la vijimungu (Ch’eng Huang), na walinzi wa mlango (Men Shen). Matokeo yakawa ni mchanganyiko wa sehemu za Dini ya Buddha, imani za ushirikina wa kimapokeo, uasiliani-roho, na ibada ya wazazi wa kale waliokufa.—1 Wakorintho 8:5.

21. Hatimaye, Dini ya Tao ilijigeuza kuwa nini, na jinsi gani?

21 Wakati ulivyozidi kupita, Dini ya Tao ilizorota polepole ikawa mfumo wa ibada ya sanamu na imani ya kishirikina. Kila mtu aliabudu vijimungu na vijimungu-vike alivyopenda zaidi kwenye mahekalu ya kwao, akiviomba vimlinde na uovu na kumpa msaada apate utajiri wa kidunia. Kwa kulipwa, makuhani waliongoza maziko; wakachagua mahali pa kufaa makaburi, nyumba, na biashara; wakawasiliana na wafu; wakazuia roho waovu na mizuka; wakaendesha sherehe za sikukuu; na kuendesha ibada nyingine za sherehe ndogo-ndogo. Kwa njia hiyo, kilichoanza kama kikundi chenye mawazo tofauti ya falsafa ya kifumbo kikawa kimebadilika sura kuwa dini iliyozama ndani ya tope la kuamini roho zisizoweza kufa, moto wa helo (mateso), vijimungu-binadamu—mawazo yaliyotolewa kutoka dimbwi la maji tuli ya imani za uwongo za Babuloni ya kale.

Mwenye Hekima Mwingine Mashuhuri wa China

22. Ni kikundi kipi chenye mawazo tofauti kilichopata kutawala katika China, na ni maswali gani tunayohitaji kufikiria?

22 Ijapokuwa tumefuatia kutokea, kusitawi, na kuzorota kwa Dini ya Tao, twapaswa kukumbuka kwamba hiyo ilikuwa moja tu ya “vikundi vyenye mawazo tofauti mia moja” vilivyovuvumuka katika China wakati wa kipindi cha Mikoa Yenye Kupigana. Kikundi chenye mawazo tofauti kingine ambacho hatimaye kilikuja kuwa mashuhuri, kwa kweli, chenye uvutano kuliko vyote, kilikuwa ni Dini ya Confucius. Lakini ni kwa nini Dini ya Confucius ikaja kuwa mashuhuri hivyo? Kati ya wenye hekima wote Wachina, Confucius bila shaka ndiye anayejulikana zaidi nje ya China, lakini kwa kweli yeye alikuwa nani? Naye alifundisha nini?

23. Ni habari gani za kibinafsi kuhusu Confucius zinazotolewa katika “Maandishi ya Kihistoria”?

23 Kuhusu Confucius, kwa mara nyingine twageukia Shih Chi (Maandishi ya Kihistoria) ya Ssu-ma Ch’ien. Tofauti na maandishi machache juu ya Lao-tzu, kuna wasifu mrefu wa Confucius. Hizi ni baadhi ya habari za kibinafsi za kirefu zilizonukuliwa kutoka tafsiri ya msomi Mchina Lin Yutang:

“Confucius alizaliwa katika mji wa Tsou, katika tarafa ya Ch’angping, katika nchi ya Lu. . . . [Mama yake] alisali kwenye kilima Nich’iu na alimzaa Confucius likiwa ni jibu kwa sala yake, katika mwaka wa ishirini na mbili wa Kiongozi Hsiang wa Lu (551 K.K.). Kulikuwako uvimbe wenye kutokeza juu ya kichwa chake alipozaliwa, na ndiyo sababu akaitwa ‘Ch’iu’ (maana yake “kilima”). Jina lake la kiusomi lilikuwa Chungni, na jina lake la ukoo lilikuwa K’ung.”b

24. Ni nini kilichotukia katika maisha ya mapema ya Confucius?

24 Muda mfupi baada ya kuzaliwa kwake, baba yake alikufa, lakini mama yake, ajapokuwa maskini, aliweza kumfanyia mpango wa elimu ya kufaa. Mvulana huyo alipendezwa sana na historia, mashairi, na muziki. Kulingana na The Analects, kimoja cha Four Books vya Dini ya Confucius, yeye alijishughulisha na uchunguzi wa kiusomi alipofika miaka 15. Akiwa na miaka 17, alipewa wadhifa wa chini wa kiserikali katika wilaya alikozaliwa ya Lu.

25. Kifo cha mama ya Confucius kilimwathirije? (Linganisha Mhubiri 9:5, 6; Yohana 11:33, 35.)

25 Hali yake ya kifedha yaonekana ilipata nafuu, hata akaoa akiwa na miaka 19 na mwaka uliofuata akapata mwana. Hata hivyo, akiwa katikati ya miaka yake ya 20, mama yake alikufa. Kwa wazi hilo lilimwathiri sana. Akiwa mfuataji mwangalifu sana wa mapokeo ya kale, Confucius alijitenga na maisha ya hadharani akaomboleza mama yake kwenye kaburi lake kwa miezi 27, kwa njia hiyo akiwapa Wachina kielelezo bora cha kuheshimu sana wazazi.

Confucius Mwalimu

26. Confucius alitwaa kazi gani baada ya kifo cha mama yake?

26 Baada ya hapo, yeye aliacha familia yake na akatwaa kazi ya mwalimu mwenye kutanga-tanga. Masomo aliyofunza ni pamoja na muziki, mashairi, fasihi, mashauri ya kiserikali, adili, na sayansi, au kadiri yayo iliyokuwapo wakati huo. Lazima iwe alijitengenezea jina kweli kweli wakati huo, kwa maana ilisemwa kwamba wakati fulani mmoja alikuwa na wanafunzi wengi kufikia 3,000.

27. Ni nini kinachojulikana juu ya Confucius akiwa mwalimu? (Linganisha Mathayo 6:26, 28; 9:16, 17; Luka 12:54-57; Yohana 4:35-38.)

27 Katika Mashariki, Confucius huheshimiwa mno hasa kuwa mwalimu stadi. Kwa kweli maneno ya kumbukumbu kwenye kaburi lake katika Ch’ü-fou, Mkoa wa Shantung, yamwita “Mwalimu wa Kale, Aliye Mtakatifu Zaidi.” Mwandikaji mmoja wa Magharibi aeleza njia yake ya kufundisha hivi: “Alitembea-tembea kutoka ‘hapa mpaka pale akiambatana na wale waliokuwa wakitwaa maoni yake juu ya maisha.’ Wakati wowote safari ilipowachukua umbali fulani yeye alipanda gari la kukokotwa na ng’ombe. Mwendo wa polepole wa mnyama huyo uliwezesha wanafunzi wake wafuate kwa mguu, na ni wazi kwamba habari ya hotuba zake mara nyingi ilitegemea matukio yaliyotokea barabarani.” Kwa kupendeza, Yesu, wakati wa tarehe ya baadaye, na bila kuongozwa na mambo ya mtu mwingine, alitumia njia kama hiyo.

28. Kulingana na mwandikaji Mchina Lin Yutang, ni nini kilichomfanya Confucius kuwa mwalimu mwenye kuheshimiwa?

28 Bila shaka, kilichomfanya Confucius awe mwalimu mwenye kuheshimiwa kati ya watu wa Mashariki, ni uhakika wa kwamba yeye mwenyewe alikuwa mwanafunzi mzuri, hasa wa historia na maadili. “Watu walivutwa kwake Confucius, hasa si kwa sababu yeye alikuwa binadamu mwenye hekima zaidi wa wakati huo, bali kwa sababu hasa alikuwa msomi mwenye elimu zaidi, wa pekee katika siku yake ambaye angeweza kuwafundisha juu ya vitabu vya kale na usomi wa kale,” akaandika Lin Yutang. Akitaja upendo huo wa kujifunza kuwa labda ndiyo sababu kuu ya Dini ya Confucius kushinda vile vikundi vingine vyenye mawazo tofauti, Lin alitoa muhtasari wa jambo hilo kwa njia hii: “Walimu wa Dini ya Confucius walikuwa na jambo la waziwazi la kufundisha na wanafunzi wa Dini ya Confucius walikuwa na jambo la waziwazi la kujifunza, yaani, kujifunza historia, hali vikundi vile vingine vyenye mawazo tofauti vililazimika kusema tu maoni yavyo vyenyewe.”

“Mbingu Ndizo Zanijua Mimi!”

29. (a) Lengo halisi maishani mwa Confucius lilikuwa nini? (b) Yeye alijaribuje kufikia lengo lake, na matokeo yakawa nini?

29 Ingawa alifanikiwa akiwa mwalimu, Confucius hakuuona ualimu kuwa kazi yake ya maisha. Yeye alihisi kwamba mawazo yake juu ya mwenendo unaofaa na maadili ungeweza kuokoa ulimwengu wenye matata wa siku yake kama tu watawala wangefuata hayo kwa kumwajiri yeye au wanafunzi wake katika serikali zao. Kwa sababu hiyo, yeye na kikundi kidogo cha wanafunzi wake wa karibu zaidi waliondoka katika wilaya ya Lu alikozaliwa wakaenda wakisafiri kutoka wilaya mpaka wilaya nyingine wakijaribu kutafuta mtawala mwenye hekima ambaye angeweza kufuata mawazo yake juu ya serikali na utengemano wa kijamii. Matokeo yalikuwa nini? Shih Chi hutoa taarifa hii: “Hatimaye akaondoka Lu, akaachwa katika Ch’i, akafukuzwa kutoka Sung na Wei, akapatwa na uhitaji kati ya Ch’en na Ts’ai.” Baada ya miaka 14 akiwa safarini, alirudi Lu, akiwa amekata tamaa lakini hajashindwa.

30. Ni vitabu gani vya fasihi vinavyofanyiza msingi wa Dini ya Confucius?

30 Kwa siku zake zilizosalia, yeye alijitoa kwa kazi ya kuandika vitabu na kufundisha. (Ona kisanduku, ukurasa 177.) Ingawa bila shaka aliomboleza kuwa hakutambuliwa, yeye alisema: “Mimi sinung’unikii Mbingu. Silalamiki juu ya binadamu. Nafuatia mafunzo yangu hapa duniani, nami nawasiliana na Mbingu juu. Mbingu ndizo zanijua mimi!” Hatimaye, katika mwaka 479 K.W.K., alikufa akiwa na miaka 73.

Kiini cha Mawazo ya Dini ya Confucius

31. Ni nini alichofundisha Confucius kuwa ndiyo njia ya kufikia utengemano wa jamii?

31 Ijapokuwa Confucius alitia fora akiwa msomi na akiwa mwalimu, uvutano wake haukuongoza nyanja za wasomi tu. Kwa kweli, lengo la Confucius halikuwa kufundisha amri za mwenendo au adili tu bali pia kurudisha amani na utengemano katika jamii, ambayo, wakati huo, ilikuwa imefarakanishwa na vita vya daima kati ya mabwana wenye kuzozana. Ili kutimiza mradi huo, Confucius alifundisha kwamba kila mtu, tangu maliki mpaka kabwela, lazima ajifunze daraka alilotazamiwa kutimiza katika jamii na kuishi kulingana nalo.

32, 33. (a) Wazo la Dini ya Confucius la li lilikuwa nini? (b) Kulingana na Confucius, matokeo ya kuzoea li yangekuwa nini?

32 Katika Dini ya Confucius wazo hilo lajulikana kama li, maana yake ufaaji, uungwana, utaratibu wa mambo, na, kwa kuongezea, ibada ya sherehe, sherehe, na utawa. Katika kujibu swali, “Hii li kuu ni nini?” Confucius alitoa maelezo yafuatayo:

“Kati ya mambo yote ambayo watu huishi kulingana nayo, li ndilo kuu zaidi. Bila li, hatujui jinsi ya kuendesha ibada inayofaa ya roho za ulimwengu wote; au jinsi ya kuweka wadhifa unaofaa wa mfalme na mawaziri, mtawala na wanaotawalwa, na wazee na wadogo wao; au jinsi ya kuweka uhusiano wa kiadili kati ya jinsia, kati ya wazazi na watoto na kati ya akina ndugu; au jinsi ya kutofautisha viwango tofauti-tofauti vya uhusiano katika familia. Ndiyo sababu muungwana huiheshimu sana li.”

33 Kwa hiyo, li ndiyo amri ya mwenendo ambao kwao muungwana wa kweli (chün-tzu, nyakati nyingine hutafsiriwa “binadamu wa ngazi ya juu”) hutimiza uhusiano wake wote wa kijumuiya. Kila mtu anapojitahidi kufanya hivyo, “kila jambo linakuwa sawa katika familia, serikalini na ulimwenguni,” akasema Confucius, na hapo ndipo Tao, au njia ya mbingu, inafanyika. Lakini li ifuatweje? Hilo latuleta kwenye jingine la mawazo makuu ya Dini ya Confucius—jen (hutamkwa ren), hisani ya ubinadamu au kuwa na moyo wa kibinadamu.

34. Ni nini wazo la Dini ya Confucius juu ya jen, na ni jinsi gani linasaidia katika kushughulika na matatizo ya kijamii?

34 Ingawa li hukazia kizuizi kwa amri za nje-nje, jen hushughulika na asili ya kibinadamu, au yule mtu wa ndani. Wazo la Dini ya Confucius, hasa kama linavyoelezwa na mwanafunzi mkuu wa Confucius, Mencius, ni kwamba kwa msingi asili ya binadamu ni nzuri. Kwa hiyo, utatuzi wa matatizo yote ya kijamii wategemea kujisitawisha mwenyewe, na mwanzo wa hilo ni elimu na maarifa. Sura ya kufungua ya The Great Learning husema:

“Maarifa ya kweli yanapopatikana, ndipo nia inapokuwa ya moyo mweupe; nia inapokuwa ya moyo mweupe, ndipo moyo unanyooka sawasawa . . . ; moyo unaponyooka sawasawa, ndipo maisha ya kibinafsi yanapositawishwa; wakati maisha ya kibinafsi yanapositawishwa, ndipo maisha ya familia yanapoongozeka; maisha ya familia yanapoongozeka, ndipo maisha ya kitaifa yanapokuwa yenye utengemano; na maisha ya kitaifa yanapokuwa yenye utengemano, ndipo kunapokuwa amani katika ulimwengu huu. Tangu maliki kwenda chini kwa makabwela, lazima wote waheshimu usitawishaji wa maisha ya kibinafsi kuwa kiini au msingi.”

35. (a) Kanuni za li na jen zaweza kuelezwaje kwa muhtasari? (b) Yote hayo yaonyeshwaje katika maoni ya Kichina juu ya maisha?

35 Kwa hiyo, twaona kwamba kulingana na Dini ya Confucius, kushika li kutawezesha watu wawe na adabu nzuri katika kila hali, na kusitawisha jen kutawafanya watendee kila mtu mwingineye yote kwa fadhili. Matokeo, kinadharia, ni amani na upatano katika jamii. Wazo la Dini ya Confucius, likitegemea kanuni za li na jen, laweza kusemwa kwa muhtasari kwa njia hii:

“Fadhili katika baba, heshima ya mwana kwa wazazi

Uungwana wa ndugu mkubwa, unyenyekevu na heshima katika aliye mdogo

Tabia ya uadilifu katika mume, utii katika mke

Ufikirio wa hisani ya kibinadamu katika wazee, staha katika wadogo

Utendaji mema katika watawala, uaminifu-mshikamanifu katika mawaziri na raia.”

Yote hayo yasaidia kuonyesha ni kwa nini Wachina walio wengi, na hata watu wengine wa Mashariki, hukazia sana vifungo vya familia, kuwa wenye bidii ya kazi, elimu, na mtu kujua cheo kimpasacho na kutenda kulingana nacho. Kwa uzuri au kwa ubaya, mawazo hayo ya Dini ya Confucius yamekazwa kikiki katika fahamu za Wachina kupitia karne nyingi za kufundishwa.

Dini ya Confucius Ikawa Kidhehebu cha Serikali

36. Dini ya Confucius ilipataje hali ya kuwa kidhehebu cha Serikali?

36 Dini ya Confucius ilipotokea, muhula wa vile “vikundi vyenye mawazo tofauti mia moja” ulifikia kikomo. Wamaliki wa nasaba ya Han waligundua katika fundisho la Dini ya Confucius la uaminifu-mshikamanifu kwa mtawala utaratibu ule waliohitaji ili kuimarisha nguvu za kiti cha enzi. Chini ya Maliki Wu Ti, ambaye tumekwisha rejezea kuhusiana na Dini ya Tao, Dini ya Confucius ilikwezwa hali ya kuwa kidhehebu cha Serikali. Ni wale tu waliozoeleana na kanuni za Dini ya Confucius ndio waliochaguliwa kuwa maofisa wa Serikali, na mtu yeyote aliyetumaini kuingia katika utumishi wa serikali alipaswa kupita mitihani ya taifa lote iliyotegemea kanuni za Dini ya Confucius. Sherehe na ibada za Dini ya Confucius zikawa dini ya nyumba ya kifalme.

37. (a) Dini ya Confucius ilipataje kuwa dini? (b) Ni kwa nini, hasa, Dini ya Confucius ni zaidi ya falsafa tu?

37 Badiliko hilo la matukio lilisaidia sana kukweza daraja la Confucius katika jumuiya ya Wachina. Wamaliki wa Han walianzisha pokeo la kutoa sadaka kwenye kaburi la Confucius. Alitunukwa wadhifa wa heshima. Halafu, katika 630 W.K., maliki wa T’ang, T’ai Tsung akaagiza kwamba hekalu la Serikali kwa ajili ya Confucius lijengwe katika kila mkoa na tarafa katika milki yote na kwamba sadaka zitolewe kwa ukawaida. Kwa sababu zote hizo za kujifaidi, Confucius alikwezwa kufikia daraja la kuwa kijimungu, na Dini ya Confucius ikawa dini ambayo si rahisi kuitofautisha na Dini ya Tao au Dini ya Buddha.—Ona kisanduku, ukurasa 175.

Urithi wa Hekima ya Mashariki

38. (a) Dini ya Tao na Dini ya Confucius zimepatwa na nini tangu 1911? (b) Lakini ingali ikoje kwa mawazo ya msingi ya dini hizo?

38 Tangu mwisho wa utawala wa kinasaba katika China mwaka 1911, Dini ya Confucius na Dini ya Tao zimelaumiwa sana, hata kuteswa. Dini ya Tao iliharibiwa sifa kwa sababu ya mazoea yayo ya kimizungu na kishirikina. Na Dini ya Confucius imebandikwa jina la kuwa ya kuzozana, ikidhamini akili ya utumwa ili kuweka watu, hasa wanawake, chini ya unyenyekeo. Hata hivyo, zijapokuwa laana hizo, mawazo ya msingi ya dini hizo yametia mizizi ya kina kirefu katika akili ya Wachina hivi kwamba yangali yanavuta sana walio wengi.

39. Ripoti moja ya habari yasema nini juu ya mazoea ya kishirikina ya kidini katika China?

39 Kwa kielelezo, chini ya kichwa cha habari “Desturi za Kidini za Wachina ni Chache Katika Beijing lakini Zinasitawi Katika Mikoa ya Pwani,” gazeti la Canada Globe and Mail liliripoti katika 1987 kwamba baada ya miaka karibu 40 ya utawala wa kiatheisti katika China, desturi za maziko, ibada za hekaluni, na mazoea mengi ya kishirikina yangali kawaida katika maeneo ya mashambani. “Vijiji vilivyo vingi vina mwanamume fengshui, ambaye kwa kawaida ni mkazi mwenye umri mkubwa anayejua jinsi ya kusoma kani za upepo (feng) na maji (shui) ili kuamua mahali panapofaa zaidi kwa ajili ya kila kitu kuanzia kaburi la wazazi wa kale waliokufa, nyumba mpya au fanicha za sebuleni,” yasema ripoti hiyo.

40. Ni mazoea gani ya kidini yanayoonekana katika Taiwan?

40 Kwingine, Dini ya Tao na Dini ya Confucius hupatikana kokote ambako tamaduni za kimapokeo za Kichina zingaliko. Katika Taiwan, mwanamume mmoja anayedai kuwa mzao wa Chang Tao-ling husimamia akiwa “kiongozi wa kimbingu” mwenye uwezo wa kuteua makuhani wa Dini ya Tao (Tao Shih). Kijimungu-kike maarufu, Matsu, kiitwacho “Mama Mtakatifu Katika Mbingu,” huabudiwa kuwa mtakatifu mfadhili wa kisiwa na wa mabaharia na wavuvi. Kwa habari ya makabwela, sana sana hujishughulisha na kutoa matoleo na sadaka kwa roho za mito, milima, na nyota; vijimungu vya kufadhili biashara zote; na vijimungu vya afya, bahati njema, na afya njema?c

41. Dini ya Confucius huendeshwaje leo?

41 Vipi juu ya Dini ya Confucius? Imepunguziwa cheo cha dini ikawa kumbukumbu ya kitaifa tu. Katika China kule Ch’ü-fou, mahali alipozaliwa Confucius, Serikali inatunza Hekalu la Confucius na ardhi ya familia kama vivutia-watalii. Huko, kulingana na jarida China Reconstructs, maonyesho yanafanywa “yanayoonyesha tamasha ya ibada ya sherehe kwa ajili ya Confucius.” Na katika Singapore, Taiwan, Hong Kong, na sehemu nyinginezo katika Asia ya Mashariki, watu wangali wanasherehekea siku ya kuzaliwa kwa Confucius.

42. Dini ya Tao na Dini ya Confucius hupungukiwaje kuwa viongozo katika jitihada ya kutafuta Mungu?

42 Katika Dini ya Confucius na Dini ya Tao, twaona jinsi mfumo unaotegemea hekima na kusababu kwa kibinadamu, hata uwe wa kiakili na wenye kusudi zuri jinsi gani unavyopungukiwa katika jitihada ya kutafuta Mungu wa kweli. Kwa nini? Kwa sababu unaacha jambo moja la lazima, yaani, mapenzi na matakwa ya Mungu mwenye utu. Dini ya Confucius hugeukia asili ya kibinadamu kuwa kani yenye kuchochea ili kufanya mema, na Dini ya Tao hugeukia asili yenyewe. Lakini huo ni uhakika uliowekwa mahali pasipofaa kwa sababu kwa ujumla huko ni kuabudu vitu vilivyoumbwa badala ya Muumba.—Zaburi 62:9; 146:3, 4; Yeremia 17:5.

43. Mapokeo ya kidini ya Wachina yamewazuiaje kwa ujumla katika jitihada ya kutafuta Mungu wa kweli?

43 Kwa upande mwingine, mapokeo ya ibada ya wazazi wa kale waliokufa na sanamu, kuwa na kicho kwa mbingu ya anga, na kuheshimu mno mizimu, na pia sherehe na ibada za sherehe zinazokamatana na mambo hayo, zimetia mizizi yenye kina kirefu katika njia ya kufikiri ya Kichina hata kwamba hayo hukubaliwa kuwa ukweli ambao haujatajwa wazi. Mara nyingi ni vigumu sana kuongea na Mchina juu ya Mungu au Muumba mwenye utu kwa sababu wazo hilo ni geni sana kwake.—Warumi 1:20-25.

44. (a) Akili zenye kusababu zaitikiaje ajabu za njia ya asili? (b) Sisi twatiwa moyo tufanye nini?

44 Ni jambo lisilokanushika kwamba asili imejaa maajabu makubwa na hekima na kwamba sisi binadamu tumetuzwa uwezo mzuri ajabu wa akili ya kusababu na dhamiri. Lakini kama ilivyotajwa katika sura juu ya Dini ya Buddha, maajabu tunayoona katika ulimwengu wa asili yamefanya akili zenye kufikiri zikate maneno kwamba lazima kuwe Mbuni au Muumba. (Ona kurasa 151-2.) Basi, ikiwa ndivyo ilivyo, je! si jambo la akili kwamba twapaswa kujitahidi kutafuta Muumba? Kwa kweli Muumba atualika tufanye hivyo: “Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina.” (Isaya 40:26) Kwa kufanya hivyo, tutapata kujua Muumba ni nani, yaani Yehova Mungu, na pia mambo aliyotuwekea kwa ajili ya wakati ujao.

45. Ni dini gani nyingine ya Mashariki tutakayochunguza halafu?

45 Pamoja na Dini ya Buddha, Dini ya Confucius, na Dini ya Tao, ambazo zimekuwa na daraka kubwa katika maisha ya kidini ya watu wa Mashariki, kuna dini nyingine, iliyo maalumu kwa watu wa Japan—Dini ya Shinto. Hiyo ni tofauti jinsi gani? Chanzo chayo ni nini? Je! imeongoza watu kwa Mungu wa kweli? Tutachunguza hilo katika sura inayofuata.

[Maelezo ya Chini]

a Tafsiri ya Lin Yutang ya aya hii yasomwa hivi: “Kuwa na upatano na Tao, ni kwa milele, na uhai wake wote huhifadhiwa usipatwe na dhara.”

b Neno “Confucius” ni utohozi wa Kilatini wa K’ung-fu-tzu la Kichina, maana yake “K’ung aliye Bwana.” Makasisi Wayesuiti waliokuja China katika karne ya 16 walibuni jina hilo la Kilatini walipopendekeza kwa papa wa Roma kwamba Confucius afanywe “mtakatifu” wa Kanisa la Roma Katoliki.

c Kikundi kimoja cha Dini ya Tao katika Taiwan, kinachoitwa T’ien Tao (Njia ya Kimbingu), hudai kuwa hicho ni mchanganyiko wa dini tano za ulimwengu—Dini ya Tao, Dini ya Confucius, Dini ya Buddha, Ukristo, na Uislamu.

[Sanduku katika ukurasa wa 162]

Matamshi ya Maneno ya Kichina

Ili kupatana na vitabu vilivyo vingi vya kiusomi,namna ya kutohoa Kichina ya Wade-Gilesyatumiwa katika kitabu hiki. Visawe vya Kiswahilivimetolewa chini:

ch j, kama katika Tao Te Ching (Jing)

ch’ ch, kama katika nasaba ya kifalme ya Ch’in (chin)

hs sh, kama katika Ta Hsüeh (shu-eh), The Great Learning

j r, kama katika jen (ren), kuwa na moyo wa kibinadamu

k g, kama katika kijimungu-kike cha Dini ya Buddha Kuan-yin (gwan-yin)

k’ k, kama katika K’ung-fu-tzu (kung-fu-tzu), au Confucius

t d, kama katika Tao (dao), ile Njia

t’ t, kama katika nasaba ya kifalme ya T’ang (tang)

[Sanduku katika ukurasa wa 175]

Dini ya Confucius—Falsafa au Dini?

Kwa sababu Confucius alitoa maelezo machache juu ya Mungu, watu wengi huiona Dini ya Confucius kuwa falsafa tu wala si dini. Hata hivyo, yale aliyosema na kufanya yalionyesha kwamba yeye alikuwa wa kidini. Hilo laweza kuonwa kwa njia mbili. Kwanza, yeye alikuwa na hofu yenye heshima kwa ajili ya nguvu kuu fulani ya kiroho ya anga, ni jambo ambalo Wachina huita T’ien, au Mbingu, aliyoichukua kuwa chanzo cha mwenendo mwema wote na wema wa adili na ambayo mapenzi yayo, alihisi, huelekeza mambo yote. Pili, yeye alikazia sana kufuatia kwa uangalifu mwingi desturi na sherehe zinazohusu ibada ya mbingu na roho za wazazi wa kale waliokufa.

Ingawa Confucius hakuunga mkono mawazo hayo kuwa namna fulani ya dini, hayo hasa ndiyo yamekuwa dini kwa vizazi vingi vya Wachina.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 177]

Vitabu Vinne vya Kawaida na Vitabu Bora Sana Vitano vya Confucius

Vile Vitabu Vinne vya Kawaida

1. The Great Learning (Ta Hsüeh), msingi wa elimu ya muungwana, kitabu cha kwanza ambacho wavulana wa shule katika China ya kale walijifunza

2. The Doctrine of the Mean (Chung Yung), mtungo juu ya ukuzi wa asili ya kibinadamu kupitia kiasi

3. The Analects (Lun Yü), mkusanyo wa semi za Confucius, zinazoonwa kuwa chanzo kikuu cha wazo la Confucius

4. The Book of Mencius (Meng-tzu), maandishi na semi za mwanafunzi mkuu zaidi wa Confucius, Meng-tzu, au Mencius

Vile Vitabu Bora Sana Vitano

1. The Book of Poetry (Shih Ching), mashairi 305 yanayoonyesha picha ya maisha ya kila siku katika nyakati za mapema za Chou (1000-600 K.W.K.)

2. The Book of History (Shu Ching), chahusisha karne 17 za historia ya Kichina kuanzia na nasaba ya kifalme ya Shang (1766-1122 K.W.K.)

3. The Book of Changes (I Ching), kitabu cha uaguzi, kinachotegemea fasiri 64 za miunganisho inayowezekana ya mistari kamili sita au yenye mapengo

4. The Book of Rites (Li Chi), mkusanyo wa amri zinazohusu sherehe na kawaida za sherehe ya ibada

5. Annals of Spring and Autumn (Ch’un Ch’iu), historia ya mkoa wa Lu alikozaliwa Confucius, kutia 721-478 K.W.K.

[Picha]

Vitabu Bora Sana Vitano, juu, na kisehemu, kushoto, cha The Great Learning (kimoja cha Vitabu Vinne), vilivyonukuliwa kwenye ukurasa 181

[Picha katika ukurasa wa 163]

Tao, ‘njia anayopaswa mtu kupitia’

[Picha katika ukurasa wa 165]

Lao-tzu, yule mwanafalsafa wa Dini ya Tao, juu ya mgongo wa nyati

[Picha katika ukurasa wa 166]

Hekalu la Dini ya Tao la Matsu, “Mama Mtakatifu Katika Mbingu,” katika Taiwan

[Picha katika ukurasa wa 171]

Milima yenye ukungu, maji matulivu, miti yenye kusuka-suka, na wasomi wanaoondoka—vichwa vya habari vipendwavyo na wengi katika sawiri za mandhari za Kichina—huonyesha wazo la Dini ya Tao la kuishi kwa upatano na asili

[Picha katika ukurasa wa 173]

Sanaa ya kuchongwa ya Dini ya Tao ya kale, kushoto, kijimungu cha Maisha Marefu pamoja na wale Wasioweza kufa Wanane

Kulia, kuhani wa Dini ya Tao amevaa mavazi kamili akiongoza maziko

[Picha katika ukurasa wa 179]

Confucius, mwenye hekima mashuhuri zaidi wa China, huheshimiwa mno kuwa mwalimu wa adili na mwenendo mwema

[Picha katika ukurasa wa 181]

Sherehe, pamoja na muziki, kwenye Sung Kyun Kwan, kitovu cha kielimu cha Dini ya Confucius cha karne ya 14 kule Seoul, Korea, huendeleza sherehe za ibada za Dini ya Confucius

[Picha katika ukurasa wa 182]

Awe ni mfuasi wa Dini ya Buddha, Dini ya Tao, au Dini ya Confucius, Mchina halisi, kutoka kushoto, huwapa shikamoo wazazi wa kale waliokufa akiwa nyumbani, huabudu kijimungu cha utajiri, na hutoa sadaka kwenye mahekalu nyakati za sikukuu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki