Sura 26
Arudi Nyumbani Kapernaumu
KUFIKIA sasa sifa ya Yesu imeenea kotekote, na watu wengi wanasafiri kwenda kule viungani anakokaa. Lakini, baada ya siku kadhaa arudi Kapernaumu kando ya Bahari ya Galilaya. Upesi habari zaenea jijini kwamba amerudi nyumbani, na watu wengi waja kwenye nyumba anamokaa. Mafarisayo na walimu wa Sheria wanatoka mbali hata Yerusalemu.
Umati wa watu ni mkubwa sana hivi kwamba wanajazana mlangoni, na hakuna nafasi ya mtu mwingine yeyote kuingia ndani. Hali ni tayari kwa tukio la kustaajabisha kweli kweli. Linalotukia katika pindi hii ni jambo la maana sana, kwa maana linatusaidia kuthamini kwamba Yesu ana uwezo wa kukiondoa kisababishi cha mateso ya binadamu na kuwarudishia afya wote anaochagua.
Yesu anapokuwa akifundisha umati wa watu, wanaume wanne waleta nyumbani mle mwanamume aliyepooza akiwa katika machela. Wanataka Yesu amponye rafiki yao, lakini kwa sababu ya umati wa watu, hawawezi kuingia ndani. Inatamausha kama nini! Hata hivyo wao hawazimiki moyo. Wanapanda juu ya dari, na kutoboa shimo, na kuiteremsha machela iliyo na yule mwanamume aliyepooza na kuifikisha pale alipo Yesu.
Je! Yesu anakasirika kwa sababu ya kukatizwa hivyo? Hata kidogo! Bali, yeye anavutwa sana na imani yao. Amwambia yule aliyepooza: “Umesamehewa dhambi zako.” Lakini je! Yesu anaweza kusamehe dhambi? Wale waandishi na Mafarisayo hawafikiri hivyo. Wawaza mioyoni mwao: “Mbona huyu asema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?”
Akijua mawazo yao, Yesu awaambia: “Mbona mnafikiri hivyo mioyoni mwenu? Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako uende?”
Kisha, Yesu aruhusu umati wa watu, kutia na wachambuzi wake, kuona wonyesho wenye kustaajabisha ambao utafunua ana mamlaka ya kusamehe dhambi duniani na kwamba yeye kweli kweli ndiye mwanadamu mkuu kupita wote waliopata kuishi. Yeye ageukia yule mwenye kupooza na kuamuru: “Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako.” Na mara hiyo yeye afanya hivyo, atembea na kutoka nje mbele ya macho yao akiwa na godoro lake! Kwa mshangao watu wale wamtukuza Mungu na kupaaza sauti: “Namna hii hatujapata kuiona kamwe”!
Je! wewe umeona kwamba Yesu anazitaja dhambi kuhusiana na magonjwa na kwamba msamaha wa dhambi unahusiana na kupata afya ya kimwili? Biblia inaeleza kwamba mzazi wetu wa kwanza, Adamu, alitenda dhambi na kwamba sisi sote tumeyarithi matokeo ya dhambi hiyo, yaani, magonjwa na kifo. Lakini chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu, Yesu atasamehe dhambi za wote wanaompenda Mungu na kutumikia Yeye, halafu magonjwa yote yataondolewa. Hilo litakuwa jambo zuri kama nini! Marko 2:1-12; Luka 5:17-26; Mathayo 9:1-8; Warumi 5:12, 17-19.
▪ Ni hali gani iliyotayarishwa ili kuwe na tukio la kustaajabisha kweli kweli?
▪ Mtu yule mwenye kupooza alimfikiaje Yesu?
▪ Ni kwa nini sote tu wenye dhambi, lakini Yesu aliandaaje tumaini la kwamba inawezekana tusamehewe dhambi zetu na kurudishiwa afya kamili?