Maisha na Huduma ya Yesu
Amerudi Nyumbani Katika Kapernaumu
KUFIKIA sasa sifa ya Yesu imeenea kote kote, na watu wengi wanasafiri mahali anakokaa kule viungani. Lakini, baada ya siku kadha anarudi Kapernaumu kwa kupitia bahari ya Galilaya. Upesi habari zinaenea mjini kwamba amerudi nyumbani, na watu wengi wanakuja kwenye nyumba anakokaa. Wafarisayo na waalimu wa Sheria wanatoka mbali kule Yerusalemu.
Mkutano wa watu ni mkubwa sana hivi kwamba wanapajaa mahali pa kuingilia, na hakuna nafasi ya mtu mwingine ye yote kuingia ndani. Mambo ni tayari kwa tukio la kustaajabisha kweli kweli. Linalotukia katika pindi hii ni jambo la maana sana, kwa maana linatusaidia kuthamini kwamba Yesu ana uwezo wa kukiondoa kisababishi cha taabu za wanadamu na kuwarudishia afya wote anaowachagua.
Yesu anapokuwa akifundisha mkutano wa watu, watu wanne wanaleta nyumbani mle mwanamume aliyepooza akiwa katika machela. Wanataka Yesu amponye rafiki yao, lakini kwa sababu ya mkutano wa watu wanashindwa kuingia ndani. Inakatisha tamaa kama nini! Hata hivyo wao hawazimii moyo. Wanapanda juu darini, wanatoboa shimo kwa kuviondoa vigae, na kuiteremsha machela iliyo na yule mwanamume aliyepooza na kuifikisha pale pale alipo Yesu.
Je, Yesu anakasirika kwa sababu ya kukatizwa hivyo? Hata kidogo! Bali, yeye anavutwa sana na imani yao. Anamwambia yule aliyepooza: “Umesamehewa dhambi zako.” Lakini je, Yesu kweli anaweza kusamehe dhambi? Waandishi na Mafarisayo hawafikiri hivyo. Wanawaza mioyoni mwao: “Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu? ”
Akijua mawazo yao, Yesu anawaambia: “Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema Ondoka, ujitwike godoro lako uende? ” Bila kungoja jibu Yesu anamrudia yule aliyepooza na kusema: “Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako.” Naye anafanya hivyo mara, akiondoka na machela yake (godoro) mbele ya wao wote! Kwa kushangaa sana watu wanapaaza sauti: “Namna hii hatujapata kuiona kamwe.”
Je, wewe umeona kwamba Yesu anazitaja dhambi kuhusiana na magonjwa na kwamba msamaha wa dhambi unahusiana na kupata afya? Biblia inaeleza kwamba mzazi wetu wa kwanza Adamu alitenda dhambi na kwamba sisi sote tumeyarithi matokeo ya dhambi hiyo, yaani, magonjwa na kifo. Lakini chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu, Yesu atasamehe dhambi za wote wanaompenda Mungu na kumtumikia, halafu magonjwa yote yataondolewa. Hilo litakuwa jambo zuri kama nini! Marko 2:1-12; Luka 5:17-26; Matayo 9:1-8; Warumi 5:12, 17-19.
◆ Ni hali gani iliyotayarishwa ili kuwe na tukio la kustaajabisha kweli kweli?
◆ Mtu yule aliyepooza alimfikiaje Yesu?
◆ Ni kwa sababu gani sote tuna dhambi, lakini Yesu aliandaaje tumaini la kwamba inawezekana tusamehewe dhambi zetu na kurudishiwa afya kamili?
[Picha ya ukurasa nzima katika ukurasa wa 8]