Neno la Mungu Li Hai
Kwa Sababu Gani Watu Wanakuwa Wagonjwa na Kufa?
Hakuna mtu anayetaka kuwa mgonjwa, kuzeeka na kufa. Hata hivyo, hayo ndiyo yanayotokea. Kwa hakika Mungu hakukusudia iwe hivyo. Kwa hiyo, ni kwa sababu gani watu wanakuwa wagonjwa na kufa? Jambo lililotokea miaka zaidi ya 1,900 iliyopita katika nyumba moja iliyokuwa imejaa watu karibu na Bahari ya Galilaya linaonyesha jibu
Yesu Kristo alikuwa amerudi tu katika mji wa nyumbani kwake, Kapernaumu. (Marko 2:1; Mt. 4:13) Sasa yeye alikuwa anajulikana sana, sana-sana kwa sababu ya mwujiza wake wa ajabu alipomponya mtu mmoja aliyekuwa mwenye ukoma. (Marko 1:40-45) Basi watu katika ujirani wote wanakuja kumwona Yesu. Umati mkubwa wa watu ulisongamana ndani ya nyumba alimokuwa akiishi, kama unavyoweza kuona hapa.
Wakati watu wanne walipomleta mtu aliyepooza, aliyekuwa amelala juu ya machela, hawakuweza kuingia katika nyumba hiyo. Lakini hawakukubali kushindwa. Walipanda juu ya paa. Ilikuwa paa tambarare, nao wakafanyiza shimo kubwa ndani yayo. Kisha wakatelemsha chini kabisa ndani ya kile chumba, machela ambayo yule mtu aliyepooza alikuwa amelalia. Hakika walikuwa na imani nyingi kwamba Yesu angeweza kumsaidia mtu huyo.
Yesu alipoona namna walivyokuwa na imani nyingi, yeye alimwambia hivi mtu yule mgonjwa: “Umesamehewa dhambi zako.” Hiyo inaonyesha kwamba kuna uhusiano kati ya magonjwa na dhambi. Lifikirie jambo hilo. Mtu wa kwanza, Adamu, alipofanya dhambi kwa kuivunja sheria ya Mungu, adhabu yake ilikuwa kutokukamilika na kifo. Hiyo ndiyo sababu watu wanakuwa wazee, wagonjwa na kufa. Sisi sote tumerithi dhambi na kifo kutoka kwa Adamu.—Ayubu 14:4; Rum. 5:12.
Walakini je! Yesu anaweza kusamehe kikweli watu dhambi? Baadhi ya watu. waliokuwamo ndani ya chumba hicho kilichokuwa kimejaa watu katika Kapernaumu, hawakufikiri angeweza. Basi Yesu aliwaambia hivi: “Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?” Baada ya hayo Yesu akamwambia mtu huyo achukue machela (godoro) yake na aende nyumbani mwake. Na mtu huyo alifanya hivyo! Alikuwa ameponywa kabisa!—Marko 2:2-12.
Ebu fikiri tu yale ambayo uwezo huo wa Yesu unaweza kutufanyia! Chini ya utawala wa ufalme wa Mungu, Kristo ataweza kusamehe dhambi za watu wote wanaompenda Mungu na kumtumikia. Hiyo inamaanisha kwamba maumivu na uchungu na magonjwa yote yataondolewa. Hakuna mtu atakayekuwa mzee na kufa tena. Hilo ni taraja zuri ajabu kama nini la wakati ujao!—Ufu. 21:3, 4.