Sura 27
Kumwita Mathayo
MUDA mfupi baada ya kuponya mtu yule aliyepooza, Yesu atoka Kapernaumu na kwenda kwenye Bahari ya Galilaya. Kwa mara nyingine umati wa watu wamwendea, naye aanza kuwafundisha. Aendeleapo kusonga mbele, amwona Mathayo, ambaye pia aitwa Lawi, akiwa ameketi katika ofisi ya kutozea kodi. “Nifuate,” ndio mwaliko wa Yesu.
Yaelekea, tayari Mathayo afahamiana na mafundisho ya Yesu, kama vile Petro, Andrea, Yakobo, na Yohana wakati walipoitwa. Na kama wao, Mathayo aitikia mwaliko huo bila kukawia. Asimama, na kuacha nyuma madaraka yake ya kuwa mkusanya kodi, na kumfuata Yesu.
Baadaye, labda ili kusherehekea kupokea kwake mwaliko, Mathayo anafanya karamu kubwa nyumbani mwake. Zaidi ya Yesu na wanafunzi Wake, watu waliokuwa wakishirikiana na Mathayo wapo. Kwa ujumla watu hao wanadharauliwa na Wayahudi wenzao kwa sababu wanawakusanyia kodi mamlaka za Kiroma zinazochukiwa. Tena, mara nyingi wao wanatoza watu kwa udanganyifu pesa zinazozidi ile kodi ya kawaida.
Wanapomwona Yesu karamuni akiwa pamoja na watu wa namna hiyo, Mafarisayo wanauliza wanafunzi wake: “Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?” Anaposikia swali hilo kwa mbali, Yesu awajibu Mafarisayo: “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
Yaonekana kwamba, Mathayo amealika wakusanya kodi hao nyumbani kwake ili waweze kumsikiliza Yesu na kupokea maponyo ya kiroho. Kwa hiyo Yesu ashirikiana nao ili awasaidie wawe na uhusiano wenye afya pamoja na Mungu. Yesu hadharau watu wa namna hiyo kama wanavyofanya Mafarisayo wenye kujiona ni wenye uadilifu. Lakini yeye anakuwa kama tabibu wa kiroho kwao kwa sababu ya kusukumwa na huruma.
Hivyo wonyesho wa Yesu wa rehema kuelekea watenda dhambi hao si kukubali dhambi zao bali ni wonyesho wa huruma ile ile nyororo aliyowadhihirishia wagonjwa wa kimwili. Kwa kielelezo, kumbuka wakati aliponyoosha mkono kwa huruma akamgusa mwenye ukoma, akisema: “Nataka; takasika.” Vivyo hivyo sisi na tuonyeshe rehema kwa kusaidia watu walio na uhitaji, hasa kuwasaidia kwa njia ya kiroho. Mathayo 8:3; 9:9-13; Marko 2:13-17; Luka 5:27-32.
▪ Mathayo yu wapi wakati Yesu anapomwona?
▪ Kazi ya Mathayo ni nini, na kwa nini watu wa namna hiyo wanadharauliwa na Wayahudi wale wengine?
▪ Ni lalamiko gani linalotolewa dhidi ya Yesu, naye ajibuje?
▪ Kwa nini Yesu anashirikiana na watenda dhambi?