Maisha na Huduma ya Yesu
Kuitwa kwa Mathayo
MUDA mfupi baada ya kuponya mtu yule aliyepooza, Yesu anatoka Kapernaumu na kwenda Bahari ya Galilaya. Kwa mara nyingine makutano ya watu wanamwendea huko naye anaanza kuwafundisha. Anapoendelea kusonga mbele, anaona Mathayo, ambaye pia anaitwa Lawi, akiwa ameketi kwenye afisi ya kutozea kodi. “Nifuate,” Yesu anamwalika.
Inaelekea kwamba Mathayo tayari amekwisha kupata habari nyingi juu ya mafundisho ya Yesu, kama vile Petro, Andrea, Yakobo, na Yohana wakati walipoitwa. Na kama wao, Mathayo anaitikia mwaliko huo bila kukawia. Anasimama, anaacha nyuma madaraka yake ya kuwa mkusanya kodi, na kumfuata Yesu.
Baadaye Mathayo anafanya karamu kubwa nyumbani mwake, labda ili asherehekee mwito alioupokea. Zaidi ya Yesu na wanafunzi Wake, watu waliokuwa wakishirikiana na Mathayo wapo. Kwa ujumla watu hao wanadharauliwa na Wayahudi wenzao kwa sababu wanawakusanyia kodi mamlaka za Kiroma zinazochukiwa. Tena, mara nyingi wao wanatoza watu kwa udanganyifu pesa zinazozidi ile kodi ya kawaida.
Wanapomwona Yesu karamuni akiwa pamoja na watu wa namna hiyo, Wafarisayo wanauliza wanafunzi wake: “Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? ” Anaposikia ulizo hilo kwa mbali, Yesu anajibu: “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
Inaonekana kwamba Mathayo amealika wakusanyaji hao wa kodi nyumbani kwake ili waweze kumsikiliza Yesu na kupokea maponyo ya kiroho. Kwa hiyo Yesu anashirikiana nao awasaidie wawe na uhusiano wenye afya pamoja na Mungu. Yesu hadharau watu wa namna hiyo, kama wanavyofanya Wafarisayo wenye kujiona ni wenye uadilifu. Lakini yeye anakuwa kama tabibu wa kiroho kwao kwa sababu ya kusukumwa na huruma.
Hivyo matumizi ya Yesu ya rehema kuelekea watenda dhambi si kukubali dhambi zao bali ni wonyesho wa huruma ile ile nyororo aliyowaonyesha wagonjwa wa kimwili. Kwa mfano, kumbuka wakati aliponyoosha mkono kwa huruma akamgusa mwenye ukoma, akisema: “Nataka; takasika.” Vivyo hivyo sisi na tuonyeshe rehema kwa kusaidia watu walio na uhitaji, hasa kuwasaidia kwa njia ya kiroho. Mathayo 8:3; 9:9-13; Marko 2:13-17; Luka 5:27-32.
◆ Yesu anakuwa wapi wakati anapomwona Mathayo?
◆ Kazi ya Mathayo ni nini, na kwa sababu gani watu wa namna hiyo wanadharauliwa na Wayahudi wale wengine?
◆ Ni lalamiko gani linalotolewa juu ya Yesu, naye anajibuje?
◆ Kwa sababu gani Yesu anashirikiana na watenda dhambi?
[Picha ya ukurasa nzima katika ukurasa wa 9]