Sura 101
Akiwa Bethania, Katika Nyumba ya Simoni
YESU aondokapo Yeriko, aelekea Bethania. Safari hiyo yachukua sehemu kubwa ya mchana huo, kwa kuwa ni mpando wa kilometa 19 hivi juu ya ardhi ngumu. Yeriko iko karibu meta 250 hivi chini ya usawa wa bahari, na Bethania iko meta 760 hivi juu ya usawa wa bahari. Huenda ukakumbuka kwamba Bethania ndilo kao la Lazaro na dada zake. Kijiji hicho kidogo kiko kilometa 3 hivi kutoka Yerusalemu, kikiwa kwenye mwinamo wa mashariki wa Mlima wa Mizeituni.
Tayari wengi wamewasili Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Kupitwa. Wamekuja mapema kujitakasa kisherehe. Labda wamegusa mwili mfu au wamefanya jambo jingine ambalo limewafanya wawe si safi. Kwa hiyo wazifuata taratibu za kujisafisha sana ili waadhimishe Sikukuu ya Kupitwa kwa njia inayokubalika. Watu hawa wenye kuwasili mapema wakusanyikapo kwenye hekalu, wengi wakisia-kisia kama Yesu atakuja kwenye Sikukuu ya Kupitwa.
Yerusalemu kumewaka moto wa kubishania habari za Yesu. Yajulikana na wengi kwamba viongozi wa kidini wataka kumkamata ili wamuue. Kwa uhakika, wao wametoa maagizo kwamba mtu yeyote akijua mahali aliko, apaswa kuwaletea ripoti. Mara tatu katika miezi ya majuzi—kwenye Sikukuu ya Tabenakulo, kwenye Sikukuu ya Wakfu, na baada ya yeye kufufua Lazaro—viongozi hawa wamejaribu kumuua. Kwa hiyo, watu washangaa wakiuliza, je! Yesu atajitokeza hadharani mara nyingine tena? “Mwaonaje?” wao waulizana.
Wakati ule ule, Yesu awasili Bethania siku sita kabla ya Sikukuu ya Kupitwa, ambayo hutukia Nisani 14 kulingana na kalenda ya Kiyahudi. Yesu afika Bethania muda fulani jioni ya Ijumaa, ambayo ni mwanzoni mwa Nisani 8. Hangaliweza kufunga safari hiyo ya kwenda Bethania siku ya Jumamosi kwa sababu kusafiri siku ya Sabato—kuanzia machweo ya jua Ijumaa mpaka machweo ya jua Jumamosi—kwazuiwa na sheria ya Kiyahudi. Labda Yesu aenda kwenye kao la Lazaro, kama vile amewahi kufanya hapo kwanza, na akaa huko usiku wa Ijumaa.
Hata hivyo, mkaaji mwingine wa Bethania aalika Yesu na waandamani wake kwa ajili ya mlo Jumamosi jioni. Mtu huyo ni Simoni, aliyekuwa na ukoma, ambaye labda alikuwa ameponywa na Yesu mapema kidogo. Kwa kupatana na tabia yake ya kuwa mwenye bidii, Martha anahudumia wageni. Lakini, kwa asili yake, Mariamu ampa Yesu uangalifu, wakati huu akifanya hivyo kwa njia ambayo yatokeza ubishi.
Mariamu afungua chombo cha marhamu, au chupa ndogo, yenye nusu-kilo hivi ya marashi, “nardo safi [halisi, NW].” Ni ya thamani kubwa sana. Kwa kweli, thamani yao yakaribia kulingana na mshahara wa mwaka mmoja! Mariamu amiminapo mafuta yale juu ya kichwa cha Yesu na juu ya nyayo zake na kufuta nyayo zake kwa nywele zake, manukato yale yaijaa nyumba nzima.
Wanafunzi wakasirika na kuliza: “Ni kwa nini upotevu huu?” Ndipo Yuda Iskariote asema: “Mbona marhamu hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini?” Lakini kwa kweli Yuda hahangaikii maskini, kwa maana yeye amekuwa akiiba kutoka kwa sanduku la pesa lenye kuwekwa na wanafunzi.
Yesu atetea Mariamu. “Mwacheni,” yeye aamuru. “Mbona mnamtaabisha? amenitendea kazi njema; maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamnami sikuzote. Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko. Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake.”
Sasa Yesu amekuwa katika Bethania kwa zaidi ya saa 24, na neno la kuwapo kwake limeenea huku na huku. Kwa hiyo, wengi waja kwenye nyumba ya Simoni wamwone Yesu, lakini waja pia ili wamwone Lazaro, ambaye pia yupo. Kwa hiyo wakuu wa makuhani washauriana ili waue si Yesu tu bali na Lazaro pia. Hii ni kwa sababu watu wengi wanatia imani katika Yesu kwa sababu ya kumwona akiwa hai yule ambaye alimfufua kutoka kwa wafu! Kwa kweli, viongozi hawa wa kidini ni waovu kama nini! Yohana 11:55-12:11; Mathayo 26:6-13; Marko 14:3-9; Matendo 1:12.
▪ Ni mazungumzo gani yanayoendelea kwenye hekalu katika Yerusalemu, na kwa nini?
▪ Kwa nini lazima Yesu awe aliwasili katika Bethania Ijumaa badala ya Jumamosi?
▪ Yesu awasilipo katika Bethania, yaelekea yeye akaa wapi wakati wa Sabato?
▪ Ni kitendo gani cha Mariamu ambacho chatokeza ubishi, na Yesu amteteaje?
▪ Ni kitu gani chatoa kielezi juu ya uovu mkubwa wa wakuu wa makuhani?