Sura 125
Maumivu Makali Juu ya Mti
PAMOJA na Yesu wanyang’anyi wawili wachukuliwa nje wakauawe. Si mbali na jiji, andamano lasimama mahali paitwapo Golgotha, au Fuvu la Kichwa.
Wafungwa hao wavuliwa mavazi yao. Halafu wapewa divai iliyotiwa manemane ambayo ni dawa ya kulevya. Inaonekana imetayarishwa na wanawake wa Yerusalemu, na Waroma huwa hawawanyimi wenye kutundikwa mchanganyo huu wa kinywaji chenye kumaliza maumivu. Hata hivyo, Yesu anapokionja, akataa kunywa. Kwa nini? Kwa wazi ataka kuwa na nguvu zake zote za kufikiri wakati wa jaribu hili la imani yake lililo kubwa kupita yote.
Sasa Yesu amenyooshwa juu ya mti huku mikono yake ikiwa imewekwa juu ya kichwa chake. Ndipo askari wanapopigilia misumari mikubwa katika mikono yake na katika miguu yake. Yeye ajigeuza-geuza kwa maumivu wakati misumari inapochoma mnofu na nyuzi za mwili. Mti unaposimamishwa wima, maumivu yazidi kweli kweli, kwa maana uzito wa mwili wake wapasua sehemu za majeraha yenye misumari. Hata hivyo, badala ya kutisha, Yesu asali hivi kwa ajili ya askari hao Waroma: “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.”
Pilato amebandika juu ya mti huo ishara ambayo inasema: “YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.” Inaonekana, yeye aandika hivi si kwa sababu tu aheshimu Yesu bali pia kwa sababu achukizwa sana na makuhani Wayahudi kwa kuwa wamemkaza mpaka akalazimika kuhukumia Yesu kifo. Ili wote waweze kusoma ishara hiyo, Pilato aagiza iandikwe katika lugha tatu—katika Kiebrania, katika Kilatini rasmi, na katika Kigiriki cha kawaida.
Makuhani wakuu, kutia na Kayafa na Anasi, wafadhaika. Tangazo hili la hakika linaharibu saa yao yenye shangwe ya ushindi. Kwa hiyo wapinga hivi: “Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.” Akiudhika kwa kuwa ametumika kama chombo cha kutimizia nia ya makuhani hao, Pilato ajibu kwa madharau yenye kukata maneno: “Niliyoandika nimeyaandika.”
Makuhani, pamoja na umati mkubwa, sasa wakusanyika mahali pa mauaji, na makuhani wajaribu kukanusha ushuhuda wa ile ishara. Warudia ule ushuhuda wa bandia uliotolewa mapema kidogo kwenye majaribu ya Sanhedrini. Kwa hiyo, haishangazi kwamba wapita njia waanza kusema kwa matusi, wakitikisa vichwa vyao kwa mzaha na kusema: “Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani [kutoka kwenye mti wa mateso, NW]”!
“Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe”! nao makuhani wakuu na marafiki wao wa kidini waingilia kama kwamba ni kwa sauti moja. “Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani [kutoka kwenye mti wa mateso, NW], nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama amtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu.”
Kwa kunaswa katika roho hiyo, askari wajiunga pia katika kufanyia Yesu mzaha. Wamtolea divai kali kwa mzaha, yaonekana ikiwa imepita kidogo tu mbele ya midomo yake iliyokauka. “Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi,” wanadhihaki vikali, “ujiokoe mwenyewe.” Hata wale wanyang’anyi—mmoja akiwa ametundikwa kulia kwa Yesu, na yule mwingine kushoto kwake—wamdhihaki. Fikiria hilo! Binadamu mkubwa zaidi aliyepata kuishi, ndiyo, yule aliyeshiriki pamoja na Yehova Mungu katika kuumba vitu vyote, apatwa na fedheha yote hiyo akiwa ameazimia kabisa!
Askari wachukua mavazi ya Yesu ya nje na kuyagawanya sehemu nne. Wapiga kura kuona yatakuwa ya nani. Hata hivyo, lile vazi la ndani halina mshono wa kuliunga, kwa kuwa ni la ubora mwingi. Hivyo basi askari hao waambiana: “Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani.” Hivyo, bila kujua, watimiza andiko linalosema: “Waligawanya nguo zangu, na vazi langu wakalipigia kura.”
Baada ya muda, mmoja wa wanyang’anyi aja kuthamini kwamba kwa kweli ni lazima iwe Yesu ni mfalme. Kwa hiyo, akikemea mwandamani wake, asema hivi: “Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.” Halafu aongea na Yesu, na kutoa ombi hili: “Nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.”
“Kweli kweli mimi nakuambia wewe leo,” Yesu ajibu, “Wewe utakuwa pamoja na mimi katika Paradiso.” (NW) Ahadi hii itatimizwa wakati Yesu atakapotawala mbinguni na kufufua mtenda maovu huyo mwenye kutubu kwenye uhai duniani katika Paradiso ambayo waokokaji wa Har–Magedoni na waandamani wao watakuwa na pendeleo la kuisitawisha. Mathayo 27:33-44; Marko 15:22-32; Luka 23:27, 32-43; Yohana 19:17-24.
▪ Kwa nini Yesu akataa kunywa divai iliyotiwa manemane ambayo ni dawa ya kulevya?
▪ Yaonekana ni kwa nini ile ishara imebandikwa juu ya mti wa Yesu, nayo yaanzisha maneno gani kati ya Pilato na makuhani wakuu?
▪ Yesu adhihakiwa zaidi namna gani juu ya mti wa mateso, na kwa wazi ni nini kinachoongoza jambo hilo?
▪ Unabii watimizwaje katika linalofanywa na mavazi ya Yesu?
▪ Mmoja wa wanyang’anyi afanya badiliko gani, na Yesu atatimizaje ombi lake?