ESTA
(Esta).
Binti Myahudi wa kabila la Benjamini na aliyekuwa yatima ambaye jina lake la Kiebrania lilikuwa Hadasa (linalomaanisha “Mhadasi”); alikuwa miongoni mwa watu waliopelekwa uhamishoni kutoka Yerusalemu pamoja na Mfalme Yehoyakini (Yekonia) katika mwaka wa 617 K.W.K. (Est 2:5-7) Alikuwa binti ya Abihaili ndugu ya baba ya Mordekai. (Est 2:15) Mlezi wake alikuwa Mordekai, ndugu ya baba yake, mmoja wa ‘watumishi wa mfalme waliokuwa katika lango la mfalme’ katika jumba la mfalme lililokuwa Shushani wakati wa utawala wa mfalme wa Uajemi Ahasuero (Shasta wa I, katika karne ya tano K.W.K.). (Est 2:7; 3:2) Baada ya Ahasuero kumwondoa malkia Vashti katika cheo chake kwa sababu ya kutotii, alitoa amri kwamba wasichana wote warembo na mabikira wakusanywe na kuwekwa pamoja kwa kipindi fulani cha wakati, wakikandwa miili yao na kurembeshwa zaidi, ili mfalme aweze kuchagua mmoja wao awe malkia na kuchukua nafasi ya Vashti. Esta alikuwa miongoni mwa waliopelekwa katika nyumba ya mfalme na kuwa chini ya utunzaji wa Hegai mlinzi wa wanawake. Akifuata maagizo ya Mordekai, Esta hakumwambia yeyote kwamba yeye ni Myahudi. (Est 2:8, 10) Esta alichaguliwa kuwa malkia katika mwaka wa saba wa utawala wa Ahasuero. (Est 2:16, 17) Wakati huo wote, aliendelea kuwasiliana na Mordekai na kufuata mashauri yake. Alizungumza kwa jina la Mordekai mbele ya mfalme wakati Mordekai alipogundua njama dhidi ya mfalme. —Est 2:20, 22.
Katika mwaka wa 12 wa utawala wa Ahasuero, Hamani Mwagagi, aliyekuwa waziri mkuu, alipanga njama za kuangamiza kabisa Wayahudi wote katika mikoa 127 ya milki. Aliruhusiwa na mfalme kuandika amri hiyo ili aitekeleze. (Est 3:7-13) Akitenda kwa kufuata taarifa na ushauri wa Mordekai, Esta alimwambia mfalme kuhusu nia mbaya ya njama ya Hamani. Itikio la Hamani lilimkasirisha hata zaidi mfalme, na mwishowe Hamani alinyongwa. (Est 4:7–7:10) Esta alimwomba Mfalme atoe amri ya pili iliyowaruhusu Wayahudi walinde uhai wao katika siku iliyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa kwao. (Est 8:3-14) Kwa sababu ya amri ya mfalme na hofu waliyokuwa nayo kumwelekea Mordekai, aliyechukua nafasi ya Hamani akiwa waziri mkuu, magavana na wakuu wa milki waliwasaidia Wayahudi kupata ushindi kamili dhidi ya adui zao. (Est 9) Maagizo ya Mordekai yaliyoidhinishwa na Esta, yaliwaamrisha Wayahudi