Chanzo cha Taabu ya Wanadamu Chakaribia Kuondolewa
1. Kulingana na Biblia, ni nini sababu ya kupatwa kwa wanadamu na taabu inayoongezeka?
NI KWELI kwamba wanadamu wenye choyo na wasiopenda si wasio na lawama. Lakini sababu kubwa ya taabu inayoongezeka ya wanadamu ni kwamba Shetani Ibilisi na malaika zake wa kishetani wametupwa nje ya mbingu takatifu kuja kwenye ujirani wetu wa dunia, nao maibilisi hawa waliotupwa wameghadhibishwa na hili. Wameghadhibika kwa maana “vita . . . mbinguni” ilitokeza ushindi wa kimungu, ushindi wa Mungu. Wameghadhibika kwa maana ufalme wa Mungu wa Masihi wake wa kweli ulizaliwa mbinguni mwishoni mwa Majira ya Mataifa mwaka wa 1914, nao hawakuweza kuuzuia. Wameghadhibika kwa maana wakati wao wa kuzuiwa hapa ni mfupi kabla hawajatupwa watoke hata duniani na kufungiwa katika shimo kubwa wasimoweza kutolea maongozi yao maovu juu ya wanadamu wote.—Ufu. 20:1-3, 7.
2, 3. (a) Ni kwa njia gani lengo la Shetani Ibilisi lilivyo kama lengo la kisiasa la mtawala-marehemu mwenye kutumia nguvu Hitler? (b) Kwa sababu gani Ufunuo 12:13-17 unatajwa kuonyesha kwamba lengo la Shetani si kuhifadhi uhai wa kibinadamu?
2 Kwa habari ya mtawala-marehemu mwenye kutumia nguvu wa Nazi, Adolf Hitler, lengo la kisiasa lilikuwa, Kutawala au kuharibu! Wazo hilo alilitoa pale pale ambapo watawala wenye kutumia nguvu waliotangulia walilitoa, yaani, kutoka kwa Shetani Ibilisi. Kwa kuwa Shetani atakuwa hawezi kuwatawala wanadamu wote karibuni kama vile alivyofanya wakati wa Majira ya Mataifa na hata kabla ya hapo, amekata shauri la kuwaharibu wanadamu wote. Ndipo, kama yeye anavyodhani, hakuna wanadamu watakaoachwa duniani ufalme wa Mungu wa Masihi wake uweze kuwatawala. Kujiua kwa wanadamu kwa vita ya atomiki au kwa kujiletea uchafu hakumwogofishi Shetani Ibilisi. Kusudi lake ni kuwaua wanadamu, nalo hili laonyeshwa katika maneno haya yafuatayo ya Ufunuo:
3 “Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume. . . . Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu.”—Ufu. 12:13-17.
VITA PENYE HAR-MAGEDONI
4, 5. (a) Shetani yule nyoka wa mfano ametangaza vita juu ya nani, na kwa muda gani? (b) Anawaelekeza watawala wa kisiasa wa dunia kwenye nini bila ya wao kujua, nalo tendo hili lake laonyeshwaje katika Ufunuo 16:13-16?
4 Shetani joka wa mfano amelitangazia tengenezo la Mungu (kama linavyofananishwa na “yule mwanamke”) vita mpaka mwisho wenyewe. Shetani “yule joka mkuu” anawaelekeza watawala wa kisiasa wa Kristendomu na milki ya upagani kwenye uharibifu katika vita ya mwisho, bila ya wao kujua. Siyo vita kati yao wenyewe yenye silaha za atomiki au zilizo na vijidudu vyenye kueneza maradhi, bali ni vita juu ya Mungu, aliye Baba ya ufalme wa kimbinguni wa Kimasihi uliotoka katika tumbo la uzazi la “mwanamke” wake, tengenezo lake. Ndivyo ilivyo, si kwa jamii ya mataifa ya Wakomunisti wenye kumpinga Mungu peke yao, bali pia na kwa mataifa ya Kristendomu mwenye kufuata dini. Watawala wa wanadamu wanaotaabika leo wanayafuata maenezi ya vita ya Shetani joka wa mfano. Kupotoa huku kwa watawala wa kisiasa kulionyeshwa kwa unabii kwa ajili yetu katika masimulizi haya ya tendo lenyewe katika Ufunuo 16:13-16:
5 “Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote, kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi. . . . Wakawakusanya hata mahali paitwapo kwa Kiebrania, Har–Magedoni.”
6. (a) Zile roho zinatoka wapi hasa, na ni roho gani iliyo kuu? (b) Ni kwa kusudi gani roho hizo zinakusanya wafalme wa dunia, na katika hali gani penye Har–Magedoni
6 Hizo roho chafu zatoka kinywani mwa Shetani joka asiyeonekana na vinywani mwa mawakili wa kidunia wa Shetani wasioonekana, yaani, taratibu ya kisasa ya kinyama ya ulimwenguni pote ya Shetani na mamlaka ya ulimwengu ya kisiasa inayotoa unabii mbalimbali wa uongo kwa makao yote ya siasa za kibinadamu. Kwa kuwa ni wa uongo, nabii huyo wa kisiasa si mnenaji wala si mwenezi wa Mungu. Kwa habari ya chanzo chazo, hizo roho chafu tatu ni chafu kama vyura, nazo zawakusanya wafalme wa kidunia na majeshi yao kwenye Har–Magedoni kwa kusudi chafu. Kutimizwa kwa hili kusudi chafu kwaweza kumaanisha “ole” tu kwa wanadamu wanaotaabika, kwa maana roho iliyo kuu yenye mfano wa chura yatoka kinywani mwa Shetani joka wa mfano, aliye na ghadhabu nyingi kwa kutupwa nje ya mbingu. Kushuka kwake duniani kwa lazima kulitabiriwa kumaanisha “ole wa nchi na bahari” tu. (Ufu. 12:12) “Wafalme wa ulimwengu wote” wanakusanywa kwa nguvu za zile roho chafu, si kupigana wao kwa wao katika vita ya mataifa yote, bali pamoja, wote wakiwa upande mmoja wa pigano la Har–Magedoni.
7. (a) Ni akina nani walioko upande ule mwingine wa uwanja wa vita wa Har–Magedoni? (b) Twajuaje ni ulizo gani litakalofanya vita ijayo ipiganwe?
7 Basi, ni akina nani walioko upande mwingine wa uwanja wa vita? Inatajwa waziwazi kwamba “joka” aliyetupwa na kushushwa alionyesha hasira na ghadhabu yake juu ya tengenezo la Mungu linalofananishwa na mwanamke lililokuwa limeuzaa ufalme wa kimbinguni wa Kimasihi. Katika Ufunuo 12:17 twasoma: “Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu.” Tangu kuzaliwa kwa ufalme wa Kimasihi mbinguni mwishoni mwa Majira ya Mataifa mwaka wa 1914, Yesu huyo ndiye Mfalme wa Kimasihi mwenye kutawala. Kwa hiyo washuhudiaji hawa hawakitolei ushuhuda kitoto Yesu kilichozaliwa karibuni, bali wanamtolea Mfalme Yesu Masihi anayetawala. Halafu? Mambo haya ya hakika yanamweka Mfalme wa Mungu mwenye kutawala Yesu Kristo na tengenezo la kimbinguni lililofananishwa na mwanamke lililouzaa Ufalme upande ule mwingine wa uwanja wa vita wa Har–Magedoni, akiwaelekea “wafalme wa ulimwengu wote” ambao wangali wakitawala. Ni wazi kwamba ulizo litakalofanya vita ijayo ipiganwe ni mamlaka ya ufalme juu ya dunia!
8. (a) Inaonyeshwaje wakati vita itakayopiganwa kwa sababu ya ulizo la Ufalme itakapotokea? (b) Yaonyeshwaje kama wafalme wa dunia wanamwunga Mungu mkono au sivyo?
8 Ili kuonyesha wakati barabara vita itakapopiganwa kwa ajili ya ulizo hilo la Ufalme, yasemekana kwamba “wafalme wa ulimwengu wote” wanakusanywa kwa ajili ya “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.” Bila ya kujali sala zote ambazo huenda viongozi wa kidini wa Kristendomu wakazitoa kwa ajili ya hao wafalme waliokusanyika, Mungu Mwenyezi hayuko pamoja na watawala hao wa kisiasa. “Wafalme” hao hawamwungi Mungu mkono; wanamwunga Ibilisi mkono. Wanampinga Kristo, kwa maana wanaupinga ufalme wa Kristo uliozaliwa karibuni. Haiwezi kuwa vingine isipokuwa kwamba Mungu Mwenyezi anatiwa katika vita hii penye Har–Magedoni, kwa kuwa Yeye ndiye Baba ya ufalme wa Kristo wake uliozaliwa karibuni. Yeye amekata shauri kwamba ufalme wake wa Kimasihi utaendelea kuwa na mamlaka tangu mwisho wa Majira ya Mataifa mwaka wa 1914, na kwamba ufalme huu wa kimbinguni utaitawala dunia yote na wakaaji wake. “Wafalme wa ulimwengu wote” wanakataa kukubali kuwapo kwa ufalme huu wa Kimasihi uliosimamishwa. Wanakataa kuzivua taji zao na kuviacha viti vyao enzi vya kidunia na kuuachia ufalme wa Mungu wa Kimasihi mamlaka yao ya ufalme.
9. Kwa sababu gani ni muhimu sasa kwetu kuuchunguza upande wa Har–Magedoni tusimamao, na imetupasa tubadilije pande?
9 Ulizo lililo la maana sana sasa ni, Kila mmoja wetu yuko upande gani wa uwanja wa vita wa Har–Magedoni? Wakati tulio nao kufanya uamuzi juu ya ulizo hili sasa unakaribia kikomo chake. Ni karibu miaka 60 tangu Majira ya Mataifa yalipokwisha mwaka wa 1914, nayo “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” haitakawia kwa wakati usiojulikana, milele. Vita hiyo lazima ianze wakati fulani. Kwa habari hii Mungu Mwenyezi ndiye anayeweka wakati wa vita hii penye Har–Magedoni. Kwa kuwa hatuujui wakati Wake barabara, lakini kuna sababu kamili kujua kwamba unakaribia, tusifikirie kujiwekea wakati wetu wenyewe wa kufanya uamuzi. Twajuaje kama sasa hivi hatuko upande wa “wafalme wa ulimwengu wote” na hivyo kumpinga Mungu? Kuna umuhimu wote kwetu kujichunguza na kuona ni wapi tulipo. Tukijiona hatuko upande wa Mungu Mwenyezi na ufalme wake wa Kimasihi, basi twaweza kutamani kubadili pande kwa unyofu. Ama sivyo, twaweza kuamua kukaa bila ya kufanya lo lote na kuyaona matokeo.
MASHAURI YA MAPEMA YA VITA KWA UONGOZI WETU
10. (a) Baada ya kuona kujipanga kwa pigano kwa majeshi ya kidunia penye Har–Magedoni, twataka kujua nini jingine? (b) Ufunuo unaonyesha ni nani ambaye majeshi ya kidunia yamejipanga yapigane naye?
10 Kitabu cha mwisho cha Biblia Takatifu hakituachi tukiwa na njozi ya unabii tu juu ya kujipanga kwa “wafalme wa ulimwengu wote” wenye kutaka vita penye Har–Magedoni, kutuacha tukiwa na mashaka juu ya matokeo ya “vita” inayokaribia sana. Ufunuo unasimulia matokeo ya vita hii. Unatueleza kinachompata yule “mnyama” wa mfano na “yule nabii wa uongo” ambao vinywani mwao zatoka zile roho chafu kama vyura. Unatueleza kinachowapata wale “wafalme wa ulimwengu wote” na majeshi yao na wafuasi wao. Ndiyo, kitabu cha Ufunuo kinatueleza waziwazi wafalme hawa na majeshi yao na “mnyama” na “yule nabii wa uongo” wamejipanga sasa wapigane, penye hali ya ulimwengu inayoitwa Har–Magedoni. Wamejipanga wapigane na Mfalme Yesu Kristo aliyevikwa taji, anayetawala na majeshi yake ya kimbinguni.
11. Ufunuo 19:11-16 unakuonyeshaje kujipanga kwa majeshi ya kimbinguni penye Har–Magedoni?
11 Kwa uongozi wa roho ya Mungu, mtume wa Kikristo Yohana anatuambia hivi: “Nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita . . . na jina lake aitwa, Neno la Mungu. Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi. . . . Naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi. Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA.”—Ufu. 19:11-16.
12, 13. (a) Kwa sababu gani inatupasa tuwe upande mmoja au mwingine kwa habari ya vita hii? (b) Yaonyeshwaje kama inaleta tofauti kwa sababu watawala wengine ni wa Kristendomu, na, kwa kuwa katika upande mmoja au mwingine, twajua nini?
12 Kwa hiyo, je! sisi tumekata shauri kusimama upande wa nani, upande wa huyu Mfalme wa wafalme au upande wa “wafalme wa ulimwengu wote”? Hakuna kutokuwamo katika hali ya ulimwengu iitwayo Har–Magedoni! Ni kwa ajili ya ulizo la uenyeji na utawala wa dunia yote kwamba vita hii inayokaribia sasa itapiganwa ikakate maneno kwa mara ya mwisho.
13 Haileti tofauti yo yote kwamba wengine wa “wafalme” au watawala wa kisiasa wanatawala mataifa yaliyomo katika Kristendomu mwenye kufuata dini; “wafalme” hawa pia wamekata shauri kuuendeleza utawala wao juu ya sehemu zao za dunia kuliko kumwacha Yesu Kristo Mfalme wa wafalme aitawale dunia yote kutoka mbinguni. Kitabu cha Ufunuo hakiwatofautishi wafalme na marais wa Kristendomu na wale wa ulimwengu usio wa Kikristo. Mtume Yohana anawachanganya wafalme wote wa dunia na kusema: “Nikamwona huyo mnyama, na wafalme wa nchi, na majeshi yao, wamekutana kufanya vita na yeye aketiye juu ya farasi yule, tena na majeshi yake.” (Ufu. 19:19) Wafalme wa Kristendomu na wale wa milki ya upagani pia wameufuata uongozi wa roho iliyotoka kwa “mnyama” huyu wa kisiasa na vile vile ile iliyotoka kinywani mwa “yule nabii wa uongo” wa kisiasa. Kwa hiyo, twajua tumejipanga tupigane na nani hasa ikiwa sisi ni wa “majeshi” na wafuasi wa hao “wafalme wa nchi.” Tukichagua kuwa upande wao, basi inatupasa tuyafikirie matokeo ya “vita” hii penye Har–Magedoni.
14. Inatupasa tufanye uamuzi gani juu ya tutakayemsikiliza kwa habari ya matokeo ya vita, naye mtume Yohana anaandika nini juu yake?
14 Kwa habari ya matokeo ya vita hii ya ulimwengu wote, je! tusikilize atakavyosema “yule nabii wa uongo,” au vile alivyosema mtume Yohana aliyeongozwa na roho ya Mungu? Kama onyo la mapema kwetu leo, Yohana aliandika hivi: “Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti; na wale waliosalia waliuawa kwa upanga wake yeye aliyeketi juu ya yule farasi, upanga utokao katika kinywa chake. Na ndege wote wakashiba kwa nyama zao.”—Ufu. 19:20, 21.
15. Tungeuita ushindi unaosimuliwa katika Ufunuo ushindi wa nani, nasi twavutwa kupaza sauti kwa maneno gani ya mtunga zaburi?
15 Tusemeje juu ya njozi hii ya mapema juu ya “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” penye Har–Magedoni? Je! yamaanisha ushindi wa kimungu? Ajapokuwa mtume Yohana mwenyewe hayashangilii matokeo ya vita katika maandishi, sisi tuupendao utawala wa haki wa dunia hatuwezi kukosa kuuita ushindi kweli kweli wa Mungu Mwenyezi. Kwa imani twavutwa kuyafuata maneno ya mtunga zaburi aliyeongozwa na roho ya Mungu na kupaza sauti: “Mwimbieni BWANA wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. BWANA ameufunua wokovu wake, machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake. . . . Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.”—Zab. 98:1-3.
MASHAHIDI WA USHINDI WA KIMUNGU
16. Je! Yohana anasema waziwazi kwamba watakuwako waokokaji wa uharibifu wa “mnyama” na “yule nabii wa uongo,” lakini tutaelewa nini kutokana na habari ya Yohana?
16 Je! twatamani kumwimbia Bwana Mungu Yehova wimbo huo mpya? Si shauri tu la kuuimba huo “wimbo mpya” sasa kwa imani, bali watakuwako hasa mashahidi wa ushindi wa Mungu watakaouokoka huo ushindi wa kimungu duniani na kuuimba “wimbo mpya” hapa duniani. Ajapokuwa mtume Yohana hakusema hivyo moja kwa moja, inaeleweka kutokana na aliyoyaandika kwamba wale walio duniani wasio upande wa “wafalme wa nchi, na majeshi yao” wataokoka wakati “mnyama” na “yule nabii wa uongo” watakapotupwa wakiwa hai katika uharibifu wa milele unaofananishwa na “lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.” Ndiyo kusema, wataokoka wakati taratibu za kisiasa zilizoundwa na wanadamu za serikali ya kichoyo zitakapoondolewa zisionekane tena.
17. (a) Katika vita hiyo, ni nini litakalowapata “wafalme wa nchi, na majeshi yao” na wafuasi wao? (b) Wale ambao Shetani yule joka aliondoka akafanye vita juu yao wataokoka, naye Yohana asemaje juu yao katika Ufunuo, sura ya kumi na tano?
17 “Wafalme wa nchi, na majeshi yao” na wafuasi wao wanauawa na upanga wa “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” nayo miili yao yalala imechinjwa katika uwanja wa vita wa Har–Magedoni ipate kuliwa nyama zake na ndege wenye kula mizoga. Lakini wale walioko upande wa Mfalme wa wafalme wataachiliwa na wataokoka. Wataishi wawe mashahidi wanenao juu ya “ushindi wa Mungu wetu,” “uwezo wenye kuokoa wa Mungu wetu.” (Zab. 98:3, Je) Kati ya waokokaji hawa watakuwamo “wazao [wa mwanamke] waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu,” ambao Shetani yule joka ‘alienda zake afanye vita’ juu yao. (Ufu. 12:17) Hawa ndio ambao mtume Yohana anawasema kama “wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake.” Yohana anawasimulia hawa kama wakiuimba wimbo wa Musa na wa Mwana-kondoo Yesu Kristo, wakisema hivi: “Kazi zako ni kubwa na za ajabu, Yehova Mungu, Mwenye Nguvu Zote. Njia zako ni za haki na za kweli, Mfalme wa umilele.”—Ufu. 15:2, 3, NW.
18. (a) Ni akina nani wengine wanaookoka vita penye Har–Magedoni, kama mtume Yohana alivyotangulia kuona? (b) Ni akina nani waliofanya vita juu ya waokokaji hao wote, na kwa njia hiyo wakamfanya nani achukue hatua?
18 Kati ya waokokaji wa kidunia watakuwamo pia wale ambao mtume Yohana anawataja pamoja kama “mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha,” kwa maana wanasimama upande wa Mungu na wa Yesu Kristo wake. Mtume Yohana anaelezwa wazi kwamba huu “mkutano mkubwa” ni wa watu ambao “wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu,” naye anawaona wamesimama kama waokokaji mbele za kiti cha enzi cha Mungu na mbele ya Mwana-kondoo wake, wakipaza sauti: “Ushindi kwa Mungu wetu aketiye juu ya kiti cha enzi, na kwa Mwana-kondoo!” (Ufu. 7:9-15; NE) Hawa wataungana na “wazao [wa mwanamke] waliosalia” katika kumwimbia Yehova Mungu “wimbo mpya” kwa ajili ya ushindi wake wa kimungu. Waokokaji hawa wote wa dunia ndio ambao Shetani yule joka mkuu alichochea “wafalme wa nchi, na majeshi yao” juu yao kwa kusudi la kuwaangamiza wote hao wenye kumwunga mkono Yehova Mungu na ufalme wake wa Kimasihi. Kwa kufanya vita juu ya hawa, kwa kweli “wafalme wa nchi, na majeshi yao” wanafanya vita juu ya Mungu na kumfanya Mungu na Mfalme wake wa wafalme achukue hatua ya vita.
19. (a) Je! waokokaji hao watainua mkono wenye jeuri juu ya wafalme wa dunia, na ni maneno gani ya manabii wa Mungu watakayoyakumbuka, kuuongoza mwenendo wao? (b) Waokokaji duniani watawaigaje Waisraeli baada ya kukombolewa kwao katika Bahari ya Shamu?
19 Waokokaji hawa hawatachukua silaha zo zote za jeuri juu ya “wafalme wa nchi, na majeshi yao” mpaka mwisho wa “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.” Watamtegemea Mungu Mwenyezi kwa ulinzi wake, kwa maana wanayakumbuka maneno ya Mungu kwa watu wake waaminifu wakati mmoja wa vita uliotangulia: “Vita si yenu bali ni ya Mungu.” (2 Nya. (Sik.) 20:15) Wanayakumbuka pia maneno ya nabii Musa katika Bahari ya Shamu, wakati ambapo magari ya vita ya Misri yalikaribia yawaangamize watu wa Musa: “Simameni, nanyi mtauona ushindi ambao BWANA atawashindieni leo.” (Kut. 14:13, NA) Na kama vile Musa na watu wake waliokombolewa walivyoimba wimbo wa sifa kwa ushindi wa Yehova, ndivyo na waokokaji hawa duniani wa “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” watakavyouimba “wimbo mpya” wa sifa kwa ushindi wa kimungu wa Yehova Mungu, Mwenyezi. (Kut. 15:1-21) Je! twataka tuwe kati ya waimbaji hao?
MWADHIMISHO WA USHINDI
20, 21. (a) Dunia itakuwaje na shangwe kwa kuuadhimisha ushindi wa kimungu? (b) Ushindi utapatwaje juu ya dunia yote kwa utimizo wa amri ya Mungu kwa Adamu na Hawa?
20 Kama vile kunapokuwa na ushindi wa kitaifa na nchi yote inakuwa na shangwe, ndivyo na baada ya “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” na kufungwa kwa Shetani yule joka mkuu na malaika zake wa kishetani katika shimo kubwa, dunia yote itakavyoanza kuwa na shangwe kwa kuuadhimisha ushindi wa kimungu. (Ufu. 16:14, 16; 20:1-3) Ndipo dunia, inayoharibiwa sasa na wataka vita na wachafuaji wake, itakapotoa ushuhuda wa kwamba Mfalme mpya aitawala dunia yote, yaani, Mfalme wa Mungu wa Kimasihi, Yesu Kristo. Mashahidi wa ushindi wa kimungu wenye kuokoka watafanya jitihada mara moja waigeuze dunia hii iwe Paradiso kutoka bahari mpaka bahari na kutoka kaskazini ya dunia mpaka kusini yake. Ushindi utapatwa juu ya dunia yote, kwa utimizo wenye ushindi wa amri ya Mungu kwa mwanamume na mwanamke wa kwanza katika Bustani ya Edeni:
21 “Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”—Mwa. 1:28.
22. (a) Ushindi huu utamaanisha nini kwa dunia kwa bahari ya uzuri na mazao ya chakula? (b) Tuna uhakikisho gani wa mambo yaliyotukia kweli wa ushindi wa Mungu juu ya mauti kwa ajili ya wanadamu waliokombolewa?
22 Kutiishwa huku kwa dunia yote hakutamaanisha uzuri wa kibustani tu kwa makao ya kidunia ya wanadamu, bali pia na chakula tele kwa wakaaji wote wa dunia, bila ya umaskini wo wote. Mungu Mwenyezi aweza kufanya kwa njia halisi na ya kiroho pia alivyoahidi katika unabii wa Isaya, sura ya 25 si kwa ajili ya mashahidi wenye kuokoka tu wa ushindi wa Yehova katika vita ya siku Yake kuu penye Har–Magedoni, bali pia na kwa ajili ya wafu wote waliokombolewa watakaofufuliwa kutoka makaburini waijaze Paradiso ya kidunia na watu bila shida: ‘kuwafanyia mataifa yote’ karamu ya vyakula vyenye kuendeleza uzima na ‘kumeza mauti hata milele.’ (Isa. 25:6-8) Ndiyo, Mungu Mwenyezi ataupata ushindi juu ya mauti kwa ajili ya wanadamu wote waliokombolewa. Alimfanyia Mwanawe Yesu Kristo hivyo, aliyemfufua kutoka kifo cha kupigania imani siku ya tatu, katika mwaka ujulikanao sana wa 33 C.E. Anafanya hivyo pia kwa ajili ya kanisa la kweli la wafuasi wa nyayo za Kristo, ambao Mungu Mwenyezi anawafufua kutoka mautini kama viumbe vya kibinadamu vya kidunia kwenye uzima usiokoma na usioharibika mbinguni kama viumbe vya kiroho.
23. Kwa habari ya ufufuo huo, mtume Paulo anamhesabia nani ushindi kwa kuimeza mauti milele?
23 Kwa habari ya ufufuo huu wa kimbinguni wa wafuasi wa kweli wa Kristo wasio wanafiki, mtume Paulo aliyaandika maneno haya kwa Wakristo walishirikio tumaini hili: “Sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa. Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda. Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako? Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati. Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.”—1 Kor. 15:53-57.
24, 25. (a) Wakati wa utawala wa Kristo wa miaka elfu Mungu ataendeleaje kushinda mauti, nao watakaofaidika kutokana na hili watakuwa na pendeleo la nafasi gani? (b) Ushindi wa kimungu ujao wa Yehova utakuwa na maana gani kwa wanadamu wanaotaabika, nako kuikumbuka kunatuvuta tutake kufanya nini?
24 Wakati wa utawala ujao wa miaka elfu wa Masihi Yesu na kanisa lake au kundi lililofufuliwa na kutukuzwa, Mungu Mwenyezi atapata ushindi juu ya mauti hata zaidi kwa kuagiza wafu wa kibinadamu waliokombolewa wafufuliwe kutoka usingizi wa mauti na kurudishwa kwenye nafasi za uzima katika dunia ya Paradiso. Mauti kama tulivyoirithi kwa mwanadamu wa kwanza mkaidi haitamezwa milele mpaka kila kaburi la taifa la kibinadamu lililokombolewa limeachwa tupu, nalo hili litatukia kwa ‘kufufuliwa kwa wenye haki na wasio haki pia.’ (Matendo 24:15) Kutii ufalme wa Mungu wa Kimasihi kwa wafu wa kibinadamu waliofufuliwa kutaelekeza kwenye furaha milele katika dunia iliyokamilishwa chini ya enzi kuu ya Mungu yenye haki ya ulimwengu wote.
25 Njia ya kuzifurahia baraka hizi zote zilizo bora itatayarishwa na ushindi wa kimungu ujao wa Yehova. Kwa kweli ushindi wa kimungu ulio mtukufu unamaanisha mazuri ya ajabu kwa wanadamu wanaotaabika leo. Ee na tuikumbuke maana yake na kujionyesha kustahili kupata baraka za milele kutokana na ushindi wa kimungu kwa sifa istahiliyo ya Mungu kupitia kwa Yesu Kristo Bwana wetu!
—Kutoka The Watchtower, Oct. 15, 1973.
[Picha katika ukurasa wa 467]
Shetani “yule joka mkuu” anawaongoza watawala wa kisiasa na kuwaelekeza kwenye uharibifu bila ya wao kujua
[Picha katika ukurasa wa 471]
WAFU WATAISHI TENA
MUNGU ANAWAHAKIKISHIA CHAKULA TELE WAKAAJI WOTE WA DUNIA