Ushindi Juu ya Ulimwengu Bila Vita Yenye Silaha
“Ulimwenguni mtakuwa na taabu. Lakini ujasiri! Ushindi ni wangu; mimi nimeushinda ulimwengu.”—Yohana 16:33, The New English Bible.
1. (a) Kwa sababu gani ushindi wa ulimwengu bila vita yenye silaha ungekuwa tendo kubwa? (b) Wafafanuzi wengine wa Biblia wanatazamia nini juu ya utawala wa kutumia nguvu wa ulimwengu, na je! utakuwapo?
USHINDI juu ya ulimwengu mzima wa wanadamu bila vita yenye silaha bila shaka ungekuwa tendo la ajabu. Waelekea kutowezekana—zaidi kwa kuwa ulimwengu ni kambi yenye silaha, kama ulivyo leo. Ushindi wa ulimwengu bila vita ya kijeshi siyo maoni ya mataifa ya kisiasa wakati huu. Wao hawaamini kwamba taifa lo lote wala mtu mmoja angeweza kupata ushindi wa ulimwengu na nyuma ya hapo autawale ulimwengu kwa ujuzi tu wenye amani wa kisiasa. Serikali za kisiasa ambazo zimekuwapo kwa muda mrefu ni zenye werevu mwingi mno juu ya hila ya ujuzi wa mataifa yote kutoweza kuruhusu zitendewe jambo kama hilo. Viongozi wachache wa kidini wa Kristendomu wanaojaribu kuufafanua unabii mbalimbali wa Biblia Takatifu wanatabiri kuwako kwa utawala wa ulimwengu wa kutumia nguvu katika wakati ujao ulio karibu. Na nani? Na yeye ambaye wanamwita “Mpinga Kristo,” ambaye vile vile wanamwelewa kuwa “mtu wa dhambi,” “mwana wa kupotea milele.” (2 The. 2:3-10, Authorized Version; 1 Yohana 2:18) Lakini, tofauti na imani hiyo, hakutakuwako mpinga Kristo mmoja atakayepata ushindi juu ya ulimwengu bila vita yenye silaha.
2, 3. (a) Kulingana na Maandiko Matakatifu, nani leo wawezao kuupata ushindi huo wa ulimwengu, nako kuupata kuna zawadi gani? (b) Ni mfano gani wa historia tulio nao kuuonyesha uwezekano wake, nasi tuna maneno gani ya ushindi ya huyo?
2 Maandiko matakatifu yaliyoongozwa na roho ya Mungu yako wazi sana juu ya shauri la ambaye anatokea akiwa mshindi juu ya ulimwengu bila kuchukua silaha kali sana za vita ya kumwaga damu. Kwa kulingana na Maandiko haya matakatifu yaliyopewa na Mungu, sisi wenyewe kama watu wamchao Mungu twaweza kuupata ushindi huo. Zawadi ya ushindi huo ndicho kipawa cha uzima wa milele katika taratibu mpya ya mambo yenye haki na furaha, ambamo hatutakuwa na ulimwengu huu mwovu wa kushindana nao. Ushindi huo unaostahili zawadi unafaa kupatikana, sivyo? Ushindi wenye thawabu kama hiyo isiyo na kifani imetupasa sote tutamani kuupata, sivyo? Ujapokuwa huenda uelekee kuwa wa ajabu mno, unaweza kufanyika. Tunao mfano wa kihistoria kuhakikisha kwamba unaweza kufanyika. Mfano huu wenye kutia moyo ni ule wa mwanamume aliyefanya hivyo miaka 1,900 iliyopita, mwanamume ambaye jina lake si lisilojulikana kwa ulimwengu mzima wa wanadamu. Mwanamume huyo alikuwa Yesu Kristo. Katika siku yake ya mwisho kama mwanadamu duniani, yeye alisema, kwa mlio wa ushindi katika sauti yake:
3 “Mimi nimewaambieni haya yote kusudi kwamba katika mimi mwe na amani. Ulimwenguni mnayo dhiki. Lakini ushikeni ujasiri wenu: Mimi nimeupata ushindi juu ya ulimwengu.”—Yohana 16:33, The New Testament in Modem Speech, na R. F. Weymouth (1902).
4. Ni kwa sababu ya matokeo gani muda mfupi tu kufuata maneno ya Yesu yaliyodai ushindi twauliza namna ambavyo alikuwa ameupata ushindi?
4 Sasa ni mwaka wa 1974 wa Wakati wetu wa Kawaida, na hali ulimwengu haujashindwa kusudi umwamini Yesu Kristo. Kwa hiyo je! ni kwa njia gani Yesu Kristo alivyoupata ushindi juu ya ulimwengu? Yeye alipokufa kama mhalifu aliyelaaniwa saa chache tu nyuma ya kudai ushindi juu ya ulimwengu, hakuwa amelishinda taifa lake mwenyewe, watu wa Kiyahudi, kusudi wamkubali yeye kama Masihi wao aliyeahidiwa, kama Mtiwa Mafuta wa Mungu. Siku 51 nyuma ya kifo chake cha aibu, kulikuwako karibu watu 120 tu kati ya Wayahudi Yerusalemu walioshikamana naye kama Masihi aliyeutimiza unabii wa Biblia. (Matendo 1:15) Basi je!, Yesu Kristo alikuwa na haki ya kusema kwamba alikuwa amekwisha kupata ushindi juu ya ulimwengu? Ni kwa njia gani iwezekanayo ambavyo ushindi wake uliodaiwa ungeweza kutufaidi leo? Ebu na tuone.
5. (a) Namna ambavyo Yesu aliuawa ilionyesha kwamba Warumi na Wayahudi walikuwa na maoni gani juu yake? (b) Yesu aliwaambia wanafunzi wake kwamba wangechukiwa na wangapi?
5 Ebu mtazame yeye pale Ijumaa hiyo, Nisani 14, ya mwaka wa 33 C.E., amepigiliwa misumari mtini namna ambavyo Warumi wapagani walivyowatundika watumwa waliolaaniwa, ndiyo, na akining’inia pale katikati ya watenda mabaya wawili! Hali hiyo ilimwaibisha kama mtu aliyechukiwa, aliyechukiwa na wote Warumi na Wayahudi waliokuwa wamemtoa kwa Warumi auawe katika njia iliyo ya aibu zaidi sana. Hata saa nyingi mbele ya kuuawa kwake huko Kalvari nje ya mji wa Yerusalemu, Yesu Kristo alikubali kwamba yeye alikuwa mtu aliyechukiwa. Ni vibaya sana kuchukiwa na mtu mwingine bila haki, lakini Yesu Kristo alichukiwa na wangapi? Kwa wale kumi na mmoja waliobaki kati ya mitume wake kumi na wawili wa kwanza Yesu Kristo alisema: “Ulimwengu ukiwachukia, mjue kwamba umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa sehemu ya ulimwengu, ulimwengu ungekipenda kilicho chake wenyewe. Sasa kwa kuwa ninyi si sehemu ya ulimwengu, bali mimi nimewachagua kutoka katika ulimwengu, kwa sababu hii ulimwengu unawachukia ninyi.”—Yohana 15:18, 19, NW.
6. Mitume mmoja mmoja walikuwa na lazima ya kufanya nini juu ya chuki ya ulimwengu kwao?
6 Hivyo Yesu aliwafahamisha mitume wake kwamba ulimwengu ulimchukia yeye, na vivyo hivyo ulimwengu ungewachukia wao. Ingewapasa kufanya nini juu ya jambo hili? Basi, ulimwengu mzima unapomchukia mtu, mtu anao ulimwengu mzima wa kushindana nao na kwa hiyo yampasa mtu apate ushindi juu ya ulimwengu mzima. Mtu anayechukiwa ulimwenguni pote lazima ama aushinde ulimwengu ama sivyo ashindwe nao. Kama sivyo angewezaje mtu kuhakikisha kwamba yeye yumo katika haki, kwamba ni wa kweli, kwamba ni mwaminifu?
KWA SABABU GANI CHUKI YA ULIMWENGU
7, 8. (a) Kuna habari gani juu ya kama chuki ya ulimwengu ilimshangaza Yesu? (b) Twasoma nini juu ya mazungumzo yake na ndugu zake za baba-mzazi mmoja muda mfupi tu mbele ya sikukuu ya vibanda katika mwaka wa 32 C.E.
7 Ili tuelewe namna Yesu Kristo alivyopata ushindi juu ya ulimwengu, lazima tuelewe ni kwa nini ulimwengu ulimchukia. Ni kwa sababu ya kuwa nini au kwa kufanya nini ilimpasa kusimama apambane na ulimwengu mzima? Yeye hakushangazwa na chuki ya ulimwengu juu yake. Yeye alifahamu kwa nini ulimchukia, na kwa hiyo angeweza kuvumilia. Alionyesha wazi sababu ya nia ya ulimwengu kumwelekea yeye nyuma ya karibu miaka mitatu ya utendaji wake wa waziwazi katika nchi ya Palestina. Hili lilitukia katika nusu ya pili ya mwaka wa 32 C.E., huko katika jimbo la Kirumi la Galilaya, ambako Yesu alikuwa amekuwa seremala katika mji wa Nazareti mpaka umri wa miaka 30. Alikuwa na ndugu kadha wachanga wa baba-mzazi mmoja, wana wa mama yake Mariamu, na, ndugu hawa wa baba-mzazi mmoja walimtolea mashauri fulani juu ya kazi yake ya waziwazi bila ya kukaribishwa. Hata wakati huo Wayahudi wakatili walikuwa wakingoja nafasi ya kumwua, kwa sababu ya chuki yao juu yake. Kwa hiyo ulizo lilikuwa, Je! angejitoa nje kwao waziwazi katika Yerusalemu katika sikukuu ya vibanda ya majira ya vuli iliyokuwa inakaribia? Kama Myahudi chini ya sheria ya Mungu kupitia kwa nabii Musa, Yesu alikuwa na lazima ya kuwapo. Juu ya mazungumzo yake na ndugu zake za baba-mzazi mmoja, twasoma:
8 “Wayahudi walikuwa wakitafuta kumwua. Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya Vibanda, ilikuwa karibu. Basi ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Uyahudi, wanafunzi wako nao wapate kuzitazama kazi zako unazozifanya. Kwa maana hakuna mtu afanyaye neno kwa siri, naye mwenyewe ataka kujulikana. Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu. Maana hata nduguze hawakumwamini. Basi Yesu akawaambia, Haujafika bado wakati wangu; ila wakati wenu sikuzote upo. Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu.”—Yohana 7:1-7.
9. Ni kwa njia gani Yesu hakushindwa kuihudhuria sikukuu hiyo ya vibanda, na ni ushindi gani alioupata huko katika hekalu?
9 Je! Yesu Kristo alipanda kwenda Yerusalemu kwa uaminifu, ambako wale waliomchukia wangekuwa wakimiminika kwa ajili ya sikukuu ya vibanda? Ndiyo, yeye alifanya hivyo, lakini si kwa upumbavu. Juu ya hili twasoma: “Hata ndugu zake walipokwisha kukwea kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipokwea, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri.” Katika wakati uliofaa, aliwahutubia waziwazi wenye kuadhimisha sikukuu huko katika hekalu. Maagizo yakapelekwa na wenye mamlaka wa Kiyahudi wakamkamate, lakini haya hayakutimilizwa na maafisa wa polisi. (Yohana 7:10, 32-48) Je! huo haukuwa ushindi kwa Yesu Kristo?
10. (a) Yesu aliwaambia nini ndugu zake za baba-mzazi mmoja juu ya iliyokuwa sababu ya ulimwengu kumchukia yeye? (b) Kwa kuwa Yesu hakutoka nje ya Uyahudi, ingewezaje kusemwa kwamba ushuhuda wake juu ya kazi za ulimwengu ulikuwa kweli?
10 Je! ni sababu gani aliyoitoa kwa ajili ya chuki ya ulimwengu juu yake? Sababu, kama ilivyosemwa kwa ndugu zake za baba-mzazi mmoja, ilikuwa: “Hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu.” (Yohana 7:7) Basi, sasa, ikiwa kazi za Wayahudi ambao kwao peke yao Yesu alikuwa amehubiri zilikuwa “mbovu,” kungeweza kusemwa nini juu ya kazi za ulimwengu wa kipagani nje ya ule wa Kiyahudi? Lazima ziwe zilikuwa mbovu kama zile za Wayahudi waliokuwa wakatili kwa Yesu Kristo. Kwa hiyo, juu ya ulimwengu mzima wa wanadamu, wa Kiyahudi na wa Mataifa, ushuhuda ungeweza kutolewa kwa ukweli kwamba kazi zake zilikuwa “mbovu.” Je! hiyo haitoshi kuchochea chuki kwa upande wa ulimwengu?
11. (a) Ni kwa mfano gani wa kipekee Yesu alivyoshuhudia kwamba kazi za ulimwengu zilikuwa mbovu? (b) Tendo la Yesu hekaluni karibu na mwanzo wa kazi yake ya waziwazi lilihakikishaje kazi za ulimwengu zilikuwa mbovu?
11 Hata hivyo, ni namna gani Yesu alivyoushuhudia ulimwengu na kuonyesha kwamba kazi zake zilikuwa “mbovu”? Kwa neno la kinywa na kwa tendo vile vile. Yeye mwenyewe alipaswa kutokuwa na hatia ya kazi mbovu. Nani wa siku zake duniani angeweza kumshtaki kwa kweli juu ya kazi moja mbovu? Hata wasioamini wa Kiyahudi alipambana nao kwa ulizo: “Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi?” (Yohana 8:46) Wakati alipoingia katika hekalu la Yerusalemu mwanzoni mwa kazi yake ya waziwazi na kuwafukuza wavunja fedha na wafanya biashara, akisema: “Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara,” alikuwa akiwashuhudia wachafuaji hao wa hekalu na wenye mamlaka wa Kiyahudi walioliruhusu jambo hili kwamba kazi zao zilikuwa “mbovu.”—Yohana 2:13-17.
12. Yesu alitoaje ushuhuda juu ya kazi mbovu, kwa kuponya wakati wa Sabato, kwa kufukuza mashetani, kwa kutokutoa ishara yo yote ya kimbinguni, kwa kutokujifanya mwenyewe sehemu ya ulimwengu?
12 Wakati hali zilipojitokeza kwake katika Siku ya Sabato ya Kiyahudi iliyo halali afanye kazi njema za kuponya naye akafanya kuponya huko ujapokuwa uhakika wa kwamba yeye alijua angelaumiwa na kulaaniwa kwa sababu hiyo, alishuhudia kwamba matendo ya wenye kumlaumu yalikuwa ‘maovu.’ (Mt. 12:9-16) Alipofukuza mashetani katika watu waliopagawa nayo naye akashtakiwa juu ya kuwa na umoja na Beelzebuli mtawala wa mashetani kwa kufanya hivyo, Yesu alionyesha wazi kwamba kazi za wapinzani wake zilikuwa mbovu. (Mt. 12:22-37) Wakati Wayahudi wasioamini walipoomba ishara kutoka mbinguni kwa uhakikisho wa kuwa kwake Masihi naye akakataa kukuondoa kutokuamini kwao kwa ishara zisizostahili, alishuhudia kwamba kazi zao mbovu zilikuwa zile za “kizazi kibaya na cha zinaa.” (Mt. 16:1-4; 12:38-45) Kukataa kwa Yesu kuuiga ulimwengu huu na kujifanya mwenyewe kama huo au sehemu yake wenyewe ulikuwa ushuhuda wa kwamba kazi za ulimwengu zilikuwa “mbovu.”
13, 14. (a) Ni kwa njia gani mbili zilizo kubwa Yesu alivyoshuhudia kwamba kazi za ulimwengu zilikuwa mbovu? (b) Kuhubiri kwake Yesu kulipatanaje na aliyoyasema katika Yohana 3:17?
13 Lakini, Yesu hakushuhudia juu ya ulimwengu huu kwa kuyaacha maisha yake yajisemee yenyewe tu ili kuionyesha wazi chuki yake. Yeye alifanya hivyo moja kwa moja kwa neno la kinywa vile vile. Hii maana yake nini?
14 Basi, Yesu mwenyewe alimwambia mtawala wa Kiyahudi Nikodemo: “Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu,” yaani, kuuhukumu vibaya au kuulaani, akilihukumia taifa la kibinadamu uharibifu. (Yohana 3:17) Kwa hiyo, Yesu hakuzunguka-zunguka nchini akilaani kila kitu alichoona, akifanya hivyo wakati wote, akiitangaza “siku ya kisasi cha Mungu wetu” peke yake. Sivyo, bali yeye alikuwa nao ujumbe hakika ulioelekeza kwenye uhuru wa laana. Huu ulikuwa ndio ujumbe wa Ufalme.—Isa. 61:1, 2; Luka 4:16-41.
15, 16. (a) Maneno ya utangulizi ya ujumbe wa Yesu wa Ufalme yalishuhudiaje kwamba kazi za ulimwengu zilikuwa mbovu? (b) Mambo yale yale yaliyokuwamo katika ujumbe wa Ufalme nayo vile vile yalitoaje ushuhuda huo?
15 Lakini je! ujumbe huu hakika uliushuhudia ulimwengu kwamba kazi zake zilikuwa mbovu? Ndiyo! Nalo hili laonyeshwa katika namna ambavyo ujumbe wa kifalme ulivyotangulizwa. Habari ya Mathayo yatueleza namna Yohana Mbatizaji alivyoutanguliza ujumbe wa Ufalme kisha namna Yesu Kristo mwenyewe alivyofanya hivyo. Nyuma ya kufungwa kwa Yohana Mbatizaji, Yesu Kristo alichukua ujumbe wa Yohana naye akaukuza. Juu ya hili, Mathayo 4:17 anatuambia: “Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”
16 Neno lile lile la utangulizi wa ujumbe, “Tubuni,” lilionyesha kwamba kazi za wasikilizaji wa ujumbe wa Ufalme zilikuwa mbovu. Iliwapasa kutubu watoke katika kazi hizo mbovu na kugeuka na kujitayarisha kwa kuja kwa Ufalme. Kwa sababu gani hivyo? Kwa sababu serikali hiyo ya kimungu isingewaruhusu raia zake wazoee kazi mbovu. Kwa kweli, wale ambao walizoea kazi mbovu wasingeruhusiwa kuingia katika vyeo vya kiserikali katika ufalme huo. (1 Kor. 6:9, 10) Ufalme huo ulipaswa kuwa serikali yenye haki, na uhakika wa kwamba Mungu wa mbingu aliiona haja ya kusimamisha ufalme huo ulizilaani falme zote za ulimwengu huu kama zilizo mbovu. Ulishuhudia kwamba taratibu hizo za kilimwengu za utawala zilikuwa mbovu na siku moja, katika wakati wa Mungu uliowekwa, zingepaswa kuharibiwa. Hii ndiyo sababu wale waliokuwa wakiutangaza na kuuendeleza “ufalme wa mbinguni” wasingeweza kwa kupatana kujitia katika siasa za ulimwengu, wasingeweza kushika vyeo vya kisiasa katika serikali yo yote iliyoundwa na mwanadamu wala kushiriki katika vita yo yote yenye silaha kushika tawala hizo za kilimwengu. Kama mabalozi na wajumbe wa ufalme wa Mungu wanajiepusha na siasa chafu za kibinadamu.
17. Kwa sababu gani watawala wa ulimwengu na wasaidizi wao walimchukia Yesu kwa ajili ya kuuhubiri ujumbe wa Ufalme?
17 Je! ulimwengu ulimchukia Yesu kwa sababu ya kuzihubiri habari njema za “ufalme wa mbinguni”? Ushuhuda waonyesha kwamba ulimwengu ulimchukia yeye kwa sababu hiyo. Watawala wa ulimwengu na wasaidizi wao walikuwa na maoni yao wenyewe na mipango juu ya namna ambavyo dunia na watu wake inavyopaswa kutawaliwa. Wao waliuchukia ujumbe uliomtokeza Yehova Mungu kama akikusudia kuziharibu falme zao na tawala katika wakati Wake mwenyewe ufaao. Wao walipendelea ujumbe uliomtokeza Mungu kama akizitegemeza serikali zao zilizoundwa na mwanadamu, ukiwakubali na kukusudia kuwaendeleza wao na kuendelea kuwaweka katika uwezo. Kwa hiyo, ujumbe uliotangaza ufalme ambao usingeshirikiana na taratibu zao za utawala na kufanya kazi kupitia kwazo ulikuwa jambo ambalo vyombo vya kisiasa vya ulimwengu huu havikupendezwa nalo. Viliuchukia huo pamoja na watangazaji wake. Vilimchukia Mtiwa Mafuta ambaye Mungu alikusudia kumweka katika uwezo katika “ufalme wa mbinguni.”
KUISHINDA CHUKI YA ULIMWENGU
18, 19. (a) N’nini kilichoufanya ulimwengu umchukie Yesu kwa ajili ya kuuhubiri ujumbe wa Ufalme? (b) Yesu aliwaambiaje mitume wake kwamba chuki ya ulimwengu haikuwa kwa ajili ya sababu halali?
18 Je! Yesu aliistahili chuki ya ulimwengu kwa sababu ya kuuhubiri ufalme wa Mungu wa Kimasihi? Je! kwa njia hiyo alikuwa akihubiri jambo fulani ambalo lingewadhuru wanadamu wote? Sivyo, bali jambo fulani kwa ajili ya faida yao ya milele. Kiburi cha kipekee na choyo ndiyo mambo yaliyouvuta ulimwengu kumchukia Yesu kwa ajili ya kuutangaza ujumbe wa Ufalme ambao ulikuwa habari njema kweli kweli, Injili. Kwamba chuki ya ulimwengu juu yake kwa kweli haikuwa kwa ajili ya sababu halali, Yesu aliwaambia mitume wake waaminifu, akisema:
19 “Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa hawana udhuru kwa dhambi yao. Yeye anichukiaye mimi humchukia na Baba yangu. Kama nisingalitenda kwao kazi asizozitenda mtu mwingine, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa wametuona mimi na Baba yangu, na kutuchukia. Lakini litimie lile neno lililoandikwa katika torati yao, Walinichukia bure.”—Yohana 15:22-25; Zab. 35:19; 69:4.
20. Wayahudi walionyeshaje kwamba Yesu alichukiwa kwa ajili ya kuuhubiri ujumbe wa Ufalme walipokuwa mbele ya Gavana Pilato?
20 Kuonyesha kwamba ulimwengu ulimchukia Yesu kwa sababu ya kuuhubiri ufalme wenye haki wa Baba yake wa kimbinguni, adui za Yesu walikimbilia hila ya kisiasa wamfanye auawe na Warumi wasiopendezwa wakati huo na maulizo ya kidini. Walikutumia kuhubiri kwa Yesu juu ya serikali kamilifu kwa ajili ya wanadamu kama chombo cha kumshtakia uhalifu wa kisiasa juu ya Milki ya Kirumi, mamlaka ya ulimwengu ya wakati huo. Wakati Gavana wa Kirumi wa Uyahudi, Pontio Pilato, alipotaka washtaki wa Yesu walitendee shauri hilo kama la kidini kabisa likitia ndani sheria yao ya kidini na kuwaambia: “Haya! mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu!” wao walijibu: “Sisi hatuna ruhusa [chini ya sheria ya Kaisari] ya kuua mtu.” (Yohana 18:31) Ili kufanya mageuzi ya kisiasa juu ya mambo ambayo Yesu alihubiri, washtaki wake walimwambia Pilato: “Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme. . . . Huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi wote, tokea Galilaya mpaka huku.”—Luka 23:1-5.
21. Washtaki wa Yesu walimfanya Pilato ajisikie mwenyewe yumo katika shauri hilo kwa njia gani?
21 Kisha, mwishowe, ili kumfanya Gavana Pilato ajisikie mwenyewe yumo katika shauri hilo, washtaki wake Yesu wakasema: “Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari. . . . Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.”—Yohana 19:12-15.
22, 23. (a) Wakati huo Yesu alifanywa chombo cha chuki moja kwa moja na “ulimwengu” kwa njia gani? (b) Wanafunzi wake Yesu waliuonyeshaje uhakika huu nyumaye katika sala?
22 Kwa kuwalazimisha Warumi wapagani namna hiyo kushiriki katika kumwondosha Mhubiri huyu wa “ufalme wa mbinguni,” washtaki wa Kiyahudi waliilazimisha Milki ya Kirumi kufanya tendo lenye chuki juu ya Yesu. Mbele ya askari za Kirumi kumpeleka kwenye mahali pa kufia katika Kalvari nje ya Yerusalemu, walimtendea kwa kumwaibisha kama mfitini mhalifu. Kwamba kwa njia hii Yesu alifanywa chombo cha chuki ya ulimwengu moja kwa moja, wanafunzi wake mwenyewe walionyesha wazi nyumaye walipokuwa wakitoa sala kwa Mungu, wakisema:
23 “Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa [roho takatifu] kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, na wakuu wamefanya shauri pamoja juu ya [Yehova] na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee.”—Matendo 4:24-28.
24. Ni kusudi gani lililofuatana na chuki ya ulimwengu juu ya Yesu lililopaswa kushindwa?
24 Hakuna mtu awezaye kutilia shaka kwamba Yesu Kristo hakupambana na chuki ya ulimwengu. Lakini ulizo lililo la muhimu ni, Je! yeye aliiruhusu chuki ya ulimwengu ipate ushindi juu yake? Je! mwishowe aliiinamia kwa kushindwa nayo? Basi, chuki hiyo ya ulimwengu ilikuwa ikijaribu kumlazimisha Yesu Kristo kufanya nini? Ilichochewa na Shetani Ibilisi kumwogofya ajitiishe. Ilikusudiwa kumvuta aache kufanya kazi zake zenye nguvu za mwujiza zilizohakikisha kwamba yeye alikuwa ndiye Masihi aliyeahidiwa aliyepelekwa na Yehova Mungu. Ilikusudiwa kumshawishi asizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu wa Kimasihi tena, kumnyamazisha kama Mwalimu na Mhubiri. Ilikusudiwa kumfanya mwasi juu ya Yehova Mungu aliyemtia mafuta na kumwagiza kama Masihi. Ndiyo, chuki hii ya ulimwengu ilichochewa juu ya Yesu Kristo kumfanya awageukie watu na kuwachukia na ajitenge na mwendo wake wa kujitoa mwenyewe wa kuutoa uhai wake mkamilifu wa kibinadamu kusudi waweze kupata uzima wa milele chini ya ufalme wa Mungu wa Kimasihi ulioahidiwa. Chuki ya ulimwengu ilikusudiwa kumharibu yeye kwa kumfanya ajaribu kuuokoa uhai wake wa kidunia wa kibinadamu, ili aipoteze nafsi yake, tumaini lake la ufufuo kwenye uzima wa milele.
25. Chuki ya kilimwengu ilishindwaje kumwachisha Yesu kufanya kazi zenye uwezo za mwujiza hata kufikia saa chache za kuuawa kwake?
25 Je! chuki ya ulimwengu ilifanikiwa katika kuyatimiliza mambo haya yote kwa habari ya Yesu Kristo? Je! yeye alikubali kushindwa na kuacha kufanya miujiza na kazi njema ambazo Masihi aliyeahidiwa aliagizwa kuzifanya? Hasha! Hata saa chache mbele ya kuhukumiwa kwake kwenye kifo, alifanya mwujiza, kuonyesha kwamba yeye alipinga vita yo yote yenye silaha. Wakati wa kusalitiwa kwake katika Bustani ya Gethsemane karibu na Yerusalemu, mtume wake Petro alichomoa upanga na kulikata sikio la mwanamume wa kundi lenye silaha lililotoka kuja kumkamata gizani. Lakini Yesu alionyesha kukataa matumizi ya upanga kisha akaliponya sikio la mwanamume huyo, kwa njia hiyo akitoa ushuhuda kwa kuhani mkuu wa Wayahudi, kwa maana mwanamume huyu aliyeponywa, Malko, alikuwa mtumishi wake kuhani mkuu.—Mt. 26:48-54; Luka 22:47-51; Yohana 18:10, 11.
26. Yaweza kusemwa nini juu ya kama Yesu aliiruhusu chuki ya ulimwengu imzuie asikuze kuhubiri kwa Ufalme hata miezi sita ya mwisho ya huduma yake ya waziwazi?
26 Basi je!, chuki iliyoendelea ya ulimwengu ilimshinda Yesu katika kujitiisha na kumlazimisha akifunge kinywa chake na asizihubiri habari njema za Ufalme tena? Ushuhuda wa watu walioyaona haya unajibu Hapana! Akiendelea peke yake katika utangazaji wa kukaribia kwa Ufalme nyuma ya kufungwa kwa Yohana Mbatizaji, Yesu alijikusanyia wanafunzi naye akachagua kumi na wawili wanaopaswa kuwa naye wakati wote na ambao aliwataja kama mitume. Mwadhimisho wa Kupitwa ulipokaribia mnamo huduma yake ya waziwazi, aliwatuma mitume kumi na wawili wakiwa wawili wawili, wakauhubiri ujumbe ule ule aliokuwa ameendelea kuuhubiri, kwa maana aliwaambia: “Katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.” (Mt. 10:1-7) Nyuma ya mwadhimisho wa tatu wa sikukuu ya vibanda ya Kiyahudi mnamo huduma yake ya waziwazi, Yesu aliwatuma wanafunzi wengine 70 kama wahubiri wa injili, vile vile wakiwa wawili wawili, nao aliwaambia: “Mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia.” (Luka 10:1-9) Hii ilikuwa mnamo miezi sita ya mwisho ya maisha yake ya kibinadamu.
27, 28. (a) Yesu alikuleta kuhubiri kwa Ufalme katika taifa lote kwenye upeo wa ajabu kwa mshindo wenye kutazamisha kwa njia gani? (b) Kwa sababu gani Yesu hakuikomesha kelele ya Ufalme wakati huo aliposihiwa afanye hivyo?
27 Sasa Kupitwa kwa nne na kwa mwisho kwa huduma yake ya waziwazi kulikaribia. Siku ya wasiwasi iliyoutikisa mji wa Yerusalemu kwa kidini ilifika. Hii ilikuwa Jumapili, Nisani 9, ya mwaka wa 33 C.E., siku tano mbele ya kifo chake chenye kushtua. Siku hiyo Yesu alikuleta kuhubiri kwake kwa ufalme wa Mungu katika taifa lote kwenye upeo wa ajabu kwa mshindo wenye kutazamisha. Juu ya Mlima wa Mizeituni kuelekea mashariki ya Yerusalemu, alikalia mwana-punda naye akaenda juu yake kama Mfalme wa Kimasihi kuelekea mji wa kifalme, bila ya kutumikiwa na kundi la askari wapanda farasi wenye mikuki, bila ya kikosi cha magari ya vita yenye kwenda mbiombio wala kikosi cha askari wa kwenda mguu wenye silaha zote, sivyo, bila ya jeshi lenye nguvu ambalo lingaliweza kuwafanya askari za Kirumi watoke katika makao ya majeshi kwa kumiminika katika Jumba la Antonia kwenye pembe ya magharibi ya kaskazini ya eneo la hekalu, ili kulizuia shambulio la Yerusalemu. Sivyo, lakini kwa utimizo wa unabii wa Zekaria 9:9, alipanda katika maandamano ya amani yenye ushindi akitumikiwa na kundi lenye shangwe la wanaume wasio na silaha, wanawake na watoto, aliowaruhusu wamtangazie Ufalme.
28 Kati ya kelele zilizotokea kwenye kundi lenye kutembea zilikuwa hizi: “Umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi.” “Ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la [Yehova].” “Hosana! Ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la [Yehova], Mfalme wa Israeli!” Wakati adui wenye kujawa na chuki walipovipinga vigelegele hivi vya Kimasihi vya watu, Yesu alisisitiza kwamba unabii ulipaswa kutimizwa kwa kusema: “Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele.”—Mt. 21:6-16; Marko 11:4-11; Luka 19:32-40; Yohana 12:12-16.
29. Hivyo Yesu alitimizaje unabii, naye alionyesha nini?
29 Hivyo unabii wa Zekaria 9:9 haukuwa umetangaza bure hivi miaka 500 mapema: “Shangilia moyo na nafsi, binti Sayuni! Piga kelele kwa furaha, binti wa Yerusalemu! Tazama sasa, mfalme wako akujia; yeye ni mwenye shangwe, ni mshindi, ni mnyenyekevu naye apanda juu ya punda, juu ya mwana-punda.” (Jerusalem Bible) “Kwa maana tazama, mfalme wako akujia, upande wake umeshinda, ushindi wake ukapatikana, ni mnyenyekevu naye apanda juu ya punda, juu ya mwana-punda, mwana wa punda-jike.” (The New English Bible) Si kama kwa kujionyesha tu, bali katika utiifu wa unabii wa Mungu usiovunjika, Yesu alipambana kishujaa na chuki ya ulimwengu naye akaushuhudia ufalme wa Mungu wa Kimasihi kwa njia ya kutazamisha. Kwa njia hii alionyesha kwa unabii namna ambavyo angepanda kwa ushindi na kujiweka mbele ya tengenezo la kitheokrasi la Yehova kama Mfalme wake wa haki, nyuma ya mwisho wa Majira ya Mataifa katika mwaka wa 1914 C.E., na nyuma ya kikomo cha vita mbinguni.—Luka 21:24; Ufu. 12:5-10.
30. (a) Ni kwa njia gani Yesu hakuiruhusu chuki ya ulimwengu iigeuze nia yake mwenyewe? (b) Aliulaumuje unafiki wa kidini kwa habari ya Ufalme?
30 Chuki ya ulimwengu haikumkomesha Yesu wala katika kufanya miujiza kwa uhakikisho wa Umasihi wake wala katika kuhubiri kwake habari njema za ufalme wa Mungu wa Kimasihi. Wala haikumfanya ajifunze roho yake wala kujawa na chuki yenye ukorofi juu ya taifa la kibinadamu alilokuwa amekuja kulikomboa, wala haikumsukuma awe mwasi juu ya Mungu na mapenzi ya kimungu. Penye hekalu, katika wonyesho wa huruma yake kwa waliodanganywa, watu walioonewa, aliulaumu unafiki wa kidini waziwazi naye akasema: “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie.” (Mt. 23:1-13) Siku tatu nyumaye, si kwa roho yo yote ya uasi juu ya Mungu, Yesu alikuadhimisha Kupitwa kwa Kiyahudi Yerusalemu pamoja na mitume wake. Mara tu nyuma ya hapo akaanzisha mwadhimisho mpya, chakula kipya cha jioni, kama ukumbusho wa kifo chake kama dhabihu ya kibinadamu.
31. Ni kwa njia gani ambavyo maneno ya Yesu juu ya kikombe cha divai na kwa habari ya Ufalme hayakukanusha dai lake nyumaye juu ya kupata ushindi juu ya ulimwengu?
31 Alipokuwa akieleza maana ya kikombe cha divai kilichopaswa kunywewa penye chakula hiki cha jioni cha ukumbusho, Yesu aliwaambia mitume wake waaminifu: “Nyweni katika hiki, ninyi nyote; kwa maana hiki chamaanisha ‘damu ya agano’ yangu, itakayomwagwa kwa ajili ya wengi kwa msamaha wa dhambi.” (Mt. 26:26-28, NW) Hakuna chuki juu ya taifa la kibinadamu iliyoonekana katika maneno hayo, wala uasi wo wote juu ya mapenzi ya Mungu kwake yaliyotia ndani kifo cha dhabihu. Ndipo, mazungumzo yalipoendelea nyumaye, Yesu aliwaambia mitume wake: “Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu. Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi; mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.” (Luka 22:28-30) Nyumaye, mwishoni mwa mazungumzo yake na mbele ya kutoa sala ya mwisho kwa Mungu, Yesu aliwaambia: “Ulimwenguni mtakuwa na taabu. Lakini jipeni moyo! ushindi ni wangu; mimi nimeushinda ulimwengu.”—Yohana 16:33, NE.
32. (a) Kwa sababu gani Yesu alikuwa na haki ya kudai ushindi juu ya ulimwengu wakati huo wa usiku? (b) Ushuhuda wake mbele ya Pilato ulilitegemezaje dai lake?
32 Katika saa hiyo ya usiku wa Nisani 14, je! Yesu alikuwa na haki ya kudai ushindi juu ya ulimwengu mzima? Kwa sababu ya mwendo wake mwaminifu wa maisha, wenye upendo mpaka wakati huo, twaweza kujibu, Ndiyo! Yesu hapo hakuwa akijivuna kwa kujitukuza mwenyewe. Mwendo wake usiogeuka wa utiifu kwa Mungu katika saa zilizofuata ulihakikisha hivyo. Alipokuwa amesimama mbele ya mjumbe aliye mkuu zaidi wa Kaisari wa Milki ya Kirumi wa mahali pake, Yesu alikataa kukana kwamba hakuwa Mfalme wa Mungu aliyetiwa mafuta lakini akamwambia Gavana Pontio Pilato: “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa. . . . Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli.” Ujapokuwa ufalme wake wa Kimasihi ni jambo aliloshtakiwa na waliomchukia kama msingi halali ili Warumi wamwue, Yesu hakuukana ufalme wa Mungu.—Yohana 18:36, 37.
33. (a) Akiwa juu ya mti wa mateso, ushindi wa Yesu ulikamilishwaje, na hii ilihakikishwaje nyumaye mbele ya kumalizika siku tatu? (b) Ni ushindi gani ambao ungali ukimngoja Yesu aliyetukuzwa kwa habari ya ulimwengu huu?
33 Muda mfupi nyumaye, Yesu alipokuwa akining’inia akiwa amepigiliwa misumari kwenye mti wa mateso katika Kalvari, waliomchukia walipopita pale nao wakimtukana, yeye hakujifanya kama wao wala kujilipizia kisasi. Wakati, karibu saa tisa alasiri, Yesu aliposema: “Imekwisha” naye akainama kichwa na kupumua mara yake ya mwisho, alikuwa ameupata ushindi kweli kweli juu ya ulimwengu, na hivyo bila vita yenye silaha. (Yohana 19:30; 1 Pet. 2:22-24) Ulimwengu ulikuwa umemwua yeye kama mwanadamu, lakini yeye akafa bila ya kushindwa. Ulimwengu wenye chuki haukupata uradhi wo wote kutokana na kifo chake. Usingeweza, nao haukuweza, kumzuia asiipate zawadi tukufu kwa ajili ya ushindi wake wa ulimwengu. Siku tatu hazikupita kabisa mbele ya Mungu Mwenyezi kumfufua kwa wafu katika ushindi wa ajabu mno juu ya kifo kisha kumkweza kwenye mkono wa kulia wa kiti cha enzi cha Baba yake wa kimbinguni, mbali sana asipoweza kufikiwa na ulimwengu wenye chuki huku duniani, mahali pa Mungu penyewe pa kuwekea miguu yake. (Flp. 2:5-11; 1 Pet. 3:22) Namna nyingine ya ushindi yamngoja yeye, nayo hii pamoja na malaika zake mashujaa watakatifu katika “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” inayokuja penye Har–Magedoni.—Ufu. 16:14, 16; 19:11-21.
[Picha katika ukurasa wa 203]
Yesu hakuiruhusu chuki ya ulimwengu iupate ushindi juu yake kwa kuikomesha miujiza yake na kazi njema. Sivyo, bali muda wa saa chache za kuhukumiwa kwake kwenye kifo aliponya sikio la mwanamume mmoja kwa mwujiza Petro alipokuwa amelikata