Maswali Kutoka kwa Wasomaji
● Je! mume akikubali kuondolewa uwezo wa kuzaa (ama wake mwenyewe ama wa mkewe) hiyo itamfanya asistahili vyeo vya madaraka ya kundi?
Biblia yaonyesha wazi heshima nyingi ya Mungu kwa uwezo wa kuzaa ambao amewapa wanadamu kama zawadi. (Mwa. 1:28; 9:1) “Uzao wa tumbo” ulihesabiwa kuwa thawabu na “urithi wa [Yehova].” (Zab. 127:3) Mtu ambaye makende yake yalikuwa yameharibika sana alikuwa hastahili chini ya agano la Torati ‘kuingia katika kusanyiko la Yehova.’ Uhakika wa kwamba maneno yanayozunguka mstari huu yaonyesha makatazo juu ya waliokuwa wa makabila fulani ‘wasiingie katika kusanyiko la Yehova’ waelekea kuonyesha kwamba mpango huu wahusu wanaume wenye kasoro kati ya wageni waliofuata ibada ya Yehova. (Kum. 23:1-8) Haitajwi kama kuharibu makende kulikuwa kwa makusudi au kwa bila kutazamia. Linalozidi kuonyesha wazi heshima nyingi ya Mungu kwa uwezo wa kuzaa ni kwamba, wakati mwanamke alipojaribu kusaidia mumewe katika mpambano kwa kushika makende ya mpinzani wake, Torati iliagiza mkono wa mwanamke huyo ukatwe. (Kum. 25:11,12) Bila shaka, Wakristo hawafungwi na agano la Torati. Hata hivyo, wanahusika kwa habari ya kanuni zilizomo.
Kutokana na haya twaweza kukata shauri kwamba mwendo wa peke yake upatanao na kusudi la Mungu ungekuwa watu waoe au kuolewa na kuzaa watoto wengi kama iwezekanavyo. Walakini, Maandiko bado yaruhusu uamuzi wa kipekee katika mashauri yanayohusiana na nguvu za uzazi. Kama isingekuwa hivyo, basi ungekuwa mwendo wa kudharau zawadi ya uwezo huo Mkristo ye yote akijizuia asioe au kuolewa na kuzaa watoto. Lakini Kristo Yesu, ambaye mwenyewe alijizuia asioe, alisema hivi: “Wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.” Hao wanaojifanya “matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni” walifanya hivyo kwa kutokuoa au kutoolewa. (Mt. 19:10-12) Kwa kufanya hivyo hawakuwa wakionyesha dharau kwa mpango wa Mungu juu ya uzazi. Mtume Paulo, kama Yesu, pia alionyesha kwamba kutooa au kutoolewa kungeweza kuwa na faida.—1 Kor. 7:25-38.
Wakati uo huo, wala Yesu wala mitume wake hawakusihi Wakristo waliooa na kuolewa wasiwe na watoto. Aliyoyasema Yesu katika Mathayo 24:19 yalikuwa maneno ya unabii yenye uhakika tu—si kusihi Wakristo wa karne ya kwanza waepuke kuwa na watoto, bali wasikawie kukimbia kutoka mji uliohukumiwa maangamizi ishara ya uharibifu wake ilipoonekana. Karibu zaidi na wakati wa uharibifu huo, mtume Paulo alikuwa bado akitia moyo ‘wajane walio vijana wenye nyege waolewe na kuzaa watoto.’—1 Tim. 5:11-14.
Kwa sababu ya mambo haya ya Maandiko, ni wazi kwamba kuzaa watoto kuna kibali ya Mungu. Hivyo, lingekuwa kosa mtu akikubali kuondolewa uwezo wa kuzaa au akikubali kuondolewa kwa uwezo wa kuzaa wa mkewe ati kwa sababu hathamini zawadi ya Mungu ya uwezo wa uzazi. Walakini, namna gani juu ya hali ambapo mke wa mtu amezaa watoto lakini imemlazimu kufanya hivyo kwa kupasuliwa mwili, kama vile kupitia mbavuni? Huenda amepasuliwa mara tatu kwa njia hiyo na daktari wake huenda akamwonya kwamba akipata mimba nyingine yaweza kumtia katika hatari kubwa ya kupasukiwa mimba, ambayo kwa kawaida ni yenye kufisha mama na kitoto kisichozaliwa. Je! kuondolewa uwezo wa kuzaa katika habari hiyo kungeonyesha kwa lazima dharau kwa zawadi ya kimungu ya uzazi?
Yaelekea kuwa wazi kwamba mume na mke hawakuonyesha dharau kwa uwezo wa uzazi, kwa kuwa wamekwisha zaa watoto. Huenda wakaona kuondoa uwezo wa kuzaa kama utaratibu ufaao kulinda uhai wa mama ya watoto waliokwisha kuzaliwa. Huenda wakaona hilo ndilo jaribio la mwisho na hakuna jinginelo liwezalo kufanywa. Hivyo katika kufanya uamuzi wao huenda wakaona kwamba ni shauri la kusawazisha heshima kwa mpango wa Mungu wa uwezo wa kuzaa na heshima kwa zawadi ya uhai yenyewe, katika habari hii uhai wa mama aliye katika hatari. Kwa sababu hii, na kwa sababu zaidi, yaelekea kuwa uamuzi huo u juu ya dhamiri za watu mmoja mmoja wahusikao.
Huenda ikapingwa kwamba, hata chini ya hali hizo, kukubali kuondolewa uwezo wa kuzaa kungeonyesha kukosa imani kwa upande wa wahusikao. Onyo la daktari haliwi kweli kwa lazima; hivyo, sababu gani usingoje na kuona litukialo? Walakini, sababu ii hii yaweza kutumiwa juu ya wanawake wakubalio kuondolewa mji wa mimba kwa kupasuliwa, ambako bila shaka kwaharibu uwezo wa kuzaa. Mara nyingi mji wa mimba huondolewa ingawa mwanamke hafi kweli. Mbali na donda baya sana lianzalo mapema, huenda kukawa na uvimbe mkubwa katika kuta za mji wa mimba unaosababisha maumivu makali au kutokwa na damu nyingi. Uvimbe usio hatari waweza kudhoofika. Kwa kuwa hatari ya ugonjwa wenye kufisha uletwao na vitu hivi ni jambo linaloweza kutokea tu, je! kuheshimu uwezo wa kuzaa kungetaka mwanamke angoje mpaka damu nyingi ianzapo kutoka kabla hajakubali kweli kuondolewa mji wa mimba na kupoteza uwezo wake wa kuzaa? Ni kweli, mwanamke ambaye amezaa watoto kadha wakipitia mbavuni huenda asiwe na uvimbe mkubwa ulio mchungu, lakini wakati uo huo haiwezi kusemwa kwamba tumbo lake la uzazi ni “lenye afya,” kwa kuwa limepasuliwa mara kadha. Mkristo ambaye dhamiri yake yamruhusu aondolewe uwezo wa kuzaa huenda akaona hali ya tumbo lake la uzazi kama jambo hatari liwezalo kutokea sawa na hali nyingine hizi zilizoelezwa.
Huenda wengine wakaona kuondolewa uwezo wa kuzaa kama kukata sehemu za mwili kwa makusudi. Walakini, mtu apasuliwapo mahali pakubwa sehemu fulani za mwili zinakatwa; kwa wazi kupasuliwa mbavuni ili mtoto atokee hapo au kuondolewa mji wa mimba ndivyo kunavyofanya. Hata hivyo, liwapo shauri la kuendeleza afya na uhai, huenda Mkristo akaona aweza kwa dhamiri kukubali apasuliwe mahali pakubwa. Tena, ni shauri la kufikiria mambo ifaavyo, kwa upande mmoja kuheshimu mwili wa mtu ifaavyo na sifa zilizowekwa humo na Mungu na, wakati uo huo, kuheshimu afya pia na kuendelezwa kwa uhai wenyewe. Hii yatoa sababu zaidi kwa nini uamuzi wa kuondolewa uwezo wa kuzaa chini ya hali hizo umepaswa uwe juu ya dhamiri za wahusikao.
Ni uhakika ujulikanao kwamba ni kuepuka ngono kabisa tu kutoako uhakikisho kamili wa kuepuka kupata mimba. Lakini kuepuka ngono kabisa hakupatani na shauri la mtume katika 1 Wakorintho 7:3-5 na, kukizoewa, kwaweza kuongeza kishawishi cha kufanya uzinzi kwa upande wa mmoja wa wenzi. Wakristo ambao kwa dhamiri wanataka kuepuka kuondolewa uwezo wa kuzaa huenda wakapendelea kutegemea kujiweza na njia za kuzuia uzazi ili kuepuka mimba iwezayo kufisha, wakiukubali uwezekano unaohusika. Walakini, je! watu hao wanaweza kwa haki kulaumu wale ambao dhamiri zao zawaruhusu waondolewe uwezo wa kuzaa kama njia ya kulinda uhai uliomo hatarini? Katika kila kisa watu mmoja mmoja wanatafuta kusudi lile lile moja: kuzuia matokeo ya uwezo wa kuzaa, kwa upande mmoja kwa kutumia vyombo au dawa za kuzuia uzazi, kwa upande mwingine kwa kupasuliwa.
Namna gani mtu akubaliye kuondolewa uwezo wa kuzaa kwa sababu mkewe yumo hatarini? Mwili wa mume sio wenye tumbo la uzazi lililodhoofika. Hata hivyo, dhamiri yake ikimruhusu kuondolewa uwezo wa kuzaa, aweza (mume) kupendelea yeye ndiye apasuliwe, badala ya kuwa lazima mkewe apasuliwe tena. Dhamiri yake huenda ikamruhusu au isimruhusu afanye hivyo.
Yanayosemwa hapa yasichukuliwe kama yenye kuonyesha mtu anatiwa moyo aondolewe uwezo wa kuzaa, kama vile tusivyoweza pia kutia moyo matumizi ya njia za kuzuia uzazi kwa wenzi wanaojaribu kuepuka wasiwe na watoto. Daraka la matokeo yo yote au mengine mabaya yasiyotazamiwa, iwe ni wakati wa sasa au ujao, lazima liwe juu ya wale wanaofanya uamuzi. Kuondolewa uwezo wa kuzaa, kama vile kuondolewa mji wa mimba, ni hatua nzito, kwa maana uwezo wa kibinadamu wa kubadili matokeo yake ni mdogo sana.
Basi, kustahili daraka la kundi kwa upande wa mwanamume akubaliye kuondolewa uwezo wa kuzaa kwa sababu mkewe yumo hatarini, lazima kufikiriwe kwa msaada wa kanuni za Biblia na baraza ya wazee ya mahali. Je! kielelezo chake cha maisha kwa ujumla chaonyesha kwamba anaheshimu sana Neno la Mungu au anadharau mashauri yake? Je! ajionyesha kuwa mwaminifu na mzito katika maamuzi yake? Ikiwa nia yake katika kukubali kuondolewa uwezo wa kuzaa ni kwa sababu ya kukosa heshima kwa kanuni za Mungu, nia hii ya dharau ingeelekea kujionyesha wazi katika njia nyingine pia. Kwa upande mwingine, ikiwa anatimiza matakwa ya Maandiko kwa wale wenye daraka la kundi kama yalivyoandikwa katika 1 Timotheo 3, Tito 1 na maandiko mengine, basi uhakika wa kwamba dhamiri yake yaruhusu kuondolewa uwezo wa kuzaa kwa kupasuliwa kama njia ya kulinda uhai si lazima jambo hili peke yake limfanye asistahili. Bila shaka, nia ya kundi lazima ifikiriwe. Kama shauri hili likiwa ulizo kubwa hata litie mashaka sana lingeweza kwa uzito kupunguza uwezo wake wa kutumikia kwa matokeo mema. Wakifikiria mambo haya, wazee wamepaswa basi wafanye uamuzi wao.