Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w99 6/15 kur. 27-28
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Habari Zinazolingana
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1985
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Ni Nani Anayepaswa Kuamua Ukubwa wa Familia?
    Amkeni!—1996
  • Kupanga Uzazi—Maoni ya Kikristo
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
w99 6/15 kur. 27-28

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Kwa kuwa inasemekana kwamba mbinu za kufunga uzazi (“sterilization”) zaweza kubadilishwa mtu akitaka, je, Mkristo anaweza kuziona mbinu hizo kuwa mojawapo ya njia za kuzuia mimba?

Kufunga uzazi kumekuwa njia ya kupanga uzazi inayotumiwa zaidi. Wengi wanaikubali njia hiyo kutokana na sababu za malezi ya kijamii na kielimu na vilevile maoni ya kidini. Jambo hilo la itikadi ya kidini lahusu Mashahidi wa Yehova, ambao wana tamaa kama ile ya mtunga-zaburi: “Ee BWANA, unifundishe njia yako, na kuniongoza katika njia iliyonyoka.” (Zaburi 27:11) Kufunga uzazi kunahusisha nini?

Mbinu ya kufunga uzazi wa wanaume kwa minajili ya kupanga uzazi inaitwa vasectomy. Mirija miwili midogo iliyo katika mfuko wa pumbu hukatwa na kufungwa. Hiyo inaweza kufanywa kupitia njia nyingi za kitiba, lakini kusudi ni kuzuia shahawa zisiweze kupita zinapotoka kwenye mapumbu. Mbinu ya kufunga uzazi wa wanawake inaitwa tubal ligation. Mara nyingi hiyo hufanywa kwa kukata na kufunga (au, kuchoma) mirija ya Falopio, ambayo hubeba mayai kutoka kwenye vifuko vya mayai hadi kwenye tumbo la uzazi.

Kwa muda mrefu mbinu hizo zilifikiriwa kuwa za kudumu—yaani kwamba zilifanya mtu asiwe na uwezo kamwe wa kuzaa tena. Lakini kwa sababu ya kughairi hatua waliyochukua au kwa sababu hali zao zilibadilika, watu wengine wametafuta msaada wa kitiba wa kuwawezesha kuzaa tena baada ya kufunga uzazi kwa kufanyiwa vasectomy au tubal ligation. Kwa sababu ya kuvumbuliwa kwa vifaa vya kipekee na upasuaji unaotumia vifaa vya kipekee, majaribio ya kubadilisha hali za waliofunga uzazi yamefanikiwa. Ni kawaida kusoma kwamba miongoni mwa watu walioteuliwa inawezekana kupata mafanikio ya asilimia 50 hadi 70 ya kubadilisha vasectomy kwa kuunganisha tena sehemu za mirija zilizokatwa. Kuna madai kwamba kuna mafanikio ya asilimia 60 hadi 80 ya kubadilisha tubal ligation miongoni mwa wanawake. Wengine ambao wamejua mambo haya wamehisi kwamba kufunga uzazi si lazima kuwe jambo la kudumu. Huenda wakaamini kwamba kufunga uzazi kwa njia ya vasectomy na tubal ligation ni sawa tu na kutumia vidonge vya kuzuia mimba, kondomu, na diaphragm—ambazo ni mbinu mtu aweza kuacha kutumia ikiwa anataka mtoto. Lakini, tusipuuze mambo fulani mazito.

Mojawapo ni kwamba matazamio ya kurudisha hali ya kuweza kuzaa tena yanaweza kuathiriwa sana na mambo kama kadiri ya madhara yaliyofanyiwa mirija hiyo wakati wa kufunga uzazi, kiasi cha mirija iliyoondolewa au kuwa na kovu, miaka ambayo imepita tangu kufunga uzazi, na katika kisa cha wanaume cha vasectomy, itategemea kama kumetokea kinga za mwili zinazokinza shahawa za mtu huyo. Na jambo ambalo hatupaswi kusahau ni kwamba hospitali za upasuaji zenye vifaa vya kipekee huenda zisiwe zinapatikana katika maeneo mengi, au huenda zina gharama kubwa sana. Basi, wengi ambao huenda wakataka sana hali yao ya kuweza kuzaa tena irudishwe hawawezi kufanikiwa. Mambo yao yamekwisha.a Basi viwango hivyo ambavyo vimetajwa vya kurudisha hali ya kuweza kuzaa tena si halisi, si vyenye kutegemeka.

Mambo fulani yanaonyesha ukweli wa mambo. Makala fulani iliyochapishwa Marekani juu ya kurudisha uwezo wa kuzaa baada ya kufunga uzazi kwa njia ya vasectomy ilisema kwamba baada ya kufanyiwa upasuaji wenye kugharimu dola 12,000, “ni asilimia 63 tu kati ya watu hao ndio wana uwezo wa kutungisha mimba.” Isitoshe, ni “asilimia sita tu ya wanaume wanaofunga uzazi kwa njia ya vasectomy ndio hatimaye hutaka hali yao ibadilishwe tena ili waweze kuzaa.” Katika uchunguzi uliofanywa Ujerumani na Ulaya ya kati, asilimia 3 hivi ya wanaume waliofunga uzazi baadaye waliamua kurudishiwa hali yao ya kuweza kuzaa tena. Hata kama nusu ya majaribio haya yanafaulu, hiyo ingemaanisha kwamba kwa asilimia 98.5 ya watu, kufunga uzazi ni kama hakuwezi kubadilishwa. Na kiwango hicho chaweza kuwa juu zaidi katika nchi iliyo na wapasuaji wachache sana wa kutumia vifaa vya kipekee au hata isiyo nao.

Basi, haifai kuchukua kufunga uzazi kijuujuu tu, kana kwamba ni kuzuia mimba kwa muda. Na Mkristo mwenye moyo mweupe anapaswa kufikiria mambo mengine vilevile.

Jambo kuu ni kwamba viungo vya uzazi ni zawadi kutoka kwa Muumba wetu. Kusudi lake la awali lilitia ndani uzazi kupitia wanadamu wakamilifu, ambao ‘wangeongezeka na kuitiisha nchi.’ (Mwanzo 1:28) Baada ya Gharika kupunguza idadi ya watu ulimwenguni kuwa wanane, Mungu alirudia kutaja maagizo hayo ya msingi. (Mwanzo 9:1) Mungu hakurudia kulitajia taifa la Israeli amri hiyo, lakini Waisraeli waliona kuzaa watoto kuwa jambo lifaalo sana.—1 Samweli 1:1-11; Zaburi 128:3.

Sheria ya Mungu aliyowapa Waisraeli ilidokeza maoni yake kuhusu kuzaa. Kwa mfano, kama mtu aliyeoa angekufa kabla ya kuzaa mwana wa kuendeleza kizazi chake, ndugu yake alipaswa kumzalia mwana kwa kumwoa yule mjane. (Kumbukumbu la Torati 25:5) Jambo linalohusika zaidi ni ile sheria iliyohusu mke aliyejaribu kumsaidia mume wake akiwa anapigana na mtu. Kama mke huyo angeshika sehemu za siri za mtu anayepigana na mume wake, mkono wake ulipasa kukatwa; na jambo muhimu ni kwamba Mungu hakutaka viungo vya huyo mwanamke wala vya mumewe viharibiwe kwa kulipiza kisasi. (Kumbukumbu la Torati 25:11, 12) Kwa wazi, sheria hiyo ingetokeza staha kwa viungo vya uzazi; havikupasa kuharibiwa pasipo sababu.b

Twajua kwamba Wakristo hawako chini ya Sheria ya Israeli, hivyo agizo lililo kwenye Kumbukumbu la Torati 25:11, 12 haliwahusu. Yesu hakuamuru wala kudokeza kwamba ni lazima wanafunzi wake wafunge ndoa na kuzaa watoto wengi kadiri iwezekanavyo, jambo ambalo wenzi wengi wamefikiria wanapoamua njia watakayotumia kuzuia mimba. (Mathayo 19:10-12) Mtume Paulo aliwatia moyo ‘wajane walio vijana zaidi wenye kuwaka tamaa waolewe na kuzaa watoto.’ (1 Timotheo 5:11-14) Yeye hakutaja kwamba Wakristo wafunge uzazi kabisa—kudhabihu kwa hiari uwezo wao wa kuzaa.

Inafaa Wakristo wapime madokezo kama hayo kwamba Mungu hustahi sana uwezo wao wa kuzaa. Ni juu ya kila wenzi kuamua mbinu zifaazo za kupanga uzazi ambazo watatumia na wakati watakapozitumia. Ni kweli kwamba uamuzi wao ungekuwa mzito ikiwa kungekuwa na ripoti za kitiba ambazo zimethibitishwa zinazoonyesha kwamba ama mama ama mtoto atakabili hatari kubwa ya kiafya, hata uwezekano wa kifo, iwapo mama atakuwa mja-mzito. Katika hali hizo, wengine wamekubali shingo upande wafunge uzazi kupitia mbinu iliyotajwa awali ili kuhakikisha kwamba mimba haitatisha uhai wa mama (ambaye huenda tayari ana watoto wengine) au wa mtoto ambaye anaweza kuzaliwa baadaye akiwa na matatizo yenye kutisha uhai wake.

Lakini kwa hakika ingefaa Wakristo ambao hawakabili hatari hususa na isiyo ya kawaida kama hiyo watake kutumia ‘utimamu wa akili’ na kuzingatia kiakili na kwa matendo jambo la kwamba Mungu anastahi uwezo wao wa kuzaa. (1 Timotheo 3:2; Tito 1:8; 2:2, 5-8) Jambo hilo lingeonyesha kufuata kwa njia ya ukomavu madokezo ya Kimaandiko. Lakini, namna gani wengi wakipata kujua kwamba Mkristo amepuuza maoni ya Mungu? Je, wengine wasingetilia shaka kama yeye ni mfano mzuri, mwenye sifa ya kufanya maamuzi yanayopatana na Biblia? Waa kama hilo lenye kusumbua lingeweza kuathiri kustahili kwa mhudumu kupata mapendeleo ya kipekee ya utumishi, ingawa huenda hali isiwe hivyo ikiwa alifanya hivyo pasipo kujua.—1 Timotheo 3:7.

[Maelezo ya Chini]

a Majaribio ya kuunganisha tena [mirija ya shahawa] kupitia upasuaji yamefanikiwa kwa angalau asilimia 40, na kuna uthibitisho wa kwamba mafanikio zaidi yanaweza kupatikana kupitia mbinu bora za kutumia vifaa vya hali ya juu. Hata hivyo, kufunga uzazi kwa njia ya vasectomy kwapasa kuonwa kuwa njia ya kudumu.” (Encyclopædia Britannica) “Kufunga uzazi kwapasa kuonwa kuwa jambo la kudumu. Licha ya mambo ambayo huenda mtu amesikia kuhusu kurudishwa kwa hali ya kuweza kuzaa tena, kuunganisha tena mirija kupitia upasuaji ni ghali, na hakuna uhakikisho kwamba utafanikiwa. Kwa wanawake wanaofanyiwa upasuaji ili waweze kuzaa tena, kuna hatari kubwa ya kushika mimba kwenye mrija wa falopio.’—Contemporary OB/GYN, Juni 1998.

b Sheria nyingine ambayo huenda ikaonekana inahusika ilisema kwamba mtu yeyote ambaye viungo vyake vya uzazi vilikuwa vimeharibika sana hakuruhusiwa kamwe kuwa katika kutaniko la Mungu. (Kumbukumbu la Torati 23:1) Lakini, kitabu Insight on the Scriptures chasema kwamba yaonekana hali hiyo “ilihusu kuhasiwa kwa hiari kwa sababu ya matendo yasiyo ya adili, kama vile ugoni wa jinsia moja.” Kwa hiyo sheria hiyo haikuhusu uhanithi au mbinu inayofanana na kuzuia mimba. Kitabu Insight chasema pia: “Kwa kufariji, Yehova alitabiri wakati ambapo matowashi wangekubalika mbele zake wakiwa watumishi wake na, wakiwa watiifu, kuwa na jina bora kuliko wana na mabinti. Sheria ilipoondolewa na Yesu Kristo, watu wote wanaodhihirisha imani, bila kujali hali zao za zamani, wangeweza kuwa wana wa kiroho wa Mungu. Ubaguzi uliotegemea mambo ya kimwili uliondolewa.—Isa 56:4, 5; Yn 1:12.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki