Yerusalemu Siku za Mitume
HUKO nyuma karne ya kwanza ya W. K. Yerusalemu ulikuwa umekwisha kuwa mji wa kale, maana historia yake iliandikwa tangu kipindi kilichokuwa karibu na mwaka wa 1943 K.W.K. Mji huu (ulioitwa Sayuni pia) haukuendelea kuwako siku za mitume wa Yesu Kristo kwa bahati. Ilikuwa lazima uweko ili unabii mbalimbali uliohusu Masihi utimizwe.—Isa. 28:16; 52:7; Zek. 9:9.
Ingawa Yerusalemu uko futi 2,500 juu ya usawa wa bahari, hauonekani wazi kwa maana umezungukwa na vilima vilima. Mtu aweza kuuona mji wote akikaribia sana tu.
Yerusalemu, ulio katikati ya safu ya milima ya Israeli, una majira ya kupendeza. Nyakati za usiku ni zenye baridi nalo joto la kawaida linakuwa karibu digirii 63 Fahrenheit. Yerusalemu hupata mvua ya karibu inchi 24, hasa kati ya Novemba na Aprili.
Siku za mitume mji wa Yerusalemu ulikuwa punde kuliko maili moja ya mraba. Mji ulilindwa na kuta zilizokuwa katika bonde lililoinama sana upande wa mashariki, kusini na magharibi. Upande wa kaskazini tu ndio usiokuwa na ulinzi wa maumbile, lakini kuta zilizojengwa upande huo zilikuwa imara sana.
HEKALU
Jengo la maana zaidi Yerusalemu lilikuwa hekalu lililojengwa na Herode Mkuu. Eneo la hekalu, kutia na nyua zote, lilichukua eka kati ya kumi na tano na ishirini. Mtu angeweza kuingia eneo hilo kupitia mmoja wa malango manane au kumi. Manne au matano yalikuwa upande wa magharibi, mawili au matatu kusini, na moja-moja upande wa mashariki na kaskazini. Pengine lango la mashariki ndilo lililoitwa “mlango Mzuri,” ambapo Petro aliponyea kiwete wa kuzaliwa.—Matendo 3:1-10.
Safu za nguzo zilikuwa katika sehemu ya nje-nje ya eneo la hekalu. Safu yenye kuvutia zaidi kati ya hizo ilikuwa Safu ya Kifalme upande wa kusini, nayo ilikuwa na nguzo 162 za ajabu ambazo sehemu zake za juu ziliundwa kwa mapambo ya Korintho. Wanaume watatu walihitajiwa wanyoshe mikono na kushikana ndipo waweze kuzunguka mojawapo nguzo hizo. Nguzo hizo zilipangwa katika mistari minne, na kulikuwa na vijia vitatu katikati, nazo zilishikilia paa la ndani la mbao lililojikunja. Njia za kutembelea za nje-nje zilikuwa karibu futi 50 juu, lakini ile ya katikati ilikuwa juu zaidi, maana paa liliinuka katikati. Safu za nguzo upande wa mashariki, kaskazini na magharibi zilikuwa na mistari miwili ya nguzo za maremare, nazo pia zilishikilia paa la ndani. Yesu na wanafunzi wake walijulisha watu kweli ya Mungu mara nyingi wakiwa katika eneo lililofunikwa na paa la safu yenye nguzo ya Sulemani, upande wa mashariki.—Yohana 10:22-24; Matendo 3:11; 5:12.
Eneo jingine lililokuwa karibu zaidi na hilo na lililozungukwa na safu za nguzo lilikuwa Ua wa Mataifa. Kwa kuwa watu wangeweza kuliingia vyepesi kupitia malango mengi, eneo hilo likawa njia kuu. Badala ya watu kuzunguka eneo la hekalu, wakawa wakipitia katika Ua wa Mataifa, wakiwa wamechukua mitungi yao wakielekea shughuli zao za kila siku. Vilevile katika ua huu au katika Safu ya Kifalme, wavunja fedha waliweka meza zao na wengine waliuza wanyama wa kutolewa kama dhabihu. Lakini, Yesu Kristo hakukubali sehemu yo yote ya eneo la hekalu itumiwe kama njia kuu au mahali pa biashara. Alikomesha mambo hayo nyakati mbili.—Mt. 21:12, 13; Marko 11:15-17; Yohana 2:13-16.
Mtu alipokuwa akipitia katika Ua wa Mataifa kutoka kusini, alifikia boma la mawe lenye matundu-matundu hapa na pale. Boma hili la mawe lilikuwa karibu futi nne na nusu kwenda juu. Juu ya boma yalikuwako mawe makubwa yenye mwandiko wa Kigiriki na Kirumi ulioonya Mataifa wasipite, ama sivyo wangeuawa. Hivyo ukuta huu ulitenganisha Myahudi na Mtaifa.—Linganisha Waefeso 2:14.
Ua uliofuata, Ua wa Wanawake, ulikuwa vipandio kumi na vinne juu ya Ua wa Mataifa. Ndio ua ambamo wanawake Wayahudi waliingia kuabudu. Masanduku ya hazina ndimo yalimokuwa, ambamo michango ya patakatifu ilitumbukizwa.—Luka 21:1-4.
Baada ya kutoka Ua wa Wanawake, wanaume Waisraeli waliokuwa safi kisherehe waliingia Ua wa Israeli. Vipandio kumi na vitano vikubwa vilivyokuwa kama nusu-duara vilikwenda kwenye ua huu, navyo vyumba vya kuwekea akiba vya ua huu vilikuwa katika ukuta wa nje.
Ua wenye utakatifu mwingi zaidi ulikuwa Ua wa Makuhani, nao ulizunguka patakatifu penyewe pa hekalu. Ndimo mlimokuwa bahari ya kusubu na madhabahu ya dhabihu za kuteketezwa.
Patakatifu penyewe palikuwa vipandio kumi na viwili juu ya Ua wa Makuhani. Milango ya dhahabu, yenye urefu wa juu wa karibu futi 80 na futi 23 upana, ilizuia mahali pa kuingilia. Upande wa mbele wa jengo ulikuwa mpana zaidi kuliko wa nyuma, nazo pande zake mbili zilikuwa na upana wa futi karibu 29 kila mmoja. Vyumba vilijengwa kando kando ya jengo hili, na kulikuwa na chumba cha juu kilichokuwa juu ya Patakatifu na Patakatifu Zaidi. Eneo la ndani la Patakatifu lilikuwa karibu futi 8 urefu na karibu futi 29 upana, napo Patakatifu Zaidi palikuwa karibu futi 29 za mraba. Jengo lote lilijengwa kwa mawe meupe na kurembeshwa kwa dhahabu iliyopigiliwa ukutani.
NGOME YA ANTONIA
Karibu na eneo la hekalu, katika pembe ya magharibi ya kaskazini, ilikuwako Ngome ya Antonia. Ilikuwa juu ya mwamba ulioinuka karibu futi 73 kwenda juu. Kuta zake za mawe zilikuwa na urefu wa kwenda juu wa futi zaidi ya 53. Kulikuwa na mnara katika kila mojawapo pembe nne za ngome. Minara mitatu ilikuwa karibu futi 73 kwenda juu. Ule wa nne, uliokuwa katika pembe ya mashariki ya kusini, ulikuwa na urefu wa kwenda juu wa futi zaidi ya 100 nao ulielekea eneo lote la hekalu. Makao ya majeshi ya Kirumi yalikuwa katika Ngome ya Antonia.
Kulikuwa na kipito kilichoshikanisha ngome hiyo na eneo la hekalu. Hiyo iliwezesha askari Warumi wachukue hatua ya haraka kumaliza matata huko. Hiyo yaonyesha sababu gani Klaudio Lisia na kikosi cha askari zake waliweza kumwokoa mtume Paulo na kundi la watu wenye ghasia pale pale nje “hekaluni.”—Matendo 21:30-32.
Wengine wanadhani kwamba Yesu Kristo alikwenda mbele ya Pilato ahukumiwe akiwa katika ua wa kati wa Ngome ya Antonia. Pengine mawe ya kutembelea katika eneo hili ndiyo Gabatha inayotajwa katika Yohana 19:13. Lakini pengine Yesu alihukumiwa katika eneo lililo wazi mbele ya jumba la kifalme la Herode, magharibi ya eneo la hekalu.
BIRIKA LA BETHZATHA
Karibu na Lango la Kondoo, ambalo pengine lilikuwa kaskazini mwa eneo la hekalu, lilikuwako birika (kidimbwi) la Bethzatha pamoja na safu zake tano za nguzo. Hapo ndipo Yesu Kristo alipoponyea mgonjwa wa miaka 38. (Yohana 5:2-9) Wachimbuzi wa ardhi walihakikisha mwaka 1888 kwamba birika hilo lilikuwako. Waliona birika lenye sehemu mbili zilizogawanywa na mwamba, zenye eneo la jumla ya karibu futi 150 kwa futi 300. Waliona pia sanamu ya malaika mwenye kuyaendesha maji ikiwa imechorwa ukutani kwa rangi, na ulikuwako ushuhuda wa kuonyesha safu za nguzo zilikuwa tano.
BIRIKA LA SILOAMU
Kusini mwa eneo la hekalu lilikuwako birika la Siloamu, ambapo Yesu Kristo aliagiza kipofu anawe apate kuona. (Yohana 9:6, 7, 11) Chemchemi ya Gihoni, inayoanza katika pango la asili katika Bonde la Kidroni, ndiyo iliyoingiza maji katika birika hili kupitia kwa mtaro uliokatwa kando ya vilima.
MLIMA WA MIZEITUNI NA GETHSEMANE
Upande wa mashariki wa Yerusalemu kuna safu ya vilima vya mviringo vyenye mawe ya chokaa. Zamani za kale mwinuko huo ulikuwa umefunikwa na mizeituni na kwa hiyo ulijulikana kama Mlima wa Mizeituni. Kwa ufupi, mwinuko huo umepita Yerusalemu kwa ujumla wa futi 400 kwenda juu na unawezesha mtu kuona eneo lote la hekalu.—Marko 13:3.
Mahali fulani juu ya Mlima wa Mizeituni au karibu yake ilikuwako bustani ya Gethsemane. Katika bustani hii Yesu Kristo alikutana na wanafunzi wake mara nyingi. (Yohana 18:1, 2) Usiku wa Kupitwa kwa 33 W.K., Yuda Iskariote alimsalitia huko kwa kumpiga busu.—Mt. 26:36, 48, 49.
GOLGOTHA, KABURI LA BUSTANI NA KONDE LA MFINYANZI
Mahali alipotundikwa Yesu palikuwa Golgotha au “Fuvu la Kichwa.” Pengine mahali hapo palikuwa kaskazini mwa Ngome ya Antonia. Karibu yadi 250 (mita karibu 270) mashariki ya kaskazini mwa Lango la Dameski kuna jabali lenye matundu yaliyo wazi yanayofanya lionekane kama fuvu la kichwa. Karibu na jabali hilo pana bustani kubwa, iliyowekewa mpaka kaskazini na kilima. Sehemu ya kuzikia imetayarishwa kwa kukata jiwe kubwa sana lililochongoka upande wa kilima hiki, na hapo pana kaburi moja lililo tayari. Mahali hapo panalingana na maelezo inayotoa Biblia juu ya alipotundikwa Yesu na kuzikwa. (Mt. 27:57-60; Marko 15:22-24; Luka 23:33; Yohana 19:38-42) Lakini, haiwezi kuamuliwa leo kama hapo ndipo mahali halisi.
Mapokeo yanaonyesha ‘konde la mfinyanzi la kuzikia wafu’ lilikuwa upande wa kusini wa Bonde la Hinomu karibu na makutano yake na Bonde la Kidroni. Kuna makaburi mengi katika eneo hilo. “Konde la mfinyanzi” ndilo lililonunuliwa kwa “vipande thelathini vya fedha” ambavyo Yuda Iskariote alimsalitia Yesu. Likaja kujulikana kama Akeldama, “konde la damu.”—Mt. 27:5-8; Matendo 1:18, 19.
HAKUNA UTAKATIFU WA PEKEE LEO
Leo mahali pengi walipotembelea Yesu na mitume wake wakati wa huduma yao ya hadharani hapajulikani sawasawa. Bila shaka kutojulikana kwa mahali hapo kwapatana na kusudi la Mungu, kwa maana ibada ya kweli sasa haitegemei mahali popote. (Yohana 4:21-24) Jambo la maana kweli kweli ni ujumbe ambao Yesu na mitume wake walitangaza. Ujumbe huo umedumu katika Maandiko Matakatifu, nayo kazi ambayo Yesu na mitume wake walianza karne ya kwanza W.K. imefikia miisho ya dunia.
[Ramani katika ukurasa wa 244]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
YERUSALEMU WAKATI WA HUDUMA YA YESU NA MITUME WAKE
Golgotha (?)
Birika la Bethzatha
Ngome ya Antonia
Ua wa Israeli
Ua wa Makuhani
Hekalu
Ua wa Wanawake
Ua wa Mataifa
Safu za nguzo
Jumba la Herode
Birika la Siloamu
Gethsemane (?)
MLIMA WA MIZEITUNI
BONDE LA KIDRONI
BONDE LA HINOMU AU JEHENUM
Akeldama (?)