“Watchtower Movement” au Kitawala
KATIKA mwaka wa 1907 alitokea mtu mmoja huko Afrika ya Kusini aitwaye “Reverend” (Kasisi) Joseph Booth. Alizaliwa katika Uingereza na alipokuwa mwenye umri wa miaka 29 alihamia kwenye nchi ya New Zealand kwenda kufuga kondoo na mwishowe akaanza biashara katika Australia. Alijiunga na wafuasi wa dini ya Kibaptisti na punde kidogo akaona amepata mwito wa kuwa mmisionari katika Afrika basi akafika katika nchi ya Nyasaland (kwa sasa ni Malawi) mwaka wa 1892 kama mmisionari wa kipekee. Booth alitiwa bidii na wazo la usawa wa Waafrika na “Afrika kwa Waafrika.” Alianzisha misheni mbalimbali.
Mnamo mwaka wa 1900 Booth alikuwa amejitenga na misheni zake karibu zote na akawa amesafirisafiri Amerika, ndio huko akawa mwongofu wa dini ya Seventh Day Baptist. Upesi baada ya hapo alirudi Nyasaland ili aanzishe misheni ya dhehebu hiyo ya Kisabato. Muda si muda, akagongana na wafuasi wa Seventh Day Baptist. Kisha akajiunga na wafuasi wa Seventh-day Adventist na kuanzisha misheni. Vile-vile alikosana na wenye mamlaka ya serikali, kwa vile walichukia sana mipango yake ya kuleta mabadiliko ya usawa katika Waafrika. Inaonekana kama katika mwaka wa 1906 Booth alianza kupendezwa na Makanisa ya Kristo na, ijapokuwa alipingwa na British Churches of Christ, alikubaliwa na tawi la Cape Town la South African Churches of Christ. Booth aliwasaidia sana kuanzisha misheni katika Nyasaland. Kulingana na habari ya kitabu Independent Africa, Booth alitoka kwenye dhehebu hii kwenda kwa dhehebu nyingine kama “mtanga-tanga wa dini.”
Kuelekea mwisho wa mwaka wa 1906 Booth, akiwa sasa katika nchi ya Scotland, alisoma baadhi ya vitabu vya Russell. Bila kupoteza wakati alisafiri kwenda United States. Alipofika huko, alipanga aonane na Ndugu Russell na mpango huu ukawa na mazungumzo yenye kukolea sana. Ndugu Russell hakujua sana habari za mwanzo wa Booth na shabaha yake kubwa ya kuirudisha nchi ya Afrika kwa Waafrika. Hakujua kwamba Booth alikuwa amekwisha kuonwa na wakuu wa serikali na wazungu katika Nyasaland kama mtu asiyetakiwa na ya kwamba alikuwa ametumia madhehebu nyingi za kidini ili ziunge mkono mipango yake mwenyewe. Tena, Ndugu Russell alitamani sana kutafuta mtu wa kufanya kazi ya mhubiri wa injili katika nchi nyingine. Kwa sababu hiyo, kwa muda Sosaiti ilimlipia Booth gharama kama mmisionari wake aliyetumwa kwa wale aliojuana nao.
Ndugu Russell hakufahamu sana kwamba kufanya hivi kungetokeza matata mengi juu ya jina la Sosaiti. Kwa vyo vyote, mapema katika mwaka wa 1907, Joseph Booth alirudi Afrika akaanza shughuli katika Cape Town na katika sehemu nyingine za nchi hiyo. Akiwa mtu asiyetakiwa katika Nyasaland, inaonekana kama Booth kwa muda fulani hakurudi huko, ijapokuwa alipashana habari na nchi ya Nyasaland kwa njia ya barua na kwa wajumbe wake mwenyewe aliokuwa akituma huko na huku kukawa na matokeo mengi katika nchi hiyo.
Habari juu ya namna mambo yalivyokuwa yakiendelea katika Afrika ya Kusini zapatikana katika The Watchtower la Januari 15, 1909. Taarifa yasema hivi: “Kuna ndugu weusi watatu wanaoihubiri Kweli kwa wenyeji. Mmoja wa hawa ameelekea kaskazini kama maili 2,000 kwao akapeleke ujumbe huko. Ijapokuwa ndugu huyu ni mchanga, anasema lugha nyingi za kienyeji, anajua sana kuandika Kiingereza. Taarifa iliyotoka kwake karibuni inatia moyo sana. Inaonekana wenyeji wanazisikia Habari Njema za Furaha Kuu, ule ujumbe wa Kurudishwa.”
Kijana Mwafrika aliyetajwa kuwa amesafiri maili 2,000 kuelekea kaskazini kwao alikuwa Elliott Kamwana. Kamwana alikuwa wa kabila ya Watonga na alikuwa amepata elimu kutokana na Livingstonia Mission (misheni ya Scotch Presbyterian) katika Bandawe upande wa magharibi wa ufuo wa Ziwa Nyasa. Walakini, yeye alikuwa amekutana na Booth katika Blantyre, Nyasaland, katika mwaka wa 1900, na akawa amebatizwa miaka miwili baadaye katika Misheni mojawapo ya zile za Seventh Day ambazo Booth alikuwa ameanzisha. Alikuwa amekuja Afrika ya Kusini baadaye, akafanya kazi kwa muda katika mashimo ya madini kisha akakutana tena na Booth katika sehemu ya Cape Town. Inaonekana Kamwana alikaa miezi michache pamoja na Booth afundishwe, kisha akarejea kwao, Nyasaland. Katika The Watchtower la Julai 1, 1909, Booth anasimulia ugawaji wa vikaratasi vya dini katika Johannesburg na Pretoria miongoni mwa Waafrika kisha anasema:
“Wamefurahia sana kuupokea ujumbe ule ule huku ambao wamesikia ukitangazwa kwao, Nyasaland, na Ndugu Elliott Kamwana. Mtu ambaye amekuwa huku miezi mitatu tu anasimulia kwamba alimwona Elliott akibatiza watu 300 siku moja; mwingine anashauri kwamba kuna wafuasi mahali pamoja 700.”
Kuelekea mwisho wa ripoti hii, Ndugu Russell alitia habari za karibuni sana juu ya kukamatwa kwa Elliott Kamwana kwa uchochezi wa Calvinistic Scotch Missionaries wa Bandawe, Ziwa Nyasa. Ndugu Russell anamalizia ripoti kwa maneno machache akisema: “Mwaka jana Ndugu Kamwana alibatiza watu 9,126.” Hakuna maelezo tena juu ya mtu huyu. Wakati huo walikuwako wachache sana kuliko hesabu hiyo waliobatizwa katika United States nzima! Lakini Kamwana alibatiza namna gani? Ni njia gani zilizotumiwa?
Kwa hakika, wala Booth wala Kamwana hawakuwa wametoka katika Babeli Mkuu, wala kuacha mafundisho ya uongo; hawakuwa wamekuwa Wanafunzi wa Biblia wala mashahidi wa Kikristo wa Yehova. Uhusiano wao na Watch Tower Society ulikuwa wa muda mfupi na wa juujuu tu. Basi si ajabu kwamba Elliott Kamwana, mwanafunzi wa kiroho wa Booth hakuzifahamu vizuri kweli zilizotolewa katika vitabu vya Sosaiti. Lakini haiwezekani kusema hasa alivyohubiri wakati aliporudia Nyasaland. Bila shaka inaonekana shughuli yake kubwa ilikuwa mabatizo ya hadharani. Lakini mabatizo haya yaliyofanywa na Kamwana hayakuhusiana na ubatizo wa kweli wa watumishi wa Yehova. Lo lote alilosema au njia yo yote aliyotumia, shughuli za Kamwana ziliendelea kwa muda mfupi tu, kama kutoka Septemba wa mwaka wa 1908 kufika Juni wa mwaka wa 1909, wakati serikali ilipochukua hatua ya kumfunga, mwishowe akahamishwa kupelekwa kwenye Visiwa vya Ushelisheli. Hakuruhusiwa arudi Nyasaland mpaka mwaka wa 1937, wakati alipoendelea kama kiongozi wa kimojawapo cha vyama vya uongo vya “Watchtower movement.”
Kwa matokeo mabaya, kulitokea hali iliyokuwa yenye kuchafua akili sana kwa muda mrefu katika Afrika ya kati kwa sababu ya kazi ya Kamwana. Vilitokea vyama vilivyotumia kidogo vitabu vya Ndugu Russell. Vyama hivi vilichanganya kweli na mawazo yao mengi na njia zao wenyewe. Kwa njia hiyo, watu wengi walipotezwa. Si vyama vyote hivi vilivyotumia majina “Watchtower” au “Watchtower Society”; kwa kweli, chama cha Kamwana kilikuja mwishowe kuitwa jina la “The Watchman Mission.”
Miaka mingi baadaye, katika mwaka wa 1947, ndugu wenye kusimamia kazi ya kuhubiri Ufalme katika Nyasaland walimwandikia Kamwana kwa sababu madhehebu hizi za uongo za “Watchtower Movement” zilikuwa bado zinachafua akili za watu. Katika jibu lililoandikwa na kutiwa sahihi na Kamwana, anasema hivi: “Watchman Mission (Mlonda Mission) haina wakati wa kupoteza juu ya uvumi kwa sababu weusi na Wazungu wanajua kwamba Watchman Mission ni tofauti na iko mbali na Watch Tower Bible and Tract Society ya Wazungu.”
Basi mambo ya hakika yanaonyesha wazi kwamba Kamwana hakuwa mtumishi wa kweli na aliyejitoa wa Yehova, na inaonekana kama alianza au alianzisha madhehebu mbalimbali za uongo ziitwazo “Watchtower movement.” Inaonekana yote haya yalianza na shughuli yake kali ya mwaka wa 1909. Nguluh, ndugu Mwafrika katika Johannesburg aliyekuwa Nyasaland wakati huo, amefananisha shughuli ya Kamwana na “moto wa mwitu wenye kuteketeza majani.” Siku hizo walikuwako wenyeji wengi waliokuwa wakihama kutoka Nyasaland kwenda kutafuta kazi na mshahara bora. Basi, kwa wazi katika njia hiyo madhehebu za uongo za “Watchtower movement” zilienea katika nchi mbili za Rhodesia, na Congo na mpaka katika Afrika ya Kusini.
Wakati Ndugu Dawson alipotembelea nchi mbili za Rhodesia, mtu mmoja aitwaye Mwana Lesa alifanyiza ogofyo miongoni mwa Waafrika katika Northern Rhodesia. Mwana Lesa (maana yake “Mwana wa Mungu”) alikuwa Mwafrika kutoka Nyasaland; jina lake hasa alikuwa Tom Nyirenda naye alikuja Northern Rhodesia kwa njia ya Congo. Ripoti zamsema kama mfuasi wa madhehebu za “Watchtower movement” aliyejifanya kuwa nabii. Kulingana na masimulizi katika Sunday Times la Julai 1, 1934, yaliyoandikwa na Scott Lindberg, alipata nakala ya kitabu kiitwacho Book of Martyrs cha Foxe. Katika hiki aliona namna wazungu katika nyakati za kale walivyowafunga “wachawi wa kike” kwenye kiti na kuwafisha kwa kuwazamisha katika maji. Kwa wazi jambo hili lilimvutia sana. Alipokuwa akisafiri kijiji kwa kijiji, alihubiri na kuwaambia wenyeji “kwamba [nchi ya] Afrika ni ya Waafrika na ya kwamba inawapasa wazungu wafukuzwe.”
Ndipo Nyirenda alipofanya ushirika na Chiwila, jumbe wa Ulala (sehemu ya mashariki-kusini ya Copper Belt ya sasa). Hawa wawili walifanya shauri pamoja ili Nyirenda aangamize adui za kisiasa za Chiwila kwa kuwaita “wachawi wa kike” kisha wafishwe kwa kuzamishwa katika maji kwa ubatizo ili aweze kushinda uchaguzi wa kuwa mfalme. Bw. Lindberg anasema: “Ndipo Tom alipoambiwa majina ya adui zote za Chiwila. Alikusanya pamoja majumbe akawaambia kwamba alikuwa ametumwa na Mungu aondoe uchawi katika kabila hilo, na kwamba ni lazima kila mwanamume, mwanamke na mtoto abatizwe katika mto.
“Wenyeji washirikina walivutwa kwa hila mahali ambapo mto wenye kwenda kwa kasi na kwa nguvu ulikuwa ukiporomoka sana bondeni kati ya vilima, na hapo, Tom akasimama juu ya jiwe kubwa kati-kati ya mto amevalia kanzu ndefu nyeupe.
“Akawaambia watu kwamba Mungu alikuwa amemtuma kutenga kondoo na mbuzi. Kisha akambatiza kila mtu kwa kuzamishwa katika maji, kwa msaada wa watu hodari wa Chiwila, waliowagandamiza adui zao chini ya maji, vichwa vyao vimeinamishwa mtoni, mpaka wakafa maji.
“Watu waliimba nyimbo wakati waliposimama wakimtazama kila mtu akikata roho, na usiku wote mwitu ulivuma mahubiri ya kiwazimu ya Mwana Lesa.
“Alipokwisha kufisha wenyeji 22 kwa kuwazamisha usiku huo, Tom aliamua avuke mpaka kwenda kukaa katika Jimbo la Katanga la Congo ya Wabelgiji, ambako wenye mamlaka wa Rhodesia hawangeweza kumkamata.”
Mojawapo la mambo ya pekee ya dhehebu hii lilikuwa kutosadiki ufufuo wa wafu. Ndugu Nguluh anasema kwamba waongo hawa walikataa kulipa kodi zao, nao walisema kwamba walikuwa watawala wa ufalme wa Mungu! Madhehebu hizi za “Watchtower movement” zilileta suto juu ya jina la Sosaiti. Mwaka wa 1937 Elliott Kamwana aliachiliwa katika uhamisho wake katika Visiwa vya Ushelisheli akarudi akiwa kiongozi wa mojawapo ya madhehebu hizi za uongo. Vilevile Willie Kavala alikuwa akiendesha shughuli yake ndogo, akijidai kuwa chini ya uongozi wa Judge Rutherford. Kwa sababu ya hali hii ilifaa Sosaiti itoe vitambulisho vya pekee kwa wale waliokubaliwa kama wahubiri. Katika njia hii tofauti ilionekana kati ya mashahidi wa Yehova, chini ya usimamizi wa Watch Tower Bible and Tract Society, na madhehebu hizi za kipagani zilizotumia jina linalofanana na hilo.
Mara nyingi kulipotukia fitina, maasi, fitina kati ya makabila na vituko vyo vyote vyenye kutazamisha kati ya wenyeji, yote haya yalihusiana na madhehebu ya “Watchtower movement.” Jina hilo lilichukiwa sana na wakuu wa serikali. Unaweza kuwazia namna jambo hili lilivyoleta suto juu ya jina la Yehova na tengenezo lake la kweli katika maeneo hayo!
Kama ilivyotangulia kuelezwa, mchafuko huu ulianza na kazi ya Joseph Booth na wafuasi wake katika Nyasaland mapema mwa karne ya 20. Bw. Booth, pamoja na mwanafunzi wake Elliott Kamwana na wengine, walitumia vibaya vile vitabu vya kwanza vya Watch Tower Bible and Tract Society, na huu ukawa ndio mwanzo wa madhehebu ya “Watchtower movement” katika Afrika ya kati. Inaonekana mafundisho haya kutoka Nyasaland yalienea kusini na magharibi ya nchi mbili za Rhodesia mpaka kuingia katika Congo.
Miaka iliyofuata, Sosaiti ilipelekea wakuu wa serikali barua katika Congo ikieleza mambo ya hakika, lakini kwa kadiri fulani wakuu wa serikali walichagua kuendelea kushirikisha shughuli za madhehebu hizi za kienyeji zenye kutumia jina “Watchtower” pamoja na Watch Tower Bible and Tract Society na kazi ya Mashahidi wa Yehova. Makanisa ndio waliokuwa wamesababisha hali hii.
Jitihada zilifanywa sikuzote na Sosaiti ili kupeleka wajumbe waliokomaa katika nchi hiyo bila matokeo mazuri. Uongozi na msaada ulihitajiwa, lakini tengenezo la Yehova halikuruhusiwa kupeleka msaada huo uliohitajiwa sana, na kwa miaka mingi wakuu wa serikali hawakutaka kutofautisha kati ya watumishi wa kweli wa Yehova na madhehebu hizo za “Watchtower movement,” au Kitawala.
Ilikuwa mapema katika mwaka wa 1948 wakati Llewelyn Phillips, mwangalizi wa ghala katika Northern Rhodesia, alipopelekwa huko Belgian Congo kwenda kutetea Mashahidi waliokuwa wakiteswa huko na kujaribu kuomba marufuku juu ya kazi iondolewe. Alikuwa na mazungumzo ya faragha na Gavana Mkuu na wakuu wengine wa serikali na aliweza kueleza juu ya kazi yetu na kuonyesha namna imani na kanuni zetu zilivyo tofauti kabisa na zile za madhehebu ya uongo ya “Watchtower movement” iitwayo Kitawala. Barua rasmi za tarehe ya Machi 15 na Aprili 7, 1948, zilitumwa kwa wakuu hawa wa serikali ili shauri hili liwe katika maandishi.
Lo! ilikuwa baraka gani wakati kazi ya watu wa Yehova ilipokubaliwa mwishowe! Tawi lilianza kutenda kazi kwa jina rasmi la “Mashahidi wa Yehova” ili kuepuka mchafuko wo wote zaidi. Sasa kutofautishwa kwa Mashahidi wa kweli na wale wanaoshirikiana na madhehebu ya uongo ya “Watchtower movement” au Kitawala kuliweza kuendelea kwa haraka. Tangu wakati huo yalikuwako maongezeko ya ajabu katika hesabu ya wale waliokuwa wakiifuata ibada safi ya Yehova Mungu.
—1976 Yearbook.