Kwa Sababu Gani Yakupasa Uzuie Ulimi?
MANENO yanayosemwa yanaweza kubadili sana wengine. Usemi mzuri unaweza sana kuwafaidi. Lakini ulimi usiozuiwa unaweza kuleta madhara makubwa sana.
Mithali ya Biblia yasema kweli kabisa: “Ulimi safi ni mti wa uzima; bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.” (Mit. 15:4) Usemi wenye utulivu unaweza kusaidia wasikilizaji waepuke mwendo unaowaelekeza kwenye kifo. Kwa upande mwingine, usemi uliopotolewa unaleta matata na kuvunja wasikiaji moyo, kuwaumiza na kuwahuzunisha.
Kwa kuwa ulimi unaweza kuwa na matokeo makubwa sana, mema au mabaya, inafaa sana kuzuia ulimi kabisa. Lakini, haiwezekani wanadamu wasiokamilika kufanya hivyo. Mwanafunzi Yakobo alikubali hivyo kwa kusema: “Twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu. . . . Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu. Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga.”—Yak. 3:2, 7, 8.
Je! hiyo yamaanisha haitupasi kamwe kujaribu kuzuia ulimi? Sivyo. Huenda kuuzuia kukawa kazi ngumu sana. Lakini hilo halitupi udhuru wa kuutumia vibaya. Angalia anayoendelea kuandika mwanafunzi Yakobo: “[Ulimi] ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.”—Yak. 3:8-10.
Inakuwa vibaya sana wakati kiungo kile kinachomhimidi Mungu kinapotumiwa kutukana na kuharibu sifa ya watu awapendao—wanadamu walioumbwa kwa mfano wake. Ingawa huenda watu wengine wakajipa udhuru kwa kusema wameghafilikiwa, ni upuzi kudhani inafaa kutumia ulimi kwa njia hiyo. Lingekuwa jambo la kuchukiza kama vile ambavyo lingekuwa kwa kutazamia chemchemi ibubujike maji matamu na machungu, au mmea mmoja au mti fulani uzae matunda ya mti wa namna nyingine. Ilifaa Yakobo akauliza hivi: “Je! chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu? Ndugu zangu, Je! mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini?”—Yak. 3:11, 12.
Zaidi ya hayo, kwa kutumia ulimi vibaya mtu aweza kujidhuru daima. Mwanafunzi Yakobo alikazia jambo hilo. Baada ya kufananisha matokeo ya kutumia ulimi vibaya na kimoto kinachoweza kuwasha msitu mkubwa, Yakobo alisema: “Ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile [huliwasha moto gurudumu la maisha ya asili, NW] , nao huwashwa moto na jehanum.”—Yak. 3:5, 6.
Kweli ulimi unaweza kuwa “ulimwengu wa uovu.” Ebu fikiria maovu yote unaoweza kuleta kupitia kwa kashifa, uchongezi, ushuhuda wa uongo, kusingizia, porojo zenye udanganyifu na mafundisho ya uongo. Mtu anayetumia ulimi vibaya ‘hutia mwili wake wote unajisi.’ Usemi wake huonyesha alivyo kwa ndani. Kwa mfano, mtu anayepatikana mara nyingi akisema uongo huonekana ana kasoro au doa katika adili zake. Yeye si mtu anayeweza kutegemewa akisema jambo, si mtu mwenye usemi mzuri na hawezi kuheshimiwa na wengine.
Lakini maana yake nini ‘kuwasha moto mfulizo wa maumbile’? Katika lugha ya asili iliyotumiwa kuandika maneno hayo (Kigiriki), maneno “gurudumu la maisha ya asili” (yanayotumiwa katika tafsiri ya New World badala ya “mfulizo wa maumbile”) yanamaanisha kwa halisi “gurudumu la uzaliwa.” Labda Yakobo alikuwa akifikiria gurudumu la mbao, kama la gari la farasi, ambalo lingeweza kuwashwa na chuma cha kati ya gurudumu chenye moto. Vivyo hivyo, ulimi unaweza kuchoma maisha yote ya mtu aliyopata alipozaliwa. Labda ulimi usiozuiwa unapotajwa kuwa “huwashwa moto na jehanum” yaonyesha una uwezo wa kuharibu. Au, huenda maana ikawa kwamba matumizi mabaya ya ulimi yaweza kuharibu maisha yote ya mtu aliyopata kwa kuzaliwa hata afikie hatua ya kustahili hukumu ya jehanum.
Yesu Kristo alionyesha wazi kwamba matumizi mabaya ya ulimi yangeweza kuwa na matokeo mabaya hayo. Alisema: “Ye yote asemaye [akimwambia ndugu yake], ‘Ewe baradhuli!’ atastahili Jehanum yenye moto.” (Mt. 5:22, NW) Naam, mtu mwenye kuhukumu vibaya ndugu yake na kumlaani kama “baradhuli,” yaani, mtu ovyo katika adili, angestahili hukumu ya jehanum. Kwa sababu gani? Kwa sababu kwa kumhukumu ndugu yake hivyo angekuwa akisema huyo anastahili hukumu ya jehanum. Katika moyo wake angekuwa akitaka ndugu yake apate hukumu mbaya hiyo. Kwa njia hiyo yeye mwenyewe angestahili hukumu kali aliyotaka ndugu yake apate. Adhabu hiyo ambayo mtu aweza kupewa yapatana na agizo la sheria ya Musa lililosema kwamba shahidi wa uongo apokee adhabu ile ile ambayo mshtakiwa angepokea kama angalipatikana na hatia.—Kum. 19:17-21.
Kwa sababu ya madhara ya daima yanayoweza kutokana na matumizi mabaya ya ulimi, bila shaka yawapasa Wakristo wa kweli watii shauri lililoongozwa na Mungu: “Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. . . . Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya.”—Efe. 4:29-31.
Twawezaje kufanya hivyo? Ulimi hausemi maneno yake wenyewe bali unaongozwa na moyo. Ni kama vile Yesu Kristo alivyoonyesha: “Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.” (Luka 6:45) Kwa hiyo ili kuzuia ndimi zetu, lazima tung’oe wivu na ugomvi mioyoni mwetu na kuendelea kupenda kikweli wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu. (Yak. 3:14-16) Lazima tujaze akili zetu mambo yenye kujenga.—Flp. 4:8.
Kwa kuwa twajua ubora wa kuzuia ulimi, yatupasa tukaze nia tuepuke kutumia vibaya kiungo hicho cha usemi. Tukijikwaa katika kunena, yatupasa tusikitike sana na kumwomba Mungu atusamehe. Vilevile yatupasa tujitahidi kufanya maendeleo tuifanye mioyo yetu nyumba yenye hazina ya mambo mema, ili usemi wetu uwe wenye kujenga wengine.