Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w77 8/15 kur. 365-369
  • ‘Kama Miche ya Mizeituni Kuizunguka Meza Yangu’

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • ‘Kama Miche ya Mizeituni Kuizunguka Meza Yangu’
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • ‘HERI MTU YULE ALIYEWAJAZA KATIKA PODO LAKE’
  • UBORA WA MFANO MWEMA WA WAZAZI
  • UBORA WA KUWA MACHO
  • KUSTAREHESHA NAFSI YANGU
  • MASOMO NA MAZOEZI YA KILIMWENGU
  • ELIMU ILIYO YA MAANA ZAIDI
  • SABABU YA KUFURAHI
  • Kutumia Neno la Mungu Katika Jamaa Zetu Wenyewe
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Kulea Watoto Wenye Furaha Katika Ulimwengu Wenye Mchafuko Mwingi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1982
  • Zoeza Mtoto Wako Tangu Utoto Mchanga Sana
    Siri ya Furaha ya Familia
  • Kuwalea Watoto Wako Wampende Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1983
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
w77 8/15 kur. 365-369

‘Kama Miche ya Mizeituni Kuizunguka Meza Yangu’

Imesimuliwa na Porfirio Caicedo, wa Colombia

KULINGANA na kanuni iliyotajwa katika Zaburi ya Biblia ya 128, mistari tatu na nne, mimi ni mtu mwenye baraka nyingi sana. Hapo panasema: “Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni wakiizunguka meza yako. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye [Yehova].”

Wajua, mimi ni baba mwenye watoto kumi na wanane. Mke wangu mpenzi Belen (Bethlehemu), ‘mzabibu wangu uzaao,’ amenizalia wana kumi na wawili na binti sita.

Mimi nilizaliwa miaka 64 iliyopita katika mji wa Libano, Tolima, Colombia. Ndimi niliyekuwa mdogo zaidi kati ya watoto kumi na wawili. Kwa sababu baba alikufa nilipokuwa kitoto kichanga tu, nilipotimia umri wa miaka kumi na miwili nililazimika kufanya kazi katika kiwanda cha kusubia madini ili kupatia mama na dada yangu mdogo riziki. Halafu nilipokuwa na umri wa miaka 26 nikamwoa Belen, na muda mfupi baada ya hapo tukahamia Bogota, ambao ndio mji mkuu.

Nilijifunza kwa njia ya posta nikawa seremala hodari zaidi, nikawa fundi wa kutengeneza vifaa vya mbao vya kuumbia madini baada ya kuyeyushwa. Nilifungua kiduka changu mwenyewe nyumbani niweze kuangalia vizuri zaidi watoto wangu waliokuwa wakiendelea kuwa wakubwa. Lakini, kabla sijawa mashuhuri katika kazi yangu, nililazimika kutafuta mapato upande mwingine. Kwa hiyo, nilipokuwa sitengenezi vifaa vya kuumbia madini, nilitengeneza gambusi na zeze za namna namna.

Sikuzote mimi nimefurahia kujifunza. Kadiri niwezavyo kukumbuka, hiyo ndiyo mojawapo sababu ambazo nimekuwa nikichukia sana dini za ulimwengu. Ibada zao zenye udanganyifu hazikutosheleza kamwe tamaa yangu ya kujifunza.

Niligundua jambo tofauti na lenye thamani katika vitabu viwili nilivyopewa na mmoja wa Mashahidi wa Yehova aliponitembelea dukani kwangu siku moja mwaka 1950. Mimi nilitaka kujifunza; Mashahidi walikuwa na mambo ya kunifundisha wazi-wazi, kwa wepesi na bila mafumbo. Nilipojifunza naye Biblia nilianza kuweka msingi wa kulea watoto wangu vizuri.

‘HERI MTU YULE ALIYEWAJAZA KATIKA PODO LAKE’

Nifuraha kulea watoto. Ingawa kuwalea ni kazi yenye mashaka inayohitaji jitihada nyingi, inafurahisha. Mimi nakubaliana kabisa na Sulemani mwenye hekima, aliyesema: “Tazama, wana ndio urithi wa [Yehova]. . . Heri mtu yule aliyelijaza podo lake hivyo.” (Zab. 127:3-5) Watoto hufurahisha sana mtu hata anasikitika sana wasipokuwa karibu naye.

Mimi napenda sana watoto wadogo. Nafurahia sana tabia zao za ajabu. Mtoto mdogo ana uzuri fulani ambao ni vigumu kuueleza. Mtoto mdogo hafichi mambo hata kidogo. Aweza kujifurahisha na kitu ambacho si kitu. Akiwa na kikaratasi au uzi anafurahi. Akipoteza kitu chake cha kuchezea, anahuzunika. Huo ndio wakati hasa ninapopenda kuwa na watoto, niwasaidie.

Kwa kuwa mke wangu nami tunapenda watoto wetu kikweli, tulihangaikia kuwapa uongozi unaofaa, tukazidi kufanya hivyo tulipojifunza kweli katika Neno la Mungu. Tulifanya hivyo kwa kuwafundisha na kuwasahihisha pia. Biblia yenyewe yaonyesha kwamba “yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; bali yeye ampendaye humrudi mapema.” (Mit. 13:24) Sikuzote tumetia bidii nyingi kuadibisha watoto wetu. Tunaogopa sana tunapofikiria jinsi ambavyo wangalikuwa kama tusingaliwaadibisha.

UBORA WA MFANO MWEMA WA WAZAZI

Sote twajua kwamba watoto huzaliwa wakiwa waigaji. Wao huiga mambo yote bila ugumu wo wote​—lugha, adabu au desturi. Hasa wao huiga daima mambo yanayofanywa na wazazi wao. Kwa sababu ya kuzaliwa wakiwa waigaji, mimi nadhani masomo bora ambayo watoto wanaweza kupokea nyumbani ni kuwekewa mfano mwema na wazazi wao. Mithali ya Biblia inayofuata inakazia jambo hilo: “Mwenye haki aendaye katika unyofu wake, watoto wake wabarikiwa baada yake.” (Mit. 20:7) Mzazi mnyofu mwenye kushika ukamilifu atakuwa akiwapa watoto wake kitu chenye thamani kuu kitakachowafurahisha wakati ujao.

Maarifa ambayo nimechuma katika Neno la Mungu yamenisaidia sana katika jambo hilo. Jinsi gani? Yamenifundisha ninavyopaswa kuishi mimi. Yaliyoandikwa humo yamenifundisha ubora wa kufuata kweli na kutii. Nimejifunza namna ya mwenendo ambao mimi niliye mume na baba yanipasa kufuata mbele za Mungu na jamaa yangu. Nasadiki kwamba, mtu akizijua sheria za Mungu zisizobadilika na kuishi kupatana nazo, mambo mengine yote ya maisha, kutia na kulea watoto, ni kazi nyepesi.

Mojawapo mambo ambayo yamefanya watoto wetu wawe na maisha mema ni uhusiano mzuri sana nilio nao na mke wangu. Tunaheshimiana sana. Naweza kuona vibaya sana nikimpigia mke wangu makelele. Ningejiona nimetenda udhalimu nikimtendea vibaya. Yeye ananisaidia niwe na maoni hayo kwa sababu hakuna jambo atendalo linalonichukiza. Yeye ni mnyenyekevu sana, anashirikiana nami sana na ni mpole sana. Yeye hutoa maoni yake juu ya jambo lo lote lakini ananiacha mimi nifanye uamuzi, kisha anauheshimu uamuzi wangu. Mmoja wetu akiwa na huzuni, mwenzake hujitahidi awezavyo amfurahishe. Tena, mmoja akiwa anaadhibu mtoto, mwenzake atamsaidia badala ya kumkataza.

UBORA WA KUWA MACHO

Njia moja ambavyo tumeepuka matatizo ya bure na watoto wetu ni kuwachunga kwa upendo, kuwa macho. Wanapaswa kulindwa kama mmea mdogo. Sikuzote tumesisitiza tukitaka kujua walikuwa wapi na walikuwa wakifanya nini. Kivulana ye yote alipoondoka nyumbani, ilikuwa lazima aende pamoja na mshiriki mkubwa zaidi wa jamaa au mtu mwingine mwenye kutumainika. Sikuzote ilikuwa lazima wasichana wapelekwe mahali na mtu, hata wawe wana umri gani.

Kwa sababu hakuna usalama siku hizi na watu hawaheshimiwi, sikuzote nimejiona kuwa na haki ya kulinda binti zangu hasa. Sikuwakataza pendeleo la kuwa na rafiki kati ya watu tunaowajua na kushirikiana nao. Lakini jambo hili la kuwaacha wawe peke yao huko nje-nje​—wataachwa na mwingine, si mimi​—siwezi kuwaacha wakiwa peke yao katika mji huu.

Kwa sababu wavulana hawamo katika hatari kubwa hivyo, tumewapa uhuru mwingi zaidi kuliko wasichana. Hata hivyo, lazima wawe wamekwisha rudi nyumbani saa fulani ikifika, hata wawe wana umri gani. Karibu nyakati zote hakuna mmoja wao amefika nyumbani akiwa amechelewa, kwa maana alipofika, alikuwa akikuta mlango umefungwa barabara. Nilikuwa nikimfungia nje kwa muda katika baridi ya usiku, kisha namfungulia. Kwa sababu wanajua jinsi ninavyoudhika wanapochelewa, hawachelewi tena.

Wakati mtu anapokuwa macho kuchunga watoto wake, mara nyingi hakuwi na haja ya kuwaadhibu. Ndiyo kusema, “Usipoziba ufa utajenga ukuta.” Huenda wazazi wasiojali watoto wao wakajikuta wakiwaadhibu kwa sababu ya kosa ambalo wao wenyewe wanashiriki lawama, kwa sababu hawakuwaonya.

KUSTAREHESHA NAFSI YANGU

Yako mambo zaidi yanayohitajiwa ili kufaulu kulea watoto, nayo ni ya maana kama kuwawekea mfano mwema na kuwa macho kuwachunga. Wasipotii kwa makusudi, fimbo halisi huwatengeneza sana, ikitumiwa vizuri. Kufanya hivyo nako kunafurahisha wazazi, kama Mithali 29:17 inavyoonyesha: “Mrudi mwanao naye atakustarehesha; naam, atakufurahisha nafsi yako.”

Nikimwagiza mtoto wangu afanye jambo naye asilifanye pronto (upesi), namkumbusha tena. Akiendelea kutolifanya namwadhibu, kwa sababu naona amekosa kutii kwa makusudi. Kwa sababu nimejaribu nyakati zote kufuata mpango huo, watoto wangu hutii bila ya kuwaambia mara mbili.

Lakini, kabla ya kutumia fimbo halisi, mimi humwita mtoto faraghani na kumpa sababu zinazofanya fimbo ihitajiwe. Namweleza waziwazi sababu gani nitamwadhibu. Tena, kufanya hivyo kunanizuia nisimwadhibu kwa hasira.

Bila shaka, namna nyingine za adhabu zaweza kuwa na matokeo mazuri pia. Kila mtoto yuko tofauti; watoto wote hawatii kwa njia ile ile. Huenda ukakaripia sana wengine kwa kuwatazama kwa jicho baya tu. Wengine hutii wakinyimwa kitu wanachopenda sana.

Nakumbuka adhabu iliyomtengeneza Horacio, mwanangu wa tano, wakati fimbo halisi iliposhindwa. Alikuwa apata umri wa miaka minane. Alidai sana ashirikiane na wavulana wabaya katika ujirani. Kwa hiyo nikamwagiza avae mavazi ya mmoja wa dada zake. Alibaki nyumbani kwa sababu ya kutotaka kuonekana na mavazi hayo.

Wakati fulani nilipoona dalili mbaya za ukaidi zikionyeshwa na mwanangu wa tatu na wa sita, Efrain na Ciceron, niliamua kuwapeleka shambani kwa babu yao. Wakati huo mmoja alikuwa na umri wa miaka kumi na minane na yule mwingine kumi na mitano. Mara walipofika, baba-mkwe wangu alijua walipelekwa huko wakaadhibiwe. Alifurahi kuweza kufanyiza kazi wajukuu wake. Yeye ni mtu anayependa kazi, kwa hiyo hukasirishwa sana na mtu mvivu au mwenye kujikalia kitako tu. Wavulana wangu walipaswa kuamka kila asubuhi saa kumi na moja na kufanya kazi mashambani katika joto la ikweta, huku mashamba yakiwa na nyoka na nyigu (wadudu wakubwa kuliko nyuki), nao wakawa na makovu mikononi. Walipofanya kazi hiyo mwezi mmoja walithamini zaidi jinsi wanavyopaswa kuwa nyumbani.

Hivi majuzi nakumbuka niliagiza wavulana wanne wangu wakanyolewe. Kulingana na maoni yangu, nywele zao zilikuwa ndefu mno. Efrain, ambaye ndiye mkubwa kati yao, alikuwa na umri wapata miaka 20 wakati huo. Baada ya siku chache walikuwa hawajakwenda bado, kwa hiyo nikawaambia: “Efrain, Rafael, Horacio, Ciceron, njoni! Mtakwenda nami.” “Haya, baba.” Hawakujua kusudi langu mpaka tulipofika kwa kinyozi. Nikamwambia kinyozi: “Tafadhali ninyolee vijana hawa kama vile ungeninyoa mimi​—uwanyoe vizuri wawe na nywele fupi, tena fupi!”

MASOMO NA MAZOEZI YA KILIMWENGU

Kwa sababu ya kutokuwa na pesa wanangu wamesoma masomo ya msingi tu. Hata hivyo, baadaye wengine walipata masomo ya mambo fulani ya ufundi. Niliogopa kuwapa wengine masomo ya juu sana wasije wakajitutumua kwa kiburi na kupiga ubwana juu ya ndugu zao wasio na elimu nyingi. Basi, kwa sababu sikuweza kuwapatia wote masomo ya juu, sikumpa ye yote.

Hata hivyo hali zangu zimeniwezesha kufuata kanuni ya wazazi wa kale Waisraeli. Licha ya kufundisha watoto wao kusema na kuandika, walifundisha wana wao kazi za ufundi zilizoweza kuwapatia fedha. Maoni yao yalikuwa kwamba mtu asiyefundisha mwanawe ufundi fulani alikuwa akimfundisha kuiba. Nimefurahi sana kufanya kazi na wanangu wote katika duka langu la ufundi, walipomaliza masomo ya msingi.

Licha ya kuweza kufundisha wanangu ufundi, yaani, kazi ya kuwapatia pesa, nimeweza kuwafundisha mambo mengine ya maana kwa kuwa pamoja nao, mambo yanayohusu maisha ya kila siku, kama kufanya kazi, jinsi ya kutatua matatizo, jinsi ya kuendelea kufanya kazi bila kuiacha mpaka imalizike, jinsi ya kuwaza na jinsi ya kufanya maamuzi.

Kwa kufanya kazi pamoja tumekuwa na umoja, tukapendana, tukawa tukipashana habari kwa njia ambayo wao na mimi tunaiona kuwa bora. Tangu walipokuwa wakikalia ubao wakinitazama nikifanya kazi na kuzungumza nami, wanangu wamekuwa hawaogopi kunieleza tatizo liwalo lote. Wao ni wenzi na washiriki wangu wa daima. Nafurahi kuheshimiwa nao, nao wanafurahi kuheshimiwa nami. Tunapofanya kazi, si lazima niwatolee maagizo ya ukali. Kunakuwa na matokeo yale yale mazuri ninapowapa mawaidha kwa upole, halafu kunakuwa na hali ya uchangamfu katika duka lote la ufundi.

Kwa kuwa najua kuna wakati wa kupumzika, nafurahi kwa vile nimeweza kufanya jambo fulani pamoja na watoto wangu niwapumzishe. Sikuzote nimependa sana muziki. Kabla sijaoa, nilijifunza habari za muziki nikajua kupiga gambusi (guitar) za namna namna. Vijana kadha wangu wanajua kupiga gambusi, nasi tunapokuwa na vikaramu vidogo binti zangu hufurahi kuimba huku vyombo vya muziki vikipigwa.

ELIMU ILIYO YA MAANA ZAIDI

Zaidi ya elimu ya kimwili na mazoezi mazuri ambayo watoto wangu wamepokea, wamepokea elimu ya namna nyingine yenye matokeo mazuri zaidi. Kwa kusema hivyo namaanisha elimu yao ya kiroho.

Katika upande huu pia, Belen nami tumejaribu kuwekea watoto wetu mfano mwema. Kwa kujifunza Neno Mungu sisi wenyewe tumejua jinsi Yehova anavyotutazamia tumwabudu na kumtii. Inakuwa vyepesi kwetu kujaribu kuishi kupatana na mapenzi Yake katika mambo yote. Kufanya mapenzi ya Mungu si desturi ya ibada yenye mambo mengi magumu. Bali, ni kufanya daima mambo fulani makuu, mambo ya akili, na kuishi kupatana na kanuni yenye haki ambayo ametuwekea.

Mojawapo mambo hayo makuu ni kujifunza Neno la Mungu kwa kawaida, kibinafsi na vilevile kwa kushirikiana waabudu wengine wa kweli wa Yehova katika mikutano ya Kikristo. Tangu nilipoanza kuhudhuria mikutano ya Mashahidi wa Yehova, mimi huenda na mke wangu na watoto wangu. Baada ya muda fulani nyumba yetu ilianza kutumiwa kama mahali pa mikutano ya kundi zima au kisehemu chake, na hata sasa inatumiwa. Wote walio katika jamaa hujitayarisha kwa ajili ya mikutano na kushiriki. Hiyo ni desturi yetu ambayo imetuletea hali njema sana ya kiroho.​—Ebr. 10:25.

Sisi tuna desturi nyingine nzuri iliyo tofauti na desturi za jamaa nyingi katika sehemu hii ya ulimwengu, yaani, desturi ya kula pamoja. Wakati ‘miche yangu ya mizeituni’ ilipokuwa mingi mno isiweze kukaa katika meza moja chumbani mwa kulia, wengine waliketi katika nyingine ndogo jikoni.

Bila shaka kula pamoja kumetuongezea umoja, kukatupa nafasi ya kusali pamoja. Kumeniwezesha nikaze katika watoto wangu semi za Mungu ‘niketipo katika nyumba yangu,’ kupatana na mapenzi Yake. (Kum. 6:6, 7) Kumenisaidia pia nijue maoni au maelekeo ya jamaa, niwasaidie kulingana na mahitaji yetu sote ya kiroho.

Bila shaka, nyakati za chakula si za kufundisha watu Biblia tu. Ni nyakati za porojo na ucheshi pia, na labda kukwaruza-kwaruza gambusi baada ya chakula.

Kwa kuwa tunajua kwamba hatupaswi kuonyesha upendo wa Kikristo nyumbani mwangu tu, mke wangu nami tuna desturi ya kupelekea watu habari njema za ufalme wa Mungu nyumbani kwao. Watoto wangu wote wanajishughulisha katika kazi hiyo ya maana, na watano kati yao wamepata kuwa watumishi wa wakati wote nyakati mbalimbali.

Katika habari hii, nakumbuka kisa kimoja kinachohusu mwanangu wa pili, Raul, alipokuwa na umri wapata miaka kumi na saba. Asubuhi moja ya Jumapili nilimwambia: “Mwanangu, twende shambani.” Akajibu: “Hapana, siendi.” Kwa kushangaa, nikamwuliza: “Sababu?” Akajibu, “Kwa sababu si lazima.” Nikajibu: “Ni kweli, si lazima. Vema.” Sikusema tena habari hiyo na Raul. Wala sikumwambia ningekwenda naye Jumapili ile nyingine. Sikumkasirikia wala sikumnunia. Sijui alivyojisikia kwa ndani, lakini Jumapili iliyofuata alikwenda tena shambani, bila kusema lo lote.

Tangu kisa hicho kilipotukia, Raul amejitoa kwa moyo wa kupenda na shauku ashiriki katika utumishi wa Ufalme wa Mungu, naye Yehova akambariki sana. Alipata pendeleo la kuhudhuria Watchtower Bible School of Gilead mjini New York, halafu baadaye akatumikia ndugu zake Wakristo katika Colombia yote akiwa mwangalizi wa wilaya. Sasa yeye na mkewe wanatumikia katika afisi ya tawi ya Watch Tower Society katika Barranquilla, na huko anasaidia kusimamia kazi ya Mashahidi wa Yehova katika Colombia.

SABABU YA KUFURAHI

Ingawa sasa nimepata mali nyingi zaidi kuliko nilizokuwa nazo miaka kadha iliyopita, hilo silo linalonifurahisha. Mali za kimwili hazileti furaha ya kweli zikiwa peke yazo. Baraka za kiroho ndizo zinazoleta furaha! Kwa mfano, kunapokuwa na mapatano nyumbani bila matatizo mazito, kunakuwa na furaha. Tena ninapoona watoto wangu wote wakimtumikia Muumba wao, na wale wana wanne wakubwa wakitumikia kama wazee katika kundi la Kikristo, nafurahi na kutosheka sana.​—Mit. 10:22.

Kwa kuwa kumi kati ya watoto wangu wameoa au wakaolewa, na wengi wao wana “miche” yao wenyewe, mimi hufurahi kuwaona wakitutembelea mara kwa mara. Wao hupenda kuwa nasi. Mama yao nami hupenda kuwa nao pia. Tungali twapendana. Bila shaka, tuna sifa iliyo ya maana sana, kumpenda Baba yetu wa mbinguni, Yehova, ‘ambaye kwa jina lake jamaa yetu yaitwa,’ na kumtegemea ili kuendelea kuwa hai. Vilevile twamtegemea Yeye tutumainiapo kwamba uhusiano wetu wa jamaa hautamalizwa na kifo, kwa sababu “tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.”​—2 Pet. 3:13; Efe. 3:14, 15.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki