Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w77 7/15 kur. 332-334
  • Je! Utaepuka Kujitakia Makuu?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je! Utaepuka Kujitakia Makuu?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MATUNDA MABAYA YA KUJITAKIA MAKUU
  • KUPATA MAONI YANAYOFAA
  • VYANZO VYA KUJITAKIA MAKUU
  • JE! WEWE HUFANYA WENGINE WAJITAKIE MAKUU?
  • UNAWEZA KUFANYA NINI?
  • Je, Ni Vibaya Kutamani Makuu?
    Amkeni!—2005
  • Jinsi Mimi Nilivyoshinda Tamaa ya Kutaka Sana Kusifiwa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • Je! Wewe Wajitahidi Kufikia?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Sababu Kwanini Tunazeeka na Tunakufa
    Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
w77 7/15 kur. 332-334

Je! Utaepuka Kujitakia Makuu?

JE! WEWE una ujuzi wa kuongoza watu? Ikiwa unao, unaweza kuwafaidi sana. Watu huthamini mtu anayeweza kupanga mambo hata yafanyike kwa utaratibu mzuri.

Lakini ingawa uwezo wa kuongoza watu unaweza kuwa baraka, nyakati nyingi kuna jambo moja linaloufanya uwe hatari. Jambo hilo ni kujitakia makuu, maana yake “tamaa nyingi mno ya kupendelewa na watu, kuheshimiwa, ya ukuu, ya kuwa na mamlaka, au kutimiza jambo fulani.”

Tamaa ya kupata umashuhuri ni nyingi sana. Hata watu wapaswao kuwekea wengine mfano mwema hushindwa na tamaa hiyo. Kwa mfano, Yesu alisema yafuatayo juu ya viongozi fulani wa dini wa siku zake: “Jilindeni na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele karamuni.” (Luka 20:46) Nyakati nyingine hata wanafunzi wa Yesu walijitakia makuu. Twasoma yafuatayo juu ya mmojawapo nyakati hizo: “Wakafika Kapernaumu; hata alipokuwamo nyumbani, akawauliza, Mlishindania nini njiani? Wakanyamaza; kwa maana njiani walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa.”​—Marko 9:33, 34; Luka 22:24.

MATUNDA MABAYA YA KUJITAKIA MAKUU

Kisa cha mkuu wa jeshi Yoabu, Mwisraeli wa zamani, chaonyesha matokeo mabaya sana ya kujitakia makuu. Yoabu aliua Abneri na Amasa kwa siri. Alikuwa akitaka kuwashinda apate cheo cha kuwa amiri wa jeshi la Mfalme Daudi. (2 Sam. 3:26, 27; 20:8-10, 23) Mfalme alipozeeka akawa mgonjwa, Yoabu alijiunga na mwana wa Daudi, Adonia, kupanga hila ya kunyakua kiti cha ufalme. (1 Fal. 1:18, 19) Aliposhindwa kisha Sulemani akafanywa mfalme, Yoabu alimwacha Adonia. Lakini mpango huo wa kujitakia makuu ulikuwa bure tu, kwa sababu Yoabu aliuawa kwa njia yenye aibu mwanzoni mwa utawala wa Sulemani.​—1 Fal. 2:5, 6, 29-34.

Pengine wewe umeona watu wengi wenye kujitakia makuu wakipata vyeo vikubwa vya usimamizi. Je! kweli wanafaidi wanadamu wenzao? Inaelekea utakubaliana na maoni ya mwandikaji Biblia aliyeongozwa na Mungu: “Liko baa nililoliona chini ya jua, nalo ni kama kosa litokalo kwake yeye atawalaye; ya kuwa upumbavu huwekwa mahali pa juu sana, nao wakwasi [yaani, wale ambao wangestahili kusimamia watu] hukaa mahali pa chini. Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi, na wakuu wakienda kwa miguu juu ya nchi kama watumwa.”​—Mhu. 10:5-7.

Matunda maovu ya kusimamiwa vibaya kwa mambo ya kibinadamu na watu wenye Kujitakia makuu yametajwa wazi katika Mhubiri 4:1: “Kisha nikarudi na kuona madhalimu yote yanayotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, walakini wale walikuwa hawana mfariji.” Je! hali hiyo haionekani wazi zaidi leo?

KUPATA MAONI YANAYOFAA

Maoni yako ni nini juu ya kupata umashuhuri, ukuu au mamlaka? Biblia yaweza kukusaidia ukuze maoni yanayofaa. Jinsi gani?

Kwanza, Maandiko yaonyesha kwamba kutia bidii ya kujitakia makuu ni kupoteza wakati bure. Mwandikaji aliyeongozwa na Mungu, aliyetangulia kutajwa, alisema hivi: “Tena nikafikiri amali zote, na kila kazi ya ustadi, ya kwamba inatoka katika mtu kupingana na mwenzake. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo.” (Mhu. 4:4) Je! si hekima kuepuka ubatili huo? Pengine umeona kwamba watu wenye kujitafutia sana makuu ndio huelekea sana kupatwa na magonjwa mabaya sana, kama ugonjwa wa moyo, kwa sababu ya kuwa na wasiwasi. Shauri la Maandiko lafaa kweli kweli: “Heri konzi moja pamoja na utulivu, kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kujilisha upepo.”​—Mhu. 4:6.

Tamaa nyingi mno ya kutambuliwa au kupata umashuhuri inaleta madhara ya kiroho pia, kwa maana Mungu asema hivi: “Kiburi na majivuno . . . nakichukia.” (Mit. 8:13) Kujitakia makuu hakudhuru mwenye nia hiyo peke yake, bali pia wenzi wake. Kwa hiyo, mwandikaji Biblia, Yakobo, alishauri Wakristo wa karne ya kwanza hivi: “Ikiwa mnaweka wivu na kujitakia makuu kwa uchoyo mioyoni mwenu, fikirieni kama madai yenu [ya kuwa wenye hekima] si ya uongo, na kuikaidi kweli. Hiyo siyo hekima itokayo juu; ni ya dunia, yenye tamaa, ya kishetani. Kwa maana mchafuko na uovu wa kila aina hutokana na wivu na kujitakia makuu.”​—Yak. 3:14-16, New English Bible.

Kisa kinachoonyesha “mchafuko” unaoweza kuletwa na kujitakia makuu ni kwamba, mitume kumi wa Yesu ‘walianza kuwakasirikia Yakobo na Yohana’ wakati hao wawili walipojitakia vyeo vilivyo vikubwa zaidi wawe karibu na Yesu katika ufalme wa mbinguni wa Mungu. (Marko 10:41) Baadaye, watu wenye kujitakia makuu walileta migawanyiko katika kundi la Kikristo. Mwishowe jambo hilo lilifanya watu waasi imani ya kweli ya Kikristo. (Matendo 20:29, 30; 2 Pet. 2:1-3) Je! wewe wataka kuweka moyoni nia ambayo imeleta madhara mengi hivyo?

VYANZO VYA KUJITAKIA MAKUU

Kwa sababu gani watu wengi sana hujitakia makuu? Kwa kuwa kujitakia makuu ni “tamaa nyingi mno” ya ukuu na kutambuliwa, ni namna ya kutamani vitu visivyo vyako. Yesu alisema: “Ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, tamaa mbaya, . . . kijicho, . . . kiburi.” (Marko 7:21, 22) Mtume Paulo atoa maelezo zaidi juu ya chanzo cha tatizo hilo, akisema: “Mimi ni mtu wa mwilini, . . . Katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu.”​—Rum. 7:1-4, 23.

Hasa, dhambi tuliyorithi ndiyo inayofanya watu wajitakie makuu, waelekee kuona mambo kwa uchoyo, kuwafanya wenye kiburi.​—Rum. 3:23; 5:12.

JE! WEWE HUFANYA WENGINE WAJITAKIE MAKUU?

Labda wewe hutawaliwi maisha yako na nia ya kujitakia makuu. Lakini huenda ukafanya wengine wajitakie makuu. Jinsi gani?

Fikiria masimulizi ya Biblia juu ya Adamu na Hawa. Hawa alijua Mungu alikuwa amewaamuru wasile tunda katika mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Ni wazi kwamba hakujisikia ametwikwa mzigo na katazo hilo la kimungu. Alipoulizwa na nyoka, Hawa hakulalamika kwamba alikuwa ametwikwa mzigo, bali alijibu kwa unyofu kwa kurudia kutaja amri ya Mungu: “Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa.”​—Mwa. 3:2, 3.

Ndipo, Shetani Ibilisi, alipomtumia nyoka kupanda kwa werevu mbegu za kujitakia makuu katika akili za Hawa, aliposema hivi: “Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu mkijua mema na mabaya.”​—Mwa. 3:4, 5.

Kumbe! kuwa “kama Mungu,” kuweza kujiamulia yaliyo mema na mabaya badala ya kukubali uamuzi wa Mungu juu ya mambo hayo, hilo lilimpendeza sana Hawa. Nia ya Hawa ya kujitakia makuu bila ya kumtegemea Mungu hata kidogo ilimwongoza kufanya nini? “Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.” (Mwa. 3:6) Katika habari hii kujitakia makuu kwa sababu ya choyo kulifanya Adamu na Hawa na vilevile watoto wao wote wasiozaliwa walazimike kufa. ​—Mwa. 3:19; Rum. 5:12.

Namna gani wewe? Inaelekea kwamba usingesihi mtu ye yote kwa makusudi avunje sheria ya Mungu. Hata hivyo huenda ukafanya wengine wajitakie makuu. Ni jambo la kawaida watu kuheshimu sana washiriki wa jamaa, watu wa ukoo na rafiki wakubwa. Lakini watu wanaotaka kumpendeza Mungu lazima wajiangalie wasisifu mno uwezo wa wapendwa wao. Kufanya hivyo kwaweza kuwaongoza wajikuze kisha wajitakie makuu.

Kwa mfano, namna gani mtu akijaribu kumfanya mwenzi wake wa ndoa, mshiriki wa jamaa au rafiki adhani kwamba anastahili sana cheo cha mwangalizi katika kundi la Kikristo? Ungekuwa msiba mtu huyo akiwa mwenye kiburi na kuanza kudai wengine wakubali kwamba astahili na ana sifa! Maandiko yana sababu nzuri ya kuonya hivi: “Mwenye kujipendekeza kwa jirani yake, hutandika wavu ili kuitega miguu yake.” (Mit. 29:5) Kusifu-sifu Mkristo isivyo kweli kungemzuia asijitahidi ‘kufikia cheo cha mwangalizi,’ badala ya kumsaidia. (1 Tim. 3:1, NW) Maandiko yanahitaji waangalizi katika kundi la Kikristo ‘wawe na nia ya kiasi,’ na hiyo yamaanisha haiwapasi ‘kunia makuu kupita inavyowapasa kunia.’ ​—1 Tim. 3:2; Rum. 12:3.

UNAWEZA KUFANYA NINI?

Kwa kuwa wanadamu walirithi dhambi, je! haiwezekani kuepuka utumwa wa kujitakia makuu? Inawezekana, kwa maana Maandiko yanaonya kwa upole watu wenye kumcha Mungu wazuie maelekeo yenye dhambi. (Rum. 6:12) Ingawa kujiweza kwahitajiwa, unaweza kuepuka kujitakia makuu. Utaona inafaa zaidi kusitawisha nia inayoonyeshwa katika Wafilipi 2:3, 4: “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.”

Kwa hiyo, kwa njia zote kujitakia makuu hakupatani na Maandiko. Vyanzo vyake ni udhambi wa wanadamu na kiburi cha ulimwengu huu. Badala ya kujikweza kwa kujitakia makuu, Biblia yatusihi tutumikie wengine kwa unyenyekevu. Ni katika roho hiyo wanaume Wakristo wanatiwa moyo ‘wafikie cheo cha mwangalizi.’​—1 Tim. 3:1; 1 Pet. 5:1-3.

Faida mojawapo ya kutii shauri hilo la Maandiko imetajwa katika Mhubiri 5:12: “Usingizi wake kibarua ni mtamu, kwamba amekula kidogo, au kwamba amekula kingi.” Vilevile, mtu wa namna hiyo, asiye na choyo, hupendwa na kuthaminiwa na wenzake, badala ya kuwekewa kinyongo moyoni. Juu ya yote, “kibarua” hupata upendeleo wa Yehova Mungu. Je! hizo si sababu zenye nguvu kumfanya mtu aepuke kujitakia makuu?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki