Vumilieni Tu—Ahadi Yakaribia Kutimizwa!
“Mnahitaji uvumilivu, kusudi . . . mpokee utimizo wa ile ahadi.”—Ebr. 10:36, NW.
1. Ahadi yenye kutegemeka iliongoza babu ya Waarabu na Waisraeli awe mtu wa namna gani?
AHADI nzuri ya mtu mwenye kutegemeka yaweza kumfanya mwenye kuipokea achukue hatua yenye faida nyingi. Ni wangapi kati yetu wangekuwa na nia ya kuwa wageni, kuwa bila nchi ya kwao, kuwa katika nchi ya kigeni mamia ya miaka, kwa sababu ya kupewa ahadi tu? Linalostaajabisha ni kwamba tuna kumbukumbu la kweli la mwanamume aliyefanya hivyo! Ni mtu ambaye Waarabu na vilevile jamaa zao wa damu, Waisraeli, wanadai alikuwa baba yao. Babu huyo alipokea ahadi ambayo itakapotimizwa italetea jamaa ya kibinadamu faida ya milele.
2. Kwa sababu gani mwenye kupokea ahadi hiyo alihitajiwa achukue hatua ili ahadi iweze kutimizwa?
2 Mtu huyo alitakiwa achukue hatua hodari ili ahadi hiyo ya maana katika ulimwengu wote itimie, kwa maana ahadi ya Mungu ilikuwa hivi: “Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”—Mwa. 12:1-3.
3. Ni kwa njia gani Ibrahimu wa Uru wa Wakaldayo alituwekea mfano mwema kuhusu ahadi?
3 Jinsi sote tulio wa “jamaa zote za dunia” tunavyoweza kushukuru kwamba aliyepewa ahadi hiyo, Abramu wa Uru wa Wakaldayo, alichukua hatua aliyoagizwa! Abramu (ambaye baadaye aliitwa Ibrahimu) alituwekea mfano mwema juu ya kuchukua hatua inayostahili ili tutimiziwe ahadi ambayo Mungu wa Ibrahimu atuahidi.
4. Ibrahimu alikaa hali ya ugeni muda gani katika Kanaani; vilevile mwanawe Isaka na mjukuu wake Yakobo?
4 Ibrahimu alipokuwa wa miaka 75, aliingia Nchi ya Ahadi, nayo wakati huo ilikuwa ngeni kwake. Alikufa akiwa wa miaka 175. Kwa hiyo alikaa hali ya ugeni karne nzima—na huo ni wakati mrefu. Hata mwanawe Isaka, aliyemzaa katika nchi hiyo ngeni aliyokuwa hajapewa bado, alikaa hali ya ugeni muda mrefu zaidi—miaka 180. Mwana wa Isaka, Yakobo, aliyepitishiwa ahadi ya Mungu, alikaa hali ya ugeni miaka 130 kabla hajaitwa ashuke kwenda Misri, alikofia. (Mwa. 47:7-9; 49:33) Lakini, mzee huyo wa ukoo mwenye umri wa miaka 147 alizikwa kwa agizo lake mwenyewe katika Nchi ya Ahadi, Kanaani.—Mwa. 50:1-14.
5, 6. Ni sifa gani iliyowatia nguvu wazee hao watatu wa ukoo wavumilie miaka mia mbili na kumi na mitano wakiwa katika nchi ngeni, nayo Waebrania 11:9, 10, 13-16 yaonyeshaje hilo?
5 Ni nini kilichotia nguvu wazee hao watatu wa ukoo wavumilie katika nchi ngeni bila kurudi Uru wa Wakaldayo? Ni nini kilichowasaidia wavumilie katika nchi ngeni ya Kanaani jumla ya miaka 215 (1943 mpaka 1728 K.W.K.)? Ni kwa sababu waliamini Yehova Mungu asingeweza kuvunja ahadi yake. Kwa hiyo, twasoma katika Waebrania 11:9, 10, 13-16 hivi:
6 “Kwa imani [Ibrahimu] alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu. Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi. Maana hao wasemao maneno kama hayo waonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurejea. Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji.”
7. Ibrahimu alichukiwaje alikozaliwa, naye alitaka “mji” wa namna gani?
7 Ibrahimu aliwekea mwanawe Isaka na mjukuu wake Yakobo mfano mwema kwa kukaza nia afe katika nchi ya mbali badala ya kurudia mji wa kwao, Uru wa Wakaldayo. Ibrahimu alichukiwa katika mji huo wa kipagani uliokuwa katika nchi ya Shinari kwa sababu alifuatia wafalme wanne wa eneo hilo wenye mwungano, akawashinda. Walikuwa Amrafeli mfalme wa Shinari, Arioko mfalme wa Elasari, Kedor-laoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu. Ibrahimu na vikosi vyake walinyang’anya wafalme hao vifaa vyote na mateka wote waliowakamata waliposhambulia nchi ya Kanaani. (Mwa. 14:1-24; Ebr. 7:1) Ibrahimu hakutaka aendelee kukaa katika Uru wa Wakaldayo. Aliukataa. Alipendelea kukaa katika nchi ya Ahadi akiwa mtu wa kuhama-hama, akatamani kitu bora kuliko mji huo alimozaliwa, wenye kuabudu sanamu na kutenda dhambi. Ibrahimu, vilevile Isaka na Yakobo, walitaka mji au serikali iliyobuniwa na kujengwa na Mungu, si na wanadamu. Misingi ya Uru wa Wakaldayo ni magofu leo, lakini sivyo ulivyo “mji” wa Mungu.
8, 9. (a) Ibrahimu atapata urithi wa namna gani afufuliwapo, na jinsi gani? (b) Kulingana na Warumi 4:11, 12, Ibrahimu akawaje “baba” ya wanafunzi wa Kristo, kwa maana ya kiroho?
8 Kwa sababu Ibrahimu aliendelea kuwa mwaminifu mpaka kufa, Yehova Mungu alimwahidi kwamba atarithi dunia, nchi ya Kanaani, si mbingu. Kwa hiyo, Ibrahimu atakapofufuliwa kwa wafu, ataishi duniani. Lakini wakati huo dunia itakuwa chini ya utawala kamili wa mji ‘wa mbinguni,’ ufalme wa Kimasihi wa Mzao bora wa Ibrahimu, yaani, Yesu Kristo. (Ebr. 11:16) Ibrahimu aliweka mfano bora kwa kumwamini Mzao huyo mtukufu, ambaye hasa ndiye ‘uzao wa Ibrahimu’ utakaotumiwa na Mungu kupatia mataifa yote ya dunia baraka ya milele. (Mwa. 22:18) Kwa maana ya kiroho, Ibrahimu asemwa kuwa “baba” ya wanafunzi wa Yesu Kristo, wawe wametolewa kati ya Wayahudi waliotahiriwa au kati ya Mataifa yasiyo ya Kiyahudi, yasiyotahiriwa. Juu ya jambo hili, twasoma yafuatayo:
9 “Naye [Ibrahimu] aliipokea dalili hii ya kutahiriwa [miaka mingi baada ya kuwa mgeni mwenye kuhama-hama katika nchi ya Kanaani], muhuri ya ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa [mpaka alipompata Isaka]; apate kuwa baba yao [Mataifa] wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki; tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu [Wayahudi], bali pia [Mataifa ambao] wanazifuasa nyayo za imani yake baba yetu Ibrahimu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa.”—Rum. 4:11, 12; Mwa. 15:6; 17:7-17.
10. (a) Ni kwa njia gani Mungu anamzidi Ibrahimu kwa kuwa “baba yao wote waaminio”? (b) Kwa hiyo, tutaingizwa katika utimizo wa ahadi za Mungu tukiwa na sifa gani?
10 Kwa sababu ya Ibrahimu kuwa kama baba wa kiroho wa wanafunzi wa Mzao wake wa asili Yesu Kristo, alitumiwa kama mfano wa Yehova Mungu, ambaye ndiye Baba wa mbinguni wa “uzao” wote ambao kupitia kwao mataifa yote ya dunia yatabarikiwa. (Gal. 3:8, 9) Hivyo Yehova Mungu ndiye Ibrahimu Mkuu. Kwake inatoka sifa ya imani, kwa sababu huwapa waabudu wake roho takatifu yake, nalo mojawapo la matunda yanayotokezwa na roho hiyo ni imani. (Gal. 5:22) Tunamwamini kwa vile anavyotimiza ahadi zake kwa uaminifu. Yehova anamzidi Ibrahimu kwa kuwa Baba ya waaminifu au wale walio na imani. Tukishikamana na imani hiyo kama Ibrahimu, tutatimiziwa ahadi ambazo Mungu ametupa. Imani yetu itatusaidia kuvumilia mpaka tutakapoyapata mambo yaliyoahidiwa na Mungu.
“WAPITAJI NA WASAFIRI” KATIKA ULIMWENGU HUU
11, 12. Sisi tunaotazamia ahadi za Mungu kama Ibrahimu tumekuwaje bila nchi, na hiyo yahakikishwaje na yaliyoandikwa katika 1 Petro 2:11, 12?
11 Ibrahimu alituwekea mfano bora sisi tunaotazamia mazuri ya ajabu tuliyoahidiwa na Mungu asiyesema uongo. Kwa sasa tungali tuna wanaume na wanawake ambao kwa usemi wa mfano hawana nchi ya kwao. Hao ndio watu wenye imani ya Ibrahimu kweli kweli. Ni wanafunzi waliojiweka wakf wakabatizwa wa Yesu Kristo, Mkuu wa ‘uzao wa Ibrahimu.’ Wao hawachukuliwi kuwa watu wasio na nchi yao kwa maoni mabaya. Maoni hayo yanategemea yaliyoandikwa na mmoja wa wanafunzi wa Kristo, mtume Petro, katika barua yake ya kwanza aliyoandikia wale anaowaita “wateule wa Utawanyiko [wakaaji wa muda, NW], wakaao hali ya ugeni katika Ponto, na Galatia, na Kapadokia, na Asia, na Bithinia.” (1 Pet. 1:1) Wakristo hao walikuwa “wakaaji wa muda” kwa njia gani? Hilo laonyeshwa katika sura ya pili, mistari kumi na moja na kumi na mbili, ambapo mtume Petro aandika:
12 “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.”—1 Pet. 2:11, 12.
13. (a) Lakini, sisi si “wapitaji” kwa maoni ya nani, na kwa sababu gani? (b) Kwa sababu gani hatutalazimika kuondoka katika taratibu yao mbovu ya mambo, kama Petro?
13 Huenda sisi wanafunzi wa Kristo tulio wakf tukawa “wapitaji” kwa maoni ya ulimwengu, lakini jinsi inavyotufariji kujua kwamba sisi si “wapitaji” kwa maoni ya Mungu! Kwake yeye sisi ‘hatukufarikishwa tena, wala si adui katika nia zetu, kwa matendo yetu yaliyokuwa mabaya.’ (Kol. 1:21) Hatutembei “kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao; ambao akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao.” (Efe. 4:17, 18) Mtume Petro na Wakristo waliotiwa mafuta wa siku zake walitazamia kuondoka katika taratibu hii ya mambo ya kilimwengu siku ya kufa kwao wasiwe tena wapitaji wala wasafiri ndani yake. Lakini leo, katika karne hii ya 20 ya kundi la Kikristo, mashahidi Wakristo wa Yehova watakaookoka “dhiki kubwa” inayokuja hawataondoka katika taratibu hii. Kwa sababu gani? Kwa sababu taratibu hii mbovu ya mambo ndiyo itakayoondolewa usoni pa dunia katika “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” itakayokuwa mwisho wa dhiki hiyo.—Mt. 24:21, 22; Ufu. 7:14; 16:14, 16; 19:11-21.
14. Petro aliwapa Wakristo watiwa mafuta sababu gani kamili ya kuenenda kama “wapitaji na wasafiri” katika ulimwengu huu?
14 Je! kweli twajidai kuwa Wakristo walio wakf? Basi, je! tunaenenda kama “wapitaji na wasafiri” kati ya mataifa ya kilimwengu kama alivyoshauri mtume Petro kwa uongozi wa Mungu? Ilikuwako sababu kamili ya kusihi Wakristo waliokuwa ‘wamezaliwa mara ya pili ili wapate tumaini lenye uzima’ waenende kwa uangalifu kama watu walio katika nchi ngeni. Kama Petro alivyosema, sababu ilikuwa kwamba “ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu.” (1 Pet. 1:3; 2:9, 10) Kwa wazi, basi, wao si tena sehemu ya ulimwengu huu uliotenganishwa na Mungu. Hawatembei tena katika giza lake, bali wanachukua nuru ya Mungu. Wamo katika hali kama ya Ibrahimu zamani za kale.
15. Kulingana na 2 Petro 3:13, 14, Wakristo hawa ‘waliozaliwa upya’ wana tumaini gani?
15 Wao hawana tumaini moja na ulimwengu huu. Tumaini lao limeongozwa na ahadi ya Mungu. Ahadi hiyo sasa inakaribia kutimizwa vizuri mno. Zaidi ya karne kumi na tisa zilizopita Petro aliandika haya: “Tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake. Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake.” (2 Pet. 3:13, 14) “Mbingu mpya” hizo ndio “mji” ambao Ibrahimu mwaminifu alingojea kwa saburi nyingi, serikali ya mbinguni ‘yenye misingi, ambayo mwenye kuibuni na kuijenga ni Mungu.’ (Ebr. 11:10) “Nchi mpya” ndiyo jamii mpya ya kibinadamu inayojipatia baraka kupitia kwa ‘uzao wa kiroho wa Ibrahimu.’—Mwa. 22:18; Ufu. 21:1.
KUTOHUSIANA NA ULIMWENGU KAMA KRISTO
16. Kwa hiyo, kwa sababu gani Wakristo hawawezi kujitia katika siasa na mabishano ya mataifa ya kilimwengu?
16 Kwa kuwa Wakristo ni “wapitaji na wasafiri” na hivyo wanangojea watimiziwe ahadi hiyo ya kimungu, wanawezaje kujitia katika siasa na mabishano makali ya mataifa ya kilimwengu? Ikiwa kweli wamekaza mioyo yao juu ya “mbingu mpya” na “nchi mpya” kuhusiana na ufalme wa Mungu, hawawezi kufanya hivyo!
17. Kutii maneno ya Kristo katika Mathayo 6:32, 33 kwaonyeshaje haifai mtu agawanye fikira zake kati ya ufalme wa Mungu na falme za kibinadamu?
17 Yesu Kristo aliambia wanafunzi wake hivi: “Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote [ya kimwili]. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake.” (Mt. 6:32, 33) Kutafuta hivyo ufalme wa Baba wa mbinguni kwanza kwatia ndani bidii ya kutimiza unabii wa Yesu: “Habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.” (Mt. 24:14) Mkristo mtiifu hawezi kutanguliza ufalme wa Mungu na kupata kibali yake akigawanya fikira na wakati wake atumikie faida za ufalme wa Mungu pamoja na faida za falme za kibinadamu.
18. Kwa sababu gani Wakristo hawana haki ya kujifanya sehemu ya ulimwengu huu?
18 Wakiisha kuwa “wapitaji na wasafiri” katika ulimwengu huu wa zamani, Wakristo hawana tena haki ya kujifanya sehemu ya ulimwengu huu. Wakifanya hivyo, hawatahusika katika, sala ambayo Yesu alimtolea Mungu: “Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.” (Yohana 17:15-17) Alikuwa na sababu kamili ya kusali hivyo, kwa maana “yule mwovu” ndiye “mkuu wa ulimwengu huu.”—Yohana 12:31; 14:30.
19. Kama “wapitaji na wasafiri,” lazima Wakristo wapatwe na nini katika ulimwengu huu?
19 Je! ulimwengu huu wa wanadamu wenye kutawalwa na Ibilisi unawapenda hawa “wapitaji na wasafiri” Wakristo wanapoendelea kukataa kuwa sehemu ya ulimwengu huu? Je! ulimwengu ulimpenda Yesu Kristo kwa sababu hakuwa “wa ulimwengu,” kama alivyosema? Mwanafunzi si bora kuliko Bwana wake. Kwa hiyo Yesu aliwaambia wanafunzi wake hivi: “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; . . . Naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.” (Yohana 15:18-20; 16:2) Ili Mkristo wa kweli atimiziwe ahadi ya Mungu, lazima avumilie kwa uaminifu chuki hiyo ya ulimwengu na matendo yake mabaya.
20. Kulingana na Waebrania 10:32-34, Wayahudi waliogeuzwa kuwa Wakristo kisha wakachukiwa kama Yesu walipaswa kukumbuka nini?
20 Wayahudi waliogeuzwa kuwa Wakristo katika jimbo la Kirumi la Uyahudi, na hasa wale waliokuwa katika mji wake mkuu Yerusalemu, waliona ukweli wa maonyo hayo ya Bwana wao wa Kimasihi, Yesu Kristo. Karibu miaka 20 baada ya Yesu kunena yaliyotangulia, mtume Paulo, aliyekuwa Myahudi akageuzwa kuwa Mkristo, alikuwa katika hali ya kuweza kuandikia waamini Waebrania katika Yerusalemu maneno haya yenye kuwarudishia nguvu: “Zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu; pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendewa hayo. Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang’anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo.”—Ebr. 10:32-34.
“MABALOZI” WAKRISTO
21, 22. (a) Kwa sababu ya ukatili wa ulimwengu, Mungu anatuma nani wafikie watu, nalo kusudi ni nini? (b) Twaonyeshwaje hilo katika 2 Wakorintho 5:19-21.
21 Ni kweli kwamba ulimwengu ni mkatili kwa Yehova Mungu na watu wake waliojitoa. Kwa sababu hiyo, Mungu amewapa utumishi wa kibalozi waabudu wake waliojiweka wakf na kubatizwa kisha wakapokea “uzaliwa mpya” kwake. (1 Pet. 1:3, NW) Kwa hiyo hawatumi kwenye ulimwengu uliotenganishwa naye kwa kusudi la kutafuta amani na kupatana na ulimwengu. Ulimwengu uliohukumiwa maangamizi sio unaopaswa kueleza Mungu masharti ya amani. (Luka 14:31, 32) Mungu hutuma mabalozi wake wakasihi watu mmoja mmoja wa ulimwengu watumie kwa faida masharti ya Mungu yenye upendo ya kuwa na uhusiano wenye amani Naye, na wenye kuokoa uhai. Myahudi aliyegeuzwa kuwa Mkristo, Paulo, pamoja na mwenzi wake nusu-Myahudi, Timotheo atueleza jambo hilo, akisema katika 2 Wakorintho 5:19-21, NW:
22 “Mungu kupitia kwa Kristo alikuwa akipatanisha ulimwengu na yeye mwenyewe, si kuwahesabia makosa yao, naye alitukabidhi neno la upatanisho. Kwa hiyo sisi tu mabalozi badala ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kupitia kwa sisi. Kama badala ya Kristo tunaomba: ‘Mpatanishwe na Mungu.’ Yeye asiyekuwa amejua dhambi alimfanya awe dhambi kwa ajili yetu, ili tupate kuwa haki kupitia kwake.”
23. Kulingana na “neno la upatanisho” ambalo “mabalozi” hawa Wakristo wanachukua, kwa sababu gani hawaruhusiwi kujitia katika siasa na mabishano ya ulimwengu?
23 Kwa sababu ya kuwa mabalozi walio badala ya Kristo kwa mataifa yote, Wakristo walioagizwa wanapaswa kupelekea watu wa siasa za namna zote “neno la upatanisho”—wenye kufuata demokrasi, wa serikali za jamhuri, wanaofuata Ujamaa, wenye mawazo ya Nazi, Wafasisti, Wakomunisti, wasiotaka mageuzi ya siasa, wenye kupigania faida za wafanya kazi, na kadhalika. ‘Neno la Mungu la upatanisho’ halipendelei chochote cha vyama hivyo vyote. Kwa hiyo ‘mabalozi wake walio badala ya Kristo’ hawawezi kujitia katika siasa za nchi yo yote wala kuwa wanachama wa chama cho chote cha kisiasa mahali po pote. Kwa kuwa ni “mabalozi” waliotumwa na Mungu, wao ni “wapitaji na wasafiri” bila kujali wanahubiri katika nchi gani “habari njema ya ufalme.” Wakikumbuka maneno ya mtume Paulo, “Wenyeji wetu uko mbinguni” (Flp. 3:20, 21), wanafahamu kwamba hawana haki wala ruhusa ya kujitia katika siasa. Lazima waendelee bila kuwamo katika siasa za kitaifa au za mitaani na mabishano yote ya kichoyo ya ulimwengu huu.
24. Ijapokuwa “mabalozi” hawa wanatii sana sheria wanapatwa na nini ulimwenguni kama Paulo anavyoonyesha katika Waefeso 6:19, 20?
24 Kwa hiyo wao ndio watu wenye kutii sheria zaidi kuliko watu wengineo, wanalipa kodi na kufaidi watu. Lakini mabalozi hawa walio badala ya Kristo wanachukiwa na ulimwengu, kama Kristo mwenyewe (Mt. 22:21; Rum. 13:1-7) Kwa hiyo, si ajabu kwamba karibu miaka sita baada ya Paulo kuandika yaliyomo katika 2 Wakorintho 5:19-21, alifungwa Rumi, Italia, na hivyo akaandika kundi la Efeso, Asia Ndogo, lisali kwa ajili yake: “Nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili: ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo.”—Efe. 6:19, 20.
25. Mtu anatakiwa afanye nini anapoendesha ubalozi wa Kikristo, na apaswa akumbuke nini juu ya mali?
25 Kama ilivyokuwa miaka mia kumi na tisa iliyopita, leo mtu anapotumikia kama ‘balozi badala ya Kristo’ kati ya watu waliotenganishwa na Mungu anatakiwa avumilie mateso hayo. Paulo alituwekea kielelezo kwa kuvumilia kwa uaminifu. Alishikilia ubalozi wake au huduma yake ya Kikristo. Alisema: “Katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika misiba, katika shida; katika mapigo, katika vifungo,” na kadhalika. (2 Kor. 6:4, 5) Kwa kuwa aliteswa pamoja na wenzake, Paulo angeweza kuambia ndugu zake Waebrania,waliogeuzwa kuwa Wakristo waendelee kuvumilia, kama walivyovumilia mengi walipopata nuru ya kweli ya Biblia mara ya kwanza. Hata kama wangepoteza mali zote zao za kidunia, wao na yeye pia walikuwa na “mali iliyo njema zaidi, idumuyo.”—Ebr. 10:32-34
26. Kwa sababu gani mabalozi na wajumbe Wakristo wanatakiwa bado waendelee kuvumilia kwa uaminifu?
26 Yatupasa sisi mashahidi Wakristo wa Yehova tulio mabalozi au wajumbe badala ya Kristo tukuze uwezo wa uvumilivu. Yatupasa tuendelee kuvumilia. Tangu mwisho wa Majira wa Mataifa mwaka wa 1914 tumepatwa na mateso mengi, tukatendwa vibaya katika ulimwengu mkatili. Bado yako mateso zaidi ya namna hiyo mbele yetu, kabla hatujatimiziwa ahadi ya Mungu kuwa na “mbingu mpya na nchi,” ambamo haki itakaa milele. (2 Pet. 3:13) Utimizo wa ahadi hiyo unazidi kukaribia. Kizazi hiki, ambamo mabalozi na wajumbe wa Mungu tangu Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ya 1914-1918 W. K. wameteswa sana isivyo haki,, ni kizazi chenye maana sana. Jinsi gani? Kwa vile ambavyo ndicho kitakachoona Mungu akitimiza ahadi yake ya kuleta taratibu mpya yenye haki ya mambo. (Mt. 24:34 Marko 13:30) Basi na tuendelee kuvumilia kwa uaminifu na tumaini hakika!