Maswali Kutoka kwa Wasomaji
● Katika Yohana 2:20 tunasoma hivi: “Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu?” Tunawezaje kuhesabu miaka hiyo 46?
Habari zinazozunguka maneno hayo zinaonyesha kwamba Yesu alikuwa Yerusalemu wakati huo kuadhimisha sikukuu yake ya kwanza ya kupitwa baada ya kubatizwa. (Yohana 1:29-33; 2:13) Kulingana na unabii wa “majuma sabini” unaopatikana katika Danieli 9:24-27, Masihi angeonekana waziwazi katika vuli ya mwaka 29 W.K. Basi sikukuu ya kupitwa ambayo ingefuata ingekuwa katika masika ya mwaka 30 W.K.
Kwa habari ya hiyo miaka 46, tunaweza kusaidiwa na kifungu kilicho katika maandishi ya mwanahistoria Myahudi, Flavio Yosefo. Katika kitabu Antiquities of the Jews tunasoma hivi: “Na sasa Herode, katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, na baada ya matendo yaliyokwisha tajwa, alianza kazi kubwa sana, yaani, kujijengea mwenyewe hekalu la Mungu, na kulifanya kubwa zaidi katika eneo, na kuliinua juu sana.”—Kitabu cha 15, sura ya 11, sehemu ya 1.
Yosefo anasema kwamba Herode aliuteka Yerusalemu miaka 27 baada ya mji huo kuangushwa na Pompei (mwaka 63 K.W.K.). Hiyo yaonyesha Herode aliuteka Yerusalemu mwaka 36 K.W.K., Julai au labda Oktoba, kulingana na maelezo ya wanafunzi fulani. Inaonekana kwamba kipindi kilichopita tangu Herode alipofanya mapinduzi akakalia kiti cha enzi, mpaka masika yaliyofuata ya mwezi Nisani, kilihesabiwa na Yosefo kuwa mwaka wa kujitayarisha kutawala. Basi mwaka wa kwanza wa “kutawala” kwa Herode ulianza katika masika yaliyofuata, tangu mwaka 35 mpaka 34 K.W.K. Tukiongeza miaka mingine kumi na saba, tunaona kwamba mwaka wa kumi na nane wa kutawala kwa Herode (ambao ndio mwaka alipoanza kujenga hekalu) ni 18-17 K.W.K. Tukiongeza miaka mingine 46 tunakuja kwenye 29-30 W.K.
● Mtu mmoja ninayejua anaendelea kukaribia ubatizo wa Kikristo, lakini cheti kinachompa ruhusa ya kukaa nchini kimemalizika. Nitamwambia nini?
Inakupasa umsifu kwa sababu anataka kuyajua mashauri ya Mungu na kuyafuata. Maandiko yanahimiza Wakristo watii sheria, wamlipe Kaisari vilivyo vya Kaisari. (Mt. 22:21) Kwa hiyo, ingefaa umhimize mtu huyo ajaribu awezavyo arekebishe hali yake, ambayo kwa sasa inaweza kuchukuliwa kama ya mgeni haramu.
Ni wazi kwamba haibi, hasemi uongo, haishi katika uasherati wala havunji sheria nyinginezo za Mungu zinazotajwa waziwazi katika Biblia. Tunasema hivyo kwa sababu mtu anayevunja sheria za Mungu lazima atubu na kugeuka kabla hajastahili kubatizwa Kikristo. (1 Kor. 6:9, 10; Matendo 26:20; 2:38) Lakini mtu huyo anataka kujua jinsi anavyoweza kufuata sheria za nchi akiwa katika hali yake.
Biblia inashauri Wakristo watii sheria za nchi katika mambo yote ikiwa hazipingani na sheria ya Mungu. (Rum. 13:1; Matendo 5:29) Mtume alieleza kwamba tukifanya hivyo hatutakuwa na haja ya kuogopa kuadhibiwa na wakuu. Vilevile, tutaweza kuwa na dhamiri safi.—Rum. 13:3-5.
Hata hivyo, Neno la Mungu haliwaambii waangalizi walipe kundi la Kikristo wajibu wa kujifahamisha habari zote za sheria zinazohusu raia na wavunja sheria, ili wazitumie kuhukumu wavunja sheria. Tunaweza kuona hivyo kwa kuangalia jinsi Paulo alivyoshughulika na kisa cha Onesimo.
Onesimo alikuwa mtumwa wa Mkristo Mkolosai, jina lake Filemoni. Kwa sababu fulani ya kichoyo Onesimo alikimbilia Rumi akajifiche kati ya watu wengi wa huko; hata labda alimnyang’anya bwana wake mali kabla ya kutoroka. Alipokuwa Rumi kama mtumwa mtoro (Kirumi, fugitivus) Onesimo alionana na Paulo, akawa Mkristo na kumhudumia Paulo. Baada ya muda fulani mtume Paulo alimhimiza Onesimo amrudie bwana wake wa kisheria, hata akamtia Filemoni moyo ampokee Onesimo kama ndugu na kumtendea fadhili.—Flm. 8-22.
Kumbuka kwamba wakati Onesimo alipokuwa Rumi, mtume Paulo hakumchakua akampeleka kwa wakuu wa Rumi ili akaadhibiwe kwa sababu alikuwa mtumwa mtoro na labda mwivi pia. Tunajua kutokana na maandiko ya Paulo kwamba, yeye mwenyewe aliamini inampasa Mkristo atii sheria ya nchi, lakini ni wazi kwamba hakulifikiria kundi kuwa lenye wajibu wa kutumikia serikali kwa kuchunguza-chunguza maisha ya watu. Vilevile, tunaweza kuona kwamba Onesimo hakuzuiwa kubatizwa kwa sababu ya hali yake. Mwishowe Onesimo aliamua kumrudia bwana wake wa kisheria, na inaonekana alifanya hivyo kwa sababu ya mashauri kama yale yaliyokuwa yameandikwa katika Warumi 13:1-5 na vilevile kwa sababu ya kuhimizwa na Paulo.
Leo kundi la Kikristo linafuata mwendo unaopatana na kielelezo hicho cha Biblia. Kabla ya kuruhusu mtu abatizwe au aendelee kuwa ndani ya kundi, halichunguzi lione kama nyumba yake imejengwa kupatana na sheria za ujenzi, kama ametimiza sheria zote zinazohitajiwa ili akae nchini, na mambo kama hayo.
Hiyo si kuonyesha kwamba watu wa Mungu hawajali sheria za Kaisari. Bali, sisi tunajulikana sana kuwa watu wanaojitahidi kutii sheria; wakuu wengi wa serikali wamesifu Mashahidi wa Yehova kwa sababu hiyo. Ni kama vile Paulo alivyoandika juu ya kutii serikali, “Fanya mema, nawe utapata sifa kwake.”—Rum. 13:3.
Hasa wanaume wanaoongoza kundi ndio wanaopaswa kuweka mfano mwema katika jambo hili. Biblia inasema kwamba wazee na watumishi wa huduma wanapaswa wawe “bila lawama,” ‘wawe na ushuhuda mzuri kutoka kwa watu walio nje’ na wawe ‘bila shtaka.’ (1 Tim. 3:2, 7, 10, tafsiri ya Kiingereza ya New World) Basi ingekuwa vigumu sana Mkristo anayeamua kupuza sheria za “Kaisari” kupendekezwa awe na vyeo hivyo katika kundi. Wanaume wanaopendekezwa wapate mapendeleo hayo wanapaswa kuwa watu ‘wenye kulishika sana neno la imani,’ si katika maneno yao tu, bali pia katika maisha wanayochagua, pamoja na kutumia mashauri ya kumlipa ‘Kaisari vitu vilivyo vya Kaisari.’—Tito 1:7-9.
Ni juu ya kila mtu, awe ni Mkristo au asiwe, kuamua mwenyewe kama atafuata sheria za serikali. Lakini ingekuwa vizuri umweleze mtu huyo mawazo ya Maandiko. Naam, mashauri ya Biblia yanayotuambia tutii sheria za serikali ni yenye hekima, tena yanatuletea faida. Wakristo wakiyafuata wanaweza kuepuka matata makubwa na kufurahia kuwa na dhamiri safi wanapomtumikia Mungu.