Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w77 11/15 kur. 507-508
  • Yehova—Anapenda Haki

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Yehova—Anapenda Haki
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Habari Zinazolingana
  • Kuteketeza Biblia Kwa Kisasa Kwashindwa Kutimiza Kusudi Lake
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Kutumikia Katika “Siku za Mwisho”
    Mungu Asema Nasi Kupitia Yeremia
  • Kutokuwamo Kwa Kikristo Vita ya Mungu Ikaribiapo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Ezekieli—Maisha na Nyakati Zake
    Hatimaye Ibada Safi ya Yehova Yarudishwa!
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
w77 11/15 kur. 507-508

Yehova​—Anapenda Haki

ALIYE Juu Zaidi anapenda haki. (Zab. 33:5) Mtumishi wake Elihu alisema hivi: “Yeye Mwenyezi hatuwezi kumwona; yeye ni mkuu mwenye uweza; tena mwenye hukumu, na mwingi wa haki, hataonea.”​—Ayubu 37:23.

Kwa sababu Yehova Mungu anaheshimu sana haki, haachilii uonezi uendelee. Lazima waonezi wapatwe na matokeo yanayotajwa na sheria ya Mungu isiyobadilika: “Cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.” (Gal. 6:7) Nyakati fulani Yehova ameongoza mabaya yakafanyika kwa njia iliyoletea wazoeao udhalimu msiba. Ili wajue kwa uhakika kwamba yeye ndiye aliyewahukumu, Mwenyezi alitangaza hukumu yake mapema kupitia kwa manabii wake.

Ndivyo ilivyokuwa kumhusu Eliakimu wa karne ya saba K.W.K. Baba yake, Mfalme Yosia, aliuawa vitani alipokuwa akijaribu kuzuia majeshi ya Wamisri yenye kuongozwa na Farao Neko yasipitie Samaria kwenda kupigana na Babeli, iliyokuwa imeshinda Ashuru. Watu wa Yuda walimfanya Yehoahazi, ndugu mdogo wa Eliakimu, awe mfalme. Karibu miezi mitatu baadaye Farao Neko alimteka Yehoahazi akampeleka Misri, kisha akamfanya Eliakimu mwenye umri wa miaka 25 awe mfalme, akalibadili jina lake likawa Yehoyakimu. Tena, Neko alitoza ufalme wa Yuda faini kubwa. Yehoyakimu aliipata kwa kutoza raia zake kodi.​—2 Fal. 23:34-36; 2 Nya. 36:1-5.

Badala ya Yehoyakimu kuufikiria mzigo mzito wa kazi uliowalemea raia zake, yeye alifanya mipango ya kujenga jumba jipya la kifalme, la anasa. Aliwanyima wafanya kazi mshahara ili gharama za kujenga jumba hilo zisiwe nyingi. Ukatili wa Yehoyakimu ulionekana na Yehova Mungu. Alimtuma nabii Yeremia nyumbani kwa mfalme. Mambo hayo yameandikwa katika Yeremia sura ya 22.

Ingawa Yehoyakimu alistahili adhabu, Yehova Mungu alimrehemu akampa mfalme huyo nafasi ya kusahihisha mambo. Yeremia aliagizwa aseme hivi: “[Yehova] asema hivi, Fanyeni hukumu na haki, mkamtoe yeye aliyetekwa katika mikono ya mdhalimu; wala msiwatende mabaya mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kuwadhulumu, wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia katika mahali hapa. Kwa maana mkifanya haya kweli kweli, ndipo watakapoingia kwa malango ya nyumba hii wafalme wenye kuketi katika kiti cha enzi cha Daudi, wanakwenda kwa magari, na wamepanda farasi, yeye, na watumishi wake, na watu wake.” (Yer. 22:3, 4) Kwa hiyo Yehoyakimu angeweza kusaidia kuendeleza utawala wa watu wa nyumba ya kifalme ya Daudi kwa kubadili mwenendo wake.

Unabii kwa Yehoyakimu uliendelea kusema, “Lakini kama hamtaki kusikia maneno haya, mimi naapa kwa nafsi yangu, asema [Yehova], ya kuwa nyumba hii itakuwa ukiwa. Kwa maana [Yehova] asema hivi, katika habari ya nyumba ya mfalme wa Yuda; Wewe u Gileadi kwangu, na kichwa cha Lebanoni; ila hakika nitakufanya kuwa jangwa, na miji isiyokaliwa na watu.”​—Yer. 22:5, 6.

Basi, Yehoyakimu angejiletea uharibifu pamoja na ufalme wake kwa kuendelea kutotii. Kwa maoni ya Yehova Mungu, “nyumba ya mfalme wa Yuda,” yaani eneo lote lililokuwa na jumba na vijumba vya kifalme, ilikuwa ‘kama Gileadi,’ “kichwa cha Lebanoni.” Jumba la kifalme lilikuwa mahali pa juu penye fahari. Lilikuwa kama Lebanoni, pamoja na mierezi yake yenye fahari. Tena, mbao za mierezi zilitumiwa sana kujenga majumba ya kifalme. (1 Fal. 7:2-12) Yehoyakimu mwenyewe alikuwa ametumia mierezi kupamba jumba lake. Kwa hiyo eneo la jumba lake lilikuwa kama mwitu wa majengo ya mierezi yenye fahari​—kama Gileadi na Lebanoni yenye miti mingi sana. Hata hivyo jumba hilo la kifalme lingeharibiwa pamoja na vijumba vyake. Miji yote ya Yuda ingekuwa ukiwa. Jambo hilo lilitukia? Je! Yehoyakimu alipatwa na mabaya kwa sababu ya udhalimu wake?

Ndiyo, Wakaldayo waliushambulia Yerusalemu. Kwa habari ya Yehoyakimu, unabii ulisema hivi: “Atazikwa maziko ya punda, akibururwa, na kutupwa nje ya malango ya Yerusalemu.” (Yer. 22:19) Mapokeo ya kale (yaliyoandikwa na mwanahistoria Myahudi Yosefo wa karne ya kwanza) yanasema kwamba Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alimwua Yehoyakimu na kuagiza maiti yake itupwe nje ya kuta za Yerusalemu. Hata ikiwa mapokeo hayo si ya kweli, Yehoyakimu hakuokoka Wababeli walipoleta mazingiwa. Hakuzikwa kwa njia yenye heshima. Mzoga wake ulilala nje ya malango ya Yerusalemu bila ya mtu wa kuuangalia, ukaachwa wazi upigwe na joto wakati wa mchana, na baridi wakati wa usiku. Mwanawe Yehoyakini alitawala karibu miezi mitatu baada ya kufa kwake; mwishowe alikubali kushindwa na mazingiwa, kisha akapelekwa Babeli uhamishoni.​—2 Fal. 24:11, 12.

Baada ya hapo Sedekia, mjomba wa Yehoyakini, aliwekwa na Mfalme Nebukadreza wa Babeli autawale Yerusalemu. Mwishowe, Sedekia aliasi, majeshi ya Babeli yakarudi Yerusalemu. (2 Fal. 24:20; 25:1) Kama ilivyokuwa imetabiriwa, Yerusalemu na nchi yote ya Yuda iliachwa ukiwa. Uvumbuzi wa wachimbua ardhi unahakikisha kwamba unabii uliotolewa kupitia kwa Yeremia ulitimizwa. W. F. Albright anasema yafuatayo katika kitabu The Bible After Twenty Years of Archaeology: “Uvumbuzi na matembezi katika nchi ya Yuda umehakikisha kwamba miji ya Yuda iliharibiwa kabisa na Wakaldayo walipoishambulia mara mbili, nayo haikukaliwa muda wa vizazi vingi​—⁠na mingi haikupata kukaliwa tena.”​—Uku. 546.

Kwa hiyo Yehoyakimu na raia zake walipata adhabu kwa sababu ya udhalimu mwingi wenye aibu walioufanya. Maneno haya yalitimizwa: “Wewe ukaaye Lebanoni [maana yake Yerusalemu, pamoja na mahali pa juu ulipokuwa mji huo na majengo yake ya mierezi] ufanyaye kioto chako katika mierezi, utakuwa na hali ya kuhurumiwa sana, upatapo utungu kama wa mwanamke azaaye.” (Yer. 22:23) Wakaaji wa Yerusalemu walishushwa kutoka mahali pa juu sana. Mji wao mkuu uliokuwa mzuri uliharibiwa kisha waokokaji wengi wakapelekwa uhamishoni Babeli.

Kweli Yehova Mungu aliuona udhalimu uliotendwa katika ufalme wa Yuda. Kwa kuwa yeye ni Mungu ambaye kanuni zake za adili hazibadiliki, tunaweza kuwa na hakika kwamba hatavumilia milele uvunjaji sheria uliopo leo. Unabii wa Biblia unaonyesha kwamba wakati tunaoishi ni “siku za mwisho” za ulimwengu usiomcha Mungu. (2 Tim. 3:1-5) Kwa hiyo inatupasa tujiangalie tusiyafuate mazoea ya ulimwengu huu na kukataliwa na Yehova, Mungu apendaye haki.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki