Kuteketeza Biblia Kwa Kisasa Kwashindwa Kutimiza Kusudi Lake
“Akalikata kwa kijembe, akalitupa katika moto wa makaa, hata gombo lote likawa limekwisha kuteketea katika huo moto wa makaa.”—Yer. 3:23.
1. Sababu gani kuteketezwa kwa Biblia ikiwa nzima au ikiwa katika visehemu si jambo jipya?
KUTEKETEZA Biblia Takatifu ikiwa nzima au ikiwa katika visehemu si jambo jipya. Kisa cha kwanza kinachoripotiwa cha jambo hilo kilitokea zaidi ya miaka 2,600 iliyopita. Hiyo ilikuwa katika siku za mfalme wa tatu kutoka mwisho wa taifa ambalo lilikuwa limepewa Biblia hapo kwanza.
2. Ni jambo gani lililofanya unabii wa Yeremia ulioandikwa uwe kitu cha kuwashia moto wa makaa?
2 Yalikuwa majira ya baridi kule Yerusalemu, ambako Mfalme Yehoyakimu alikuwa ameketi karibu na moto wa makaa uliokuwa unawaka ili kupasha moto chumba chenye kiti cha enzi. Namna sehemu ya maana ya Biblia Takatifu ilivyopata kuwa kitu cha kuwashia moto huo wa makaa, masimulizi ya kweli yanatuarifu. Kutokana nayo twayaandika maneno haya:
“Ikawa katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili likamjia Yeremia, kutoka kwa [Yehova], kusema, Twaa gombo la chuo, ukaandike ndani yake maneno yote niliyokuambia juu ya Israeli, na juu ya Yuda, na juu ya mataifa yote, tangu siku ile niliponena nawe, tangu siku za Yosia, hata siku hii ya leo. Huenda nyumba ya Yuda watasikia mabaya yote niliyokusudia kuwatenda; wapate kurudi, kila mtu akaiache njia yake mbaya; nami nitawasamehe uovu wao na dhambi yao.” (Yer. 36:1-3)
Tukisoma sura 35 zinazotangulia za kitabu cha Yeremia, twaweza kuthamini namna ambavyo kwa hakika ujumbe wake ulioandikwa usingependwa na watu wengi.
3. Sababu gani Yeremia hakuwa akisumbua-sumbua tu watu, nao watu hao walibaki na muda gani wa kufanya jambo fulani juu ya hali hiyo?
3 Vilevile leo ujumbe unaofanana na ule ambao Yeremia aliambiwa aandike juu ya “gombo la chuo” haupendwi na watu wengi. Si kwamba kusudi peke yake la ujumbe huo ni kukasirisha watu, kuwasumbua, kwa kuwapigia mayowe juu ya msiba. Wakristo wale ambao leo wanafanana na nabii Yeremia hawajaribu kusumbua-sumbua tu. Hasha, bali wanatoa utumishi kwa watu wote kwa kuonya watu juu ya msiba wa mataifa yote unaokuja. Jambo hilo laweza kuchochea watu wengine watubu na kugeuka wakati Yehova angali ana maelekeo yenye kibali. Kwa ajili ya mwendo huo, wao wanaweza kuokolewa na msiba wa ulimwengu ulio mbele. Huko nyuma katika siku za Yeremia taifa la Yuda lilikuwa limebakiza miaka 18 ili Wababeli wapate kuharibu mji mtakatifu Yerusalemu. Leo, baada ya miaka 60 ya utendaji wa jamii ya Yeremia ya kisasa, mfano wa kisasa wa Yerusalemu, Jumuiya ya Wakristo, ina muda mrefu kadiri gani kabla ya uharibifu wake wenye msiba kuanzisha “dhiki kubwa” juu ya ulimwengu wote?—Mt 24:21, 22.
KUTOA UJUMBE WA MAANGAMIZI WAZIWAZI
4. Baada ya Yeremia kumaliza kuandika unabii wake tangu mwanzo na kuendelea, ujumbe huo ulitolewaje kwa Yerusalemu, na sababu gani?
4 Kwa kutii, Yeremia alimsomea mwandishi wake, Baruku mwana wa Neria ujumbe huo apate kuuandika. Hati iliyoteketezwa ilitia ndani maneno yote ya Yehova aliyomwambia Yeremia tangu mwaka wa 13 wa utawala wa Mfalme Yosia kuendelea, mwaka ule ambao Yehova alimtokeza kuhani-mkusudiwa kijana Yeremia awe nabii. Alipomaliza hati hiyo, Yeremia alijiona hawezi kwenda Yerusalemu, maili tatu (kilometres 5) hivi toka mji wa nyumbani kwake wa Kilawi wa Anathothi, akaisome hati hiyo kwa sauti kuu katika nyua za hekalu. Hivyo, alimtuma mwandishi wake Baruku huko akafanye hivyo, akiongeza hivi: “Labda wataomba dua zao mbele za [Yehova], na kurudi, kila mtu akiiacha njia yake mbaya; kwa maana hasira na ghadhabu ni kuu sana, alizotamka [Yehova] juu ya watu hawa.”—Yer. 36:4-7.
5. Ni wakati gani ungeelekea kufaa ili hati ya unabii wa Yeremia isomwe katika hekalu la Yerusalemu.
5 Kuna ye yote wetu ambaye angependa kusoma hivyo kwa sauti katika mahali pa watu wote ambapo watu wanapitia? Baruku alihitaji kuwa na uhodari. Hata hivyo, kwa nguvu za Mungu, alifanya jambo hilo! Walakini twapaswa kukumbuka kwamba ilimchukua Baruku wakati kunakili yote yale ambayo Yeremia alimwambia. (Yer. 36:17, 18) Kwa kuwa hati hiyo ilikuwa na ujumbe mkali wa Yehova juu ya mataifa, kutia ndani Israeli na Yuda, tukio la watu wote lingetokeza wakati unaofaa kwa hati hiyo kusomwa kwa sauti. Kama vile siku ya taifa zima kufunga kula! Kisha watu wenye kufunga wangejazana kwenye hekalu la Yerusalemu. Wakati ungepaswa kungojea tukio kama hilo!
6. Katika mwaka ambao Yeremia aliandika hati yake, yule ambaye angetumiwa kutimiza unabii wa Yeremia wa kupinduliwa kwa Yerusalemu alidhihirithwaje (alifunuliwaje)?
6 Kwa hiyo Baruku hakusoma mbele ya watu wote hati hiyo iliyomaliza kuandikwa katika mwaka wa nne wa Mfalme Yehoyakimu, mwaka ambao katika huo Mfalme Nebukadreza wa Babeli alishinda vikosi vya majeshi ya Farao Neko wa Misri na kujiimarisha akawa mtawala mkuu mpya wa ulimwengu. Nebukadreza huyo ndiye mtawala Mtaifa ambaye Yeremia alitabiri kuwa ndiye angepindua Yuda na Yerusalemu, jambo ambalo lingefuatwa na kukaa mahame kwa nchi hiyo pasipo mtu au mnyama wa kufugwa kwa miaka 70.—Yer. 36:6; 25:1-11.
7. Baruku alisoma hati ya Yeremia katika hekalu la Yerusalemu katika mwaka gani na katika pindi gani?
7 Sasa waja mwaka wa tano wa Mfalme Yehoyakimu wa Yuda. Walingana na mwaka wa pili wa Nebukadreza kama mtawala wa ulimwengu. Masimulizi ya Yeremia 36:9, 10 yanahakikisha jambo hilo. Yanasema hivi:
Basi, ikawa katika mwaka wa tano [624-623 K.W.K.] wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kenda [Kisleu, au, Novemba-Desemba], watu wote waliokuwa katika Yerusalemu, na watu wote waliokuja Yerusalemu kutoka miji yote ya Yuda, wakapiga mbiu ya kufunga mbele za [Yehova]. Basi, wakati huo Baruku akayasoma maneno ya Yeremia katika nyumba ya [Yehova], katika chumba cha Gemaria, mwana wa Shafani, mwandishi, katika ua wa juu, mahali pa kuingilia kwa lango jipya la nyumba ya [Yehova], akiyasoma katika masikio ya watu wote.
8. Baruku alitekeleza maagizo aliyopewa na Yeremia katika majira gani ya mwaka?
8 Kutawala kwa wafalme wa Yuda kulikuwa kukihesabiwa kuanzia mwezi wa masika wa Abibu, au Nisani. Mwezi wa tisa wa mwaka wao, ambao ulikuja kuitwa Kisleu, ulifika katika majira ya baridi. Ungetia ndani sehemu ya ule tunaoita Desemba (jina hilo la Kilatini lamaanisha mwezi wa kumi). Katika nyakati za Wamakabayo “sikukuu ya kuwekwa wakf” ya hekalu la Yerusalemu iliadhimishwa katika Kisleu 25, nao unasemekana ulikuwa “wakati wa baridi.” (Yohana 10:22) Ijapokuwa hali ya hewa ya baridi-baridi ya mwezi wa Kisleu, Baruku, mwandishi wa Yeremia, alitekeleza maagizo ya Yeremia.
9. Maono ya ndani ya wakuu wa Yuda yalikuwa nini kuhusiana na hati hiyo kama walivyosomewa, nao walimwambia Baruku, pamoja na Yeremia, afanye nini?
9 Maneno ya Yeremia ambayo Baruku alisomea watu kwa sauti hekaluni yalihusu taifa zima. Kwa hiyo wakuu wa Yuda wakamwita Baruku awasomee ujumbe huo wa kiunabii. (Yer. 36:11-15) Tukikumbuka yale ambayo sura zinazotangulia za unabii wa Yeremia zinasema juu ya kuhukumiwa maangamizi kwa ufalme wa Yuda, twaweza kuthamini sababu gani wakuu hao waliogopa walipoyasikia yale aliyowasomea Baruku. Wakiwa watukuzaji wa taifa walijiona kuwa na wajibu wa kumwambia Mfalme Yehoyakimu. Walichukua kitabu hicho cha hati kutoka kwa Baruku, walakini, wakifadhili mwandishi na mnakili wa kitabu hicho, walimwambia Baruku aende akajifiche pamoja na Yeremia. Mambo yakawa barabara.—Yer. 36:16-20.
KUTEKETEZWA KWA BIBLIA KWA KWANZA KULIKOANDIKWA
10. Mfalme Yehoyakimu alifanya nini Yehudi alipokuwa akimsomea kitabu hicho, nayo matokeo ya jambo hilo yalikuwa nini?
10 Wakuu hao walienda kwenye nyumba ya wakati wa baridi ya Mfalme Yehoyakimu ili kutoa ripoti yao. Yeye alitaka kutwaa unabii wa Yeremia ulioandikwa katika kitabu cha kukunja. Kwa hiyo akamtuma mkuu wa mahakma aliyeitwa Yehudi akalete kitabu hicho toka hekaluni ambapo kilikuwa kimeachwa. Ni jambo gani lililotokea wakati Yehudi alipokifungua kitabu hicho cha kukunja na kusoma kwa sauti safu kwa safu? “Ikawa, Yehudi alipokuwa amekwisha kusoma [kurasa] tatu nne, mfalme [Yehoyakimu] akalikata kwa kijembe, akalitupa katika moto wa makaa, hata gombo lote likawa limekwisha kuteketea katika huo moto wa makaa. Lakini hawakuogopa, wala hawakurarua mavazi yao, wala mfalme, wala watumishi wake hata mmoja waliosikia maneno hayo yote.”—Yer. 36:21-24.
11. Mwenendo wa Yehoyakimu ulitofautianaje na ule wa babaye Yosia aliposikia Kumbukumbu la Torati likisomwa, na je! Yehoyakimu alikuwa ametii Kumbukumbu la Torati 17:18-20?
11 Ni kukosa heshima kama nini kwa neno lililoandikwa la Mungu ambalo liliongozwa kwa roho! Lo! namna tendo hilo la Mfalme Yehoyakimu lilivyotofautiana sana na mwenendo wa babaye Yosia! Wakati kitabu cha kukunja cha Kumbukumbu la Torati kilipogunduliwa wakati wa kusafisha hekalu lililochafuliwa, Yosia aliagiza mwandishi mmoja amsomee kitabu hicho. Yosia alilichukua jambo hilo moyoni na kuyararua mavazi yake. Kisha akawaongoza watu wake wafanye agano la pekee pamoja na Yehova la kumtii na kuendesha ibada yake safi. (2 Nya. 34:14-33) Tena, orodha iyo hiyo ya sheria iliamuru mfalme ye yote wa wakati ujao wa Israeli aandike nakala kama hiyo kabisa ya sheria na kuisoma kwa ukawaida na kuishika. (Kum. 17:18-20) Ni vionyesho gani vilivyoko vinavyoonyesha kwamba Mfalme Yehoyakimu alifanya jambo la utawa kama hilo? Hakuna! Mfano wake ulikuwa mbaya!
12. Hapa pametajwa visa gani viwili kuonyesha kama kuna wo wote walio kama Mfalme Yehoyakimu leo?
12 Je! kuna Mayehoyakimu wa kisasa? Ndiyo, kwa habari ya kuteketeza nakala za Maandiko Matakatifu. Ndiyo, ndani ya Jumuiya ya Wakristo kabisa! Kumbuka namna, katika mwaka 1961, huko Ejutla, Oaxaca, Mexico (Amerika ya Kati), kasisi wa Katoliki ya Rumi alivyochochea kikundi cha watu wenye ghasia kishambulie na kupekua nyumba fulani ambamo mikutano ya utamaduni ilikuwa ikifanywa kwa ukawaida, nacho kikanyakua Biblia zote zilizopatikana na kuziteketeza katika uwanja wa mji. Gazeti la mahali hapo liliripoti kwamba walitenda jambo hilo kana kwamba walikuwa wakifanya “tendo la imani.” Vilevile, katika Februari wa 1962 tangazo lilitolewa katika Ureno lililokataza uenezaji wa vitabu vya Mashahidi wa Yehova kupitia kwa njia za usafirishaji wa barua. Ingawa hakukuwa tangazo rasmi lililotangazwa na serikali ya Ureno la kupiga marufuku Mashahidi wa Yehova, hesabu kubwa ya vitabu vyao vya kidini na vilevile Biblia zilinyakuliwa na kuteketezwa.
13, 14. (a) Kuhusiana na hilo, ni jambo gani lililotokea miaka miwili iliyopita kule Argentina? (b) hilo linatokeza ulizo gani, nayo ni nini sababu ya kweli ya viongozi wa kidini kujaribu kuzuia Mashahidi wa Yehova wasifanye utendaji wao wa Kikristo?
13 Katika mwaka wa 1976 Mashahidi wa Yehova walipigwa marufuku katika Argentina (Amerika ya Kusini), na miaka miwili tu iliyopita katika makao yao makuu katika Buenos Aires hesabu kubwa ya vitabu ilitwaliwa, kutia na nakala 250 za tafsiri ya New World Translation of the Holy Scriptures katika Kispania. Vyote hivyo waliuziwa watengenezaji wa karatasi na kukatwa-katwa na kuchemshwa viwe karatasi. Zaidi ya hayo, Mashahidi wa Yehova waliotambuliwa walipokuwa wakivuka toka Uruguay (nchi jirani) kuja Argentina walinyang’anywa Biblia zao, nazo zikateketezwa. Visa vingine vya kuteketeza Biblia wanaweza kuandikiwa wasomaji wetu, walakini yote haya yanatokeza ulizo.
14 Ni nini kinachofanya Biblia ionekane kuwa chombo hatari mikononi mwa Mashahidi wa Yehova, hata kwamba katika nchi zinazoitwa za Kikristo, wananyang’anywa pasipo haki na kuharibiwa? Je! ni kwa sababu watu wanaotukuza taifa wanawaona Mashahidi wa Yehova kama vile Mfalme Yehoyakimu alivyomwona Yeremia na Baruku—wafitini wa kisiasa walio hatari kwa serikali, wenye kuzuia njia za taifa za kujilinda. Hilo ndilo jambo ambalo viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo wangependa wanasiasa na watu wengine wa serikali waamini! Walakini sababu yenyewe ambayo wakuu wa serikali na viongozi wa kidini wanataka kukomesha utendaji wa Kikristo wa Mashahidi wa Yehova ni hii: Wao wanamtumikia Mungu yule yule ambaye Yeremia na Baruku walitumikia, na kutoka katika Maandiko ya Kiebrania wanatoa ujumbe unaofanana na ule wa nabii Yeremia. Kisha, kama vile Yeremia, wanatii amri ya Yehova kama ilivyoandikwa katika Maandiko hayo na kutangaza ujumbe Wake juu ya taratibu mbovu ya mambo iliyopo, kutia ndani Jumuiya ya Wakristo na sehemu nyingine zote za kilimwengu ambazo inaendeleza pamoja nazo uhusiano wa kirafiki, ili ipate kuungwa mkono nazo. Kwa hiyo, Waangamie Mashahidi wa Yehova, wanaofunua wazi makosa ya Jumuiya ya Wakristo!
15, 16. (a) Tuna visa gani katika karne ya saba K.W.K. kuonyesha kama wakuu wote wenye vyeo vya chini wanaunga mkono kusumbuliwa kwa Mashahidi wa Yehova? (b) Yehova alifanyia watumishi wake nini?
15 Kumekuwako na kungaliko wakuu wachache wa serikali wenye cheo cha chini ambao hawaungi mkono wakuu wao katika mateso hayo mabaya ya Mashahidi wa Yehova. Wanapinga kwa sababu ya kupenda haki na kwa sababu ya kuheshimu Mungu ambaye Wakristo hao wanaosumbuliwa ni mashahidi wake—walakini imekuwa kazi bure! Hiyo inalingana na kisa chenye kutokeza sana cha karne ya saba K.W.K. “Hata hivyo, Elnathani, na Delaya, na Gemaria, walikuwa wamemsihi mfalme asiliteketeze gombo lile, lakini hakukubali kuwasikia. Mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, na Seraya, mwana wa Azrieli, na Shelemia, mwana wa Abdeeli, wamkamate Baruku, mwandishi, na Yeremia, nabii; lakini [Yehova] aliwaficha.”—Yer. 36:25, 26.
16 Mfalme Yehoyakimu alituma si mrithi wake wa kifalme Yehoyakini bali “mwana” wake Yerameeli pamoja na wakuu wengine wawili wakawinde Yeremia na mwandishi wake. Kwa wazi kusudi la mfalme huyo lilikuwa baya. Walakini mahali walipoenda kujificha Yehova hakukubali pajulikane, pawe palikuwa katika Yerusalemu au katika Anathothi uliokuwa karibu au mahali penginepo. Mwanzoni kabisa mwa kazi yake ya unabii, Yeremia alikuwa amepewa uhakikisho huu wa Yehova: “Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema [Yehova], ili nikuokoe.”—Yer. 1:19.
17, 18. (a) Kulingana na unabii wa mapema zaidi wa Isaya 40:8, kusudi la Yehoyakimu la kuteketeza Biblia lingekuwa na matokeo gani? (b) Yeremia aliamriwa aandike nini katika kitabu cha kukunja juu ya Yehoyakimu?
17 Katika karne iliyotangulia Yeremia, nabii Isaya aliandika hivi: “Neno la Mungu wetu litasimama milele.” (Isa. 40:8; 1 Pet. 1:25) Kwa hiyo kusudi la Mfalme Yehoyakimu la kuteketeza hati ya kitabu cha kukunja cha Yeremia lazima lingeshindwa kutimia, kwa kuwa Mungu alihakikisha jambo hilo. Yeye alikusudia kwamba yatupasa sisi leo kuwa na unabii kamili wa Yeremia, zaidi ya miaka elfu mbili na mia tano baadaye. Jambo hilo limekuwaje hivyo? Yeremia anatuambia wakati yeye na Baruku walipokuwa wangali wamefichwa na Yehova.
18 “Ndipo neno la [Yehova] likamjia Yeremia, hapo mfalme alipokuwa amekwisha kuliteketeza gombo lile, na maneno yale aliyoandika Baruku, yaliyotoka katika kinywa cha Yeremia, kusema, Haya! twaa wewe gombo lingine, ukaandike ndani yake maneno yote ya kwanza, yaliyokuwa katika gombo la kwanza, ambalo Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ameliteketeza. Na katika habari za Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, utasema, [Yehova] asema hivi, Umeliteketeza gombo hili, ukisema, Mbona umeandika ndani yake, ukisema, Bila shaka mfalme wa Babeli atakuja, na kuiharibu nchi hii, na kukomesha mwanadamu na mnyama pia ndani yake? Basi, [Yehova] asema hivi, katika habari za Yehoyakimu, mfalme wa Yuda; Hatakuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Daudi; na mzoga wake utatupwa nje wakati wa mchana upigwe kwa hari, na wakati wa usiku upigwe kwa baridi. Nami nitamwadhibu yeye, na wazao wake, na watumishi wake, kwa sababu ya uovu wao, nami nitaleta juu yao, na juu ya wenyeji wa Yerusalemu, na juu ya watu wa Yuda, mabaya yote niliyoyatamka juu yao, lakini hawakukubali kusikiliza.”—Yer. 36:27-31.
19. Kutii amri ya Mungu kungemaanisha kazi ya namna gani kwa Yeremia na Baruku, nayo hati hiyo ya kuchukua mahali pa ile ya kwanza ilikuwa kubwa kadiri gani?
19 Kutii amri ya Mungu kulimaanisha kwamba nabii huyo na mwandishi wake wangeifanya kazi hiyo kwa siri, lakini je! Yeremia alitii? “Ndipo Yeremia akatwaa gombo lingine, akampa Baruku, mwandishi, mwana wa Neria, naye akayaandika maneno yote yaliyotoka katika kinywa cha Yeremia, ya kitabu kile alichokiteketeza Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika moto; tena maneno mengi zaidi kama yale yakatiwa ndani yake.”—Yer. 36:32.
20. Yehoyakimu alipata maziko ya namna gani wakati wa kufa, na je! mwanawe Yehoyakini alipata kuwa na wana wo wote waliokalia kiti cha enzi cha Yerusalemu?
20 Kulingana na vile mambo yalivyotokea, Yehoyakimu alipatwa na kifo cha aibu naye hakuzikwa katika makaburi ya wafalme kule Yerusalemu, kama vile asivyoweza kuzikwa punda kule. (Yer. 22:18, 19) Mwanawe Yehoyakini (au, Konia) alitawala miezi mitatu na siku 10 tu katika Yerusalemu kisha akakubali kushindwa na Wababeli naye akahamishwa mpaka Babeli, ambako hakutoka tena. (Yer. 22:24-30; 37:1) Kufikia wakati wa kuharibiwa kwa mji uliojengwa upya wa Yerusalemu na Warumi katika mwaka 70 W.K., hakuna mzao wa Yehoyakini, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, aliyekalia kiti cha ufalme katika Yerusalemu. Maneno ya kiunabii ya Yeremia, yaliyoandikwa katika makao yake ya siri, hayakukosa kutimia!
21. Wanapolazimishwa kufanya kazi kisiri-siri, Mashahidi wa Yehova wa leo wamefanya nini, nako kuteketeza Biblia kwa kisasa kumekuwa na matokeo gani?
21 Siku hizi Mashahidi wa Yehova wamelazimishwa kufanya kazi kisiri-siri katika nchi nyingi. Wakati Biblia zao wanazotumia zinapotwaliwa na kuteketezwa, wao wanafanya nini? Wanalofanya tu ni kuchapa Biblia zaidi wao wenyewe au kuchukua tafsiri za Biblia nyingine na kuzitumia. Inapokuwa lazima, hata wakati wanapofanya kazi kisiri-siri wanaendelea kutangaza ujumbe unaofanana na ule Yeremia aliotangaza wa maangamizi juu ya ulimwengu wenye kumkaidi Mungu. Kuteketeza Biblia, ili kunyamazisha Mashahidi wa Yehova leo, kumeshindwa kutimiza kusudi lake. Wala jambo hilo halikuwaogopesha wasieneze vitabu vya Biblia wala halitazuia Neno la Yehova lisitimie kikamilifu katika nyakati ngumu zijazo! Wapinzani wanajionyesha kuwa wanastahili uharibifu wa milele tu wakati huo!
[Picha katika ukurasa wa 11]
Jehoiakimu ateketeza neno la Mungu—kielelezo kinachofuatwa katika nyakati za kisasa