Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w79 10/15 kur. 22-23
  • Maswali Kutoka kwa WASOMAJI

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maswali Kutoka kwa WASOMAJI
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
  • Habari Zinazolingana
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2017
  • Kupanga Uzazi—Maoni ya Kikristo
    Amkeni!—1993
  • Tumbo la Uzazi—Makao Yetu ya Kwanza ya Ajabu
    Amkeni!—1992
  • Maswali kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
w79 10/15 kur. 22-23

Maswali Kutoka kwa WASOMAJI

● Je! kutumia njia ya kuzuia uzazi kwa kutumia kadude kanakojulikana kama IUD, yaani, intrauterine device (kadude kanakotiwa katika tumbo la uzazi la mwanamke) kunapatana na kanuni za Kikristo?

IUD ni kadude kadogo kanakotiwa katika tumbo la uzazi (mji wa mimba) la mwanamke ili kuzuia uzazi. Jambo la kuhangaikiwa na Wakristo ni kama kadude IUD kanafanya kazi katika njia ya kutoa mimba au hapana. Kuna ushuhuda unaoongezeka kuonyesha kwamba ndivyo kanafanya.

Jambo hilo laweza kufahamika vizuri zaidi kwa kufikiria matukio ya kawaida wakati wa mtungo wa mimba. Mbegu ya uzazi ya mwanamke (ovum) inatoka katika kifuko cha mayai tumboni (ovary) na kuingia katika mrija unaounganisha kifuko cha mayai ya mwanamke na mji wa mimba tumboni. Mbegu za mwanamume ambazo zimepitia katika tumbo la mwanamke la uzazi huenda zikakutana na mbegu ya uzazi ya mwanamke katika ule mrija. Mbegu hizo mbili zikiungana hapo (mrijani), mimba imetungika, uhai mpya umeanza. Baada ya muda wa juma moja hivi mbegu ya mwanamke iliyoungana na ya mwanamume inafika katika tumbo la uzazi na kupenya katika tabaka yake, ambapo itakaa katika muda wote unaobaki wa kuchukua mimba.

Kwa muda wa miaka mingi kulikuwako na makisio yenye kupingana juu ya namna kadude IUD kanavyofanya kazi. Katika toleo la Mnara wa Mlinzi (Kiingereza) la Desemba 15, 1969 tulitaja kwamba wanasayansi fulani waliamini wakati huo kwamba kadude IUD kanazuia mbegu ya mwanamume isiifikie mbegu ya mwanamke na kutokeza mtungo wa mimba. Hata hivyo, wataalam wengine walishikilia kwamba mimba inatungwa walakini kadude hako kanazuia kule kupenya kwa mbegu ya mwanamke iliyoungana na ya mwanamume katika tabaka ya mji wa mimba. Kwa habari ya uwezekano huu wa pili, ilielezwa kwamba “hiyo ingekuwa sawasawa na kutoa mimba kulingana na maoni ya Biblia.” (Kut. 23:26; 1 Kor. 15:8, maneno ya chini, NW; Moffat) Hata hivyo, kwa sababu ya uhakika wa kwamba maoni ya wataalam yalitofautiana juu ya namna kadude IUD kanavyofanya kazi, maoni yalitolewa kwamba watu wo wote wawili waliooana wanaohusika watafanya uamuzi wao wenyewe wakiongozwa na dhamiri zao.

Katika muda wa miaka iliyofuata madaktari (waganga) wamefanya uchunguzi mwingi sana juu ya namna kadude IUD kanavyofanya kazi. Wamejifunza jambo gani?

Makala ndefu juu ya habari hiyo katika gazeti liitwalo Canadian Medical Association Journal la Januari 7, 1978, ilitoa uamuzi huu:

“Haijulikani hasa namna kadude IUD kanavyofanya kazi. Matokeo mbalimbali yameonekana [kadude] IUD kanapotumiwa na labda yote hayo yakiunganishwa pamoja yanatokeza tendo la kuzuia uzazi.”‏

Makala hiyo ilitaja mengine ya matokeo hayo:

1. “[kadude] IUD kanazuia kule kupenya [kwa mbegu ya mwanamke iliyoungana na ya mwanamume katika tabaka ya mji wa mimba].”‏

2. Kanatokeza tendo lenye kuchochea tumbo la uzazi, linalotokeza chembe zinazozunguka na kuzuia mbegu ya mwanamume [pamoja na mbegu ya mwanamke iliyoungana na mbegu ya mwanamume, kulingana na maoni ya wachunguzi wengine].

3. Kanaongeza utendaji wa misuli ya ile mirija au tumbo la uzazi hivi kwamba mbegu ya mwanamke [iliyoungana na mbegu ya mwanamume au hapana] inatembea kwa haraka sana.

4. Kanageuza hali ya dawa zilizo hai za tabaka ya tumbo la uzazi ambapo mbegu ya mwanamke iliyoungana na ya mwanamume ingepenya na kukaa.

Maelezo zaidi yalitolewa juu ya kadude IUD kwamba ndani yake mna madini ya shaba, yanayoelekea “kutokeza utendaji zaidi,” kama vile: kupunguza uwezo wa kujiendesha kwa mbegu ya mwanamume, kutokeza badiliko katika namna ya dawa ya mwilini iitwayo enzyme katika tabaka ya tumbo la uzazi ambayo huzuia kule kupenya kwa mbegu ya mwanamke iliyoungana na ya mwanamume katika tabaka ya tumbo la uzazi, na kutokeza utendaji uliochochewa zaidi.

Mazungumzo kama hayo ya kitaalam mara nyingi yanatia ndani maelezo juu ya uwezekano wa kwamba kadude IUD huenda kakaizuia mbegu ya mwanamume kabla haijaungana na ile ya mwanamke. Walakini, mengi ya maelezo juu ya namna kadude IUD kanavyoelekea kufanya kazi yanahusu namna kanavyozuia kule kupenya kwa mbegu ya mwanamke iliyoungana na ya mwanamume katika tabaka ya mji wa mimba. Gazeti American Family Physician la Nov. 1977 lilisema hivi: “Majaribio yanayofanywa katika wanyama yanaonyesha kwamba [kadude] IUD ka shaba kanatokeza tendo lake la kuzuia uzazi sana sana kwa kuzuia kule kupenya [kwa mbegu ya mwanamke iliyoungana na ya mwanamume katika tabaka ya mji wa mimba].”

Hata kadude IUD kakiwa kanatumiwa nyakati nyingine mwanamke huchukua mimba. Vilevile kuna ushuhuda unaoonyesha hatari inayoendelea kuongezeka ya mimba zinazokulia nje ya tumbo la uzazi, kama vile katika ule mrija. Makala hiyo inayotajwa hapo juu inamalizia hivi:

‘Ijapokuwa kadude IUD kanakuwa na matokeo katika kuzuia zaidi ya 98 kwa mia ya mimba katika mji wa mimba, kanakuwa na matokeo yaliyo chini ya 90 kwa mia katika kuzuia mimba zinazokaa katika ule mrija. Ikiwa mgonjwa anapata mimba akiwa anatumia kadude IUD, inaelekea sana sana kwamba moja kati ya 20 itakuwa nje ya mji wa mimba, (yaani, katika ule mrija).’

Gazeti Canadian Medical Association Journal linasema hivi:

“Kati ya mimba zinazochukuliwa hali [kadude] IUD kanatumiwa kadiri ya mimba zinazojitoa zenyewe ni 41 kwa mia, . . . Kwa kutofautisha, kadiri ya mimba [zinazojitoa zenyewe] kati ya wanawake wasiotumia [kadude] IUD ni 10 mpaka 15 kwa mia.”

Watu wengi wanaokubaliana na kutoa mimba makusudi wanashikilia kwamba (baada ya mtungo wa mimba) mpaka kitoto kifikie umri wa juma kadha hakuna uhai au mtu aliye hai anayehusika. Walakini Muumba-uhai, Yehova Mungu, hatoi maoni kama hayo katika Neno lake. Tofauti na hilo, Biblia inaonyesha waziwazi kwamba Mungu anakubali na kuheshimu uhai hata wakati unapokuwa katika mwanzo-mwanzo wa ukuzi wake. (Zab. 139:13-16; Yer. 1:5) Chini ya torati ya Musa, tendo ambalo lingetokeza kuharibiwa kwa uhai uliokuwa ukikua lingeleta adhabu kali.​—⁠Kut. 21:22, 23.a

Kuheshimu uhai namna hiyo kunahusika tunapofikiria ulizo la kutumia kadude IUD. Uhakika ni kwamba katika wakati huu hakuna mtu awezaye kusema akiwa na uhakika kabisa kama kadude IUD kanazuia mtungo wa mimba. Mahali pake, kuna ushuhuda unaoongezeka kwamba hata kadude IUD kajapotumiwa mtungo wa mimba unawezekana, na unatukia nayo mimba hiyo iliyofanyika inazuiliwa isikue kama kawaida na kuwa mtoto. Mkristo mnyofu anayefikiria sana juu ya kama inafaa kutumia kadude IUD anapaswa kufikiria habari hiyo kwa uzito kupatana na maoni ya Biblia ya kuheshimu utakatifu wa uhai.

[Maelezo ya Chini]

a Mnara wa Mlinzi (Kiingereza) wa Agosti 1, 1977, kur. 478-480.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki