“Mfalme wa Mataifa”—Msaada Wetu Peke Yake
“Ni nani asiyekucha wewe, Ee mfalme wa mataifa? maana hii ni sifa yako wewe; kwa kuwa miongoni mwa wenye hekima wote wa mataifa, na katika hali yao ya enzi yote pia, hapana hata mmoja kama wewe.”—Yer. 10:7.
1. Kilio kwa ajili ya msaada kinatoka kwa nani ulimwenguni pote, na sababu gani?
“SAIDIA! SAIDIA!” Kutoka kila sehemu ya dunia kilio hiki kinatokea. Kinatoka kwa watu wanaoona mwendo ambao ulimwengu huu unaendelea kuchukua na matokeo yenye kuleta msiba ambayo katika hayo utamalizikia hivi karibuni sana. Wanaogopeshwa sana na namna mambo yalivyo nao wanahuzunika sana. Wanaelekea kusema, kama vile nabii Yeremia alivyosema muda mfupi kabla ya kuharibiwa kwa Yerusalemu, ambako alikutabiri: “Laiti kichwa changu kingekuwa maji, na macho yangu kuwa chemchemi ya machozi, ili nipate kulia mchana na usiku kwa ajili yao waliouawa wa binti ya watu wangu [Israeli]!”—Yer. 9:1.
2. Mtu mwenye huruma aweza kulia kwa kufaa kwa sababu ya mambo kuwa namna gani?
2 Sababu gani mtu mwenye huruma leo asilie? Kwa kuwa sasa kimewakaribia wanadamu kitu ambacho kilifananishwa zamani sana na msiba wa taifa zima ambao juu yake Yeremia aliambiwa aseme hivi: “Mkawafundishe binti zenu kuomboleza, Na kila [mwanamke amfunze mwenzake] kulia. Kwa maana mauti imepanda madirishani mwetu [kwenye nyumba zetu kabisa], imeingia majumbani mwetu; ipate kuwakatilia watoto walio nje, na vijana katika njia kuu. . . . Mizoga ya watu itaanguka kama samadi juu ya mashamba [itapakae kama mbolea], Na kama konzi ya ngano nyuma yake avunaye, wala hapana mtu atakayeikusanya.”—Yer. 9:20-22.
3. Kwa sababu ya taabu ya ulimwengu inayoonekana wazi mbeleni, watu wanaenda kupata uongozi kwa nini au kwa nani?
3 Ni nani asiyeweza kuona taabu ulimwenguni pote wakati ujao, mbaya kushinda yote katika historia yote ya kibinadamu? Si lazima tuwe na maono ya mbele ya kiunabii ya Yeremia wa zamani kusudi tuone hili. Kwa hiyo, basi, ye yote wetu anawezaje kuokoka yale ambayo watazamaji wa mwendo wa mambo ya ulimwengu wasioongozwa kwa roho wanatabiri leo? Kwa sababu ya namna mambo yanavyoogofya, hata watu wasio wa dini bila kufahamu wanasukumwa kuitia chanzo cha juu zaidi na kilicho zaidi ya wanadamu kijiingize na kuokoa jamii ya kibinadamu. Watawala wa kisiasa, hata na wale wa Jumuiya ya Wakristo, kwa kuhangaika wanawaendea wachawi na watu wanaodai kuweza kuona vitu visivyoweza kuonwa na wengine. Kwa kukosa kwao uhakika juu ya kuchukua hatua moja ya muhimu (maana), wanawaendea wanajimu wapate kufanya uaguzi wao wa nyota na kuzisoma ishara za mbinguni. Wengine wanaitia miungu wao, sanamu zao zilizotengezwa kwa mbao na kufunikwa kwa fedha na dhahabu na kupambwa kwa mavazi mazuri sana yaliyotengezwa kwa mikono au kwa mashine. Je! mambo hayo yaliyo desturi yenye kupendwa na wengi ndivyo vitu vya kutumainia kupata msaada sasa kadiri hali ya ulimwengu inavyokuwa yenye kuogopesha sana na kuonyesha msiba wa ulimwengu katika wakati ujao ulio karibu sana? Hasha! —Yer. 10:1-5.
4. Sababu gani “mtoaji mwenye fadhili” na asiyeona si ndio msaada wetu wa pekee, na msaada wa kweli unapatikana wapi?
4 Msaada wa kweli unapatikana wapi? Ni nini au ni nani aliye msaada wetu wa pekee? Si “mtoaji mwenye fadhili” asiyeona tena asiye na akili. Ni lazima awe mtu halisi anayeona hatari za hali yetu kwa kadiri ile kama watabiri wetu wa kisiasa wenye hekima, ndiyo, hata zaidi ya wanaume hao wenye akili sana. Kitu kisicho na akili hakiwezi kusaidia hasa watu wenye akili kama sisi. Msaada wetu wa pekee ni Yule aliyekuwa na akili ya kutosha kuufanya ulimwengu wote, kutia na sisi tulio na akili. Yeye yu “juu” ya hali hii. Yeye ndiye Ambaye manabii humwita “[M]falme wa mataifa.”
5. Katika Yeremia 10:6-8, nabii anasimuliaje msaada wetu wa pekee?
5 Je! twauliza Huyu ndiye nani? Yeye ndiye Yule asiyeweza kufananishwa na cho chote, kwa kuwa Yeremia asema hivi: “Hapana hata mmoja aliye kama wewe, Ee [Yehova]; wewe ndiwe uliye mkuu, na jina lako ni kuu katika uweza. Ni nani [asiyekuhofu] wewe, Ee mfalme wa mataifa? maana hii [hofu ya namna hiyo] ni sifa yako wewe; kwa kuwa miongoni mwa wenye hekima wote wa mataifa, na katika hali yao ya enzi yote pia, hapana hata moja kama wewe. Lakini wote [mataifa na falme zao] pia huwa kama wanyama, ni wapumbavu. Haya ni maelezo ya sanamu, ni shina la mti tu [sanamu ya mbao iliyofunikwa kwa fedha na dhahabu na kupambwa kwa mavazi kama mungu].”—Yer. 10:6-8.
6. Ni mataifa gani mawili yanayotajwa kwanza baada ya gharika ya siku za Nuhu, na Biblia inaonyeshaje juu ya kama Yehova alikuwa Mfalme wao?
6 Ni katika njia gani Yehova Mungu alikuwa “mfalme wa mataifa” katika siku za Yeremia? Je! mataifa yasiyo ya Kiyahudi au watu wa Mataifa walimtambua yeye kuwa Mfalme wao? Je! alikuwa amesimamisha falme zao au wafalme wao? Je! ndiye aliyewapa namna zao za serikali na sheria au kuingia kwenye agano nao kusudi awaweke katika uhusiano wenye kuwafungamanisha naye? Mataifa ya kwanza ambayo Biblia hutaja baada ya gharika ya siku za Nuhu ni ya Babeli na Ashuru. Je! tuelewe (tufahamu) kwamba Yehova alikuwa Mfalme wao? Jambo kama hilo lingewezaje kuwa hivyo? Kwa kuwa Mwanzo 10:8-12 latuambia hivi:
“Kushi [mjukuu wa Nuhu] akamzaa Nimrodi, akaanza kuwa mtu hodari katika nchi. Alikuwa hodari kuwinda . . . mbele za [Yehova]. Kwa hiyo watu hunena, Kama Nimrodi, hodari wa kuwinda . . . mbele za [Yehova]. Mwanzo wa ufalme wake ulikuwa Babeli na Ereku, na Akadi, na Kalne, katika nchi ya Shinari. Akatoka katika nchi ile akaenda mpaka Ashuru, akajenga Ninawi, na Kehobothi-iri, na Kala; na Reseni, kati, ya Ninawi na Kala, nao ni mji mkubwa.”—Tazama Mwanzo 2:14; Mambo ya Nyakati 1:10.
7. Ni Msingi gani wa zamani unaoweza kuonyesha kama Yehova alikuwa Mfalme wa Mamlaka ya Babeli ya siku za Yeremia?
7 Wakati wajenzi wa Babeli walipokuwa wakiendelea kujenga ‘mnara wao wa Babeli,’ au zigareti (kinara cha hekalu), kwa ajili ya ibada ya kidini, ni nini kilichotukia kusudi kiwazuie wasiimalize kazi hii? Kwani, Yehova alifanya kama alivyosema: “Tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane [kwa kufahamiana] maneno wao kwa wao.” Matokeo yalikuwa nini? Mataifa, yenye kuzungumza lugha tofauti; kwa kuwa twasoma hivi: “Basi [Yehova] akawatawanya kutoka huko [Babeli] waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji. Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli [mvurugo], maana hapo ndipo [Yehova] alipoichafua lugha ya dunia yote.” (Mwa. 11:7-9) Kwa wazi, basi, Yehova hakuwa Mfalme wa Mamlaka hiyo ya kwanza ya Babeli kama vile asivyokuwa Mfalme wa Mamlaka ya Babeli ya siku za Yeremia. Aliyekuwa mungu wa Mamlaka ya Babeli ya siku za Yeremia alikuwa Beli au Merodaki (Marduki), ambaye Mfalme Nebukadreza aliabudu. (Yer. 50:1, 2) Yehova hakuwa mungu wa Kibabeli.
8, 9. (a) Wale mataifa wengine waliabudu nani kama watawala wao wasio wa kibinadamu? (b) Shetani alionyeshaje Yesu kwamba alikuwa kile ambacho Yesu alimwita, “mkuu wa ulimwengu huu”?
8 Watu wengine wa Mataifa walikuwa na miungu wao wa taifa, ambao waliwaona kuwa watawala wao na ambao walifanyiwa sanamu za kuabudiwa ziwawakilishe. Kwa mfano, taifa la Waamoni liliabudu mungu wa uongo ambaye lilimwita Moleki, jina linalomaanisha “Anayetawala,” au “Mfalme.” (Law. 18:21; 20:2-5; 1 Fal. 11:7; Matendo 7:43) Kwa kweli mataifa hayo yalikuwa yakiabudu mashetani wa kiroho au maibilisi. (1 Kor. 10:20) Aliye juu ya mashetani hawa wasioonekana ni Shetani Ibilisi. Katika 2 Wakorintho 4:4 NW, anaitwa ‘mungu wa taratibu hii ya mambo.’
9 Akidai kuwa mfalme juu ya mataifa yote ya kilimwengu, Shetani Ibilisi alijaribu kumshawishi Yesu kwa kusema hivi: “Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake [falme zote za dunia inayokaliwa na watu], kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako.” (Luka 4:5-7) Walakini Yesu alikataa kuwa mfalme wa kibinadamu chini ya adui mkuu wa Mungu. Kwa hiyo, muda mfupi kabla ya kifo chake, Yesu alimtaja Shetani Ibilisi kuwa “mkuu wa ulimwengu huu.” (Yohana 12:31; 14:30; 16:11) Kitabu cha mwisho cha Biblia, kilichoandikwa karne saba baada ya siku za Yeremia, kinasema kwamba “dunia yote” inamwabudu Shetani Ibilisi na tengenezo lake la kisiasa lionekanalo, linalofananishwa kama mnyama mwenye vichwa saba.—Ufu. 13:3, 4.
10. (a) Ni kwa msingi gani Yehova alikuwa Mfalme wa taifa la Israeli peke yake mpaka wakati lilipomkataa Masihi? (b) Ujapokuwa ‘‘ufalme wa dunia” ulipata kuwa wa Yehova na wa Kristo wake katika mwaka 1914, mataifa yanakataa kufanya nini?
10 Katika siku za zamani Waisraeli walimkubali Yehova Mungu kuwa Bwana wao na Mfalme. Kwa kupatana na hilo mtunga zaburi aliyeongozwa kwa roho alisema: “Humhubiri Yakobo neno lake, Na Israeli amri zake na hukumu zake. Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo, Wala hukumu zake hawakuzijua. Haleluya [au, Msifuni Yah].” (Zab. 147:5, 19, 20; 145:1, 12, 13) Kama matokeo, Mataifa ya kilimwengu hayakuwa falme za Yehova Mungu. Serikali ya kitheokrasi ambayo aliisimamisha katika siku za nabii Musa ilikuwa ufalme wa pekee wa kidunia wa Mungu mpaka wakati taifa la Israeli lilipomkataa Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, kuwa Masihi kutoka kwa Mungu. (Kut. 15:18-21; Kum. 33:2-5; 1 Nya. 29:11, 12, 23; Mt. 21:43) Kwanza tangu kumalizika kwa Nyakati za Mataifa katika mwaka 1914 W.K. ‘ufalme wa dunia ulipata kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake’; na bado mataifa ya kilimwengu yangali yanamkataa Yehova kuwa Mfalme wao.—Ufu. 11:15-18.
“MFALME WA MATAIFA” NAMNA GANI?
11. Ni kwa habari gani Yeremia alimtaja Yehova kuwa “mfalme wa mataifa”?
11 Basi, ni kwa habari gani, Yeremia aweza kumwita Yehova kuwa “mfalme wa mataifa”? Kwa habari ya kwamba kati ya wale waliokuwa wafalme wa mataifa na ambao kwa hiyo walikuwa na ufalme alikuwa ndiye Mfalme mwenye kutokeza. Alitawala kama Mfalme wa wafalme, Mfalme Mkuu Zaidi, Ambaye anatawala wafalme wengine wote. “Kwa maana,” akasema Musa kwa Israeli huko nyuma katika mwaka 1473 K.W.K., “[Yehova], Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye kuogofya.” (Kum. 10:17) Baadaye mtunga zaburi aliyeongozwa kwa roho alisema hivi kwa watu wa Yehova: “Mshukuruni Mungu wa miungu; kwa maana fadhili zake ni za milele. Mshukuruni Bwana wa mabwana; . . . Yeye aliyewapiga wafalme wakuu; . . . Sihoni, mfalme wa Waamori; . . . Na Ogu, mfalme wa Bashani; . . . akaitoa nchi yao iwe urithi; . . . Urithi wa Israeli mtumishi wake.” (Zab. 136:2, 3, 17-22) Kwa njia hii anayatawala “mataifa yote,” yajapokuwa yana wafalme wao wa kishetani na wa kibinadamu.—Yer. 9:25, 26.
12. Yehova alionyeshaje kwa mfano na kumweleza Yeremia kwamba Yeye alikuwa “mfalme wa mataifa”
12 Kwa hiyo, basi, Yehova angeweza kumwambia Yeremia hivi: “Angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme.” (Yer. 1:10) Yehova alimwonyesha Yeremia kwa mfano kwamba alimwita kwa kufaa, “mfalme wa mataifa.” Yehova alimwamuru aende kwenye nyumba ya mfinyanzi. Baada ya mfinyanzi huyo kutengeza chombo kilichoharibika na kisha akafinyanga huo udongo tena ukawa chombo anachokubali, Yehova alisema hivi:
“Je! siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi huyu alivyotenda? . . . Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo ninyi , katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli. Wakati wo wote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuung’oa, na kuuvunja, na kuuangamiza; ikiwa taifa lile nililolitaja litageuka, na kuacha maovu yake, nitaghairi, nisitende mabaya yale niliyoazimia kuwatenda. Na wakati wo wote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuujenga na kuupanda; ikiwa watatenda maovu mbele za macho yangu, wasitii sauti yangu, basi nitaghairi, nisitende mema yale niliyoazimia kuwatendea.”—Yer. 18:1-10; tazama pia Yeremia 1:10.
13. Yehova aliye mfinyanzi Mkuu aliifuataje amri ile ile ya kutenda kuielekea Misri ya kale na kuelekea Israeli?
13 Karne nyingi kabla ya usemi huu, Yehova alikuwa amependelea nchi ya Misri katika siku zile ambazo Yusufu mwana wa Yakobo alifanywa msimamizi wake wa chakula. Walakini muda fulani baada ya Yusufu kufa, wakati mafarao wa Misri walipoanza kuwaonea watu wa Yusufu, wazao wa Yakobo (au, Israeli), na hata wakajaribu kuwafagilia mbali wasiwepo tena, Yehova aliingilia jambo hilo. Aliipiga nchi ya Misri na kumharibu Farao na majeshi yake na kuwaweka huru watu Wake wateule, Waisraeli (Zab. 136:10-16; Rum. 9:17, 18, 21-24) Kulingana na amri iyo hiyo ya kutenda, wakati ufalme wa Yuda ulipomwasi Mungu wa agano lake na kudumu katika njia zake mbaya, Yehova aliye Mfinyanzi Mkuu alikusudia kuupindua ufalme huo wa Kiisraeli. (Yer. 18:11-17) Waasi hao hata walimtendea vibaya nabii wa Yehova Yeremia kwa ajili ya wema aliokuwa akijaribu kuwafanyia. Kwani, si hata walifanya hila kumwua Yeremia. (Yer. 18:18-20, 23) Hivyo, mwishowe, likawa jambo lenye kukubalika kwa Yeremia kwamba hukumu kali za Yehova zifikilizwe juu ya waasi hao.—Yer. 18:21, 22.
14. Sababu gani sisi leo, kama mtu mmoja mmoja, twapaswa kuweka moyoni mifano hiyo ya kihistoria ya matendo ya Mfinyanzi Mkuu?
14 Mifano hii ya kihistoria ni jambo kwa mataifa yote, sana sana yale ya Jumuiya ya Wakristo, kuweka moyoni leo. Angaa sisi watu wa kawaida, kama mtu mmoja mmoja, twapaswa kufanya hivyo. Yehova aliye Mfinyanzi Mkuu yungali mkuu kupita wote, na karibuni ataonyesha wanadamu wote kwamba yungali “mfalme wa mataifa.” Leo, kupita wakati mwingine wo wote uliopata kuwapo, maneno yanayofuata ya Yeremia yangali ni ya kweli:
‘Bali [tofauti na miungu wa uongo waliosimuliwa mara kabla ya haya] Yehova ndiye Mungu wa kweli; Ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele; Mbele ya ghadhabu zake nchi yatetemeka, wala mataifa hawawezi kustahimili hasira yake. Mtaambiwa hivi [mataifa], Miungu hiyo isiyofanya mbingu na nchi, hiyo itaangamia katika nchi, nayo itatoweka chini ya mbingu.a Ameiumba dunia kwa uweza wake, Ameuthibitisha ulimwengu kwa hekima yake, Na kwa ufahamu wake amezitandika mbingu.’ —Yer. 10:10-12.
15. Sababu gani Yehova ana sababu nzuri ya kukasirikia mataifa, naye ataionyeshaje hasira yake?
15 Je! kuna sababu hakika kwa Yehova Mungu aliye Muumba kuwa na hasira leo? Ebu na tufikirie kutokuheshimu sheria zake kulikoenea sana, kuchukiwa kwa jina lake, uvunjaji wa sheria, kupenda anasa kuliko kumpenda Mungu, uasherati, unafiki wa kidini, mateso juu ya washiriki wa jamii ya Yeremia ya kisasa, kukataa kwa mataifa kunyenyekea ufalme wa Yehova kupitia kwa Kristo. Bila shaka, yakiwapo mambo haya yote, kuna kila sababu nzuri kwa Yehova Mungu aliye Mfinyanzi Mkuu kuwa na hasira. Karibuni ataionyesha, kama vile alivyofanya katika siku za Yeremia kwa kuuharibu Yerusalemu na ufalme wa Yuda.
16. Sababu gani mataifa maovu ‘hayatastahimili’ chini ya ghadhabu ya Yehova itakayoonyeshwa?
16 Katika Neno lake lililoandikwa, Biblia, Yehova ameukataa uovu wote. Karibuni ataviharibu vitu ambavyo amevikataa. Chini ya hasira yake hakuna ‘taifa litakalostahimili.’ Vitu ambavyo wamevifanya kuwa miungu na kuviabudu, “miungu” wao, itajionyesha kuwa isiyojiweza na kuangamia. Waabudu wake wataangamia pamoja nao.
17. Vilio kwa ajili ya msaada vinamwendea aliye Msaada wetu wa pekee kutoka kwa nani, na kwa sababu gani?
17 Ni jambo la akili, kuwa msaada wetu wa pekee ni Mungu mmoja anayeishi na wa kweli, “mfalme wa mataifa.” Vilio vya kuomba msaada vinamwendea kutoka kila mahali, kutoka kwa wale ambao kama Yeremia, wanachukia hali zisizo za kimungu na kutoka kwa wengine wote “wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika,” sana sana katika Jumuiya ya Wakristo iliyo ya kinafiki. (Eze. 9:4) Mioyo yao imevunjika kwa sababu “jeraha” kama lile linalosimuliwa na Yeremia limeyakaribia mataifa yote kwa ajili ya uhakika wa kwamba watawala wao hawakumtafuta Yehova kama msaada wetu wa pekee. (Yer. 10:19-22) Tengenezo lao la Umoja wa Mataifa litashindwa kama kitu cha kuleta amani na usalama wa ulimwengu. Mipango yote ya kibinadamu ya kuongoza mwendo wa historia na ya kuzuia uharibifu kutoka kwa Mfinyanzi Mkuu itajionyesha kuwa isiyofaa kitu.
18, 19. Watawala wa kisiasa wanajaribuje kuongoza hatua zao za kiutawala, na itaonyeshwaje kwamba si katika uwezo wao kufanya hivyo?
18 Baada ya kuichunguza mifano ya kuonya ya historia, inatulazimu kukubaliana na Yeremia aliposema: “Ee [Yehova], najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.”—Yer. 10:23.
19 Kwa sababu mwanadamu aweza kutembea huenda akafikiri kwamba aweza kutembea katika njia yo yote anayotaka na bado afike anakokwenda. Huenda akaona moyoni kwamba Yehova Mungu hahusiki katika jambo ‘hili. Kwa hiyo viongozi wa kisiasa wanajaribu kuongoza mambo ya kitaifa huku wakipuza masomo ya historia ya Biblia. Wanaidhihaki jamii ya kisasa ya Yeremia kwa ajili ya kutabiri juu ya msiba wa ulimwengu katika ‘dhiki kuu.’ (Mt. 24:3, 21, 22) Hawausikilizi unabii wa Biblia na wanafikiri kwamba wanaweza kuamua matokeo ya mambo, wakiongoza hatua zao kuelekea amani na fanaka yenye kudumu. Wangali, hata hivyo, wakienenda kisiasa, kiuchumi na kidini kama watakavyo, Yehova akiwa “mfalme wa mataifa” atawakwaza kwenye uharibifu uliotabiriwa wakati wa ‘dhiki kuu’ isiyoepukika.
20. Kama vile Yeremia, twamwomba Yehova atusahihishe kwa kadiri gani, na sababu gani?
20 Kusahihishwa na Mungu ni jambo tunalohitaji sote. Kwa hiyo tutataka kusali kama alivyosali Yeremia, kwa ajili ya tamaa ya kutaka kuepuka kuharibiwa pamoja na wanadamu: “Ee [Yehova], unirudi kwa haki [yaani, kulingana na uhitaji wangu]; si kwa hasira yako [wakati wa dhiki kuu], usije ukaniangamiza. Hasira yako uwamwagie mataifa wasiokujua [au waliokupuza], na jamaa zao wasioliitia jina lako; kwa maana [Wababeli na wenzi wao] wamemla Yakobo, naam, wamemla kabisa na kumwangamiza, na kuyafanya makao yake kuwa ukiwa.”—Yer. 10:24, 25, maneno ya pambizoni; Zab. 79:6, 7.
21. Twaweza kumwachia nani daraka la kufikiliza hukumu ya haki juu ya wale wanaojaribu kutuangamiza kwa ajili ya mwendo wetu wa kutenda?
21 Sala hiyo inaelekezwa kwa “mfalme wa mataifa.” Twaweza kumwachia yeye daraka la kufikiliza hukumu yake ya haki juu ya wale wanaompuza na kwa kulipiza kisasi wakijaribu kuwaangamiza wote wanaoikubali na kuishikilia kwa ushikamanifu enzi kuu yake ya ulimwenguni pote. Twainua vilio vyetu kwa ajili ya msaada kwake yeye aliye msaada wetu wa pekee.
“Lakini ziko mbingu mpya na dunia mpya ambazo sisi tunangojea kulingana na ahadi yake, na katika hizi haki itakaa.”—2 Pet. 3:13, NW.
[Maelezo ya Chini]
a Mstari huu, Yeremia 10:11, pamoja na maneno yake yaliyotajwa, hutofautishwa hasa kwa kuandikwa katika lugha ya Kiaramu hali sehemu nyingine yote ya unabii wa Yeremia imeandikwa katika lugha ya Kiebrania.