Mefiboshethi Mwanamume Mwenye Kuthamini
MEFIBOSHETHI au Merib-baali alikuwa mwana wa Yonathani na mjukuu wa Mfalme Sauli. Hata hivyo, kuwa kwake mmoja wa jamii ya kwanza ya kifalme ya Israeli hakukumpa tumaini la wakati ujao lenye utukufu. Alizaliwa baada ya babu yake Sauli kupoteza ufalme. Halafu, wakati Mefiboshethi alipokuwa na umri wa miaka mitano, baba yake na babu yake waliuawa katika vita. Kwa kusikia habari kuhusu jambo hilo, yaya (mwanamke mwenye kumtunza) wake Mefiboshethi alibabaika akatoroka, akimchukua kivulana huyo pamoja naye. Wakati wa kukimbia, Mefiboshethi alianguka akawa kiwete wa maisha, kilema miguu yote miwili. Karibu miaka saba baadaye, mjomba wake Ish-boshethi aliuawa. (2 Sam. 4:4-8) Kwa kweli Mefiboshethi alipatwa na msiba. Lakini hilo halikumfanya awe na uchungu. Alikua, akawa mtu mwenye kuthamini.
Mefiboshethi alioa mapema maishani mwake akawa na mtoto wa kiume jina lake Mika. Pamoja na jamaa yake, Mefiboshethi alitengeneza nyumba yake na Makiri, mtu mashuhuru na tajiri aliyeishi huko Lo-debari; mji mmoja katika Gileadi.—2 Sam. 9:4, 12; linganisha 2 Sam. 17:27-29.
Muda si muda, mwana huyo wa Yonathani alionyeshwa fadhili na Mfalme Daudi. Baada ya Daudi kuimarishwa kwenye ufalme wa Israeli kwa miaka kadha, alifikiria sana juu ya ahadi ya kiapo ambayo alikuwa amemfanyia rafiki yake Yonathani. (1 Sam. 20:42) Kwa ajili ya Yonathani, Daudi alitamani kuonyesha fadhili mtu ye yote aliyebaki wa nyumba ya Sauli. Kupitia kwa mtumishi wa Sauli, Siba, Daudi alipata habari ya Mefiboshethi naye hakukawia kumwita mwana huyo wa Yonathani. Kwa unyenyekevu Mefiboshethi aliinama mbele ya Daudi. “Kisha Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitikia, Mimi hapa, mtumwa wako!” Inaelekea sauti ya Mefiboshethi ilionyesha woga, sababu Daudi alimwambia: “Usiogope maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli babu yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima.”—2 Sam. 9:1-7.
Sababu gani Mefiboshethi aliogopa? Lazima ikumbukwe kwamba mjomba wake Ish-boshethi alitawala akiwa mfalme mshindani wa Daudi, na kwa hivyo Mefiboshethi angeonekana kuwa anataka ufalme. Kwa vile ilikuwa kawaida kwa watawala wa Mashariki kufanya cheo chao salama kwa kuwaua wapinzani wote, Mefiboshethi angaliweza kuhofia uhai wake.
Lazima iwe ilikuwa mshangao kwa Mefiboshethi kufikiriwa kwa huruma na mfalme huyo. Kwanza, pakawa lile shamba lililokuwa la Sauli. Inaweza kuwa kwamba Daudi, alipopata ufalme juu ya Israeli yote, alipata usimamizi wa shamba hilo. Au, baada ya kifo cha Sauli, wengine walilimiliki. Kwa vyo vyote, Daudi aliazimia kwamba shamba hilo lirudishwe kwa mrithi aliyestahili, Mefiboshethi. Lakini hayo hayakuwa mwisho. Mefiboshethi alipaswa afurahie mahali pa heshima katika baraza ya Daudi. Ingekuwa haki yake kula kwa kawaida katika meza ya kifalme. Hilo lilikuwa pendeleo ambalo lilionyeshwa, si kwa viwete wasiojiweza, bali kwa watu waliojipatia sifa kwa matendo mazuri.
Kwa kuthamini sana Mefiboshethi aliinama mbele za Daudi, akasema: “Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi?” (2 Sam. 9:8) Alivutiwa sana na fadhili za Daudi. Kwa maoni yake mwenyewe Mefiboshethi alijiona kuwa hastahili jambo hilo. Na alipojiita “mbwa mfu” alikuwa akikubali ya kwamba alikuwa na mahali pa chini sana.
Daudi alifanya mpango Siba alime shamba alilokuwa akirudishiwa Mefiboshethi. Mazao yake yangetumiwa kuruzuku (kusaidia) jamaa na watumishi wa Mefiboshethi. Eneo la shamba hilo lazima liwe lilikuwa kubwa kutosha, kwa vile Siba alitakiwa alifanyie kazi, pamoja na wana wake 15 na watumishi wake 20.—2 Sam. 9:9, 10; 19:17.
Siba alifuata maagizo ya Daudi lakini inaelekea alikuwa akitafuta njia ya kuchukua mali yote ya Mefiboshethi. Nafasi hiyo ilipatikana wakati mwana wa Daudi, Absalomu alipoasi. Daudi alipokuwa akitoroka kutoka Yerusalemu, Siba alimfikia akiwa na vitu alivyohitaji. Kwa kujibu ulizo la Daudi kuhusu Mefiboshethi, Siba alijibu kwa kusingizia hivi: “Angalia, anakaa Yerusalemu; kwani alisema, Leo nyumba ya Israeli watanirudishia ufalme wa baba yangu.” (2 Sam. 16:3) Kwa huzuni, Daudi alikubali masingizio hayo bila kushuku (kutia shaka). Akifuatwa na mwanawe Absalomu, kwa wazi Daudi alikuwa amevurugika akili hata akaamini kwamba Mefiboshethi alikuwa amekosa ushikamanifu. Kwa hiyo Daudi akaahidi kumpa Siba shamba la Mefiboshethi.
Kwa kipindi chote ambacho Daudi alilazimishwa kuishi mbali na mji mkuu, Mefiboshethi kwa kusikitika kwa ajili ya hali mbaya ya Daudi, alikosa kuangalia sura yake mwenyewe. Baada ya uasi wa Absalomu kushindwa, Mefiboshethi, katika hali hiyo ya kuomboleza, alikutana na Daudi huko Yerusalemu. Alisalimiwa kwa maneno haya: “Mbona hukwenda pamoja nami, Mefiboshethi?” (2 Sam. 19:25) Kwa sababu ya yale ambayo Siba alikuwa amesema, lilikuwa jambo la kawaida kwa Daudi kuuliza ulizo hilo. Mefiboshethi alijibu:
“Bwana wangu, Ee Mfalme, mtumwa wangu alinidanganya; kwa kuwa mimi mtumwa wako nilisema, Nitajitandikia punda, nipate kumpanda, na kwenda pamoja na mfalme; kwa sababu mimi mtumwa wako ni kiwete. Naye amenisingizia mimi mtumwa wako kwa bwana wangu mfalme; lakini Bwana wangu mfalme ni malaika wa Mungu; utende basi yaliyo mema machoni pako. Kwa kuwa jamaa yote ya baba yangu walikuwa kama watu wa kufa tu mbele ya Bwana wangu mfalme; ila uliniweka mimi mtumwa wako kati ya hao walao mezani pako. Basi ni haki gani sasa niliyo nayo, hata nimlilie mfalme zaidi?”—2 Sam. 19:26-28.
Kwa kusikia hayo Daudi kwa lazima aliona kosa lake kwa kukubali maneno ya Siba, na hiyo ikamhuzunisha. Hakutaka kusikia jambo lo lote zaidi kuhusu habari hiyo, kwa vile alimwambia Mefiboshethi: “Kwa nini unazidi kuyanena mambo yako? Mimi naamua, Wewe na Siba mwigawanye hiyo nchi.”—2 Sam. 19:29.
Mefiboshethi hakuona uchungu kwa sababu ya njia ambayo Daudi alifanya mambo. Yeye hakuwa anahangaikia hasara ya kimwili. Jambo la maana kwake lilikuwa kwamba Daudi alikuwa amerudi Yerusalemu bila kuumizwa. Hivyo, Mefiboshethi alisema hivi: “Hata yote [Siba] na atwae yeye, kwa kuwa bwana wangu mfalme amekuja kwa amani nyumbani kwake.”—2 Sam. 19:30.
Ingawa Mefiboshethi angeweza kuona uchungu kwa ajili ya mambo yaliyompata maishani, yeye alithamini uzima. Kwa sababu ya hali zilizokuwako wakati huo, angeweza kuuawa na Daudi. Hiyo ilimfanya ashukuru sana kwa kuwa na pendeleo la kula penye meza ya kifalme, naye kwa unyenyekevu na ushikamanifu akatii maamuzi ya mfalme Daudi.Hivyo Mefiboshethi ni mfano bora wa mwanamume aliyethamini alivyokuwa navyo naye hakuomboleza kwa ajili ya vitu asivyokuwa navyo. Na tuwe na kuthamini kama Mefiboshethi.