Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w80 7/15 kur. 17-22
  • Mtumikie “Mfalme wa Mataifa” Ukaokoke

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mtumikie “Mfalme wa Mataifa” Ukaokoke
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MWENDO WA HEKIMA SI WA KUPINDUA SERIKALI
  • MFANO WA KISASA WA EBED-MELEKI
  • Mthawabishaji wa Wote Wanaomtumikia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Utachagua Marafiki wa Aina Gani?
    Mungu Asema Nasi Kupitia Yeremia
  • Kuvumilia Kwa Uaminifu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Kutumikia Katika “Siku za Mwisho”
    Mungu Asema Nasi Kupitia Yeremia
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
w80 7/15 kur. 17-22

Mtumikie “Mfalme wa Mataifa” Ukaokoke

1. Kulingana na kielelezo kilichowekwa na Mfalme Yehoyakimu na mrithi wake, nduguye Sedekia, je! watawala ulimwengu leo watageuza mwendo wao kwa ajili ya yale yanayosemwa na jamii ya Yeremia?

INGEKUWAJE kama watawala wa ulimwengu, sana sana wale wa Jumuiya ya Wakristo, wangetambua kwamba kuna jamii ya kisasa ya Yeremia? Ingekuwaje kama wangeiita ili wafahamu kutokana na neno la kiunabii la Yehova juu ya jambo litakalowapata? Je! hiyo ingemaanisha wanakaribia kugeuza mwendo wao na kuchukua mwendo utakaowawezesha kuokoka “dhiki kubwa” iliyotabiriwa kuja juu ya ulimwengu huu? HASHA! Sivyo tukichukua mfalme Myuda wa mwisho wa Yerusalemu kama mfano, yaani, ndugu ya Mfalme Yehoyakimu, Sedekia. Mfalme Yehoyakimu alikuwa amelazimisha Yeremia na mwandishi wake Baruku wafanye kazi kisiri-siri​—haijaandikwa ni kwa muda mrefu namna gani. Walakini Sedekia, ndugu ya Mfalme Yehoyakimu alimfanya mabaya zaidi shahidi mwaminifu wa Yehova, Yeremia. Vivyo hivyo, pia, watawala wa leo wa kilimwengu hawatageuza mwendo wao wa upumbavu. Mambo mengi sana yanahusika kwa habari ya faida za kisiasa. Jambo hilo halimaanishi mema kwa watu wanaowatawala.​—Yer. 37:2.

2. Sedekia alimwita Yeremia aombee Waisraeli chini ya hali gani, walakini Yeremia alimwonyesha jambo gani?

2 Kwa habari ya wakati, ilikuwa katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia. Mazingiwa ya tatu na ya mwisho ya Yerusalemu yakifanywa na Wababeli yalikuwa yanaendelea! Vikosi vya kijeshi vilikuwa vikitoka Misri kusaidia mji huo uliozingiwa. Ili kukabiliana na tisho hilo, watekaji Wababeli waliondoka. Ukaonekana kama ni wakati wa kumwomba Yehova kwa ajili ya baraka yake juu ya vikosi vya Wamisri vyenye kusaidia. Kwa hiyo Mfalme Sedekia akamwita Yeremia ‘awaombee kwa [Yehova], Mungu wetu.’ Lakini Yehova alikuwa amemwagiza Yeremia asiombe kwa ajili ya jambo hilo. Yehova hangesikiliza sala hiyo. (Yer. 37:3; 11:14; 14:11, 12) Kwa hiyo Yeremia alionyesha kwamba Wababeli wangeshinda vikosi vyenye kusaidia vya Wamisri kwa kumwambia Mfalme Sedekia kwamba Wababeli wangerudi na kuteketeza Yerusalemu kabisa.​—Yer. 37:4-10.

3. Sababu gani wakuu wa mji wa Yerusalemu waliamuru Yeremia atupwe “gerezani”?

3 Wakati wa kuondoka kwa Wababeli, Yeremia alijiona huru kutoka Yerusalemu na kwenda kwenye mji wa makuhani wa Anathothi, katika eneo la kabila la Benyamini. Alipokamatwa katika lango la kaskazini la Yerusalemu, Lango la Benyamini, alikataa kwamba hakuwa akitoroka kwa maadui Wababeli. Wakimtenda kama kwamba alikuwa mfitini serikali, msaliti, wakuu wa mji waliamuru awekwe “gerezani,” ambapo alizuiliwa kwa “siku nyingi.” (Yer. 37:11-16) Lo! jinsi inavyofanana na namna jamii ya Yeremia inavyotendwa leo!

4. Yeremia alimshaurije Mfalme Sedekia ili ajirahisishie mambo, na sababu gani Yeremia alihamishwa kwenye Ua wa Walinzi?

4 Wakati ule angekabiliana na Mfalme Sedekia, je! Yeremia angeachana na ujumbe wake mkali? Wakati Mfalme Sedekia alipoamuru atolewe katika nyumba ya kizuizi na kupelekwa mahali palipofichika ili ahojiwe faraghani, yeye alimwambia mfalme huyo kwa ujasiri kwamba angekuwa mfungwa wa Wababeli, ambao Yehova alikuwa akitumia kama vyombo vyake. Kama mfalme huyo angekubali kushindwa nao au kama ingemlazimu akamatwe na kufanywa mfungwa bila kupenda, vyo vyote iwavyo, matokeo yangekuwa yale yale. Yeremia alipendelea mfalme huyo ajirahisishie mambo. Yeremia hakumpa mfalme huyo mahakikisho ya uongo. Kwa unyofu, Yeremia hakuwa akitenda jambo lo lote baya kwa watu wake na kwa mfalme wao, na hivyo sababu gani awekwe katika mahali pa kizuizi ambapo pangemaanisha kifo chake cha mapema? Alipomwomba, Mfalme Sedekia aliamuru ahamishwe kwenye Ua wa Walinzi, namna fulani ya gereza la kijeshi kwa Yeremia. Chakula chake kilikuwa mkate na maji.​—Yer. 37:17-21.

MWENDO WA HEKIMA SI WA KUPINDUA SERIKALI

5. Ni jambo gani la haki na la kufaa alilopaswa kufanya Mfalme Sedekia kuhusiana na Milki ya Babeli, na sababu gani ukawa wajibu wa mtu mmoja mmoja kuchukua hatua kuhusiana na Yerusalemu?

5 Sedekia alikuwa amefanywa mfalme wa Yerusalemu na Mfalme Nebukadreza. Hata hivyo, baada ya kuwa mfalme msaidizi wa Nebukadreza kwa miaka minane, Sedekia akamwasi. Mwendo wa haki na wenye kufaa ulikuwa kuachana na uasi na kujitiisha kwa amani chini ya Ufalme ambao Yehova alikuwa ameruhusu uwe Mamlaka ya Tatu ya Ulimwengu ya historia ya Biblia. Ikiwa yeye kama mfalme angekataa kufanya jambo hilo, basi ingekuwa kwa faida ya watu hao kufanya hivyo. Ndiyo, kufanya kama vile Yeremia alikuwa ametangazia watu hao katika Yerusalemu:

“[Yehova] asema hivi, Akaaye ndani ya mji huu atakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; bali yeye atokaye kwenda kwa Wakaldayo ataishi, naye atapewa maisha yake yawe kama nyara, naye ataishi. [Yehova] asema hivi, Bila shaka mji huu utatiwa katika mikono ya jeshi la mfalme wa Babeli, naye atautwaa.” (Yer. 38:2, 3)

Mfalme Sedekia alipaswa kuchukua uongozi katika kufuata shauri hilo lililoongozwa kwa roho. Walakini kwa kuwa hakufanya hivyo, ilikuwa juu ya raia mmoja mmoja wachukue hatua kwa imani katika uongozi wa Yehova.

6. Sababu gani wakuu waliamuru Yeremia atupwe ndani ya shimo lililokuwa katika ua wa mwana wa mfalme?

6 Wakuu wa Yerusalemu walitaka sana Yeremia auawe, kwa kuwa walidai kwamba yeye alikuwa akidhoofisha mikono ya majeshi yenye kulinda mji huo; alikuwa akiharibu nia ya watu ya kupigana. Kwa hiyo, bila ruhusa ya mfalme, waliamuru Yeremia atupwe shimoni katika Ua wa Walinzi, lililokuwa nyumbani mwa Malkiya “mwana” wa Sedekia. Humo shimoni, Yeremia alizama matopeni. Sasa asingeweza kufuata shauri lake alilowapa wengine.

7. Ni nani sasa aliyekuja kumwokoa Yeremia, na Juu ya msingi gani?

7 Sasa, wakati mambo yalipoonekana hayana tumaini kabisa kwa Yeremia, kamba zilikuwa zikitelemshwa kwenye shimo hilo, pamoja na matambara yazuie makwapa yake yasiumie, ili kumnyanyua kutoka katika shimo hilo lenye matope. Towashi Mwethiopia aliyeitwa Ebed-meleki, mfanya kazi wa mfalme, alikuwa amepata kusikia juu ya hali ya nabii huyo. Akiogopa juu ya Yeremia kufia mle chini katika shimo, alizungumza na mfalme kwa ujasiri. Aliamriwa na mfalme achukue pamoja naye wanaume 30 na kumnyanyua Yeremia atoke nje.​—Yer. 38:10-12.

8, 9. (a) Katika mahojiano ya siri, Mfalme Sedekia alimwekaje Yeremia huru kutokana na mkazo wote wa kumfanya awe nabii wa uongo kwake? (b) Yeremia alimpa Sedekia shauri gani lisilobadilika, akiweka mbele yake mambo mengine gani tofauti ya kufanya?

8 Mfalme Sedekia, ambaye alikuwa ameamuru Yeremia aokolewe, alimwita Yeremia kwa mara nyingine amhoji kisiri katika kijia hekaluni. Sedekia aliapa kwa Yehova mwenye kutoa uhai kwamba hataamuru nabii huyo auawe kwa kumwambia kweli ya Mungu, walakini hakuahidi kuisikiliza. Akiwa amewekwa huru na tisho la kifo ambalo lingeweza kumbadili kuwa nabii wa uongo, Yeremia alishikamana kabisa na ujumbe ule ule ambao mapema zaidi ulikuwa umemweka katika hatari ya kifo:

9 ‘Mfalme Sedekia, ama wewe mwenyewe ukiwa mfalme ukubali kuutoa Yerusalemu kwa Wakaldayo ama Yehova mwenyewe atautoa uteketezwe kabisa na Wakaldayo. Usiogope kutendwa vibaya na Wayahudi ambao tayari wamesikiliza shauri langu na kukimbia kwa watekaji. Usipojitoa ni jambo gani litatokea? Ndipo wanawake watakaookoka wataongozwa kutoka huku wakiimba namna wale walioendelea kuwa na amani nawe walivyokupotoa na kukudanganya na kukuacha kwa hila ili utumbukie matopeni, hali wao wenyewe walikimbia. Vilevile, wake zako na watoto wako wenyewe watachukuliwa mateka. Wewe mwenyewe hutaponyoka usikamatwe na mfalme wa Babeli. Ole! ndiwe utakayelaumiwa kwa kuteketezwa kabisa kwa mji!’​—Yer. 38:17-23.

10. Yeremia alifanyaje mambo yawe rahisi kwa Mfalme Sedekia kwa yale aliyowaambia wakuu wenye kutaka kujua, naye aliendelea kuzuiliwa katika makao yake mapya mpaka wakati wa tukio gani?

10 Wakuu wa Yerusalemu ndio watu ambao walitenda kama ‘watu wenye amani’ pamoja na Mfalme Sedekia. Akiwaogopa wao, yeye alimwambia Yeremia, huku akimwogopesha kwa kifo, asiwaambie mambo hayo ya hakika, iwapo wangeuliza. Angeepa maulizo yao kwa kusema mfalme amekubali tu kuzungumza naye, kwa kuwa hakutaka kurudishwa kwenye kizuizi katika nyumba ya Yehonathani, mwandishi, akafie huko. Kwa kutowaambia watu wenye kutaka kujua hadithi yote juu ya mahojiano hayo ya siri, angemrahisishia mfalme mambo. Kwa kupatana na yale ambayo Yeremia aliwaambia wakuu hao wenye mashaka, alifungiwa mahali pengine, Ua wa Walinzi. Hapo alivumilia kuzuiliwa mpaka siku ya tisa ya mwezi wa nne (Tamuzi) wa mwaka 607 K.W.K., wakati Wababeli walipouteketeza Yerusalemu, wakiuteka, kumfanya Mfalme Sedekia pamoja na majeshi yake watoroke.​—2 Fal. 25:2-5.

11. Katika siku ile Yerusalemu ulipoanguka, njia ya kutorokea kupitia Lango la Kati ilizuiwaje kwa Wayahudi waliozingiwa?

11 Kwa hiyo, kama vile Yeremia alivyoonya, Yehova, ambaye juu ya kiti chake cha enzi cha kidunia Mfalme Sedekia alikuwa akikalia kule Yerusalemu, akawa na daraka la kuutoa mji kwa watekaji hao. Hivyo, katika siku hiyo ya kiangazi ya Tamuzi 9, 607 K.W.K., mahali pa mahakimu Wayahudi kuketi katika Lango la Kati la Yerusalemu ili kuendesha kesi kisheria, wakuu watano Wababeli, ambao majina yao yameandikwa, waliketi langoni mwa mji huo. Hivyo wakazuia njia ya kutorokea ya Wayahudi wale waliozingiwa. (Yer. 39:1-3; 1 Nya. 29:23) Ole!

12. Mfalme Sedekia alikosaje kuushinda unabii wa Yeremia juu yake, naye alilazimishwa kushuhudia tamasha gani mbele ya Mfalme Nebukadreza?

12 Huenda ikawa Mfalme Sedekia alipokuwa akitoroka na majeshi yake kutoka katika mji ulioshambuliwa wakifichwa na usiku, alijipongeza mwenyewe kwamba alikuwa ameshinda unabii wenye msiba wa Yeremia juu yake. Walakini alishindwa kufika kwa Farao Hofra wa Misri, mwenye mapatano naye. (Yer. 44:30) Wababeli wenye kumfuata walimpata katika uwanda wa jangwa la Yeriko, katika Araba au Mpasuko wa Bonde, maili kadha kuelekea kaskazini-mashariki mwa Yerusalemu. Akiwa katika vifungo vya shaba alipelekwa kaskazini kwenye mji wa Ribla katika nchi ya Hamathi, ili apambane na Mfalme Nebukadreza. Kabla ya Sedekia kupofushwa kwa amri ya Nebukadreza, alilazimishwa kushuhudia tamasha yenye kuogopesha ya wanawe wenyewe wakiuawa. Wengi wa wakuu wake wa mahakma na kijeshi nao vilevile waliuawa. Kuhani Mkuu Seraya na msaidizi wake, Sefania, ambao hawakumwunga mkono kuhani mwenzao, Yeremia, waliuawa, pamoja na mabawabu (walinda mlango) watatu wa hekalu.​—2 Fal. 25:6, 7, 18-21.

13. (a) Historia yote hiyo ya kale inahusianaje na mwaka 1914 W.K.? (b) Sababu gani ni jambo la akili kuuliza kama Ebed-meleki alifananisha jamii fulani leo, nalo jibu ni nini?

13 Je! historia yote hiyo ya kale inahusu karne yetu ya 20? Ndiyo! Miezi mwili baada ya msiba huo juu ya Mfalme Sedekia, milki yake, nchi ya Yuda, iliachwa mahame kabisa. Hapo “nyakati saba” za mataifa, “nyakati za Mataifa,” zilianza kipindi chake cha miaka 2,520, zimalizike mwaka 1914 W.K. (Dan. 4; Luka 21:24, Authorized Version) Leo kile kilichofananishwa na Yerusalemu wa siku za Mfalme Sedekia kinakaribia uharibifu wake, kulingana na uamuzi wa hukumu ya Yehova, ‘Mfalme wa mataifa.’ (Yer. 10:7) Basi, inafaa kama nini kuwepo duniani wakati huu wenye hatari jamii ya waabudu wa Yehova Mungu ambao walifananishwa kimbele na nabii-kuhani Yeremia! Kwa sababu ya hilo twauliza kwa kufaa, Je! vilevile duniani kuna jamii ambayo ilifananishwa kimbele na towashi Mwethiopia aliyefanya urafiki na Yeremia, yaani, Ebed-meleki mtumishi wa Mfalme Sedekia? Mambo ya hakika ya kisasa yanaonyesha iko.

14. (a) Kwa habari ya rangi ya ngozi, Ebed-meleki alikuwa nani? (b) Sababu gani hakujaribu kutoroka Yerusalemu pamoja na bwana wake wa kifalme?

14 Ebed-meleki hakujaribu kutoroka kutoka Yerusalemu pamoja na bwana wake wa kifalme, Sedekia. Yeye alikuwa Mwethiopia, namna ya mtu ambaye Yeremia aliuliza ulizo hili, “Je! Mkushi [au, Mwethiopia] aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake?” (Yer. 13:23) Ebed-meleki alikuwa Mweusi,a na katika tafsiri ya Biblia ya Byington anaitwa “Ebed-Meleki aliye Mweusi.” (Yer. 38:7, 12; 39:15, The Bible in Living English) Hakupaswa kukimbia toka Yerusalemu katika kujaribu kupata usalama. Yeye alikuwa amepewa ahadi na Mungu wa Yeremia juu ya kuhifadhiwa kwake. Hiyo ndiyo sababu, baada ya kuambiwa jambo ambalo Wayahudi maskini sana walifanyiwa na Nebukadreza na jambo alilofanyiwa Yeremia, masimulizi yake yanashikamana na Yeremia 38:28. Kwa kweli, tafsiri ya Moffatt A New Translation of the Bible inaweka Yeremia 39:15-18 mara baada ya Yeremia 38:28, ili isomeke kama hadithi isiyokatishwa.

15. (a) Yeremia alilipata neno la Yehova kumhusu Ebed-meleki wakati gani? (b) Neno hilo lilisema nini kwa habari ya Mwethiopia huyo?

15 Kwa hiyo mistari ambayo imetajwa chini yapaswa kufahamika kuwa ilihusu wakati wa kabla ya Yerusalemu kuanguka kwa Wababeli wenye kuteka katika Tamuzi 9, 607 K.W.K., katika mwaka wa 11 wa utawala wa Mfalme Sedekia:

“Basi neno la [Yehova] likamjia Yeremia wakati ule alipokuwa amefungwa katika uwanda wa walinzi [na kabla ya askari wa Kiyahudi kutoroka hapo Yerusalemu ulipoanguka], kusema, Haya! enenda ukaseme na Ebed-meleki Mkushi kusema, [Yehova] wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitaupatiliza mji huu maneno yangu kwa mabaya, wala si kwa mema; nayo yatatimizwa mbele yako katika siku hiyo, asema [Yehova]; wala hutatiwa katika mikono ya watu wale unaowaogopa. Kwa maana ni yakini, nitakuokoa, wala hutaanguka kwa upanga [wa Wababeli], lakini nafsi yako itakuwa kama nyara kwako; kwa kuwa ulinitumaini mimi, asema [Yehova].”​—Yer. 39:15-18.

16. Kwa hiyo Ebed-meleki alipaswa kufurahia nini kama vile wanavyofurahia wale wanaoteka nyara, nacho ni nini kilichobaki ijapokuwa hatuna historia yake zaidi?

16 Kwa hiyo, wakati wa kuanguka kwa Yerusalemu rafiki huyo wa nabii wa Yehova alijiacha mikononi mwa Mungu wa Yeremia. Awe alihamishwa mpaka Babeli na kufa kifo cha kawaida huko au awe aliachwa katika nchi ya Yuda kama mmojawapo wa watu maskini wa nchi chini ya Liwali Gedalia, Biblia haisemi. Vyo vyote iwavyo, nafsi au maisha yake hayakuangamizwa na askari Wababeli bali aliruhusiwa aendelee kuwa na nafsi yake ya kibinadamu kama mtu yule anayefurahia nyara. Kwa hiyo angeweza kuendelea kuishi na kumwabudu Mungu yule ambaye alikuwa amemtumaini, Mungu ambaye aliokoa nabii wake kutoka katika shimo lenye matope la Yerusalemu uliozingiwa. Bila shaka kwa kufanya jambo hilo alikuwa amejiletea chuki ya wakuu ambao walikuwa wamemweka Yeremia katika shimo gerezani ili afe. Lakini Ebed-meleki hakutiwa mikononi mwao ili walipize kisasi. Chini ya ulinzi ulioahidiwa wa Yehova hakuwa na sababu ya kuogopa yale ambayo wakuu hao wangetaka kufanya ili kulipa kisasi. Kufikia hapo anatoweka kutoka katika historia ya Biblia, walakini sivyo jina lake wala ahadi aliyompa Mungu.

MFANO WA KISASA WA EBED-MELEKI

17. Jina la Mwethiopia huyo, Ebed-meleki, lamaanisha nini, na ni katika njia gani jina hilo ilipatana na hali yake?

17 Je! kuna mfano wa kisasa wa Ebed-meleki kuhusiana na jamii ya Yeremia ya kisasa? Ndiyo! Basi, ni nani walio washiriki wa mfano wa kisasa wa Ebed-meleki? Namna alivyoitwa kwa jina hilo hatujui. Jina Ebed-meleki linamaanisha “Mtumishi wa Mfalme.” Akiwa towashi pengine alikuwa amefanywa kuwa mhasi (aliyetolewa uwezo wa uzazi)b na kutoweza kuwa na jamaa yake mwenyewe. Lakini, kwa kupatana na jina lake, alikuwa akitumika nyumbani mwa mfalme wa Yuda. Pamoja na hayo, kwa sababu ya kumtumaini Yehova, alipata kuwa katika utumishi wa mfalme mkuu kuliko mfalme wa kidunia. Sedekia aliketi juu ya kiti cha enzi cha kifalme kilichoitwa ‘kiti cha enzi cha Yehova.’ (1 Nya. 29:23) Basi, ni jambo la akili kwamba Ebed-meleki alijionyesha kwa hakika kuwa katika utumishi wa ‘Mfalme wa mataifa,’ Yehova. Kwa kuwa katika utumishi wa ufalme wa mfano wa Yehova katika nchi ya Yuda, alithawabishwa vya kutosha kwa kuhifadhiwa wakati Yerusalemu usioaminika ulipoharibiwa.

18. Kulingana na maelezo ya Ufunuo 7:14, 15, “mkutano mkubwa” ulifananishwa na mtu gani mmoja wa siku za Yeremia?

18 Juu ya kuhifadhiwa kupita ‘dhiki kuu’ ya Jumuiya ya Wakristo, Ufunuo 7:14, 15 unasema hivi kuhusu “mkutano mkubwa” unaoelezwa humo: “Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo. Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake.” Wakiwa jamii, wale walio washiriki wa “mkutano mkubwa” wa waokokaji wa dhiki walifananishwa na Ebed-meleki, mwokokaji mwenye kutokeza sana wa uharibifu wa Yerusalemu.

19. Tamaa kubwa zaidi ya jamii ya Ebed-meleki ni kuwa katika utumishi wa nani, nao wana nia ya kujiletea nini kwa ajili ya jamii ya Yeremia?

19 Jamii hiyo inajifunza kweli kweli kumwogopa Yehova na kumtumaini. Tamaa yao kubwa zaidi ni kuwa katika utumishi wa Mwenye Enzi Kuu ya Ulimwengu Wote, ‘Mfalme wa mataifa,’ kuliko kutumikia watawala wa kisiasa na wafalme wa serikali zilizofanywa na wanadamu. Wanaona namna watawala wenye pupa ya kuwa na mamlaka, kama vile Adolf Hitler aliyepata mamlaka katika Ujeremani katika mwaka 1933 W.K., wakijaribu kufutilia mbali mabaki watiwa mafuta wa Yehova ambao walifananishwa na nabii wake Yeremia. Kwa hiyo jamii ya Ebed-meleki inapinga na kutaka haki ifanywe katika jitihada yenye uhodari ya kusaidia jamii ya Yeremia, ingawa jambo hilo linamaanisha kujiletea chuki na mateso ya maadui wa kidini na kisiasa wa jamii ya Yeremia.

20, 21. (a) Jamii ya Ebed-meleki ilianza kuonekana kuanzia mwaka gani sana sana? (b) Jamii hiyo inajaribuje kumwiga Ebed-meleki wa siku za Yeremia, nao wanatia moyo watu wote wachukue hatua gani kwa habari ya milki ya ulimwengu ya dini ya uongo?

20 Watu hao wenye kuunga mkono mabaki watiwa mafuta wa mashahidi wa Yehova walianza kuonekana sana sana katika mwaka 1935, wakati “mkutano mkubwa” wa waokokaji wa “dhiki” ulipotambulishwa.

21 Bila kujali kama jamii ya Ebed-meleki ina uongozi wo wote juu ya serikali za Jumuiya ya Wakristo au hapana, hawajapendelea wakati wo wote jitihada ya kidini na kisiasa ya kuiua jamii ya Yeremia au kuifanya jamii ya Yeremia isiwe na matokeo katika utumishi wa waziwazi wa Yehova kama kwamba kuwatelemsha kwenye shimo lenye matope katika nyumba ya walinzi. Wajapoelekeana na kukosa kibali ya mamlaka ya kidini na kisiasa ambako kunaleta woga, wamefanya yote wawezayo kunyanyua jamii ya Yeremia kutoka katika “shimo” lenye matope la kutotenda. Mpaka siku hii ya leo wamekuwa wakitenda kwa uhodari ulimwenguni pote katika upande wa jamii ya Yeremia, wakitangaza maangamizi ya Jumuiya ya Wakristo na ya milki ya ulimwengu ya dini ya uongo, Babeli Mkuu. Wanawatia watu wa namna zote moyo waikimbie taratibu hii ya mambo iliyohukumiwa maangamizi na kuchukua msimamo imara upande wa majeshi yenye kuua ya Yehova chini ya jemadari mkuu zaidi kuliko Nebukadreza, yaani, Yesu Kristo. Hivyo wanathibitisha wanamtumaini Yehova kabisa, ‘Mfalme wa mataifa.’

22. Jamii hiyo haitauawa kwa “upanga” gani wa mfano?

22 Kwa sababu ya kujitoa bila kusita-sita kwake na kwa jamii yake ya kisasa ya Yeremia, Yehova anapenda jamii hii ya Ebed-meleki. Yeye anaahidi kwamba jamii hiyo haitaangamia kwa “upanga” wa vita ya “siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” katika Har–Magedoni.​—Ufu. 16:13-16.

23. Nyara watakazoteka zitakuwa nini, nao wametendaje kama “kondoo” katika mfano wa Yesu katika Mathayo 25:31-34?

23 Kama zawadi kutoka kwa Yehova, maisha zao za kidunia, nafsi zao, zitahifadhiwa kama nyara za vita, kwa kustahili wakipata maisha yaliyohifadhiwa (yaliyolindwa). Kama vile watu wenye mfano wa kondoo katika mfano wa Yesu wa “kondoo” na “mbuzi,” wamefanyia mema mabaki ya ndugu za Kristo za kiroho. Wakati wao walipokuwa “kifungoni,” katika “Shimo” lenye matope au nyumba ya kifo, waliwatembelea kisiri-siri au waziwazi nao wametumikia katika kuwaweka huru kwa ajili ya utendaji zaidi katika utimizo mkuu wa kazi ya Yehova ya kutoa ushuhuda katikati ya taratibu ya mambo ya kilimwengu iliyohukumiwa maangamizi.​—Mt. 25:31-36, 46.

24. Jamii ya Yeremia inamshukuru Mungu leo kwa ajili ya utumishi wa jamii gani, nalo ni tendo gani la umoja watakaloendelea kufanya baada ya kuiokoka “dhiki kubwa”?

24 Na ifahamike kila mahali kwamba jamii ya Yeremia inamshukuru Yehova kwa ajili ya kutokeza “mkutano mkubwa” wa “kondoo wengine,” waliofananishwa kimbele na towashi Mwethiopia Ebed-meleki wa siku za mwisho za Yerusalemu usioaminika, mji mkuu wa ufalme wa Yuda. Itakuwa furaha isiyoelezeka kwa jamii ya Yeremia kuiokoka “dhiki kubwa” pamoja na jamii ya Ebed-meleki ikiwa upande wayo. Wataanza kufanya kazi karibu karibu pamoja katika Taratibu Mpya ambayo wataingizwa ndani yake chini ya ufalme wa miaka elfu wa Kristo. Kuingizwa huko kwenye Taratibu Mpya yenye kuangaza kutakuwa ndiyo zawadi yao kwa ajili ya kutumikia sasa Mwenye Enzi Kuu ya ulimwengu wote, Yehova, ‘Mfalme wa mataifa.’

—Kutoka The Watchtower Feb. 1, 1980

[Maelezo ya Chini]

a Kulingana na kitabu A Greek-Engish Lexicon, kilichotungwa na Liddell na Scott (1948), neno la Kigiriki Mwethiopia (Aithiops) lamaanisha “Uso Ulioungua, yaani, Mwethiopia, mweusi, Homer (mtunga mashairi Mgiriki), n.k.”

b Hakuna towashi mgeni aliyefanywa mhasi ambaye angeweza kuwa mwongofu Myahudi au mshiriki wa kundi la Israeli lililoahiriwa.​—Kum. 23:1; linganisha Isaya 56:3-5.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki