Ufahamu Katika Habari
Kuhesabu Wakatoliki
● Kanisa Rumi Katoliki linadai kuwa na washiriki wengi wanaofika milioni 700 ulimwenguni pote. Ni watu wa namna gani wanaohesabiwa kuwa Wakatoliki? Kionyesho kimoja kinatoka katika Makao ya Mtakatifu Augustino katika mji wa New York. Katika kujibu barua ya karibuni iliyokuwa ikiliomba kanisa hilo liondoe jina lake katika maandishi yake, mwanamume ambaye alikuwa amekuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova alipata jibu hili: “Kwa vyo vyote hatuwezi kuliondoa jina lako katika maandishi ya Kubatizwa au mengineyo ya Sakramenti. Kama unavyojua Kanisa Katoliki ndilo Kanisa pekee la kweli lililoanzishwa na Yesu (Mt 16) nako kuliondoa jina lake kungekuwa kuitenda dhambi Roho Takatifu. Pasipo kujali unaoshirikiana nao wakati huu wewe ni Mkatoliki nawe utaendelea milele kuwa Mkatoliki Aliyebatizwa . . .”
Iwapo hilo ndilo zoea la kawaida wakati watu wanapoomba majina yao yaondolewe wasiwe washiriki wa kanisa, bila shaka jambo hilo linatilia shaka ubora wa hesabu za washiriki zinazotolewa hadharani. Vilevile jambo hilo linaendeleza zaidi namna ya unafiki wa kidini uliotabiriwa ungekuwako katika “siku za mwisho,” wakati Biblia inaposema watu watakuwa na “namna ya utawa” tu.—2 Tim. 3:1, 5, NW.