Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w81 11/1 kur. 14-19
  • Uwe Mwenye Hekima—Jiendeshe Mwenyewe kama Mtu Mdogo Zaidi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uwe Mwenye Hekima—Jiendeshe Mwenyewe kama Mtu Mdogo Zaidi
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • KUJIFUNZA KUTOKANA NA MIFANO YA BIBLIA
  • KWA SABABU GANI TATIZO HILO LIPO?
  • HEKIMA YA KIDUNIA, YA MNYAMA, YA KISHETANI
  • MIFANO MYEMA YA MUSA, YESU NA PAULO
  • Misaada Katika Kujiendesha Wenyewe kama Watu Wadogo Zaidi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
  • Sitawisha Ile Roho ya Aliye Mdogo Zaidi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Tukijiongoza Wenyewe Kama “Aliye Mdogo Zaidi”
    Mwimbieni Yehova Sifa
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
w81 11/1 kur. 14-19

Uwe Mwenye Hekima—Jiendeshe Mwenyewe kama Mtu Mdogo Zaidi

“Yeye ajiendeshaye mwenyewe kama mtu mdogo zaidi kati ya ninyi nyote ndiye ambaye ni mkubwa.”​—Luka 9:48, NW.

1, 2. (a) Ni nani waliokuwa kati ya watu wenye kupendelewa zaidi sana waliopata kuikanyaga dunia hii, na kwa sababu gani? (b) Lakini, inashangaza kwamba ni tatizo gani lililoonekana-onekana kati yao?

NI NANI waliokuwa kati ya watu wenye kupendelewa zaidi sana waliopata kuikanyaga dunia hii? Bila shaka, wale wanafunzi 12 wa Yesu Kristo aliowachagua wawe mitume walikuwa kati yao. Walikuwa na mapendeleo makubwa sana ya kufuatana naye alipokwenda “akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu.” (Luka 8:1) Lazima wawe walifurahi sana kuzisikia hotuba za Yesu, kama yale Mahubiri ya Mlimani, na kumshuhudia akifanya mwujiza baada ya mwujiza mwingine! Isitoshe, je! Yesu hakuwapa daima maagizo ya faraghani? Naam, ilikuwa hivyo.

2 Hata hivyo, jambo la ajabu ni kwamba watu hawa wenye kupendelewa zaidi sana walikuwa wakibishana-bishana kati yao wenyewe habari za aliyekuwa mkubwa au wa kwanza kabisa kati yao. Hakuna mmoja wao aliyetaka kujiendesha mwenyewe kama mtu mdogo zaidi. Je! ushindani huo ulileta amani, upatano na furaha? Je! ulimpendeza Yehova Mungu? Je! ulikuwa ndio mwendo wa hekima? Haiwezi kuwa hivyo, kwa maana wakati mmoja Yesu aliwaambia nini? Baada ya kuweka mtoto mdogo kando yake, aliwaambia hivi: “Mtu awaye yote anipokeaye mtoto mdogo huyu juu ya msingi wa jina langu anipokea mimi pia, na mtu awaye yote anipokeaye mimi ampokea yule pia ambaye alinituma niende. Kwa maana yeye ajiendeshaye mwenyewe, kama mtu mdogo zaidi kati ya ninyi nyote ndiye ambaye ni mkubwa.”​—Luka 9:48, NW.

3. Ni baadhi ya mifano gani ya kilimwengu iliyopo ya kutokutaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi.?

3 Ni nani leo ambao kwa hekima wanaridhika na kujiendesha wenyewe kama watu wadogo zaidi? Ni wachache sana! Ndiyo sababu kuna mvurugo mwingi sana, mashindano yenye ubishi, ugomvi na vita katika ulimwengu huu wa zamani. Mataifa na makundi ya mataifa yanaendela kushindana; kila mtu anataka kuwa juu, kuwa wa kwanza kabisa, kuwa ndiye mwenye uwezo kupita watu wote. Kwa hiyo mataifa yamelemea watu wao kwa gharama nyingi sana zinazotumiwa kununua silaha. Tena lile hangaiko kubwa la wanawake kutaka kujipigania wawe huru na kuwa na haki za kufanya mambo sawa na wanaume limetokea kwa sababu wanawake wanaoshiriki utendaji huo wamekataa kujiendesha wenyewe kama watu wadogo zaidi wakilinganishwa na waume zao. Na je! jambo ilo hilo silo linalosumbua vijana wengi wa ki-siku-hizi? Wanachukizwa na daraka la wazee wao; hawataki kujiendesha wenyewe kama watu wadogo zaidi kuhusiana na wazee wao, wazazi wao. Je! hali hizo zote za kutokutaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi zimeleta furaha? Je! ni jambo la hekima? Aka!

KUJIFUNZA KUTOKANA NA MIFANO YA BIBLIA

4. Mtu wa kwanza kuwa na hali hiyo ya akili ya kujitukuza alikuwa nani, na ni jambo gani linaloonyesha hivyo?

4 Kwamba kutokutaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi ni upumbavu inaweza kuonekana katika uhakika wa kwamba matata yote yaliyo katika ulimwengu yalianza kwa sababu malaika fulani hakutaka kujiendesha hivyo. Kwa sababu gani inaweza kusemwa hivyo? Kwa sababu malaika huyo, aliyewaingiza wazazi wetu wa kwanza katika barabara ya dhambi na kifo, alionyesha wazi makusudi yake ya kweli katika kishawishi cha tatu cha jangwani alichotolea Mwana wa Mungu. Katika kishawishi hicho alimtolea Yesu falme zote za ulimwengu kama angekubali kufanya tendo moja tu la kumwabudu Shetani. Hiyo ilionyesha nini? Kwamba Shetani alitaka kuwa sawa na Yehova Mungu, kwamba hakutaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi kuhusiana na Yeye. Hilo linaweza kuonekana katika jibu ambalo Yesu alimpa Shetani: “Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” Kwa sababu hakutaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi, Shetani alijivika aibu na fedheha na mwishowe atapunguzwa awe si kitu tena.​—Mt. 4:8-10; Ebr. 2:14.

5. (a) Hawa alionyeshaje kwamba hakutaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi? (b) Ni jambo gani linaloonyesha kwamba Kaini alijisikia ivyo hivyo?

5 Vilevile, je! kutokutaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi siyo sababu iliyomfanya Hawa ashindwe na ujanja-ujanja wa Shetani kisha akakosa kumtii Yehova Mungu? Shetani alimhakikishia kwamba kwa kula lile tunda lililokatazwa angekuwa kama Mungu, akiweza kujiamulia mwenyewe mema na mabaya. (Mwa. 3:5) Kutokutaka kwa Hawa kujiendesha kama mtu mdogo zaidi kulimletea msiba mkuu. Namna gani mwanawe mzaliwa wa kwanza? Je! si kweli kwamba Kaini alimwua Habili nduguye kwa sababu tu alishindwa kujiendesha kama mtu mdogo zaidi kuhusiana na nduguye? Kwa kumwona Habili akipendelewa, Kaini aliona uchungu mwingi kama wa nyongo. Nia hiyo ya akili yenye kiburi ilimfanya Kaini afukuziwe mbali akiwa ndiye mwuaji wa kwanza wa kibinadamu.​—Mwa. 4:1-16.

6. Kutokutaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi kulionyeshwaje na (a) ndugu-mzazi-mmoja za Yusufu? (b) Haruni na Miriamu? (c) Kora, Dathani na Abiramu?

6 Halafu tena walikuwako wale ndugu-mzazi-mmoja za Yusufu. Kwa sababu Yakobo baba yao alikuwa akimpendelea Yusufu zaidi—kwa sababu alikuwa ndiye mwana wa mkewe kipenzi, Raheli—wao walijawa na uadui mkali hata wakakosa amani mpaka walipomwondolea mbali. (Mwa. 37:3-35) Baadaye, wao pia walilazimika kujuta kwa sababu ya mwendo wao. Miaka mingi baadaye hata Miriamu na Haruni walikataa kutii wajiendeshe kama watu wadogo zaidi kuhusiana na Musa, ndugu yao mdogo. Walilalamika wakisema: “Je! ni kweli [Yehova] amenena na Musa tu? hakunena na sisi pia?” Lakini kama maandishi yanavyoendelea kuonyesha, Yehova Mungu alikuwa akisikiliza. Alichukizwa sana na nia yao ya akili, kwa maana aliwaambia hivi walalamikaji hao wawili: “Sikizeni basi maneno yangu; . . . mtumishi wangu, Musa . . . yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote [anakabidhiwa nyumba yangu yote, NW]; kwake nitanena [ninanena, NW] mdomo kwa mdomo . . . Mbona basi ninyi hamkuogopa kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?” Yehova Mungu alichukizwa sana hata akamchapa Miriamu kwa ukoma. Halafu walikuwako Kora, Dathani na Abiramu walioasi kwa uzito mwingi zaidi wakikataa kuliendesha kama watu wadogo zaidi kisha wakaharibiwa kwa sababu hiyo,—Hes. 12:1-15; 16:1-35; 26:9-11.

7, 8. (a) Ni wafalme gani wawili wa kale waliopatwa na huzuni nyingi kwa sababu hawakutaka kujiendesha kama watu wadogo zaidi? (b) Tuna mifano gani katika nyakati za ki-mitume?

7 Mtumishi mwingine wa Yehova Mungu aliyekuwa akitatizwa upande huu ni Mfalme Sauli. Yeye alikasirika vilivyo alipowasikia wanawake wa Israeli wakiimba: “Sauli amewaua elfu zake, na Daudi makumi elfu yake.” Jambo hilo lilimkasirisha sana Sauli hata kwamba kuanzia siku hiyo ‘akawa akimwonea Daudi wivu,’ hata kumtafuta-tafuta akijaribu kumwua kama vile mbwa afanyavyo mawindoni. Looo, maisha ya Sauli yaliingiwa na uchungu mwingi namna gani kwa sababu hakutaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi kuhusiana na Daudi katika jambo hilo! Naye akapata mwisho wenye msiba, wooo! (1 Sam. 18:7-9; 31:3-6) Halafu alikuwako Mfalme Uzia. Mafanikio yake ya kijeshi, ambayo kweli yalikuwa makubwa, yalimfanya awe na kiburi moyoni. Kwa hiyo, hakuwa tena na hekima ya kuridhika akiwa mfalme tu mwenye kufanya mambo ya serikali na kujiendesha kama mtu mdogo zaidi kuhusiana na mpango wa makuhani, basi akataka awe sawa na makuhani katika ibada ya hekaluni. Kwa sababu ya kimbelembele cha Uzia, Yehova Mungu alimchapa kwa ukoma. Akafa akiwa bado mwenye ukoma.​—2 Nya. 26:16-21; Mit. 11:2.

8 Tukija kwenye Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, tayari tumekwisha kuona tatizo walilokuwa nalo wale mitume 12 wakati Yesu alipokuwa angali nao, kukawa hakuna hata mmoja kati yao aliyetaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi. Walakini, na iangaliwe kwamba hatusomi jambo kama hilo kuwahusu walipokwisha kupokea roho takatifu ya Mungu kwenye Pentekoste. Lakini Wakristo wengine wa karne ya kwanza walikuwa na tatizo hilo. Inaonekana kwamba Wakristo huko Korintho, angaa wengine wao, hawakuridhika kujiendesha kama watu wadogo zaidi kuhusiana na mtume Paulo. Naye mtume Yohana aliona uhitaji mkubwa wa kumkemea Diotrefe vikali kwa sababu alitaka awe wa kwanza, naye hakuyaheshimu maneno ambayo mtume Yohana aliwaambia Wakristo zamani hizo.​—2 Kor. 10:1-11; 12:5-9; 3 Yohana 9, 10.

KWA SABABU GANI TATIZO HILO LIPO?

9. Chanzo halisi cha kutokutaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi ni nini?

9 Kwa sababu gani tatizo hili limekuwapo sana katika historia yote ya mwanadamu, likihusu si walimwengu peke yao, mataifa na watu mmoja mmoja bali hata watumishi wa Yehova Mungu? Ni kwa sababu ya uchoyo uliorithiwa. Ni kama vile tunavyosoma kwenye Mwanzo 8:21: “Mawazo [maelekeo, NW] ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake.” Kwa sababu hiyo, “moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?”​—Yer. 17:9.

10-12. Ni mifano gani inayoonyesha mahali hasa na sababu hasa tatizo hili hutokea?

10 Kwa ujumla, Mashahidi wa Yehova hawatatizwi sana kujiendesha kama watu wadogo zaidi kuhusiana na wale ambao ni wazi wana cheo kikubwa zaidi. Lakini tatizo hutokea inapokuwa habari ya kujiendesha kama watu wadogo zaidi kati ya wale walio na daraja moja nao, kati ya wale wanalingana nao kwa kiasi fulani. Kwa mfano, hakuna hata mmoja wa wale mitume 12 aliyetatizwa kujiendesha kama mtu mdogo zaidi kuhusiana na Bwana wake, Yesu Kristo. Lakini ilipokuwa habari ya kujilinganisha na ye yote wa wale mitume 11 wengine, hapo ndipo palipokuwa na mambo. Hakuna ye yote aliyetaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi kati ya wale wengine wote!

11 Vivyo hivyo leo, katika kundi la Kikristo huenda kukawa na mashindano madogo yenye ugomvi, au huenda ka-wivu kadogo ka kike kakaonekana, hasa kati ya wale ambao huenda wakawa wana vipawa vinavyolingana vya kufanya mambo au baraka fulani. Inaelekea hii ndiyo iliyokuwa hali kati ya wanawake wawili Wakristo katika kundi la huko Filipi, hata ikamfanya mtume Paulo aandike hivi: “Namsihi Euodia, namsihi na Sintike, wawe na nia moja katika Bwana. Naam, nataka na wewe pia, mjoli wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na . . . wale wengine waliotenda kazi pamoja nami.” (Flp. 4:2, 3) Inaelekea sana kwamba dada wawili hawa wote walikuwa wahubiri hodari na wenye juhudi wa “Injili” (habari njema), hata roho ya mashindano yenye ugomvi ikaingia mioyoni mwao, ikaleta kugombana.

12 Katika njia iyo hiyo, huenda kukawa na matatizo nyakati nyingine kati ya kina ndugu waliowekwa kwenye vyeo vinavyolingana. Katika tengenezo la Kikristo, kwa wingi watumishi wa huduma hawatatizwi kujiendesha kama watu wadogo zaidi kuhusiana na wazee; wazee hawatatizwi kuhusiana na mwangalizi wa mzunguko; waangalizi wa mizunguko hawatatizwi kuhusiana na waangalizi wa wilaya, na kadhalika. Lakini jaribu linakuja kuhusiana na watu wenye daraja moja, juu ya kama watumishi wa huduma watakuwa na nia ya kujiendesha kama watu wadogo zaidi kuhusiana na watumishi wa huduma wengine, wazee kuhusiana na wazee wengine katika kundi fulani, na kadhalika.

HEKIMA YA KIDUNIA, YA MNYAMA, YA KISHETANI

13-15. Kwa sababu gani mashindano yenye ugomvi na wivu yanaweza kuitwa (a) hekima ya kidunia? (b) hekima ya mnyama?

13 Kwa sababu wengi hawataki kujiendesha kama watu wadogo zaidi kwa sababu ya kutokukamilika kwa kibinadamu, mwanafunzi Yakobo aliona uhitaji mkubwa wa kuandika hivi: “Ikiwa mna wivu wenye uchungu na mashindano yenye ugomvi katika mioyo yenu, msiwe mkijigamba na kusema uongo juu ya ile kweli. Hii si ile hekima ambayo yaja chini kutoka juu, bali ni ile ya kidunia, ya mnyama, ya kishetani. Kwa maana mahali wivu na mashindano yenye ugomvi yalipo, hapo ukosefu wa utaratibu na kila jambo ovu lipo.”​—Yak. 3:14-16, NW.

14 Mwanafunzi Yakobo anasema haki kabisa anaponena kwamba wivu na mashindano yenye ugomvi ni ya kidunia, ya mnyama, ya kishetani? Hayo kweli ni ya kidunia, ya kimwili, alama yenye kuonyesha wanadamu wachoyo wasio na ukamilifu, nayo yanatofautiana na yale yanayotoka juu, ya kimbinguni. Roho iyo hiyo ni ya mnyama pia, kwa maana ndiyo alama yenye kuonyesha wanyama walivyo. Wanasayansi wenye kuchunguza tabia za wanyama katika mazingira yao ya asili wamegundua kati ya wanyama mbalimbali, kama ng’ombe na kuku, jambo linalojulikana kama “kawaida ya kudonoa wengine kwa mdomo,” ambapo wanajitanguliza mbele ya wenzao nyakati zote.

15 Kwa mfano, miaka kadha iliyopita magazeti ya habari za kila siku yalieleza juu ya mchezo uliofanywa na simba-milia (tiger) 12 kwenye sarakasi moja jijini New York. Baada ya mchezo huo kumalizika, simba-milia hao walikuwa wakielekea kwenye kijia cha kuwapeleka kwenye vyumba vyao wakati kwa ghafula simba-milia mwenye kuongoza, Rajah, alipolikaba koo la Ila, simba-milia wa kike. Kufikia wakati ambao watumishi wa sarakasi walifaulu kuwaamua wanyama wawili hao, simba-milia wa kike alikuwa amekwisha kupata jeraha la kifo. Mambo yaliharibikaje? Badala ya huyo wa kike kubaki mahali pake nyuma ya Raja, yeye kwa kimbelembele alijitanguliza mbele yake na kumkasirisha sana Rajah mpaka akamshambulia. Simba-milia huyo wa kike alipoteza maisha yake kwa sababu hakutaka kujiendesha kama mdogo zaidi.

MIFANO MYEMA YA MUSA, YESU NA PAULO

16. Musa aliweka mfano gani mwema wa kutaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi?

16 Mmoja wa watumishi wa kale wa Yehova aliyejiendesha kama mtu mdogo zaidi kwa njia yenye kutokeza alikuwa Musa. Yeye alitumiwa sana na Yehova Mungu: katika kumtolea Farao ushuhuda, katika kuyatokeza yale mapigo 10, katika kuigawanya ile Bahari Nyekundu na katika kuwapa watu wake maji kwa kutumia nguvu zisizo za kibinadamu! Lakini ajapopewa mapendeleo haya yote na umashuhuri wake, tunasoma kwamba “huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi.” Kwa sababu ya nia yake ya kujiendesha kama mtu mdogo zaidi, Yehova Mungu alimfanya mkubwa machoni pa ulimwengu, vilevile machoni pa watu wake mwenyewe.​—Hes. 12:3.

17-19. Ni jambo gani linaloonyesha kwamba Yesu alijiendesha kama mtu mdogo zaidi (a) kabla ya kuja duniani? (b) alipokuwa duniani? (c) tangu kufufuliwa kwake na kurudi mbinguni?

17 Na lo! Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, aliweka mfano mwema ulioje katika kujiendesha kama mtu mdogo zaidi! Tofauti na malaika aliyepata kuwa Shetani yule Ibilisi, yeye Neno, au Logos. “mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho.” Alitumikia kwa furaha kama “stadi wa kazi,” akishirikiana karibu-karibu na Baba yake katika kazi za uumbaji.​—Mit. 8:30; Yohana 1:1-3,14; 1 Kor. 11:3; Flp. 2:6-8.

18 Alipokuwa duniani, Yesu aliendelea kujiendesha kama mtu mdogo zaidi kuhusiana na Baba yake, akisema, “Baba ni mkuu kuliko mimi” na kwamba hakuna mtu mwema ila Mungu peke yake. (Luka 18:19; Yohana 14:28) Kwa kweli, Yesu alipokuwa duniani alijiendesha kama mtu mdogo zaidi kuhusiana na wanadamu wenzake, akichukua cheo cha mtumishi. Ni kama vile yeye mwenyewe alivyolieleza jambo hilo: “Kama vile Mwana wa watu asivyokuja kutumikiwa, lakini kutumikia, na kutoa uzima wake uwe ukombozi kwa watu wengi.” Hata alifanya kikazi kilicho cha cheo cha chini zaidi cha kuwaosha mitume wake miguu. Na lo! jinsi alivyotukuzwa sana kwa sababu ya unyenyekevu wake wa akili!—Mt. 20:28, Zaire Swahili Bible; Yohana 13:2-16; Flp. 2:9-11.

19 Tangu kufufuliwa kwake na kupaa kwenye mbingu, Kristo ameendelea kujiendesha kama mtu mdogo zaidi kuhusiana na Yehova Baba yake, akiwa na nia ya kungoja kwa subira mpaka Yehova awekapo adui zake kama kibago (kiti) cha kuwekea nyayo zake. Halafu, baada ya utawala wa Yesu wa mileani, Yehova atakapokuwa ameweka adui zake wote chini ya nyayo zake, “Mwana Mwenyewe atajitiisha mwenyewe pia kwa Huyo aliyetiisha vitu vyote kwake yeye, kwamba Mungu apate kuwa vitu vyote kwa kila mmoja.”​—Zab. 110:1; 1 Kor. 15:25-28, NW.

20, 21. (a) Mtume Paulo alijionyeshaje kuwa mwigaji mwema wa Yesu Kristo katika mambo haya? (b)  Makala ifuatayo itaonyesha nini wazi kwa faida yetu?

20 Kati ya wafuasi wa Kristo, mtume Paulo hasa alikuwa mwigaji mwema wa Yesu Kristo katika habari hii. Kwa ajili ya “Injili,” yeye akawa mtumwa wa wote. Kwa uhakika kufanya hivyo kulikuwa kujiendesha kama mtu mdogo zaidi. (1 Kor. 9:19) Alijiendesha kama mtu mdogo zaidi kuhusiana na baraza yenye kuongoza katika Yerusalemu, kuhusu utendaji wa huduma yake, juu ya mambo aliyopaswa kuhubiri, na katika mafundisho yake. (Matendo 15:2; Gal. 2:7-10) Wakati mmoja, alijiona na wajibu wa kuliuliza hivi kundi la Kikristo la huko Korintho: “Je! nalifanya dhambi kwa kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe?” Si ajabu kwamba Yehova Mungu aliibariki sana huduma ya Paulo!—2 Kor. 11:7.

21 Kama vile ambavyo tumeona, kwa kuwa kutokutaka kujiendesha kama mtu mdogo zaidi ni upumbavu, na kutaka kufanya hivyo ni uthibitisho wa kuwa na hekima, tutataka tuufuate mwendo huu wa hekima. Ili kufanya hivyo tutahitaji msaada kwa sababu ya makosa ya kutokukamilika tulikorithi. Makala ifuatayo itaonyesha wazi misaada ya kutuwezesha ”‏ tuipate hali hiyo ifaayo ya akili.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kisha “Haruni akamwangalia Miriamu, tazama, yu mwenye ukoma”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki