Je! Biblia Ilitabiri Mashindano ya Mamlaka Yaliyopo Sasa?
SIASA ZA KUSHINDANIA MAMLAKA zimekuwa zikiendelea ulimwenguni kwa maelfu ya miaka. Zilionekana zimefunikwa na mambo mengine wakati wa miaka ya mwisho-mwisho ya 1960 na miaka ya kuanza na wa 1970, wakati yenye kuelekea kuwa “mazingira mapya” katika uhusiano wa kimataifa (unaoitwa mazungumzo ya kuondoa wasiwasi) yalipofanya wengine waamini kwamba ugomvi ulio mkubwa kati ya Mashariki na Magharibi ulikuwa unapungua. Hata hivyo, matukio ya karibuni yameonyesha kwamba mashindano ya mamlaka si jambo lililokwisha kupita.
Kujiheshimu kwa Amerika kulipunguzwa sana wakati wa lile tukio la kuteka nyara Waamerika katika Iran, na jambo hilo likachochea kutokea tena kwa utukuzaji wa taifa katika United States. Kisha Ronald Reagan akachaguliwa kwa kura awe rais mpya wa Amerika. Moja la maongozi yake makuu limekuwa kusawazisha silaha za kijeshi ambazo Urusi imelundika kwa haraka sana. Hata kabla ya uchaguzi wa kirais wa Amerika, kiongozi wa Urusi Leonid Brezhnev alisema hivi kwa kusisitiza: “Hakuna shaka lo lote kwamba United States haitakuwa yenye nguvu zaidi za kijeshi kamwe.”
Upesi baada ya Bw. Reagan kuchaguliwa kwa kura awe rais alijibu kwa ukali, akasisitiza kwamba mazungumzo ya kuondoa wasiwasi yalikuwa yamekuwa “barabara yenye kuelekea upande mmoja” yenye kutumiwa na Urusi “kufuatia malengo yake tu.” Alisema maoni ya kwamba viongozi wa Urusi wangali wanakusudia kuleta “mapinduzi ulimwenguni” na iliripotiwa kuwa alisema kwamba “adili peke yake wanayoikubali ni jambo lile litakaloimarisha kusudi lao, kumaanisha wanajiwekea wao wenyewe haki ya kutenda uhalifu wo wote, kudanganya, kusema uongo ili watimize kusudi hilo.” Moscow ilijibu kwa kusema kwamba shambulio la Rais Reagan ni “tendo la werevu lisilofaa.” Likiripoti juu ya mashambuliano hayo ya maneno, gazeti la Ufaransa Le Monde lilisema kwamba namna ya usemaji uliotumiwa ni ya “Vita vya Maneno.”
HAKUNA KUPUNGUZA MASHINDANO YA SILAHA
Kulingana na Shirika la Mataifa Yote la Mafunzo ya Kivita, wakati wa miaka ya mwisho-mwisho ya 1970 Urusi ilitumia kati ya asilimia (%) 11 na 14 ya thamani ya mali zake kwa matumizi ya kijeshi, ikilinganishwa na asilimia 5 katika United States. Kwa hiyo Urusi sasa inazidi Amerika kwa silaha za kivita. Ina silaha zaidi za mizinga inayoweza kulengwa kutoka bara moja kufika bara nyingine (walakini haina silaha zaidi za visehemu vya mizinga vinavyolipuka), mizinga zaidi inayotupwa na manowari zinazopita chini ya maji (merikebu), manowari zinazopita chini ya maji zenye kuendeshwa kwa nguvu za nuklea na mafuta ya dizeli, merikebu kubwa zinazopita juu ya maji (walakini si zile zenye kubeba ndege wala ndege-kipanga), ndege za kivita na vifaru. Pamoja na hayo kufikia Desemba 1980 kulikuwako wanaume na wanawake 3,658,000 katika vikosi vya majeshi ya Urusi, ikilinganishwa na 2,050,000 katika vikosi vya Amerika.
Mamlaka mpya ya Bw. Reagan inakusudia kurekebisha hali hiyo. Katika ujumbe wake wa kwanza kwa jeshi la Amerika, Katibu wa Ulinzi Caspar Weinberger, alisema kwamba mgawo wake ulikuwa “kupatia tena Amerika silaha.” Ingawa imekadiriwa kwamba Urusi kwa sasa inatumia dola bilioni 165 kwa mwaka kwa ajili ya vikosi vya majeshi yake, United States inakusudia kuinua fedha za matumizi ya kijeshi toka dola bilioni 157.9 mwaka huu, kukiwa na maongezeko ya kawaida ya kila mwaka mpaka zifike dola bilioni 250 mwaka 1984.
Kwa sababu ya usemi wa Bw. Brezhnev kwamba “United States haitakuwa na nguvu zaidi za kijeshi kamwe,” inaonekana wazi kwamba Urusi pia itaongeza matumizi yake ya fedha za kijeshi. Pamoja na hayo, mataifa yenye kuunga mkono mataifa hayo mawili yenye nguvu nyingi sana za kijeshi (kama vile mataifa yaliyo washiriki wa Mkataba wa Tengenezo la Atlantiki Kaskazini [NATO] na yale yaliyofanya Mkataba wa Warsaw [mji wa huko Poland]) yatazamiwa kufanya vivyo hivyo. Bila shaka, basi, mashindano ya kulundika silaha yangali yanaendelea—ya kulipa kisasi!
KUSONGA MBELE KWA MAMLAKA ZA ULIMWENGU
Pande zote mbili katika mashindano ya mamlaka ya sasa tayari zina silaha za kutosha kuharibu jamii yote ya kibinadamu mara nyingi, kutia ndani wanaume na wanawake ambao wamejiweka wakf kwa Mungu Mwenye Nguvu Zote, Yehova. Kwa hiyo haishangazi kwamba Neno la Mungu, Biblia, linazungumza juu ya hali ya sasa. Na kwa uzuri zaidi, inaonyesha matokeo ni nini.
Kitabu cha Biblia cha Danieli (sura za 2 na 7) kinasimulia mfuatano wa mamlaka za ulimwengu zinazofananishwa na sehemu mbalimbali za mnyama mkubwa sana, na pia na wanyama wanne. Wao wanafananisha Mamlaka za Ulimwengu za Babeli, Umedi-Uajemi, Ugiriki na Rumi. Rumi ikiwa inaendelea mpaka mwishowe inatokeza Mamlaka ya Ulimwengu ya Waingereza na Waamerika.a
Katika sura ya 11, unabii wa Danieli unaonyesha kushindania mamlaka ya ulimwengu kati ya “wafalme” wawili wa mfano. Wao ni “mfalme wa kaskazini” na “mfalme wa kusini,” na mng’ang’ano huo wa kutawala ulimwengu unafikia upeo “wakati wa mwisho.” (Mst. 40) “Wafalme” hao wanafananisha nani? Matokeo ya kushindana kwao yatakuwa nini? Tutachunguza maulizo hayo katika makala inayofuata.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa maelezo marefu ya unabii huo mbalimbali tafadhali tazama Mnara wa Mlinzi wa Oktoba 15 1981, kurasa 12-18, na kurasa 92-98 za kitabu Our Incoming World Government—God’s Kingdom, kilichochapishwa mwaka 1977.