Kuhifadi Uhai Katika Wakati wa Njaa
1. Ni kitendo gani chenye hekima alichofanya Yusufu wakati wa miaka ile ya utele, na tokeo likawa nini?
MARA tu baada ya kuwekwa kwake rasmi awe Msimamizi wa chakula, Yusufu alitalii nchi ya Misri. Aliagiza mambo yatengenezwe vizuri kufikia wakati miaka ya utele ilianza. Sasa nchi ilizaa mazao tele! Yusufu aliendelea kukusanya vyakula kutoka shamba lililouzunguka kila mji, akiviweka akibani katika mji. Aliendeiea ‘kukusanya nafaka kama mchanga wa pwani, nyingi mno, hata akaacha kuihesabu, maana ilikuwa haina hesabu.’—Mwanzo 41:46-49.
2. Ni kwa kufanya dhabihu gani ya kibinafsi watu waliweza kupata riziki?
2 Miaka ile saba ya utele ikaisha, na njaa ikaanza sawa na vile Yehova alivyokuwa ametabiri—njaa, si katika Misri tu, bali “juu ya uso wa dunia.” Wakati watu wenye kuku-mbwa na njaa katika Misri walipoanza kumlilia Farao awape mkate, Farao aliwaambia: “Nendeni kwa Yusufu. Lo lote awaambialo yeye, ndilo mtakalopasa kufanywa.” Yusufu aliuzia Wamisri nafaka mpaka pesa zao zikamalizika kabisa. Ndipo alipokubali mifugo yao iwe malipo. Mwisho, watu wakamjia Yusufu, wakisema: “Tununue sisi na nchi yetu kwa ajili ya mkate, nasi pamoja na nchi yetu tutakuwa watumwa kwa Farao.” Kwa hiyo Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Wamisri.—Mwanzo 41:53-57; 47:13-20, NW.
Uandalizi kwa Ajili ya Ulishaji wa Kiroho
3. Ni chombo gani ambacho Yesu alitabiri cha kuandalia chakula katika wakati unaofaa?
3 Sawa na vile nafaka iliyogawanywa na Yusufu ilivyomaanisha uzima kwa Wamisri, ndivyo chakula cha kiroho cha kweli kilivyo cha maana kabisa ili kuendeleza Wakristo wanaokuwa watumwa wa Yehova kwa kujiweka wakfu Kwake kupitia Yusufu Mkubwa Zaidi, Yesu Kristo. Wakati wa huduma yake ya kidunia, Yesu alitabiri kwamba wafuasi wa hatua zake waliopakwa mafuta wangelichukua daraka la kuwatolea watu maandalizi hayo. Yeye aliuliza hivi: “Ni nani mtumwa mwaminifu na mwenye akili ambaye bwana yake aliweka juu ya watu wa nyumba yake, kuwapa chakula kwa wakati unaofaa? Mwenye furaha ni mtumwa huyo ikiwa bwana yake anapofika anamkuta akifanya hivyo.”—Mathayo 24:45, 46, NW.
4. Uandalizi uanofanywa na jamii ya “mtumwa” leo unalinganaje na ule uliotengenezwa katika siku za Yusufu?
4 Mabaki yenye uaminifu ya jamii ya “mtumwa mwenye akili” huyo wanajitahidi Ki-maandiko vyo vyote wawezavyo wahakikishe kwamba Mashahidi walio wakfu wa Yehova, na pia watu wenye kupendeza walioko nje ulimwenguni, wanapokea chakula cha kiroho kinachoendeleza uhai. Amana hiyo inatambuliwa kuwa wajibu mtakatifu na inafanywa kama utumishi mtakatifu kwa Yehova. Tena, “mtumwa” huyo ametengeneza makundi na akayatolea vitabu vya Kibiblia kwa wingi hivi kwamba yana “mbegu” ya kutosha, ya Ufalme ya kutawanya peupe katika mashamba waliyogawiwa. Jambo hilo linalingana na siku za Yusufu, wakati yeye alipowakusanya watu ndani ya miji na kuwaandalia nafaka si kwa ajili ya kujiendeleza wenyewe tu bali pia kwa ajili ya kupanda wakifikiria mavuno ya baadaye.—Mwanzo 47:21-25; Marko 4:14, 20; Mathayo 28:19, 20.
5. (a) Ni fikira gani za pekee ambazo “mtumwa” anaelekeza kwa mahitaji ya watu wa nyumba katika wakati wa shida kubwa? (b) “Mfuriko” wa maandalizi ya kiroho katika 1986 unalingana kwa kadiri gani na yaliyotolewa kule nyuma katika wakati wa Yusufu?
5 Hata wakati kazi ya kuhubiri peupe inapokuwa chini ya marufuku na Mashahidi wa Yehova wanateswa, ‘mtumwa mwaminifu’ anauona uandaaji huo wa chakula cha kiroho kuwa amana takatifu. (Matendo 5:29, 41, 42; 14:19-22) Wakati maafa yanapokumba, kama vile dhoruba, gharika, na matetemeko ya dunia, “mtumwa” anahakikisha kwamba mahitaji ya kimwili na kiroho pia ya watu wa nyumba ya Mungu yanatolewa. Hata wale walio katika kambi za mateso wamefikiwa kwa ukawaida na neno lililopigwa chapa. Mipaka ya taifa hairuhusiwi ikomeshe mtiririko wa chakula cha kiroho kwa wale wanaokihitaji. Kuendelea kutoa chakula hicho bila kuchelewa kunataka ushujaa, imani katika Yehova, na mara nyingi kutumia akili nyingi. Ulimwenguni pote wakati wa 1986 tu, “mtumwa” alitokeza mfuriko wa Biblia na vitabu vyenye majalada magumu 43,958,303, na pia magazeti 550,216,455—kweli kweli kiasi kilicho ‘kingi mno kama mchanga wa pwani.’
Kulipa Kisasi, Adhabu, au Rehema?
6, 7. (a) Njaa ilikujaje kuwa na tokeo la kufanya ndugu-nusu kumi wajiinamishe kifudifudi mbele ya Yusufu? (b) Ni katika njia gani mbalimbali Yusufu mwenyewe sasa akawa jaribuni?
6 Hatimaye njaa ikaja kwenye nchi ya Kanaani. Yakobo akawatuma ndugu-nusu kumi za Yusufu washuke kwenda Misri kununua nafaka. Lakini yeye hakutuma Benyamini, aliyekuwa ndiye ndugu wa pekee kamili wa Yusufu, kwa kuogopa kwamba, kama yeye alivyosema: “Mabaya yasimpate.” Kwa kuwa Yusufu ndiye aliyefanya uuzaji, ndugu zake walimjia yeye na wakajiinamisha kifudifudi mbele yake. Ingawa hawakumtambua ndugu yao, Yusufu aliwajua wao.—Mwanzo 42:1-7.
7 Sasa Yusufu akakumbuka ndoto zake za kwanza-kwanza kuwahusu wao. Lakini angefanya nini? Je! alipe kisasi? Katika wakati wao wa uhitaji mkubwa, je! yeye asamehe utendaji aliokuwa amepokea mikononi mwao? Namna gani juu ya kihoro cha baba yake chenye maumivu makali sana? Je! hicho kisahauliwe? Sasa ndugu zake walihisi namna gani juu ya kosa kubwa walilokuwa wametenda? Yusufu, pia, alikuwa jaribuni katika jambo hili. Je! vitendo vyake vingepatana na mwelekeo ambao Yusufu Mkubwa Zaidi, Yesu Kristo, angeonyesha baadaye, kama inavyoelezwa kwenye 1 Petro 2:22, 23, NW: “Yeye hakufanya dhambi, wala udanganyifu haukupatikana katika kinywa chake. Alipokuwa akitukanwa yeye hakurudisha kutukana. Alipokuwa akiteswa, yeye hakutisha, bali aliendelea kujikabidhi mwenyewe kwa yeye anayehukumu kwa uadilifu.”
8. Yusufu angeongozwa na nini, likionyesha nini kwa habari ya Yesu na wanafunzi Wake?
8 Kwa kuwa Yusufu angeweza kuona mkono wa Yehova katika kutendeka hatua-hatua kwa matukio hayo, angekuwa mwangalifu kuzishika sheria na kanuni za Mungu. Katika njia iyo hiyo, sikuzote Yesu alikuwa na shauku nyingi ya ‘kuyafanya mapenzi ya Baba yake’ alipokuwa akitoa uzima wa milele kwa ‘kila mtu anayejizoeza imani katika yeye.’ (Yohana 6:37-40, NW) Kama “mabalozi badala ya Kristo,” wanafunzi wake wapakwa-mafuta wanatimiza pia amana takatifu yao katika ‘kuwaambia watu maneno yote ya Uzima huu.’—2 Wakorintho 5:20, NW; Matendo 5:20, UV.
9, 10. (a) Sasa ni mwendo gani aliouchukua Yusufu, na kwa sababu gani? (b) Yusufu alionyeshaje huruma inayolingana na ile ambayo Yesu angeonyesha?
9 Yusufu hakujifunua mwenyewe kwa ndugu zake papo hapo. Badala ya hivyo, alisema nao kwa ukali kupitia mfasiri, akisema: “Wapelelezi ninyi”! Kwa kuwa walikuwa wametaja ndugu mwenye umri mdogo zaidi, Yusufu alidai kwamba wathibitishe ukweli wao kwa kumshusha huyo Misri. Yusufu aliwasikia kwa mbali wakiambiana kwa kutubu kwamba badiliko hili la matukio lazima liwe lilitokea kulipia tendo lao la kumwuza yeye, Yusufu, katika utumwa. Akigeukia kando, Yusufu akalia machozi. Hata hivyo, aliagiza Simeoni ashikwe mateka mpaka warudi wakiwa pamoja na Benyamini.—Mwanzo 42:9-24.
10 Yusufu hakuwa akilipa kisasi kwa kosa alilotendwa. Yeye alitaka kujua kama toba yao ilikuwa ya kweli, yenye kutoka katika vina vya mioyo yao, ili waweze kuonyeshwa rehema. (Malaki 3:7; Yakobo 4:8) Akiwa na mwelekeo wenye huruma, unaolingana na ule ambao Yesu angeonyesha, si kwamba Yusufu alijaza magunia yao nafaka bali pia aliwaru-dishia pesa zao katika kinywa cha gunia la kila mmoja. Kuongezea hilo, aliwapa maandalizi kwa ajili ya safari yao.—Mwanzo 42:25-35; linganisha Mathayo 11:28-30.
11. (a) Baada ya muda fulani, Yakobo alilazimika kufanya nini, na kwa sababu gani mwishowe akakubali? (b) Maandiko ya Warumi 8:32 na 1 Yohana 4:10 yanatuhakikishiaje vilevile upendo wa Mungu?
11 Baada ya muda fulani, wakamaliza chakula walichokuwa wamenunua Misri. Yakobo akawaomba wana hao tisa warudi wakanunue zaidi. Hapo kwanza, alikuwa amesihi sana kwa habari ya Benyamini, akisema: “Mwanangu hatashuka pamoja nanyi wanaume, kwa sababu ndugu yake amekufa na yeye ameachwa akiwa peke yake mwenyewe. Kama tukio lisilotazamiwa la kifo lingemwangukia katika njia ambayo ninyi mngeendea, ndipo ninyi kwa uhakika mngeshusha mvi zangu kwa kihoro mpaka Sheoli.” Hata hivyo, baada ya usadikishi mwingi na kujitolea kwa Yuda awe mwenye daraka kwa yatakayompata Benyamini, Yakobo anakubali kwa kusita-sita kuwaruhusu waende na mvulana yule.—Mwanzo 42:36–43:14, NW.
12, 13. (a) Yusufu aliwekaje mchunguzo wa kufunua mwelekeo wa moyoni wa ndugu zake? (b) Tokeo la mchunguzo huo lilimpaje Yusufu msingi wa kuonyesha rehema?
12 Yusufu alipoona kwamba Benyamini alikuwa amekuja pamoja na ndugu wale, aliwaalika kwenye nyumba yake, ambako alitandaza karamu. Alimwandalia Benyamini kisehemu kilicho mara tano ya kisehemu alichoandalia kila mmoja wa wengine. Ndipo Yusufu akafanya mchunguzo wa mwisho juu ya ndugu zake. Tena, akarudisha pesa zao zote katika magunia yao moja moja, lakini kikombe chake cha pekee cha fedha kikawekwa katika kinywa cha gunia la Benyamini. Baada ya kuondoka kwao, Yusufu alimtuma msimamizi wa nyumba yake akawashtaki juu ya wivi na kupekua-pekua magunia yao akitafuta kikombe chake. Kilipopatikana katika gunia la Benyamini, ndugu wale waliyararua majoho yao. Walirudishwa wakaelekeane uso kwa uso na Yusufu. Yuda aliomba rehema kwa hisia nyingi za moyoni, akajitolea awe mtumwa mahali pa Benyamini ili mvulana huyo aweze kurudishwa kwa baba yake.—Mwanzo 43:15–44:34.
13 Akiwa sasa amesadikishwa juu ya badiliko la moyoni la ndugu zake, Yusufu hangeweza tena kuzuia maoni yake ya moyoni. Baada ya kuagiza kila mtu mwingineye yote atoke mbele yake, Yusufu akatangaza: “Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi, sasa msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha za watu. . . . Kuwahifadhia masazo katika nchi na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu.” Ndipo akawaambia ndugu zake: “Fanyeni haraka, mmwendee baba yangu, mkamwambie, . . . Unishukie, usikawie. Nawe utakaa katika nchi ya Gosheni, . . . Nami nitakulisha huko; maana bado imesalia miaka mitano ya njaa; usije ukaingia katika uhitaji, wewe, na nyumba yako, na yote uliyo nayo.”—Mwanzo 45:4-15.
14. Ni habari gani za furaha alizopelekewa Yakobo?
14 Farao alipozisikia habari juu ya ndugu za Yusufu, aliambia Yusufu aagize magari-mi-kokoteni yachukuliwe kutoka nchi ya Misri kuleta baba yake na jamaa yake yote Misri kwa sababu wao wangepata sehemu iliyo bora zaidi ya nchi. Aliposikia yote yaliyokuwa ya-metukia, Yakobo alirudiwa na nguvu katika roho yake na akapaaza sauti hivi: “Yatosha! Yusufu mwanangu angali hai; nitakwenda, nionane naye kabla sijafa”!—Mwanzo 45:16-28.
Chakula cha Kiroho Ni Tele
15. Sasa sisi tunategemea nani kwa riziki ya kiroho, nasi tunaweza kuhakikishiwaje kupata wingi?
15 Yote haya yanamaanisha nini kwetu leo? Tukiwa daima wenye kuujua uhitaji wetu wa kiroho, sisi tunategemea Mmoja aliye mku-bwa kuliko Farao mwenye fadhili wa wakati wa Yusufu. Ni Bwana Mwenye Enzi Kuu, Yehova, anayeandaa riziki na mwongozo kupitia siku hizi zenye giza za ulimwengu wenye njaa kubwa ya ukweli wa Biblia. Sisi tumejitahidi sana katika mapendezi ya Ufalme wake, kama kwamba ni kuleta zaka zetu zote ndani ya nyumba ya akiba yake. Yeye ametufungulia kwa ukarimu kama nini “malango ya gharika ya mbingu,” akimimina baraka “mpaka hakuna tena ukosefu”!—Malaki 3:10, NW.
16. (a) Ni wapi tu “chakula” cha kuhifadhi uhai kinapopatikana leo? (b) Kupanda “nafaka” kwa ajili ya wanadamu waliotaabishwa sana kwa njaa kumepanuliwaje?
16 Kwenye mkono wa kuume wa Yehova yuko Msimamizi wa Chakula wake, akiwa Mfalme aliyetawazwa, Yesu mtukuzwa. (Matendo 2:34-36) Kama vile ilivyowalazimu watu kujiuza wenyewe wawe watumwa ili waendelee kuwa hai, ndivyo ilivyo lazima leo wote wanaotaka kuendelea kuishi wamjie Yesu, wawe wafuasi wake waliojiweka wakfu kwa Mungu. (Luka 9:23, 24) Kama vile Yakobo alivyowaelekeza wana wake wamwendee Yusufu wakapate chakula, ndivyo Yehova anavyowatolea mwongozo wanadamu wenye kutubu wamwendee Mwana wake mpendwa, Yesu Kristo. (Yohana 6:44, 48-51) Yesu ana-wakusanya wafuasi wake ndani ya makundi yaliyo kama miji—zaidi ya 52,000 katika se-hemu zote za ulimwengu leo—ambamo wana-lishwa kutokana na wingi wa chakula cha kiroho na kutolewa mfuriko wa “nafaka”, kama “mbegu” ya kupanda shambani. (Mwanzo 47:23, 24; Mathayo 13:4-9, 18-23) Mashahidi hao wa Yehova ni wafanya kazi wenye nia kweli kweli! Wengi zaidi na zaidi kati yao wanajitolea kwa utumishi wa painia wa wakati wote, na wengi kufikia 595,896 kati yao walishiriki, wakiwa kilele, katika kazi hiyo iliyopendelewa katika mwezi mmoja mwaka jana. Huo unakuwa wastani wa mapainia zaidi ya 11 katika kila kundi!
17. Ni usimulizi gani mwingine wa kiunabii ulio na ufanani fulani na kuungana kwa ndugu-nusu kumi pamoja na Yusufu?
17 Inastahili kuangaliwa kwamba wote kati ya ndugu-nusu kumi za Yusufu, ambao sasa walikuwa wametubia mielekeo na vitendo vyao vya kwanza, waliungana pamoja naye kule chini Misri, nchi ambayo pamoja na Sodoma, ni kifananishi cha ulimwengu ambamo Yesu alitundikwa. (Ufunuo 11:8) Jambo hilo linatukumbusha juu ya Zekaria 8:20-23, andiko ambalo linafikia upeo kwa elezo juu ya “watu kumi” wanaosema, “Tutakwenda pamoja nanyi,” yaani, pamoja na wapakwa-mafuta wa Yehova, ambao baki lao lingali likitumikia hapa duniani.
18. Upendeleo ule wa pekee alioonyeshwa Benyamini unafanana na nini katika nyakati za kisasa?
18 Hata hivyo, namna gani juu ya ndugu-kamili mmoja wa Yusufu, Benyamini, amba-ye uzaliwa wake mgumu uligharimu uhai wa Raheli mke mpendwa wa Yakobo? Benyamini alipendelewa kwa njia ya pekee na Yusufu, ambaye bila shaka alihisi uhusiano wa kindani ulio wa karibu zaidi pamoja na mwana huyo wa mama yake mwenyewe. Bila shaka jambo hilo ndilo lililofanya Benyamini apokee kisehemu kilicho mara tano wakati ndugu wote 12 walipoungana tena kwa mara ya kwanza kwenye karamu katika nyumba ya Yusufu. Je! Benyamini hafananishi vizuri mabaki ya Mashahidi wapakwa-mafuta leo, kwa maana walio wengi kati ya wale ambao wangali hai wamekwisha kukusanywa upande wa Bwana tangu 1919? Jamii hiyo ya “Benyamini” imepokea kweli kweli kisehemu cha pekee kutoka kwa Yehova, maadamu ‘roho yake inatoa ushuhuda pamoja na roho yao.’ (Warumi 8:16, NW) Hao, pia, wamechunguzwa juu ya kama wana ukamilifu huku “kondoo” za Bwana wakiwahudu-mia wao.—Mathayo 25:34-40.
19. Ni ulinganifu gani unaoonwa kati ya kuhama kwa watu na vitu vya Israeli kwenda Gosheni na kukusanywa kwa watu wa Mungu leo?
19 Inapendeza kuangalia kwamba, wakati Farao alipopanga kusafirisha Yakobo na watu na vitu vya nyumbani mwake kwenda Misri, vichwa vya jamaa vya Israeli waliofunga safari hiyo walikuwa 70, hicho kikiwa ni kizidisho cha 7 na 10. Namba mbili hizo zinatumi-wa kwa njia yenye maana katika sehemu zote za Maandiko, mara nyingi “7” ikionyesha ukamili wa kimbingu na “10” wa kidunia. (Ufunuo 1:4, 12, 16; 2:10; 17:12) Jambo hilo linalingana na hali ya leo, wakati ambao sisi tunaweza kutazamia kwamba Yehova atamkusanya kila mtu wa jamaa yake ya Mashahidi aingie ndani ya “nchi” yake, paradiso ya kiroho ambamo tunafurahi sana sasa. (Linganisha Waefeso 1:10.) “[Yehova] awajua walio wake,” na hata sasa anawaleta watulie katika “sehemu iliyo bora zaidi ya nchi,” kama ilivyokuwa Gosheni kule nyuma katika milki ya Farao.—Mwanzo 47:5, 6, NW; 2 Timotheo 2:19, NW.
20. Kujapokuwa na njaa ya kiroho leo, kwa sababu gani ni lazima sisi tufurahi sana?
20 Katika siku za Yusufu, miaka ile ya njaa iliifuata miaka ya utele. Leo, vipindi hivyo viwili vya miaka vinaendelea pamoja kwa wakati mmoja. Tofauti na njaa ya kiroho katika nchi iliyo nje ya pendeleo la Yehova, kuna wingi wa chakula cha kiroho katika mahali pa ibada pa Yehova. (Isaya 25:6-9; Ufunuo 7:16, 17) Ndiyo, ijapokuwa kuna njaa ya kuyasikia maneno ya Yehova katika Jumuiya ya Wakristo, kama Amosi alivyotabiri, neno la Yehova linachomoza kutoka Yerusalemu wa kimbingu. Lo! jambo hilo linatufurahisha kama nini!—Amosi 8:11; Isaya 2:2, 3; 65:17, 18.
21. (a) Ni pendeleo gani kubwa tunalofurahia leo? (b) Inatupasa tushukuru kwa jambo gani, nasi tunaweza kuonyesha asante zetu jinsi gani?
21 Leo, chini ya mwelekezo wa Yusufu Mkubwa Zaidi, Yesu Kristo, sisi tuna pendeleo kubwa la kukusanywa tuingie ndani ya makundi yaliyo kama miji. Humo tunaweza kula karamu ya wingi wa chakula cha kiroho na pia kupanda mbegu za ukweli na kuzieneza habari njema za kwamba chakula cha kiroho kinapatikana. Tunafanya hivyo kwa manufaa ya wote wanaoyakubali masharti na maandalizi yaliyopangwa kwa upendo na Mtawala Mwenye Enzi Kuu, Yehova. Tunaweza kuwa wenye shukrani kama nini kwa Mungu wetu kwa ajili ya zawadi ya Mwana wake, Yusufu Mkubwa Zaidi, anayetumikia akiwa Msimamizi wa chakula cha kiroho mwenye hekima! Yeye ndiye amekabidhiwa na Yehova kutenda akiwa Mhifadhi uhai katika wakati huu wa njaa ya kiroho. Kila mmoja wetu na aonyeshe bidii katika kutoa utumishi mtakatifu kwa kufuata mfano wake na akiwa chini ya uongozi wake!
◻ Yusufu alifananaje na Yesu akiwa Msimamizi wa Chakula?
◻ Ni jambo gani katika mwigizo wa Yusufu linalolingana na kuwa watumwa kwa Mungu kupitia wakfu?
◻ Ni sifa gani inayoonyeshwa na Yusufu na Yesu kama mfano kwetu sisi leo?
◻ Kama ilivyokuwa katika wakati wa Yusufu, ni mpango gani kamili-kamili kwa ajili ya ugawaji chakula uliopo leo?
◻ Kufikiria kwetu mwigizo huo kunapasa kutusukume sisi kufanya nini?
[Maswali ya Funzo]
[Picha katika ukurasa wa 16 na 17]
Katika ulimwengu uliozungukwa na njaa ya kiroho, Yusufu Mkubwa Zaidi anawaandalia kwa utele wale wanaomjia yeye katika imani
Kama vile ndugu-nusu kumi walivyojiweka chini ya Yusufu, sasa mkutano mkubwa unamkubali Kristo
Kama ilivyokuwa kwa habari ya nafsi zile 70 za watu wa nyumba ya Yakobo, ndivyo hesabu kamili ya kondoo za Yehova watakavyofika katika “nchi” njema—urithi wao katika mfumo mpya wa Mungu
[Picha katika ukurasa wa 18]
Jamii ya kisasa ya Benyamini imependelewa kwa njia ya pekee na Kristo, ikipokea wingi wa “chakula kwa wakati unaofaa”