Dini na Ushirikina Ni Marafiki au Ni Maadui?
ILIKUWA Jumamosi, Juni 11, 1983. Wanakijiji katika kisiwa cha Kiindonesia cha Java waliweza kuonekana wakiharakisha kwenda kwenya nyumba zao, wakiziba kiwazimu nyufa zote kwenye madari, madirisha, na milango. Sababu gani woga huo wa ghafula? Kupatwa kwa jua kulikuwa kumeanza nao wanakijiji waliogopa kwamba kivuli cha kupatwa huko kwa jua kingeweza kuingia nyumba zao na kusababisha balaa.
Wakazi wa zile zinazoitwa eti nchi za ulimwengu wenye kuendelea mara nyingi wanafuata itikadi kama hizo kwa bidii ya kidini. Hivyo, katika sehemu fulani za Afrika, watu wanaepuka kutembea katika jua wakati wa adhuhuri kwa sababu wao “huenda wakawa na kichaa.” Watoto wanakatazwa kula mayai kwa kuogopa “wao watakuwa wezi.” Wazazi hawatasema hesabu kamili ya watoto wao, kwa kuwa “wachawi huenda wakakusikia ukijivuna na kuchukua mmoja wao.”—African Primal Religions.
Watu wa Magharibi wanaelekea kuchekelea mazoea kama hayo kuwa wonyesho wa woga wa kiushirikina, lile zao la ‘kutojua kwa kipagani.’ Hata hivyo, itikadi kama hizo haziwekewi mipaka kwa wasio Wakristo. Hizo “zinapatikana miongoni mwa watu kote kote ulimwenguni,” asema Dakt. Wayland Hand, profesa wa itikadi za kimapokeo na lugha za Kijeremani. Yeye na mwenzake Dakt. Tally tayari wamekusanya mifano karibu milioni moja ya maushirikina katika United States pekee.
Wakitamani sana kujua yatakayowapata, wengi wanaoitwa eti Wakristo, wanategemea unajimu—mojapo namna zilizo za kale zaidi sana za ushirikina. Na kwa kushangaza, itikadi za kiushirikina nyakati nyingine hupokea tegemezo la wazi na kuungwa mkono na viongozi wa kidini. Mathalani, katika siku moja yenye baridi katika New York, Januari 10, 1982, Vasilios askofu mkuu wa Orthodoksi ya Kigiriki ya Mashariki alisimamia Misa iliyofanyiwa mahali peupe kuadhimisha Sherehe ya Epifani. Baada ya hilo, linaripoti New York Post, yeye alivurumisha msalaba wa dhahabu ndani ya East River na akaambia waliokuwapo kwamba yule mtu wa kwanza kupata na kurudisha msalaba huo angepata bahati njema kwa muda wote unaobaki wa maisha yake.
Lakini je! itikadi za Kikristo na ushirikina zinafaana? Mwandikaji mmoja alionelea hivi wakati mmoja: “Kwenye kaburi la imani linasitawi ua la ushirikina.” Kwa hiyo, je! wewe hungetazamia dini ya Kikristo ipinge na kufukuzia mbali woga wa kiushirikina?
Dini—Je! Inafukuzia Mbali Woga wa Kiushirikina?
Dini ya kweli yapasa kufanya hivyo, na katika karne ya kwanza ilifanya hivyo. Ijapokuwa Wakristo wa mapema walikuwa wakiishi kati ya ulimwengu wa Kiroma wenye ushirikina, wao walikataa maushirikina. Lakini baada ya kifo cha mitume wa Kristo, mafundisho ya kidini yasiyo ya kweli, kutia na ushirikina, yalianza kupenya polepole ndani ya lile kundi. (1 Timotheo 4:1, 7; Matendo 20:30) Jamii ya viongozi wa kidini ilianza kutokea ambayo, kulingana na kitabu A History of the Christian Church, walifuatana na lile zoea la kutumia matabiri ya nyota na kufuata maushirikina mengineyo. Baada ya wakati mazoea kama hayo yenye kupendwa na wengi yalibandikwa jina ‘Ukristo.’
Namna gani leo? Dini ingali inavumilia desturi za kiushirikina. Ebu fikiria Suriname, ambako wanaoitwa eti Wakristo wa asili ya Kiafrika wanaweza mara nyingi kuonekana wakivalia hirizi ziwe ile inayodhaniwa kuwa himaya dhidi ya roho waovu. Anasema hivi mwelezaji mmoja: “Kila siku watu hawa wanaishi, kula, kufanya kazi na kulala katika hofu kuu.” Mamilioni ulimwenguni kote wana woga kama huo wa “roho” za wafu. Na ukweli ulio kinyume cha mambo, dini mara nyingi imeendeleza itikadi kama hizo za kiushirikina.
Chukua kama mfano jambo lililotukia katika kisiwa cha Kiafrika cha Madagaska. Wakati wamisionari wa Jumuiya ya Wakristo walipoanza kueneza itikadi zao, Wamadagaska walikuwa waitikifu lakini wasikubali kuacha itikadi zao za kimapokeo. Itikio la makanisa lilikuwa nini? Yasema Daily Nation, karatasi yenye habari kutoka Kenya: “Wale wamisionari wa mapema walikuwa wavumilivu na wenye kubadilikana na walikuja kukubali hali hii.” Tokeo? Leo nusu ya watu wa Madagaska wameorodheshwa kuwa Wakristo. Hata hivyo, wao pia wanaogopa zile “roho” za mababu wafu! Hivyo, wao kwa kawaida hualika kasisi au pasta abariki mifupa ya babu kabla haijarudishwa katika kaburi la kuchongwa la jamaa. Ndiyo, viongozi wa kidini wameendeleza ule uwongo wa kwamba Mungu, Ibilisi, na mababu wafu wanaweza kushawishwa kwa ubembelezi, kwa kuwasifu-sifu mno na kuhongwa kwa kushika mazoea ya kiushirikina.
Ndivyo ilivyo katika Afrika Kusini, ambako asilimia 77 ya idadi ya watu hudai kuwa Wakristo na hadhirina kanisani iko juu. Hata hivyo, dini ya Kiafrika ya kimapokeo, ikiwa na ule woga wayo wa kiushirikina wa mababu wafu, imekaa-kaa miongoni mwa mamilioni ya hao waenda-kanisani. Hivyo, katika nchi nyingi zinazoitwa eti za Kikristo, dini ni kibandiko tu. Kwaruza-kwaruza juu, nayo yale maushirikina ya kale yanaweza kuonekana kuwa yalisalimika na kusitawi.
Dini ya kweli, hata hivyo, inafukuzia mbali woga wa kiushirikina. Jinsi gani? Ule ufunguo ni maarifa. Maarifa ya nini? Na wewe unaweza kuyapataje?