Ni Jinsi Gani Makutano Yalivyomsikia Yesu?
GOSPELI ya Mathayo inaripoti kwamba katika pindi moja Yesu Kristo “alienda juu ya mashua na kuketi chini, na kutano lote lilikuwa limesimama juu ya ufuo. Ndipo yeye akawaambia mambo mengi kwa vielezi.” (Mathayo 13:1-35; Marko 4:1-9, NW) Katika kitabu chao Come See the Place: The Holy Land Jesus Knew, Robert J. Bull na B. Cobbey Crisler wanatokeza maswali fulani ya kupendeza kuhusu usimulizi huu. Wao wanauliza hivi: “Ni jinsi gani mtu angaliweza kusikiwa na ‘umati mkubwa’ bila kutumia namna fulani ya kikuza-sauti? Na je! inawezekana kupata mahali fulani ufuoni mwa bahari palipo na hali za mazingira yenye kukuza sauti, ambazo zingetokeza mkuzo kama huo?” Labda wewe pia umeshangaa ukitaka kujua jambo hili.
Basi, angalia jibu lao: “Miongoni mwa vihori kadhaa vya maji karibu na Kapernaumu, kuna kimoja ambacho hivi karibuni kimepatikana kuwa ni mahali pa kiasili penye hali hizo hizo za kupaaza sauti kama katika jumba kuu la mawonyesho. Michunguzo ya kama mahali hapo pana hali za mazingira yenye kukuza sauti imefanywa ikaonyesha kwamba ‘umati mkubwa’ wa watu wapatao elfu tano mpaka elfu saba, waliokusanyika hapa, wangaliweza kweli kuwa waliona na kusikia waziwazi mtu fulani mwenye kunena akiwa kwenye mashua iliyowekwa mahali fulani karibu na katikati ya kihori cha maji.” Na majaribio haya ya hali za mazingira yenye kukuza sauti yalifanywa jinsi gani? Virginia Bortin, mwandikaji mmoja kuhusu habari za uchimbuzi wa vitu vya kale, anaeleza katika The San Juan Star, karatasi-habari moja katika Puerto Riko.
Kulingana na Bortin, mchimbuzi wa vitu vya kale B. Cobbey Crisler, mtungaji-mwenzi wa kitabu kilichotajwa juu, na Mark Myles mhandisi wa hali zenye kukuza sauti waliendesha michunguzo “karibu na Tell Hum, mahali ulipokuwa Kapernaumu wa kale.” Huko “bara linainama kwa uanana likiinuka kutoka kwenye Bahari ya Galilaya kwenda kwenye barabara moja ya ki-siku-hizi zaidi ya mwendo unaolingana na uwanja wa mpira kutoka hapo.” Crisler alipita-pita ndani ya maji hayo ya kihori na kutoka humo akasimama juu ya mwamba mkubwa humo. Halafu akaondoa pumzi katika vibofu vya kupuliza vyenye ukubwa mmoja ili kutokeza mlio unaopatana, na kuvitoboa-toboa kwa zamu za vipindi vilivyopimiwa urefu. Myles, akitumia meta ya kielektroni ya kupimia nguvu za sauti, aliandika kadiri za desibeli (viwango vya sauti) huku akitembea kuelekea juu kwenye barabara. Ndipo Crisler akaja ufuoni na kurudia kule kutoboa-toboa vibofu vya mpulizo akiwa hapo. Tokeo lilikuwa nini? Mlio wa kutoka kwenye mwamba ulio nje ya maji katika kihori kile ulikuwa mzito kuliko ule wa kutoka ufuoni! Jambo la kupendeza ni kwamba, wakati Crisler alipokuwa nje katika kihori kile cha maji, magari kadhaa yenye watalii yalisimama barabarani juu yake. Yeye angeweza kusikia waziwazi mtu mmoja akiuliza: “Yeye anafanya nini kule chini?” Mwingine alijibu: “Mimi sijui. Yeye anasimama huko tu akiwa ameshika vibofu vyekundu vya mpulizo.”
Kwa uwazi, wakati watu wanapokuwa wamesimama au kuketi juu ya mahali fulani pa usawa mmoja, mlio wa sauti yenye kutokezwa unafyonzwa na miili, nywele, mavazi, majani-majani, na nafasi. Hata hivyo, wakiwa juu ya kilima au mwinamio kama vile kule Kapernaumu, mnenaji, akiwa umbali fulani unaofaa kule chini na mbali kutoka walipo, anaweza kusikiwa, sauti yake ikikuzwa sana. Bila shaka, usio wa kukosa kufikiriwa ni ule usikizi wa kutega sana sikio unaofanywa na wasikilizaji wakati huo, na kutokuwapo sana kwa makelele ya ki-siku-hizi yanayotokea kule nyuma kutokana na ndege-abiria, magari, malori, na kadhalika.
Lakini namna gani juu ya pindi nyinginezo ambapo Biblia inaripoti kwamba Yesu alihutubia makutano makubwa? Crisler na Myles wanatoa nadharia ya kwamba Yesu na watu wengine wa Kibiblia waliohutubia wasikilizaji wengi “walitafuta [kwa makusudi] maeneo ya mahali peupe yaliyojulikana kuwa yenye hali za mazingira yenye kukuza sauti na wakayatumia kwa uwasiliano wa tungamano la watu.”
Crisler na Myles wamefanya uchunguzi mbalimbali pia “ili kuamua ni watu wangapi wangaliweza kumwona Yesu waziwazi siku aliyonena akiwa hapo.” Kwa kuchukua kwamba hiyo ilikuwa siku nyangavu, isiyo na mawingu, wao walikadiria kwamba “wasikilizaji 5,000 na 7,000 wangaliweza kuwa walimsikia na kumwona Yesu akihutubu akiwa mbali na ufuo.” Jambo hili lilisababisha Bortin mwandikaji wa karatasi-habari akate shauri kwamba “hii inaunga mkono masimulizi ya Gospeli juu ya makutano makubwa kutoka sehemu zote za Palestina yaliyoenda Galilaya makundi-makundi kushuhudia yule mponyaji wa kimwujiza alipokuwa akiwahutubia kwa kutumia mifano ya maneno. Kwa kweli pale mahali pa Kapernaumu penye jumba la kimawonyesho lililofanyika kiasilia likiwa na umbo kama bakuli liliruhusu kila mmoja amwone waziwazi.”
Bila shaka, haiwezi kutaarifiwa kwa kushikilia kauli kama itikadi kwamba Crisler na Myles wamegundua mahali penyewe hasa pa hotuba ya Yesu ya kando ya ufuo. Hata hivyo, inapendeza kuangalia kwamba mahali panapodokezewa ni mahali ambapo vichaka vya miiba na miamba vinapatikana kwa wingi, huku maua-haradali ya manjano yakikua miongoni mwavyo. Kuvikazia kwa Yesu katika vielezi vyake kungaliongezea fundisho lake kwa njia hiyo. Akiwa katika eneo la hizo hali nzuri za mazingira yenye kukuza sauti, amri ya Yesu ya ‘kusikiliza’ ingalikuwa pia ilifaa sana. (Marko 4:3 NW) Vivyo hivyo, utumizi wake wa neno “masikio” na namna zile nyingi za kitenzi “kusikia” zingaliweza kwa urahisi kuwa zilithaminiwa na wasikilizaji wake wote katika mahali pa namna hiyo. Ndiyo, zaidi ya kuwa wangaliweza kumsikia na kumwona Yesu waziwazi kabisa, wote waliokuwa hapo katika hilo “jumba la kiasili” wangaliweza kuwa walishika sana uzito kamili wa vielezi vyake kwa kutazama-tazama tu hapa na pale.
[Ramani katika ukurasa wa 25]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Mahali palipokuwa:
1. Kapernaumu
2. Uwanda wa Genesareti
3. Tiberia
4. Mwondokeo wa Mto Yordani upande wa kusini
5. Mlima Tabori
Bahari ya Galilaya
Galilaya
[Credit Line]
Based on a map copyrighted by Pictorial Archive (Near Eastern History) Est. and Survey of Israel
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kutazama upande wa kaskazini-mashariki kando-kando ya Bahari ya Galilaya kuelekea Kapernaumu; yaonekana kutoka kwenye ukingo wa Uwanda wa Genesareti
[Credit Line]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Pembe ya Kaskazini-magharibi ya Bahari ya Galilaya. Inaelekea ilikuwa karibu na Kapernaumu kwamba Yesu alilihutubia kutano akiwa kwenye mashua
[Credit Line]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.