Ithibati ya Uhifadhi wa Kimungu
NENO la Mungu lililovuviwa limepitishwa kwetu kwa usahihi, na kwa ajili ya uhifadhi huo mzuri sana ni lazima sisi tutoe asante hasa kwa Mtungaji wa Biblia. Labda kuna hati 6,000 za Maandiko ya Kiebrania yote mazima au sehemu zayo na hati zipatazo 5,000 za Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo.
“Neno la Bwana [Yehova, NW] hudumu hata milele.” (1 Petro 1:25) Lakini utafiti wa ki-siku-hizi umetokeza nini kwenye nuru kuhusu uhifadhi wa Neno Takatifu lake?
Ni Maandishi-Awali Yenye Kutegemeka kwa Kadiri Gani?
Maandishi-awali ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo yanategemeka kwa kadiri gani hasa? Ni yenye kutegemeka sana kwa njia isiyo na ulinganifu wakati tunapofikiria miandiko ya mambo mengineyo ambayo imeendelea kuwako tangu zamani. Uhakika huo ulikaziwa katika kitabu Auf den Spuren Jesu (Katia Hatua za Nyayo za Yesu), kilichotungwa na Gerhard Kroll. Mtungaji alionyesha, mathalani, kwamba kati ya miandiko ya mwanafalsafa Mgiriki Aristotle (karne ya nne K.W.K.) ni mafunjo sita tu yaliyo katika hifadhi, yaliyo mengi yakiwa ya tarehe zinazoanzia karne ya kumi W.K. au baada ya hapo. Kazi za Plato (karne ya nne K.W.K.) zilidumu kwa kadiri bora kidogo. Kuna hati kumi za kazi zake zilizo za tarehe zinazoanzia kabla ya kame ya 13. Kwa habari ya Herodoto (karne ya tano K.W.K.), kuna vipande vya mafunjo karibu 20 vyenye tarehe zinazoanzia karne ya kwanza W.K. na baadaye. Hati za kwanza zilizo kamili za kazi yake ni za tarehe zinazoanzia karne ya kumi. Na hati zilizo za mapema zaidi za kazi za Yosefo ni za tarehe zinazoanzia karne ya 11 tu.
Kwa utofautiano na hayo, maandishi-awali ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo (yaliyokamilishwa katika karne ya kwanza W.K.) yanashuhudizwa na vipande vya kuanzia karne ya pili na nakala kamili za kuanzia karne ya nne. Kulingana na Kroll, kuna mafunjo 81 kuanzia karne ya 2 mpaka ya 7, hati 266 zenye mwandiko wa herufi-ansiali za kuanzia karne ya 4 mpaka ya 10, na hati 2,754 zenye mwandiko wa herufi-kasivu za kuanzia karne ya 9 mpaka ya 15, na pia maandishi mengine kama hayo 2,135 yaliyo na mwendelezo kidogo tu wa herufi. Yote hayo yanatusaidia kuthibitisha maandishi-awali ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Kwa hiyo, ndivyo ilivyo, hayo maandishi-awali yanashuhudizwa kweli kweli.
Kipande Muhimu cha Gospeli ya Yohana
Ni nani angetarajia kupata sehemu ya hati ya Biblia yenye thamani kubwa katika rundo la takataka? Hata hivyo, humo ndimo kilipatikana kipande kilicho hazina kubwa cha sura ya 18 ya Gospeli ya Yohana. Sasa kikiwa kinajulikana kuwa John Rylands Papyrus 457 (P52), kimehifadhiwa katika Manchester, Uingereza. Kiligunduliwa jinsi gani, na kwa nini ni cha maana sana?
Karne hii ilipokuwa ikianza, wachimbuzi wa vitu vya kale walichimbua tungamo la vipande vya mafunjo, kutia na barua, stakabadhi (risiti), nasaha, na hati za kuhesabu watu, pamoja na maandishi mengine mengi, nje ya mji wa Oxyrhynchus katika wilaya ya El Faiyûm, Misri. Vingi vyavyo vikiwa vimeandikwa katika Kigiriki, vyote vilikuwa vimehifadhiwa kwa karne kadhaa katika mchanga mkavu.
Katika mwaka 1920, Maktaba ya John Rylands ya Manchester ilijitwalia mafunjo hayo. Miaka kumi na minne baadaye, wakati mwana-chuo C. H. Roberts alipokuwa akichagua-chagua baadhi ya vipande hivyo, aliona maneno machache yaliyoonekana ni kama amewahi kuyaona hapo kwanza. Wazia taharuki yake alipong’amua kwamba yalikuwa ya kutoka kwenye Yohana sura ya 18, sehemu za mistari 31 hadi 33 zikiwa upande mmoja wa kipande hicho na sehemu za mistari 37 na 38 zikiwa upande ule mwingine (verso). Kipande hicho cha mafunjo kikathibitika kuwa ndicho kisehemu cha mapema zaidi kijulikanacho cha hati za Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo ambazo zimepata kugunduliwa. Kikiwa kimeandikwa kwa herufi kubwa za Kigiriki zinazoitwa ansiali, awali yacho ilikuwa katika nusu ya kwanza ya kame ya pili ya Wakati wa Kawaida wetu.
Kipande hicho kina kipimo cha sentimeta 8.9 kwa 6.4. Ni jinsi gani inawezekana kukipa kipande hicho cha mafunjo tarehe ya usahihi hivyo? Hasa ni kwa kuchunguza mtindo wa mwandiko, huo ukiwa ni uchunguzi unaojulikana kuwa paleografia. Mwandiko wote hubadilika pole kwa pole kwa kadiri miaka inavyopita, na mabadiliko hayo ndiyo yanayoonyesha umri wa hati, kukiwa na mruhusio wa kuweza kukosea kwa miaka kadhaa ya kurudi nyuma au kwenda mbele. Kwa hiyo hati kamili ambayo kipande hicho ni sehemu yacho iliyo ndogo sana ilinakiliwa karibu sana na wakati wa usimulizi wa Gospeli ya awali ambao uliandikwa na Yohana mwenyewe. Inaelekea kuwa hilo lilikuwa pengo dogo la kama miaka 30 au 40. Sisi tunaweza kuwa na uhakika pia kwamba usimulizi wa Yohana haukubadilishwa kwa njia kubwa na waandishi wa baadaye kwa maana maandishi ya kipande hicho yanakaribia kuwa na uafikiano kamili na yale yanayopatikana katika hati za baadaye.
Kabla ya pato hilo, wachambuzi walikuwa wamebisha kwamba Gospeli ya Yohana haikuwa mwandiko halisi wa mtume wa Yesu bali ilikuwa imeandikwa wakati fulani baadaye, kuelekea mwisho wa karne ya pili. Tofauti na hivyo, sasa ni wazi kutokana na kipande hicho kwamba Gospeli ya Yohana ilikuwa katika Misri katika ile nusu ya kwanza ya karne ya pili W.K., si ikiwa hati-kunjo, bali kwa namna ya kitabu ambacho ni kodeksi. Inashangaza kama nini kwamba kipande hicho cha mafunjo chenye kuonekana kama kisicho cha maana sana kingeweza kunyamazisha wachambuzi kwa athari ya jinsi hiyo!
[Sanduku katika ukurasa wa 31]
MAFUNJO
MAFUNJO ni mmea ambao husitawi katika maji yaliyotulia yasiyo na kina kirefu, au mabwawa yenye matope-matope na kandokando ya kingo za mito inayoenda pole, kama vile Naili. (Ayubu 8:11) Huenda ikawa karatasi ya mafunjo ilitumiwa kuwa kiandikio mapema sana hata wakati wa Abrahamu. Baadaye, kufanyizwa kwayo kulikuwa moja ya kazi kubwa za ufanyizaji-vitu wa Wamisri wa kale. Katika kuifanyiza, walifuata utaratibu ulio rahisi kidogo. Marefu ya ganda la ndani lililo jororo yalikatwa-katwa kuwa vichane virefu vyembamba na kulazwa kando kwa kando, huku kitabaka kingine kikiwa kimepakwa gundi na kulazwa juu kwa kukingamana navyo. Ndipo kitu hicho kilipofinyiliwa na kukunjwa kiwe karatasi moja, kikakaushwa katika jua, halafu kikang’arishwa kwa jiwe la kusugulia, magamba laini ya magegereka, au meno ya ndovu. Karatasi zingeweza kuunganishwa ziwe hati-kunjo moja, urefu wa wastani ukiwa kati ya meta 4 na 6, ingawa moja imehifadhiwa iliyo na urefu wa meta 41. Au sivyo, kurasa zingeweza kukunjamanishwa ziwe kodeksi iliyo kama kitabu, hiyo ikiwa ndiyo hati ya namna iliyotumiwa sana miongoni mwa Wakristo wa mapema.
[Sanduku katika ukurasa wa 31]
PACHIMENTI na VELAMU
KODEKSI Alexandrine ya karne ya tano, moja ambayo hapo awali ilikuwa na Biblia nzima, imeandikwa juu ya velamu. Kifaa hicho ni nini, na ni jinsi gani kinavyotofautiana na pachimenti?
Kuanzia nyakati za mapema, pachimenti (kiandikio cha ngozi) kilifanyizwa kutokana na ngozi ya kondoo, ya mbuzi, au ya ndama. Ilitayarishwa kwa kuparuza nywele zitoke kwenye ngozi zilizooshwa, halafu ngozi hizo zikanyooshwa juu ya viangikio ili zikauke. (Linganisha 2 Timotheo 4:13.) Kufikia karne za tatu na nne za Wakati wa Kawaida wetu, ilikubaliwa kwamba utofautisho uwekwe kati ya viwango vya ubora wa kifaa hicho, kile kisicho laini sana kikiendelea kujulikana kuwa pachimenti, kile kilicho laini zaidi kikijulikana kuwa velamu. Ili kupata velamu, ngozi zilizotumiwa ni zile tu zilizokuwa nyororo sana za ndama au mtoto wa mbuzi au za ndama au wana-kondoo waliozaliwa wakiwa wamekufa. Hizo zilitokeza kifaa cha kuandikia kilicho chembamba na laini, kilichokaribia kuwa cheupe, nacho kilitumiwa kwa vitabu vya maana mpaka ulipofanywa uvumbuzi wa uchapaji, na utumizi wa karatasi ukawa wa bei ndogo zaidi na bora zaidi kwa uchapaji huo.